Kusoma Vitabu Vya Mapenzi Na Tendo La Ndoa Inajuzu?

SWALI:

JE KUSOMA VITABU VINAVYOZUNGUMZIA MASUALA YA MAPENZI NI SAHIHI? NA KAMA SI SAHIHI JE VYA KIDINI VINAVYOELEZEA MASUALA YA TENDO LA NDOA?

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Qiyaamah.

Ama kusoma vitabu vinavyozungumzia masuala ya mapenzi havina tatizo ikiwa vitakuwa vinakwenda sambamba na mafundisho ya Uislamu. Hivyo, vikiwa na picha zenye kuonyesha mume na mke wakiwa uchi katika kufafanua au kueleza vitakuwa havifai kabisa. Au katika maelezo yake ikiwa vitakwenda kinyume na mafundisho ya Kiislamu pia vitakuwa havifai.

 

Ama vitabu vilivyoandikwa na wanachuoni kwa kufuatana na maagizo ya Qur-aan na Sunnah hivyo ndivyo vinavyohitajiwa kusomwa ili tupate muongozo sahihi wa wana ndoa kufanya tendo la ndoa kwa njia zilizo sahihi. Ni muhimu kwa sababu    aghlabu wana ndoa wa Kiislamu huwa hawapati mafunzo hayo kiuwazi na wengi wanaona aibu kuuliza, kisha wanaishia kujinyima haki zao katika tendo la ndoa na huenda wakaingiwa na shauku ya kutafuta njia nyingine za kupata mafunzo hayo ambazo sio halali kama kutazama sinema za ngono n.k. Lakini watakapopata vitabu vyetu vya Kiislamu watapata mafunzo sahihi na khaswa yanayotokana na mafunzo ya dini yetu. 

 

Tutambue kuwa dini yetu haifichi haki, na hakuna aibu kuelezea mambo ya ndani ya ndoa yaliyo haki ili mafunzo hayo yawekwe wazi kwa Waislamu watambue yanayowapasa kutenda kihalali hata waweze kujitosheleza na starehe za kitendo cha ndoa, waweze kuimarisha ndoa zao na kujiepusha na vishawishi vya haramu. 

 

Kwa hakika vitabu hivi viko vingi katika lugha ya Kiarabu na kwa Kiswahili vimeanzwa kuandikwa kama kwa mfano Furaha ya Ndoa na Siri ya Unyumba na pia Zawadi kwa Wanandoa ambacho tayari kiko katika hii tovuti yenu kwenye kitengo cha vitabu, ingia hapa ukisome: ZAWADI KWA WANANDOA. Na chengine ambacho kimetafsiriwa ni Malezi ya Kijinsiya lakini bado kuchapishwa.

 

Na Allah Anajua zaidi

 

 

Share