Zingatio 8: Utaipata Wapi Tena Fursa Hii Ya Ramadhwaan?

 

 

 

Zingatio 8: Utaipata Wapi Tena Fursa Hii Ya Ramadhwaan?

 

Naaswir Haamid

 

 

 Alhidaaya.com

 

 

Ramadhwaan ndio inaondosha nanga na hakuna ajuaye nani ataipata tena fursa hii adhimu. Hili ni kundi la mwisho lenye Laylatul-Qadr ndani yake na hivyo tujiweke vizuri kushinda bila ya kujali muda. Hatuna nafasi ya kusubiri ila ni hii.

 

 

Huu ndio mwezi wa kuoneshana mapenzi ili kutaraji Rahma mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Hili linadhihirishwa kwa kumtumikia Rabb wa mbingu na ardhi. Tusiwe ni wenye kutenda mema mwezi huu tukayaacha miezi iliyobaki nyuma ya migongo yetu. Hio itakuwa ni sawa na shirk, kwani tulimuabudu Ramadhwaan na kumuacha Rabb wa Haki.

 

 

Ramadhwaan ni mwezi wa kusoma, kukutana katika kheri, kuhurumiana, kuacha fitnah na mengineyo. Haya yote yawe mara tatu zaidi kwenye kipindi hichi cha siku za mwisho za Ramadhwaan.

 

 

Basi, huu sio wakati wa kulegeza kamba kwa kuweka matumaini ya kukutana na Bwana ‘Iyd kwenye pombe, zinaa, kamari na mengineyo maovu. Ni lazima kumuheshimu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  ili tupate kujiheshimu mbele ya wanaotuzunguka kwa matendo, matamshi na kivazi. Kujiheshimu huku kuwe kwa siri na kwa dhahiri.

 

 

Huu ni mwezi wa ‘ibaadah na katu sio mwezi wa mchezo. Huu ni mwezi wa kujifunza taqwa ili tuwe wenye kumcha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kipindi chote cha miezi 11 iliyobaki. Sio uungwana kuwa wenye taqwa mwezi wa Ramadhwaan na kugeuka mnyama miezi kumi na moja.

 

 

Siku zilizobaki sio za kwenda kufanya manunuzi ya mambo yasiyo maana, hizi ni siku za kukaa I’tikaaf Msikitini kwa kutubu na kutaraji malipo mema mbele ya Allaah ('Azza wa Jalla). Ustahamilie usingizi wako kwenye mwezi huu mmoja na uyaheshimu masiku yaliyobaki kwa lengo la kupata Jannah. Tukumbuke kwamba moja miongoni mwa siku hizi kuna siku iliyo bora, nayo ni Laylatul-Qadr yenye ubora wa miezi alfu moja. Na mwenye kunyimwa kheri ya siku hii, amenyimwa kheri zote.

 

 

Imepokewa kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), kwamba amesema: ((Umekujieni mwezi wa Ramadhwaan, ni mwezi wa Baraka.  Imefanywa Swawm kwenu kuwa ni fardh, milango ya Jannh hufunguliwa na milango ya moto hufungwa na mashaytwaan hufungwa. Umo katika mwezi huu usiku ulio bora kuliko miezi alfu.  Atakayenyimwa kheri zake hakika kanyimwa [yote ya kheri])) [Imepokewa na Imaam Ahmad]

 

 

Kwa wale waliowaasi wazee wao, huu ndio wakati wa kurudi kabla ya kuzikosa radhi zao zitakazopelekea kukosa radhi za Muumba. Hivyo, turudi kwa wazee tuliowaasi, tuombeane radhi na du’aa zenye kheri.

 

 

Ama kwa wanandoa waliofarikiana kwa sababu zisizo na msingi, hizi ni siku za kuombeana radhi na kurudiana kwa wema. Kwani haitokuwa na maana kufarikiana ilhali kila mmoja anaishi na kimada.

 

 

Kumi hili sio la kujilazimisha kuacha kula na kunywa. Hizi ndio siku za kukaza kamba, kujipinda barabara kwa kumfurahisha Allaah ('Azza wa Jalla). Malipo ya Jannah sio mepesi. Yanahitaji kazi, na bila ya shaka kazi yake ipo hapa Duniani, na inaanzia kwa kumtumika Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na sio Ramadhwaan pekee.

 

Share