Kuoa Mwanamke Mwenye Mimba Ya Mtu Mwingine

SWALI:

Bismilahi rahmani rahim

sifa zote kamilifu ni zake mweneyezi mungu (sw)na mjumbe wake muhamad swalahu alaihi wasalam baada yakumshukuru mola ninazidi kumuomba mungu awazidishiyekila la gheri katika hiyi jitihada yenui ya manufaa kwetu kama waislam hususan sisi tuko nchi zakikafiri (ulaya)bila nguvu zenu tungelikuwa hatupati sabuni hii ya roho tunayo ipata katuka mtandao huu baada ya hayo nina swali lililonitatiza kwa mda mzefu alhamdulilah nilipata anuani yenu nikamshukuru mola zote hizi ni barka na neema zake swala langu ni ili lifwatalo:

mimi nilimuingiza mwanamke katika dini kwa kutafuta kwanza swawabu za kuingiza mtu katika uislam pia nikasema ivi amekubali kuingia acha nimuowe ili niwe karibu nae kwa kuzidi kumfundisha dini lakini matarajio yangu hayakuwa nilivyo fikiria alhmdulilah, tulikuwa marafiki kabla sijamuowa na shaitwani akanishinda nguvu sikuweza kujikinga na zina na baada ya hapo nikalaumu nafsi yangu nikaamuwa kufunga nae ndowa kwa imam. Mwanamke alikuwa mjamzito wa mwezi mmoja wakati tulifunga ndo sikuwa najuwa. Nilijuwa wakati wakujifunguwa kwa kuangalia miezi yaani alizaa tunamiezi minane tumeunga ndowa.

Kisheria mtoto sio wangu kwasababu ya kitendo niliofanya na nazidi kumuomba msamaha mola.   Na Itakuwaje kwa haki za baba kwa mtoto ao haki za mtoto kwa baba? Najuwa kama hawezi kunirisi au mimi nikamrisi nikimlea uyo mtoto kiislamu inshaallah anaweza akaniombea dua kama dua ya mtoto kwa baba?  Kwasabu nilisikia kwa mashehe wetu wanasema fundisheni watoto zenu dini il wawaombeeni dua.

Na haki za mtoto kwa baba zinaswihi?

msichoke vingozi wetu sisi niwagonjwa tuna hitaji dawa kwenu inshaalah swali lifwatalo na kama ndowa yetu inaswihi ? 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Qiyaamah.

Kwanza tunapenda na sisi kutoa shukurani kwa du'aa zenu nzuri mnazotuombea nyote mnaotuma maswali yenu pamoja na wengineo wanaoingia ALHIDAAYA kutafuta faida mbali mbali. Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atutakabalie hizo du'aa na Atuzidishie uwezo wa kuelimishana kwa kadiri Anavyotujaalia. Aamiyn

Twashukuru kwa swali lako.

Inapaswa tufahamu kuwa hata ukawa na nia nzuri namna gani ni lazima uchukue tahadhari za hali ya juu. Na mara nyingi huona kuwa sisi hatuwezi kuingia katika maasiya hivyo kumpelekea mtu kuingia katika kuwa faragha na mwanamke ambaye si maharimu yake. Na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kuwa:

)) لا يخلون رجل بامرأة إلا كان ثالثهما الشيطان))  صحيح الترمذي

((Hawakai mwanamme na mwanamke peke yao isipokuwa shetani anakuwa watatu wao))  [Sahiyh At-Tirmidhiy]

Huku kuilaumu nafsi pindi mtu anapofanya makosa ni njia ya kutubia na kuonyesha Imani katika moyo wa Muislamu. Kwani Muislamu aliye bora ni yule anapokosa anajirudi na kuomba msamaha, na nafsi yenye kujilaumu (Nafsul-Lawaamah) huwa inakaribia ile nafsi iliyotulia (Nafsul-Mutwmainah).

Katika Uislamu haifai kumuoa mwanamke aliye na mimba mpaka azae kwani Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kumwaga mbegu za kiume kwa mwanamke ambaye tayari ashatiwa mbegu za mtu mwengine:

((لا يحل لامرئ يؤمن بالله واليوم الآخر أن يسقي ماءه زرع غيره)) ابن حبان  

((Haimpasi mtu mwenye kumuamini Allaah na Siku ya Mwisho amwage maji (ya uzazi) juu ya mbegu aliyootesha mwingine)) [Ibn Hibbaan]

Lakini kosa hilo lishafanyika bila ya mtu kujua au kufahamu na kosa lililofanyika bila ya kujua linasamehewa katika Uislamu. Hata hivyo, kwa rai iliyo salama zaidi na sahihi zaidi, Wanachuoni wanasema kuwa ni bora mtu ajutie na afanye tawbah ya kweli kwa matendo hayo aliyoyafanya, kisha afunge ndoa nyingine mpya. Tunapaswa kufahamu ya kwamba ikiwa umezini na mwanamke na kisha unataka kumuoa ni lazima kufanyike tawbah ya kweli na kupite kipindi fulani ya kutengana baina ya mume na mke kabla ya kuoana, na kuweze kuonekana mabadiliko ya kitabia na kimaadili baina ya hao waliofanya makosa. Ingawa na hilo pia halikufanyika kwa sababu ya kutojua, basi kwa rai hiyo ya Wanachuoni, ni bora kujutia na kufanya tawbah na kisha kufungwa tena hiyo ndoa..

Vizuri pia ujue suala la ndoa kwa uliyezini naye, ambalo linapatikana katika kiungo hichi hapa:

Ndoa Ya Waliofanya Zinaa

Ni vyema kuwa umetambua kuwa mtoto si wako kishari'ah na kuwa hakuna anayeweza kumrithi mwenziwe katika mali anayoiacha pindi anapokufa. Lakini katika mas-ala ya mirathi kuna kipengele cha wasiya ambacho mtoto au mwengine anaweza kumrithisha mtu ambaye kwa kawaida harithi kwa kumpatia kiwango kisichozidi thuluthi (1/3).

Tufahamu kuwa malezi bora anafaa baba ampatie mtoto wake wa damu na mtoto mwengine yeyote ambaye anamlea kama wake, hivyo katika mas-ala ya kumlea mtoto huyo kwa njia iliyo nzuri utapata ujira wako kwa Mola Mlezi. Waislamu wao kwa wao wanatakiwa waombeane kheri iwashukie kutoka kwa Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) na dua kama hizo huwa zinakubaliwa na Mola. Lakini kwa kuwa huyo si mtoto wako du'aa anayoombewa itakuwa ni sawa na ile wanaoombewa Waislamu wengine kwa ujumla wake.

Na Allaah Anajua zaidi  

 

Share