Zingatio 6: Tuikirimu Ramadhwaan

 

Zingatio 6: Tuikirimu Ramadhwaan

 

Naaswir Haamid

 

 

 Alhidaaya.com

 

 

Ni juu yetu kuelewa kwamba wakati haupo nasi, kila sekunde inayokatika hakika itakuwa imeandikwa. Andiko litakaloangukia kuwa ni thawabu au dhambi. Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Atughufirie madhambi yetu kwenye mwezi huu mtukufu wa Ramadhwaan.

 

Ramadhwaan ni mgeni mwema,

Mazuri kwake yametuwama,

Ni sisi kujitahidi kuyachuma,

Kwa nguvu, bidii na hima.

 

Wangapi wamepita kabla yetu na kushuhudia Ramadhwaan zikija na kuondoka hali ya kuwa ni wenye kukhasirika? Lakini wapo wema waliopita ambao walielewa kuwa bidhaa ya Ramadhwaan ni ghali kuinunua, bei yake inayouzwa si rahisi hata kidogo, nayo si bidhaa nyengine ila ni Jannah. Hao ndio wakuwaiga mwendo wao. Na hakuna mwengine aliye bora wa mfano zaidi ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Tufuate Sunnah zake bila ya kinyongo na kwa faida yetu sisi wenyewe.

 

Ramadhwaan imejaa fadhila kede kede, na moja wapo ni kuachiwa huru na moto. Ni sawa na mfano wa Raisi anapowaachia huru wafungwa kadhaa kwa mnasaba wa kuadhimisha sherehe za taifa. Ndivyo ilivyo kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa mwezi huu wa Ramadhwaan. Wala hatuna haja ya kufichana kwamba yawezekana kabisa kuwa sisi ni miongoni mwa watu wa Motoni. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Atuepushe na adhabu ya Jahannam! Tujipinde kwenye mwezi huu mtukufu ili tuachiwe huru na moto kama anavyosema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):  "Swawm ni kinga, itamukoa mja kutokana na moto (siku ya Qiyaamah)"
[Imesimuliwa na Jaabir (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na kupokelewa na At-Twabaraaniy kutoka kwa ‘Uthmaan bin Abil ‘Aasw]

 

Hivyo tuishi naye kwa vizuri kwani hana siku nyingi kwetu sisi, tumtayarishie yale mazuri ayapendayo sio tu kwenye maakulati bali kuanzia kwa Qiyaamul-layl (kisimamo cha usiku kuswali), tabia njema, ‘ibaadah zilizothibiti, hadi futari ya halaal. Tusiwe ni wenye kumkasirisha Rabb wetu kwa kutoitumikia Ramadhwaan kwani abadan Ramadhwaan hajajia mabaya. Ramadhwaan katu hajafika kututilia rangi vikao vya karata wala kuwaweka kitako wanawake kufanya ‘ibaadah ya kupika tu mchana na usiku. Basi tumfanyie mema ili tufaidike na ugeni wake.

 

 

Share