047 - Muhammad

 

مُحَمَّد

 

047-Muhammad

 

047-Muhammad: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

 

الَّذِينَ كَفَرُوا وَصَدُّوا عَن سَبِيلِ اللَّـهِ أَضَلَّ أَعْمَالَهُمْ﴿١﴾

1. Wale waliokufuru na wakazuia Njia ya Allaah, Atazipoteza amali zao.[1]

 

 

 

 

 

وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَآمَنُوا بِمَا نُزِّلَ عَلَىٰ مُحَمَّدٍ وَهُوَ الْحَقُّ مِن رَّبِّهِمْ ۙ كَفَّرَ عَنْهُمْ سَيِّئَاتِهِمْ وَأَصْلَحَ بَالَهُمْ﴿٢﴾

2. Na wale walioamini na wakatenda mema na wakaamini yale aliyoteremshiwa Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم), nayo ni ya haki kutoka kwa Rabb wao, Atawafutia maovu yao na Atatengeneza hali zao. 

 

 

 

 

 

ذَٰلِكَ بِأَنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا اتَّبَعُوا الْبَاطِلَ وَأَنَّ الَّذِينَ آمَنُوا اتَّبَعُوا الْحَقَّ مِن رَّبِّهِمْ ۚ كَذَٰلِكَ يَضْرِبُ اللَّـهُ لِلنَّاسِ أَمْثَالَهُمْ﴿٣﴾

3. Hivyo kwa kuwa wale waliokufuru wamefuata ubatilifu, na kwamba wale walioamini wamefuata haki kutoka kwa Rabb wao. Hivyo ndivyo Allaah Anavyowapigia watu mifano yao.

 

 

 

 

فَإِذَا لَقِيتُمُ الَّذِينَ كَفَرُوا فَضَرْبَ الرِّقَابِ حَتَّىٰ إِذَا أَثْخَنتُمُوهُمْ فَشُدُّوا الْوَثَاقَ فَإِمَّا مَنًّا بَعْدُ وَإِمَّا فِدَاءً حَتَّىٰ تَضَعَ الْحَرْبُ أَوْزَارَهَا ۚ ذَٰلِكَ وَلَوْ يَشَاءُ اللَّـهُ لَانتَصَرَ مِنْهُمْ وَلَـٰكِن لِّيَبْلُوَ بَعْضَكُم بِبَعْضٍ ۗ وَالَّذِينَ قُتِلُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ فَلَن يُضِلَّ أَعْمَالَهُمْ﴿٤﴾

4. Na mtakapokutana (vitani) na wale waliokufuru, basi wapigeni shingo zao, mpaka muwashinde kwa kuwajeruhi na kuwaua, na hapo wafungeni pingu barabara. Kisha ima (wafanyieni) ihsaan baada ya hapo au wajifidie mpaka vita vitue mizigo yake. Ndio hivyo, na lau Allaah Angelitaka basi Angewalipiza kisasi Mwenyewe, lakini (Ameamrisha Jihaad) ili Akujaribuni nyinyi kwa nyinyi. Na wale waliouliwa katika Njia ya Allaah, basi Hatopoteza amali zao.[2] 

 

 

 

 

سَيَهْدِيهِمْ وَيُصْلِحُ بَالَهُمْ﴿٥﴾

5. Atawaongoza na Atatengeneza hali zao.

 

 

 

 

وَيُدْخِلُهُمُ الْجَنَّةَ عَرَّفَهَا لَهُمْ﴿٦﴾

6. Na Atawaingiza Jannah Aliyoitambulisha kwao.[3]

 

 

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن تَنصُرُوا اللَّـهَ يَنصُرْكُمْ وَيُثَبِّتْ أَقْدَامَكُمْ﴿٧﴾

7. Enyi walioamini! Mkisaidia kunusuru Dini ya Allaah,[4] (Allaah) Atakunusuruni na Ataithibitisha miguu yenu.

 

 

 

 

 

وَالَّذِينَ كَفَرُوا فَتَعْسًا لَّهُمْ وَأَضَلَّ أَعْمَالَهُمْ﴿٨﴾

8. Na wale waliokufuru, basi ni maangamizo kwao, na Atapoteza amali zao.

 

 

 

 

 

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ كَرِهُوا مَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأَحْبَطَ أَعْمَالَهُمْ﴿٩﴾

9. Hivyo ni kwa sababu wao wamekirihika na ambayo Allaah Ameyateremsha basi Amezibatilisha amali zao.

 

 

 

 

 

أَفَلَمْ يَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَيَنظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ ۚ دَمَّرَ اللَّـهُ عَلَيْهِمْ ۖ وَلِلْكَافِرِينَ أَمْثَالُهَا﴿١٠﴾

10. Je, hawakutembea katika ardhi wakatazama vipi imekuwa hatima ya waliopita kabla yao? Allaah Amewadamirisha mbali, na kwa makafiri (itakuwa) mfano wa hayo.[5]

 

 

 

 

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ مَوْلَى الَّذِينَ آمَنُوا وَأَنَّ الْكَافِرِينَ لَا مَوْلَىٰ لَهُمْ﴿١١﴾

11. Hivyo ni kwa kuwa Allaah Ni Mlinzi wa wale walioamini na kwamba makafiri hawana mlinzi.

 

 

 

 

 

إِنَّ اللَّـهَ يُدْخِلُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ۖ وَالَّذِينَ كَفَرُوا يَتَمَتَّعُونَ وَيَأْكُلُونَ كَمَا تَأْكُلُ الْأَنْعَامُ وَالنَّارُ مَثْوًى لَّهُمْ﴿١٢﴾

12. Hakika Allaah Atawaingiza wale walioamini na wakatenda mema Jannaat zipitazo chini yake mito. Na wale waliokufuru wanastarehe na wanakula kama walavyo wanyama wa mifugo, na moto ndio makazi yao.

 

 

 

 

 

وَكَأَيِّن مِّن قَرْيَةٍ هِيَ أَشَدُّ قُوَّةً مِّن قَرْيَتِكَ الَّتِي أَخْرَجَتْكَ أَهْلَكْنَاهُمْ فَلَا نَاصِرَ لَهُمْ﴿١٣﴾

13. Na miji mingapi iliyokuwa yenye nguvu zaidi kuliko mji wako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) ambao umekutoa? Tuliwaangamiza! Na hawakuwa na wa kuwanusuru.

 

 

 

 

 

أَفَمَن كَانَ عَلَىٰ بَيِّنَةٍ مِّن رَّبِّهِ كَمَن زُيِّنَ لَهُ سُوءُ عَمَلِهِ وَاتَّبَعُوا أَهْوَاءَهُم﴿١٤﴾

14. Je, basi aliye kwenye hoja bayana kutoka kwa Rabb wake, ni sawa na ambaye amepambiwa uovu wa amali zake na wakafuata hawaa zao?

 

 

 

 

 

مَّثَلُ الْجَنَّةِ الَّتِي وُعِدَ الْمُتَّقُونَ ۖ فِيهَا أَنْهَارٌ مِّن مَّاءٍ غَيْرِ آسِنٍ وَأَنْهَارٌ مِّن لَّبَنٍ لَّمْ يَتَغَيَّرْ طَعْمُهُ وَأَنْهَارٌ مِّنْ خَمْرٍ لَّذَّةٍ لِّلشَّارِبِينَ وَأَنْهَارٌ مِّنْ عَسَلٍ مُّصَفًّى ۖ وَلَهُمْ فِيهَا مِن كُلِّ الثَّمَرَاتِ وَمَغْفِرَةٌ مِّن رَّبِّهِمْ ۖ كَمَنْ هُوَ خَالِدٌ فِي النَّارِ وَسُقُوا مَاءً حَمِيمًا فَقَطَّعَ أَمْعَاءَهُمْ﴿١٥﴾

15. Mfano wa Jannah ambayo wameahidiwa wenye taqwa; humo mna mito ya maji yasiyovunda, na mito ya maziwa isiyotaghayari ladha yake, na mito ya mvinyo yenye burudisho kwa wanywaji, na mito ya asali iliyosafishwa.[6] Tena watapata humo kila aina ya matunda, na pia maghfirah kutoka kwa Rabb wao. (Je hao) ni kama yule mwenye kudumu motoni? Na watanyweshwa maji yachemkayo yakatekate machango yao?

 

 

 

 

 

وَمِنْهُم مَّن يَسْتَمِعُ إِلَيْكَ حَتَّىٰ إِذَا خَرَجُوا مِنْ عِندِكَ قَالُوا لِلَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ مَاذَا قَالَ آنِفًا ۚ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ طَبَعَ اللَّـهُ عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ وَاتَّبَعُوا أَهْوَاءَهُمْ﴿١٦﴾

16. Na wapo miongoni mwao ambao wanakusikiliza kwa makini, mpaka wanapotoka kwako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) huwaambia wale waliopewa ilimu: Amesema nini sasa hivi?  Hao ndio ambao Allaah Amepiga chapa juu ya nyoyo zao, na wakafuata hawaa zao.

 

 

 

 

وَالَّذِينَ اهْتَدَوْا زَادَهُمْ هُدًى وَآتَاهُمْ تَقْوَاهُمْ﴿١٧﴾

17. Na wale waliohidika, Anawazidishia Hidaya na Huwajaza taqwa yao.

 

 

 

 

 

فَهَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا السَّاعَةَ أَن تَأْتِيَهُم بَغْتَةً ۖ فَقَدْ جَاءَ أَشْرَاطُهَا ۚ فَأَنَّىٰ لَهُمْ إِذَا جَاءَتْهُمْ ذِكْرَاهُمْ﴿١٨﴾

18. Je, basi wanangojea nini isipokuwa Saa iwafikie ghafla? Na kwa yakini zimekwishakuja ishara zake (Qiyamaah). Basi kutawafaa nini kukumbuka kwao itakapowajia (hiyo Saa)?[7]

 

 

 

 

فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ مُتَقَلَّبَكُمْ وَمَثْوَاكُمْ﴿١٩﴾

19. Basi jua kwamba: hapana muabudiwa wa haki ila Allaah,[8] na omba Maghfirah kwa dhambi zako na kwa ajili ya Waumini wa kiume na Waumini wa kike. Na Allaah Anajua harakati zenu huku na kule na pahala penu pa kupumzikia.

 

 

 

 

وَيَقُولُ الَّذِينَ آمَنُوا لَوْلَا نُزِّلَتْ سُورَةٌ ۖ فَإِذَا أُنزِلَتْ سُورَةٌ مُّحْكَمَةٌ وَذُكِرَ فِيهَا الْقِتَالُ ۙ رَأَيْتَ الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ يَنظُرُونَ إِلَيْكَ نَظَرَ الْمَغْشِيِّ عَلَيْهِ مِنَ الْمَوْتِ ۖ فَأَوْلَىٰ لَهُمْ﴿٢٠﴾

20. Na wanasema wale walioamini: Kwa nini isiteremshwe Suwrah? Inapoteremshwa Suwrah iliyo wazi na ikatajwa humo kupigana vita, utawaona wale ambao katika nyoyo zao mna maradhi[9] wanakutazama mtazamo wa mwenye kughumiwa na mauti.  Basi ni awla kwao (kumtii Allaah).

 

 

 

طَاعَةٌ وَقَوْلٌ مَّعْرُوفٌ ۚ فَإِذَا عَزَمَ الْأَمْرُ فَلَوْ صَدَقُوا اللَّـهَ لَكَانَ خَيْرًا لَّهُمْ﴿٢١﴾

21. Utiifu na kauli njema. Na likiazimiwa jambo (la kupigana), basi kama wangekuwa wakweli kwa Allaah, bila shaka ingalikuwa kheri kwao.

 

 

 

فَهَلْ عَسَيْتُمْ إِن تَوَلَّيْتُمْ أَن تُفْسِدُوا فِي الْأَرْضِ وَتُقَطِّعُوا أَرْحَامَكُمْ﴿٢٢﴾

22. Basi lipi zaidi litarajiwalo kwenu mkigeuka isipokuwa kufanya ufisadi katika ardhi na kuwakata jamaa zenu wa damu?[10]

 

 

 

 

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ لَعَنَهُمُ اللَّـهُ فَأَصَمَّهُمْ وَأَعْمَىٰ أَبْصَارَهُمْ﴿٢٣﴾

23. Hao ndio ambao Allaah Amewalaani, Akawafanya viziwi na Akawapofua macho yao.

 

 

 

أَفَلَا يَتَدَبَّرُونَ الْقُرْآنَ أَمْ عَلَىٰ قُلُوبٍ أَقْفَالُهَا﴿٢٤﴾

24. Je, hawaizingatii Qur-aan! Au nyoyoni (mwao) mna kufuli?

 

 

 

 

إِنَّ الَّذِينَ ارْتَدُّوا عَلَىٰ أَدْبَارِهِم مِّن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُمُ الْهُدَى ۙ الشَّيْطَانُ سَوَّلَ لَهُمْ وَأَمْلَىٰ لَهُمْ﴿٢٥﴾

25. Hakika wale walioritadi kurudi nyuma baada ya kuwa Hidaya imewabainikia, hao shaytwaan amewarubuni na akawarefushia matumaini ya uongo.

 

 

 

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَالُوا لِلَّذِينَ كَرِهُوا مَا نَزَّلَ اللَّـهُ سَنُطِيعُكُمْ فِي بَعْضِ الْأَمْرِ ۖ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ إِسْرَارَهُمْ﴿٢٦﴾

26. Hivyo ni kwa sababu wao wamewaambia wale waliokirihika na yale Aliyoyateremsha Allaah: Tutakutiini katika baadhi ya mambo. Na Allaah Anajua siri zao.

 

 

 

فَكَيْفَ إِذَا تَوَفَّتْهُمُ الْمَلَائِكَةُ يَضْرِبُونَ وُجُوهَهُمْ وَأَدْبَارَهُمْ﴿٢٧﴾

 

27. Basi itakuwa vipi pale Malaika watakapowafisha wakiwapiga nyuso zao na migongo yao?

 

 

 

 

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمُ اتَّبَعُوا مَا أَسْخَطَ اللَّـهَ وَكَرِهُوا رِضْوَانَهُ فَأَحْبَطَ أَعْمَالَهُمْ﴿٢٨﴾

28. Hivyo ni kwa sababu wao wamefuata yaliyomghadhibisha Allaah, na wakachukia yanayomfurahisha, basi Akaziporomosha amali zao.

 

 

 

 

أَمْ حَسِبَ الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ أَن لَّن يُخْرِجَ اللَّـهُ أَضْغَانَهُمْ﴿٢٩﴾

29. Je, wanadhania wale ambao nyoyoni mwao mna maradhi[11] kwamba Allaah Hatafichua kamwe vinyongo vyao vya chuki na niya mbaya?

 

 

وَلَوْ نَشَاءُ لَأَرَيْنَاكَهُمْ فَلَعَرَفْتَهُم بِسِيمَاهُمْ ۚ وَلَتَعْرِفَنَّهُمْ فِي لَحْنِ الْقَوْلِ ۚ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ أَعْمَالَكُمْ﴿٣٠﴾

30. Na lau Tungelitaka, Tungelikuonyesha hao, ukawatambua kwa alama zao dhahiri. Na bila shaka utawatambua kwa kwa jinsi wanavyoyafumbia maneno (yao). Na Allaah Anajua amali zenu.  

 

 

وَلَنَبْلُوَنَّكُمْ حَتَّىٰ نَعْلَمَ الْمُجَاهِدِينَ مِنكُمْ وَالصَّابِرِينَ وَنَبْلُوَ أَخْبَارَكُمْ﴿٣١﴾

31. Na bila shaka Tutakujaribuni mpaka Tuwadhihirishe wenye kufanya Jihaad miongoni mwenu na wenye kuvuta subira, na Tutazibainisha khabari zenu.

 

 

 

 

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا وَصَدُّوا عَن سَبِيلِ اللَّـهِ وَشَاقُّوا الرَّسُولَ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُمُ الْهُدَىٰ لَن يَضُرُّوا اللَّـهَ شَيْئًا وَسَيُحْبِطُ أَعْمَالَهُمْ﴿٣٢﴾

32. Hakika wale waliokufuru na wakazuia Njia ya Allaah, na wakampinga kwa uadui Rasuli baada ya kuwabainikia Hidaya   hawatoweza kumdhuru Allaah kwa chochote, na Ataziporomosha amali zao.

 

 

 

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَلَا تُبْطِلُوا أَعْمَالَكُمْ﴿٣٣﴾

33. Enyi walioamini! Mtiini Allaah na mtiini Rasuli, na wala msitengue amali zenu.

 

 

 

 

 

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا وَصَدُّوا عَن سَبِيلِ اللَّـهِ ثُمَّ مَاتُوا وَهُمْ كُفَّارٌ فَلَن يَغْفِرَ اللَّـهُ لَهُمْ﴿٣٤﴾

34. Hakika wale waliokufuru na wakazuia Njia ya Allaah, kisha wakafa hali ya kuwa ni makafiri, Allaah Hatowaghufuria kamwe.

 

 

 

 

 

فَلَا تَهِنُوا وَتَدْعُوا إِلَى السَّلْمِ وَأَنتُمُ الْأَعْلَوْنَ وَاللَّـهُ مَعَكُمْ وَلَن يَتِرَكُمْ أَعْمَالَكُمْ﴿٣٥﴾

35. Basi msinyong’onyee    mkataka suluhu, kwani nyinyi ndio mko juu. Na Allaah Yu pamoja nanyi, na Hatawapunguzieni (thawabu za) amali zenu.

 

 

 

 

 

إِنَّمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا لَعِبٌ وَلَهْوٌ ۚ وَإِن تُؤْمِنُوا وَتَتَّقُوا يُؤْتِكُمْ أُجُورَكُمْ وَلَا يَسْأَلْكُمْ أَمْوَالَكُمْ﴿٣٦﴾

36. Hakika uhai wa dunia ni mchezo na pumbao. Lakini mkiamini na mkawa na taqwa, (Allaah) Atakupeni ujira wenu na wala Hatokutakeni mtoe mali zenu.

 

 

 

 

إِن يَسْأَلْكُمُوهَا فَيُحْفِكُمْ تَبْخَلُوا وَيُخْرِجْ أَضْغَانَكُمْ﴿٣٧﴾

37. Akikutakeni hayo Akakukazanieni mtafanya ubakhili, na Atatoa vinyongo vyenu vya kukirihika na niyyah mbaya.

 

 

 

 

 

هَا أَنتُمْ هَـٰؤُلَاءِ تُدْعَوْنَ لِتُنفِقُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ فَمِنكُم مَّن يَبْخَلُ ۖ وَمَن يَبْخَلْ فَإِنَّمَا يَبْخَلُ عَن نَّفْسِهِ ۚ وَاللَّـهُ الْغَنِيُّ وَأَنتُمُ الْفُقَرَاءُ ۚ وَإِن تَتَوَلَّوْا يَسْتَبْدِلْ قَوْمًا غَيْرَكُمْ ثُمَّ لَا يَكُونُوا أَمْثَالَكُم﴿٣٨﴾

38. Ha! Nyinyi ndio hawa mnaoitwa ili mtoe katika Njia ya Allaah. Basi yuko miongoni mwenu ambaye anafanya ubakhili, na afanyaye ubakhili, basi hakika hapana ila anafanya ubakhili dhidi ya nafsi yake. Na Allaah Ni Mkwasi, nanyi ni mafakiri. Na mkikengeuka Atabadilisha watu ghairi yenu kisha hawatokuwa mfano wenu.

 

 

 

[1] Waumini Kulipwa Thawabu Na Makafiri Kulipwa Adhabu:

 

Kuanzia Aayah hii namba (1) hadi namba (3), Tafsiyr ya Imaam As-Sa’diy inaeleza kama ifuatavyo:

 

Aayaat hizi zinajumuisha kutajwa malipo (thawabu) ya Waumini na adhabu za walioasi na sababu zake, na daawah (wito) kwa viumbe kupata mafunzo kutokana nayo. Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:

الَّذِينَ كَفَرُوا وَصَدُّوا عَن سَبِيلِ اللَّـهِ

Wale waliokufuru na wakazuia Njia ya Allaah.

 

Hawa ni wakuu wa makafiri na viongozi wa wapotovu ambao wamekusanya mambo mawili kwa pamoja; kumkanusha Allaah na Ishara Zake, na kujizuilia wao na kuzuia wengineo katika Njia ya Allaah ambayo ni kuamini na kufuata waliyolingania Rusuli (wa Allaah). Basi watu hao Allaah Atazipoteza amali zao, yaani, Atazibatilisha na Atawasababishia adhabu kwa sababu ya hayo. Hii ni pamoja na juhudi zao za kupinga haqq (haki) na kuwapinga vipenzi vya Allaah. Basi Allaah Atajaalia hila zao katika shingo zao (yaani ziwarudie wenyewe). Na matendo yao ambayo wametaraji walipwe mema, Allaah Atayabatilisha. Hivyo ni kwa sababu ya kufuata kwao baatwil, nayo inajumuisha kila juhudi ambazo hazifanywi kwa ajili ya Allaah kama kuabudu masanamu na mizimu na juhudi za kuunga mkono upotofu kwa sababu malengo hayo ni baatwil na matendo yoyote yanayofanywa kwa ajili yake, nayo pia ni baatwil. [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

[2] Namna Ya Kupambana Na Maadui Na Nini La Kufanya Kwa Mateka:

 

Basi mkipambana, enyi Waumini, na wale waliokufuru katika viwanja vya vita, piganeni nao kidhati na mzipige shingo zao. Hata mtakapowadhoofisha kwa kuwaua kwa wingi na mkazivunja nguvu zao, wafungeni kisawasawa wale mnaowateka. Kisha basi ima muwasamehe kwa kuwafungua na kuwaacha bila kutoa fidia badala yake, au wajikomboe kwa kutoa fidia, au watiwe utumwani au wauawe. Na endeleeni kufanya hivyo mpaka vita vimalizike. Hiyo ndiyo hukumu iliyotajwa ya kuwatahini Waumini kwa makafiri na ushindi kuzunguka baina yao. Na lau Allaah Angalitaka, wangalipata ushindi Waumini bila ya vita, lakini Allaah Amejaalia mateso yao yawe mikononi mwenu ndipo Akaweka sharia ya Jihaad ili Awajaribu nyinyi kwa wao na Ainusuru kwa sababu yenu Dini Yake. Na wale Waumini waliouawa katika Njia ya Allaah, Hatayapomosha Allaah malipo mema ya matendo yao. [Tafsiyr Al-Muyassar]

 

[3] Jannah Imetambulishwa Kwa Waumini:

 

Yaani: (Allaah) Aliifanya (Jannah) ijulikane kwanza kabisa ili kuwafanya (Waumini) waitamani. Aliwaeleza na kuwaambia amali zitakazowafikisha katika Jannah (Pepo), ambapo mojawapo ya amali hizo ni kupigana katika Njia Yake, na Akawawezesha wafanye Alichowaamuru na Akawatia raghba watekeleze. Kisha wanapoingia Jannah, Atawaonyesha makazi yao na yale yaliyomo humo ya raha za kudumu milele na maisha mema. [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

Na Hadiyth ifuatayo ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) imethibitisha kuwa Waumini watatambua makazi yao ya Jannah (Peponi):

 

عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ ـ رضى الله عنه ـ عَنْ رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ ‏ "‏ إِذَا خَلَصَ الْمُؤْمِنُونَ مِنَ النَّارِ حُبِسُوا بِقَنْطَرَةٍ بَيْنَ الْجَنَّةِ وَالنَّارِ، فَيَتَقَاصُّونَ مَظَالِمَ كَانَتْ بَيْنَهُمْ فِي الدُّنْيَا، حَتَّى إِذَا نُقُّوا وَهُذِّبُوا أُذِنَ لَهُمْ بِدُخُولِ الْجَنَّةِ، فَوَالَّذِي نَفْسُ مُحَمَّدٍ صلى الله عليه وسلم بِيَدِهِ لأَحَدُهُمْ بِمَسْكَنِهِ فِي الْجَنَّةِ أَدَلُّ بِمَنْزِلِهِ كَانَ فِي الدُّنْيَا ‏"‏‏.‏ وَقَالَ يُونُسُ بْنُ مُحَمَّدٍ حَدَّثَنَا شَيْبَانُ عَنْ قَتَادَةَ حَدَّثَنَا أَبُو الْمُتَوَكِّلِ‏.‏

 

Amesimulia Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Waumini watakaposalimika na moto, watazuiliwa darajani baina ya moto na Jannah, mahali ambapo watalipizana kisasi kwa dhulma walizofanyiana baina yao duniani. Watakapotakaswa na madhambi yao, wataingizwa Jannah. Naapa kwa Yule Ambaye nafsi ya Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) imo Mikononi Mwake, kila mmoja atatambua makazi yake Jannah zaidi kuliko anavyotambua makazi yake duniani.” [Al-Bukhaariy – Kitaab Al-Madhwaalim (46)]

 

[4] Kunusuru Dini Ya Allaah:

 

Hii ni sawa na Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):

وَلَيَنصُرَنَّ اللَّـهُ مَن يَنصُرُهُ ۗ

“Na bila shaka Allaah Atamnusuru yeyote yule anayenusuru Dini Yake.” [Al-Hajj (22:40)]

 

Na Tafsiyr ya Imaam As-Sa’diy (رحمه الله):

Hii ni Amri ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa Waumini wamnusuru Allaah kwa kusimamisha Dini Yake, kuwalingania watu Kwake, kufanya Jihaad dhidi ya maadui Wake, na kukusudia kwa yote hayo Wajihi wa Allaah. Watakapofanya hivyo, Allaah Atawanusuru na Atawathibitisha miguu yao, yaani: Ataunga nyoyo zao kwa subira na utulivu na uthabiti, Atawapa uvumilivu wa kimwili na Atawasaidia dhidi ya maadui zao. Hii ni Ahadi kutoka kwa Yule Ambaye Ni Mkarimu na Mkweli katika Ahadi Zake kwamba yeyote anayeunga mkono jambo Lake kwa kauli na matendo, basi Rabb Wake Atamsaidia na kumpa njia ya ushindi kama vile uthabiti na kadhaalika. [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

[5] Makafiri Wanatakiwa Watembee Maeneo Mbalimbali Wakatambue Hatima Za Waliokanusha Kabla Yao:

 

Rejea Al-An’aam (6:11).

 

[6] Katika Jannah (Pepo) Kuna Mito:

 

Hadiyth ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):

 

حَدَّثَنَا يَحْيَى بْنُ صَالِحٍ، حَدَّثَنَا فُلَيْحٌ، عَنْ هِلاَلِ بْنِ عَلِيٍّ، عَنْ عَطَاءِ بْنِ يَسَارٍ، عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ ـ رضى الله عنه ـ قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏"‏ مَنْ آمَنَ بِاللَّهِ وَبِرَسُولِهِ وَأَقَامَ الصَّلاَةَ وَصَامَ رَمَضَانَ، كَانَ حَقًّا عَلَى اللَّهِ أَنْ يُدْخِلَهُ الْجَنَّةَ جَاهَدَ فِي سَبِيلِ اللَّهِ، أَوْ جَلَسَ فِي أَرْضِهِ الَّتِي وُلِدَ فِيهَا ‏"‏‏.‏ فَقَالُوا يَا رَسُولَ اللَّهِ أَفَلاَ نُبَشِّرُ النَّاسَ‏.‏ قَالَ ‏"‏ إِنَّ فِي الْجَنَّةِ مِائَةَ دَرَجَةٍ أَعَدَّهَا اللَّهُ لِلْمُجَاهِدِينَ فِي سَبِيلِ اللَّهِ، مَا بَيْنَ الدَّرَجَتَيْنِ كَمَا بَيْنَ السَّمَاءِ وَالأَرْضِ، فَإِذَا سَأَلْتُمُ اللَّهَ فَاسْأَلُوهُ الْفِرْدَوْسَ، فَإِنَّهُ أَوْسَطُ الْجَنَّةِ وَأَعْلَى الْجَنَّةِ، أُرَاهُ فَوْقَهُ عَرْشُ الرَّحْمَنِ، وَمِنْهُ تَفَجَّرُ أَنْهَارُ الْجَنَّةِ ‏"‏‏.‏ قَالَ مُحَمَّدُ بْنُ فُلَيْحٍ عَنْ أَبِيهِ ‏"‏ وَفَوْقَهُ عَرْشُ الرَّحْمَنِ ‏"‏‏.‏

 

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Yeyote anayemuamini Allaah na Rasuli Wake, akasimamisha Swalaah na akafunga (Swiyaam) Ramadhwaan, imekuwa haki juu ya Allaah kumuingiza Jannah (Peponi), ni sawa ikiwa amepigana katika Njia ya Allaah au ameketi nchini mwake alimozaliwa.” Watu wakasema: Ee Rasuli wa Allaah! Je, tuwape bishara hii watu? Akasema (صلى الله عليه وآله وسلم): “Hakika katika Jannah kuna daraja mia moja ambazo Allaah Amewaandalia Mujaahidina wanaopigana katika Njia ya Allaah, na masafa baina ya daraja mbili ni baina ya mbingu na ardhi. Hivyo, mnapomuomba Allaah, muombeni (Jannah ya) Al-Firdaws, kwani ndiyo iliyo nzuri (katikati) na ya juu zaidi Peponi.” Naona alisema: “Na juu yake (Al-Firdaws) kipo Kiti cha Enzi cha Ar-Rahmaan (Allaah), na kwayo kunachepuza mito ya Jannah.” Na imepokewa toka kwa Muhammad bin Fulayh kutoka kwa babake kwamba, “Na juu yake kuna Kiti cha Enzi cha Ar-Rahmaan.” [Al-Bukhaariy Kitaab Al-Jihaad Was-Sayr (56)]

 

[7] Alama Za Qiyaamah:

 

Rejea Al-An’aam (6:158).

 

[8] Yanayopelekea Kutambua Ujuzi Wa Laa Ilaaha Illa-Allaah:

 

Tafsiyr ya Imaam As-Sa’diy (رحمه الله):

 

Kulijua ipasavyo neno “Laa Ilaaha Illa Allaah” kunahitajia moyo kulikiri na kulijua, kwa maana kwamba Rasuli (pamoja na sisi) anatakiwa alijue neno hilo inavyotakikana, halafu akamilishe ujuzi huo kwa kutenda kwa mujibu wa vipengele vyake.

 

Ilimu hiyo ambayo Allaah (سبحانه وتعالى) Ameiamuru - ambayo ni ilimu ya Tawhiyd (Kumpwekesha Allaah) ni fardhw ‘ayn (faradhi kwa kila mtu binafsi), kwa kila mwanaadam, na haisamehewi kwa yeyote yule, na haijalishi yeye ni nani. Bali kila mtu amewajibika kuijua. Na njia ya kujua kwamba hakuna mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye (Allaah عزّ وجلّ) ni kwa haya yafuatayo:   

 

(i) Ya kwanza bali iliyo kuu kabisa ni kuzingatia Majina Yake (Allaah عزّ وجلّ) na Sifa Zake na Matendo Yake yanayodalilisha Ukamilifu Wake, na U’adhwama Wake, na Ujalali Wake, kwani yanampelekea mtu kufanya jitihada ya kujisabilia Kwake, na kumwamudu Rabb Anayemiliki Majina Mazuri Kabisa Na Sifa, na Ambaye Himdi zote ni Zake, Utukufu, Ujalali na Uzuri. 

 

 

(ii) Kujua kwamba Yeye (Allaah عزّ وجلّ) Ndiye Muumbaji Pekee na Msimamizi. Hivyo basi mtu atambue kuwa Yeye (Allaah عزّ وجلّ) Ndiye Pekee Mwenye Kustahiki kuabudiwa.

 

(iii) Kujua kwamba Yeye (Allaah عزّ وجلّ) Ndiye Pekee Mwenye Neema za dhahiri (zinazoonekana) na za siri (zisizoonekana) za kidini na za kidunia. Kujua hilo kunaulazimisha moyo kushikamana Naye na Kumpenda na kujisabilia Kwake Yeye Pekee, Asiye na mshirika.

 

(iv) Yale tunayoyaona na kuyasikia juu ya malipo kwa mawalii Wake waliosimamisha Tawhiyd Yake (Allaah عزّ وجلّ), kama vile ushindi na neema za haraka za hapa duniani, pamoja na adhabu zake kwa maadui Zake wanaomshirikisha, hayo yote ni chachu ya kujua kwamba Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Pekee Anayestahiki kuelekezewa ibaada zote.

 

(v) Kujua hali halisi ya masanamu na mizimu na wanaolinganishwa sawa na Allaah (سبحانه وتعالى) ambao wanaabudiwa pamoja na Allaah, na kufanywa ni waabudiwa, na kwamba hao ni wenye upungufu kwa kila upande, ni madhaifu wa dhati, hawana uwezo wa kujinufaisha au kujidhuru nafsi zao wala kwa wanaowaabudia,   wala hawana uwezo wa kufisha, wala kuhuisha, wala kufufua, wala hawawezi kuwanusuru wanaowaabudia, wala hawawezi kuwanufaisha hata kwa uzito wa chembe ya atomu kwa kuleta kheri au kukinga shari. Basi kwa kujua hayo, kunawajibisha kujua kwamba hapana Mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na kwamba miungu inayoabudiwa badala Yake (Allaah عزّ وجلّ) ni ya uongo.

 

(vi)  Vitabu vya Allaah vyote vimeafikiana juu ya hilo (Neno la Tawhiyd; laa ilaaha illa-Allaah) na vyote kimoja baada ya kingine vimeelezea hilo.

 

(vii) Viumbe bora kabisa ambao wamekamilika katika khulqa (tabia) njema, akili, busara, fikira sahihi, hikma, na ilimu, yaani Rusuli wa Allaah na Manabii na ‘Ulamaa wenye taqwa, wameshuhudia hayo (kwamba laa ilaaha illa-Allaah).

 

(viii) Ishara za kilimwengu na za kinafsi (namna tulivyoumbwa) Alizozisimamisha Allaah na ambazo zinaonyesha kwamba Yeye Ni Mmoja Asiye na mshirika, ndizo dalili kubwa kuliko zote. Dalili hizi kwa namna Alivyoziumba kwa uzuri wa ajabu, kwa umadhubuti usiyo na kombo, na kwa uumbaji wa ajabu, zote zinamtangaza Allaah kwa jinsi zilivyo kwa namna ya kipekee kabisa isiyo na ruwaza. Ishara hizi ambazo Allaah Amekithirisha kwazo kuwazindusha viumbe, Akiwajulisha kwamba hakuna mwingine wa kuabudiwa isipokuwa Yeye, Akazieleza katika Kitabu Chake na Akazitawanya kote kote, ikiwa mtu atataamuli kwa kina baadhi yake tu, basi ni lazima atapata yakini na ujuzi wa kweli wa maana ya kumpwekesha Allaah (Tawhiyd). Sasa hali itakuwa vipi ikiwa dalili zote zitakusanyika pamoja, zikaoana, zikakubaliana na zikasimama toka pande zote?! Hapa ndipo pale iymaan na ujuzi wa hilo vinapojikita na kutuama ndani ya moyo wa mja na kuwa mithili ya mlima mrefu usiyoweza kutikiswa na shubha au dhana hewa, bali huzidi nguvu na ustawi kila mtu anapokutana na upotoshaji na propaganda chafuzi. Mwisho wa yote, unabakia mlango mkubwa na mpana zaidi wa kumwezesha mtu kuijua Tawhiyd kwa mapana yake na marefu yake. Mlango huu ni kuizingatia Qur-aan Tukufu na kuzitafakari Aayaat zake, na hili halipatikani toka chanzo kingine chochote isipokuwa humo.

[Tafsiyr As-Sa’diy]

 

[9] Nyoyo Zenye Maradhi Ya Kufru, Shirki, Unafiki, Shaka, Matamanio, Ukaidi Wa Kukubali Haqq, Maasi Na Kila Aina Ya Maovu:

 

Rejea Al-Hajj (22:46) kwenye uchambuzi na rejea mbalimbali kuhusu moyo uliopofuka na nyoyo zenye maradhi na moyo uliosalimika.  

 

Ama kuhusu nyoyo zenye maradhi, rejea Suwrah na Aayah zifuatazo: Al-Baqarah (2:10), Al-Maaidah (5:52), Al-Anfaal (8:49), At-Tawbah (9:125), Al-Hajj (22:53), An-Nuwr (24:50), Al-Ahzaab (33:12), (33:32), (33:60), Suwrah hii ya Muhammad (47:29), Al-Muddath-thir (74:31).

 

[10] Kuunga Undugu Wa Uhusiano Wa Damu Na Hatari Za Kutokuunga:

 

Umuhimu wa kuunga udugu wa uhusiano wa damu umesisitizwa katika Qur-aan na Sunnah na Fadhila zake ni nyingi na adhimu mno. Miongoni mwazo ni kumiminikiwa rizki na umri mrefu.

 

عن أنسٍ رضي الله عنه: أن رَسُول الله صلى الله عليه وسلم، قَالَ : (( من أحَبَّ أنْ يُبْسَطَ لَهُ في رِزْقِهِ ، ويُنْسأَ لَهُ في أثَرِهِ ، فَلْيَصِلْ رَحِمَهُ )) مُتَّفَقٌ عَلَيهِ .

Amesimulia Anas (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:  "Anayependa akunjuliwe riziki yake, na arefushiwe maisha yake, basi aunge kizazi chake." [Al-Bukhaariy, Muslim na Abu Daawuud] 

 

Kukata undugu ni tatizo sugu la jamii ya Kiislamu na linachukuliwa kuwa ni jepesi ilhali ni zito mno kutokana na hatari zake kubwa kabisa!  Miongoni mwazo ni kama inavyotajwa katika Aayah tukufu inayofuatia ya namba (23) kuwa Laana ya Allaah inamfikia mwenye kukata undugu.  Pia hatari zake zimetajwa katika Hadiyth kadhaa ikiwa ni pamoja na kutokuingizwa mtu Peponi na kukatwa na Allaah (عزّ وجلّ) kama ilivyothibiti katika Hadiyth zifuatazo:

 

عن أَبي محمد جبيرِ بن مطعم رضي الله عنه: أن رَسُول الله صلى الله عليه وسلم، قَالَ : لاَ يَدْخُلُ الجَنَّةَ قَاطِعٌ  . قَالَ سفيان في روايته : يَعْنِي  قَاطِع رَحِم . مُتَّفَقٌ عَلَيهِ

Amesimulia Abuu Muhammad Jubayr bin Mutw‘im  (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  amesema: “Hatoingia Jannah mwenye kukata (uhusiano wa damu).” [Al-Bukhaariy na Muslim, At-Tirmidhiy]

 

 

عن عائشة ، قَالَتْ : قَالَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم  :  الرَّحِمُ مُعَلَّقَةٌ بِالعَرْشِ تَقُولُ : مَنْ وَصَلَنِي ، وَصَلَهُ اللهُ ، وَمَنْ قَطَعَنِي ، قَطَعَهُ اللهُ .  مُتَّفَقٌ عَلَيهِ

Amesimulia ‘Aaishah (رضي الله عنها): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: "Kizazi kimetundikwa katika 'Arshi, kinasema: Anayeniunga, Allaah Atamuunga, na anayenikata, Allaah Atamkata." [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Bonyeza viungo vifuatavyo kupata faida tele:

040-Riyaadhw Asw-Swaalihiyn: Mlango Wa Kuwafanyia Wema Wazazi na Kuunga Kizazi (Ujamaa)

001-Aayah Na Mafunzo: Fadhila Za Swillatur-Rahm (Kuunga Undugu) Na Matahadharisho Ya Kukata Undugu

027-Aayah Na Mafunzo: Miongoni Mwa Hatari Za Kukata Undugu

038-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Allaah Anamuunga Anayeunga Kizazi Na Anamkata Anayekata Kizazi

Kukata Undugu

 

[11] Nyoyo Zenye Maradhi:

 

Rejea Suwrah hii Muhammad (47:20).  

 

Rejea pia Al-Hajj (22:46) kwenye maelezo kuhusu moyo uliopofuka na faida nyenginezo.

 

Rejea pia Ash-Shu’araa (26:88-89) kwenye ufafanuzi na maelezo kuhusu moyo uliosalimika.

 

Share