24-Umuhimu Wa Tawhiyd Na Fadhila Zake: Wanyama Na Alivyoumba Allaah Vinathibitisha Tawhiyd

 

Umuhimu Na Fadhila Za Tawhiyd

 

24-Wanyama Na Alivyoumba Allaah Vinathibitisha Tawhiyd

 

 Alhidaaya.com

 

 

Hud-hud (ndege) alikuwa miongoni mwa jeshi la Nabiy Sulaymaan (‘Alayhis-Salaam). Aliporuka na kufikia mji wa Sabaa alikuta watu huko wanaabudu jua, akarudi kumpa taarifa Nabiy Sulaymaan (‘Alayhis-Salaam) huku akidhihirisha kuikanusha ‘ibaadah hiyo batili. Uzuri ulioje ndege huyo kuikanusha ‘ibaadah ya kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na badala yake kuithibitisha Tawhiyd ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa)! Kisa chake kinaanza katika Qur-aan pale alipokosekana katika jeshi la Nabiy Sulaymaan (‘Alayhis-Salaam). Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَتَفَقَّدَ الطَّيْرَ فَقَالَ مَا لِيَ لَا أَرَى الْهُدْهُدَ أَمْ كَانَ مِنَ الْغَائِبِينَ ﴿٢٠﴾

Akakagua ndege, akasema: “Imekuwaje, mbona simuoni Al-Hud-hud, au amekuwa miongoni mwa walioghibu? 

 

 

لَأُعَذِّبَنَّهُ عَذَابًا شَدِيدًا أَوْ لَأَذْبَحَنَّهُ أَوْ لَيَأْتِيَنِّي بِسُلْطَانٍ مُّبِينٍ ﴿٢١﴾

Bila shaka nitamuadhibu adhabu kali, au nitamchinja, au aniletee hoja bayana.”

 

 

فَمَكَثَ غَيْرَ بَعِيدٍ فَقَالَ أَحَطتُ بِمَا لَمْ تُحِطْ بِهِ وَجِئْتُكَ مِن سَبَإٍ بِنَبَإٍ يَقِينٍ ﴿٢٢﴾

Basi (Hud-hud) hakukaa mbali akasema: “Nimegundua ambayo wewe hukuyagundua na nimekujia kutoka Sabaa na habari za yakini.

 

 

إِنِّي وَجَدتُّ امْرَأَةً تَمْلِكُهُمْ وَأُوتِيَتْ مِن كُلِّ شَيْءٍ وَلَهَا عَرْشٌ عَظِيمٌ ﴿٢٣﴾

Hakika mimi nimemkuta mwanamke anawamiliki, na amepewa kila kitu, na anacho kiti cha enzi kikubwa mno.

 

 

وَجَدتُّهَا وَقَوْمَهَا يَسْجُدُونَ لِلشَّمْسِ مِن دُونِ اللَّـهِ وَزَيَّنَ لَهُمُ الشَّيْطَانُ أَعْمَالَهُمْ فَصَدَّهُمْ عَنِ السَّبِيلِ فَهُمْ لَا يَهْتَدُونَ ﴿٢٤﴾

Nimemkuta na watu wake wanalisujudia jua badala ya Allaah, na shaytwaan amewapambia ‘amali zao basi akawazuia na njia, kwa hiyo hawakuongoka.

 

 

أَلَّا يَسْجُدُوا لِلَّـهِ الَّذِي يُخْرِجُ الْخَبْءَ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَيَعْلَمُ مَا تُخْفُونَ وَمَا تُعْلِنُونَ ﴿٢٥﴾

Kwamba hawamsujudii Allaah Ambaye Anatoa yenye kufichika katika mbingu na ardhi na Anayajua yale mnayoyaficha na yale mnayoyadhihirisha.

 

 

اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ رَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ ۩﴿٢٦﴾

Allaah; hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye, Rabb wa Al-‘Arsh adhimu”. [An-Naml: 20-26]

 

 

Tumepata mafunzo yafuatayo kutokana na ndege huyo Al-Hud-hud:

 

  1. Alikuwa mwenye ‘Aqiydah swahiyh.

 

  1. Aikuwa ni mwenye kumwamini Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

 

  1. Alikuwa mwerevu kuweza kuchungua na kutambua wanayoyaabudu watu katika safari yake hiyo ya haraka kabisa.

 

  1. Aliungulika moyoni kuona watu wanakanusha Tawhiyd ya Allaah (Subhaanahu wa Taa’alaa).

 

  1. Amefanya kazi ya Rasuli kulingania katika Dini ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

 

  1. Jambo kuu alolingania ni la kukanusha shirki na kuthibitisha Tawhiyd.

 

  1. Ameonya kuhusu udanganyifu, uchochezi wa shaytwaan kuwa anawapambia watu ‘amali zao.

 

  1. Ametafakari Utukufu wa Muumba wake, neema Zake na uwezo Wake wa kuyajua yaliyo dhahiri na yaliyofichika.

 

  1. Amefadhilisha Aakhirah kuliko dunia kwani hakujali mali na starehe alizojaaliwa nazo Malkia wa Sabaa.    

 

  1. Akathibitisha tena baada yote hayo Tawhiyd ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

    

    11.  Ndege huyu Hud-hud amekuwa ni sababu ya Malkia wa Saba-a kusilimu katika Uislamu.

 

 

 

Basi tujiulize yafuatayo:

 

  • Je, ingekuwaje kama Hud-hud angepitia watu katika zama zetu hizi ambazo watu wanamshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aa’aa) kwa kila aina ya shirki? 

 

  • Je, ni wangapi wenye mfano wa Hud-hud?  

 

Ni dhahiri kwamba Hud-hud alikuwa mbora kuliko baadhi yetu juu ya kuwa yeye ni mnyama dhaifu anayeruka angani. Bali viumbe wote walioko mbinguni na wanyama ardhini, na vitu vyote Alivyoumba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) vinashuhudia Tawhiyd kwani vyote vinamsujudia na kumsabbih Allaah (Subhanaahu wa Ta’aalaa) kama Anavyosema:

 

أَوَلَمْ يَرَوْا إِلَىٰ مَا خَلَقَ اللَّـهُ مِن شَيْءٍ يَتَفَيَّأُ ظِلَالُهُ عَنِ الْيَمِينِ وَالشَّمَائِلِ سُجَّدًا لِّلَّـهِ وَهُمْ دَاخِرُونَ﴿٤٨﴾

Je, hawaoni vile vitu Alivyoumba Allaah ambavyo vivuli vyake vinasogea huku na kule, kuliani na kushotoni vikimsujudia Allaah na huku vinanyenyekea?  

 

 

وَلِلَّـهِ يَسْجُدُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ مِن دَابَّةٍ وَالْمَلَائِكَةُ وَهُمْ لَا يَسْتَكْبِرُونَ﴿٤٩﴾

Na ni kwa Allaah pekee vinasujudia vyote vilivyomo mbinguni na ardhini katika viumbe vitembeavyo, na Malaika, nao hawatakabari.

 

يَخَافُونَ رَبَّهُم مِّن فَوْقِهِمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ ۩﴿٥٠﴾

Wanamkhofu Rabb wao Aliye juu yao, na wanafanya yale wanayoamrishwa. [An-Nahl: 48-50]

 

 

Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ يَسْجُدُ لَهُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَمَن فِي الْأَرْضِ وَالشَّمْسُ وَالْقَمَرُ وَالنُّجُومُ وَالْجِبَالُ وَالشَّجَرُ وَالدَّوَابُّ وَكَثِيرٌ مِّنَ النَّاسِ ۖ وَكَثِيرٌ حَقَّ عَلَيْهِ الْعَذَابُ ۗ وَمَن يُهِنِ اللَّـهُ فَمَا لَهُ مِن مُّكْرِمٍ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَفْعَلُ مَا يَشَاءُ ۩﴿١٨﴾

Je, huoni kwamba wanamsujudia Allaah walioko mbinguni na ardhini, na jua, na mwezi na nyota, na majabali na miti na viumbe vinavyotembea, na wengi miongoni mwa watu? Na wengi imewastahiki adhabu. Na ambaye Allaah Amemdhalilisha, basi hatopata wa kumkirimu. Hakika Allaah Anafanya Atakavyo. [Al-Hajj: 18]

 

Na Anasema pia (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

تُسَبِّحُ لَهُ السَّمَاوَاتُ السَّبْعُ وَالْأَرْضُ وَمَن فِيهِنَّ ۚ وَإِن مِّن شَيْءٍ إِلَّا يُسَبِّحُ بِحَمْدِهِ وَلَـٰكِن لَّا تَفْقَهُونَ تَسْبِيحَهُمْ ۗ إِنَّهُ كَانَ حَلِيمًا غَفُورًا ﴿٤٤﴾

Zinamsabbih mbingu saba na ardhi na waliyomo humo. Na hakuna kitu chochote isipokuwa kinasabbih kwa Himidi Zake, lakini hamzifahamu tasbiyh zao. Hakika Yeye ni Mvumilivu, Mwingi wa kughufuria. [Al-Israa: 44]

 

 

 

Share