03-Madhara Ya Ghiybah: Ulimi Ni Kufaulu Kwako Au Kuangamia Kwako

Madhara Ya Ghiybah (Kusengenya) Na An-Namiymah (Kufitinisha)

 

03-  Ulimi Ni Kufaulu Kwako Au Kuangamia Kwako

 

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameuhifadhi ulimi ndani ya mdomo, ili usiwe wazi kila mara ukanena maneno mengi ambayo huenda yakamuangamiza binaadamu kwa kumuharibia ‘amali zake, au kukosa radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) hata mtu akitamka neno moja tu ovu ni hatari kwa sababu  linaweza kumfikisha motoni. Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameonya:

 

عن أَبي هريرة رضي اللهُ عنه ، عن النبيّ صلى الله عليه وسلم قَالَ : (( إنَّ العَبْدَ لَيَتَكَلَّمُ بِالكَلِمَةِ مِنْ رِضْوَانِ الله تَعَالَى مَا يُلْقِي لَهَا بَالاً يَرْفَعُهُ اللهُ بِهَا دَرَجاتٍ ، وإنَّ العَبْدَ لَيَتَكَلَّمُ بِالكَلَمَةِ مِنْ سَخَطِ اللهِ تَعَالَى لا يُلْقِي لَهَا بَالاً يَهْوِي بِهَا في جَهَنَّمَ )) . رواه البخاري .

 

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: "Hakika mja huzungumza maneno yenye kumridhisha Allaah (سبحانه وتعالى) bila kuyapa umuhimu wowote, na Allaah Akamnyanyulia kwayo daraja nyingi Na hakika mja huzungumza maneno yenye kumkasirisha Allaah (سبحانه وتعالى) bila kuyapa umuhimu wowote, yakaja kumporomosha ndani ya Jahannam.” [Al-Bukhaariy]

 

Kutokana na Hadiyth hii, tunapata funzo kwamba, ulimi unaweza kuwa ni kiungo kizuri kabisa katika mwili wa binaadamu na unaweza kuwa ni kiungo kiovu kabisa vile vile.

 

Kisa kifuatacho cha Luqmaan kinatuthibitishia funzo hili:

 

Ibn Jariyr amenukuu kwamba Khaalid Ar-Rabaai alisema: "Luqmaan alikuwa mtumwa wa Kiethiopia aliyekuwa na ujuzi wa useremala. Bwana (Tajiri) wake alimwambia: "Tuchinjie huyu kondoo." Akamchinja, kisha akamwambia: "Niletee viungo viwili vilivyokuwa ni bora kabisa." Akampelekea ulimi na moyo. Baada ya siku kupita, alimtaka tena amchinjie kondoo, akachinja kisha Bwana wake akamwambia tena: "Niletee viungo viwili vilivyokuwa ni viovu kabisa." Akameletea vile vile ulimi na moyo. Bwana wake akamuuliza: "Nilipokutaka uniletee viungo bora kabisa umeniletea ulimi na moyo; na nilipokutaka uniletee viungo viovu kabisa umeniletea hivyo hivyo." Luqmaan akamwambia: "Hakuna vilivyo bora kuliko hivi vinapokuwa vizuri, na hakuna vilivyo viovu kabisa kuliko hivi vinapokuwa vibaya." [At-Twabariy: 20:135]

 

Mafunzo mengineyo kuhusu ulimi:

 

 

  1. Ulimi ni kipande kidogo cha nyama kisichokuwa na mifupa lakini kinaweza kumvunja mtu mifupa yake siku ya Qiyaamah.
  1. Ulimi ni kama nyoka utakaomtia sumu binaadamu, au ni kama mkuki utakaomuangamiza binaadamu siku ya Qiyaamah.
  1. Hivyo hivyo, ulimi huenda ukawa ni sababu ya kumuingiza mtu Peponi japo kama hakuwa na matendo mengi ya wema. 

 

  1. Ulimi ni kiungo kikuu katika mwili wa binaadamu kinachodhibiti viungo vingine vyote vya mwili wa binaadamu kutokana na Hadiyth ifuatayo ya Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ رَفَعَهُ قَالَ : قال رسول الله صلى الله عليه وسلم:  (( إِذَا أَصْبَحَ ابْنُ آدَمَ، فَإِنَّ الْأَعْضَاءَ كُلَّهَا تُكَفِّرُ  اللِّسَانَ، فَتَقُولُ : اتَّقِ اللَّهَ فِينَا، فَإِنَّمَا نَحْنُ بِكَ، فَإِنِ اسْتَقَمْتَ اسْتَقَمْنَا، وَإِنِ اعْوَجَجْتَ اعْوَجَجْنَا))  أخرجه الترمذي وأحمد وابن خزيمة والبيهقي بسند حسن. رياض الصالحين

Kutoka kwa Abuu Sa'iydil-Khudriyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah  (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Anapoamka mwana Aadam viungo vyote vinaulaumu ulimi vikisema: Mche Allaah kwetu, kwani sisi tuko katika hifadhi yako; ukiimarika nasi tutaimarika, ukienda pogo, nasi tutakwenda pogo)) [At-Tirmidhiy, Ahmad, Ibn Khuzaymah, Al-Bayhaqiy ikiwa ni sanad hasan. Riyaadhwus-Swaalihiyn]

 

Ni vyema kuzuia ulimi usitoke kuzungumza maneno yoyote ila pale unapohitajika kwani kuuachia ulimi utamke tu ya kutamkwa bila ya kutahadhari, utampeleka mtu kutoa porojo na kuzungumza yasiyofaa na kumharibia mja Aakhirah yake.

 

 

 

Share