04-Madhara Ya Ghiybah: Kuharamishwa Kwake Na Adhabu Zake Katika Quraan

Madhara Ya Ghiybah (Kusengenya) Na An-Namiymah (Kufitinisha)

 

04- Kuharamishwa Kwake Na Adhabu Zake Katika Quraan

 

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَلَا تَقْفُ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ ۚ إِنَّ السَّمْعَ وَالْبَصَرَ وَالْفُؤَادَ كُلُّ أُولَـٰئِكَ كَانَ عَنْهُ مَسْئُولًا ﴿٣٦﴾

Na wala usifuatilie ambayo usiyokuwa nayo ujuzi. Hakika masikio na macho na moyo; vyote hivyo vitakuwa vya kuulizwa (Siku ya Qiyaamah). [Al-Israa: 36]  

 

 

Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَلَا يَغْتَب بَّعْضُكُم بَعْضًا ۚ أَيُحِبُّ أَحَدُكُمْ أَن يَأْكُلَ لَحْمَ أَخِيهِ مَيْتًا فَكَرِهْتُمُوهُ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ تَوَّابٌ رَّحِيمٌ﴿١٢﴾

na wala wasisengenyane baadhi yenu wengineo. Je, anapenda mmoja wenu kwamba ale nyama ya nduguye aliyekufa? Basi mmelichukia hilo! Na mcheni Allaah! Hakika Allaah ni Mwingi wa kupokea tawbah, Mwenye kurehemu. [Al-Hujuraat: 12]

 

Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) amesema: Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameharamisha Muumimi kumsengenya mwenziwe kama Alivyoharamisha nyamafu.

 

‘Ulamaa wamekubaliana kuwa Ghiybah ni haraam kutokana na kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) iliyotangulia. Na kuhusu kauli Yake:

 

فَكَرِهْتُمُوهُ

((Basi mmelichukia hilo))

 

kwa maana kama mnavyochukia kula nyama ya ndugu yenu aliyekufa basi vile vile mchukie kumtaja mwenzenu kwa ubaya.

 

Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَلَا تَلْمِزُوا أَنفُسَكُمْ وَلَا تَنَابَزُوا بِالْأَلْقَابِ ۖ بِئْسَ الِاسْمُ الْفُسُوقُ بَعْدَ الْإِيمَانِ ۚ وَمَن لَّمْ يَتُبْ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ﴿١١﴾

Na wala msifedheheshane kwa kutukanana na wala msiitane majina (mabaya) ya utani. Ubaya ulioje kuita jina la ufasiki baada ya iymaan. Na yeyote asiyetubu, basi hao ndio madhalimu. [Al-Hujuraat: 11]

 

Mwenye kufanya hivyo; mwenye kusengenya na mwenye kumzushia mwenziwe uongo wamelaaniwa na kushutumiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika Aayah ifuatayo:

وَيْلٌ لِّكُلِّ هُمَزَةٍ لُّمَزَةٍ ﴿١﴾

 

Ole kwa kila mwenye kukebehi na kukashifu watu kwa ishara na vitendo na kwa kila mwenye kufedhehesha kwa ulimi. [Al-Humazah: 1]

 

 

Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) amesema: "Humazah ina maana yule anayetukana na kufedhehesha wenziwe." [At-Twabariy 24: 596] 

 

Al-Hammaaz:   Mwenye kusengenya kwa vitendo kwa mkono au kwa macho kama kukonyeza.  

 

Al-Lammaaz: Mwenye kusengenya kwa ulimi (kunena).

 

[Kauli ya Mujaahid katika Tafsiyr ya Ibn Kathiyr]

 

Yote hayo ni  Ghiybah na adhabu zake ni  kama zilivyotajwa katika Aayah zilizotangulia.

   

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa wanaosengenya kwa kuzulia watu maovu:

 

إِنَّ الَّذِينَ يُحِبُّونَ أَن تَشِيعَ الْفَاحِشَةُ فِي الَّذِينَ آمَنُوا لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ ۚ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿١٩﴾

Hakika wale wanaopenda uenee uchafu wa kashfa kwa wale walioamini; watapata adhabu iumizayo duniani na Aakhirah. Na Allaah Anajua nanyi hamjui. [An-Nuwr: 19].

 

 

 

 

Share