049 - Al-Hujuraat

 

الْحُجُرَات

 

049-Al-Hujuraat

 

049-Al-Hujuraat: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُقَدِّمُوا بَيْنَ يَدَيِ اللَّـهِ وَرَسُولِهِ ۖ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ عَلِيمٌ﴿١﴾

1. Enyi walioamini! Msikadimishe (lolote) mbele ya Allaah na Rasuli Wake. Na mcheni Allaah, hakika Allaah Ni Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote.[1]

 

 

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَرْفَعُوا أَصْوَاتَكُمْ فَوْقَ صَوْتِ النَّبِيِّ وَلَا تَجْهَرُوا لَهُ بِالْقَوْلِ كَجَهْرِ بَعْضِكُمْ لِبَعْضٍ أَن تَحْبَطَ أَعْمَالُكُمْ وَأَنتُمْ لَا تَشْعُرُونَ﴿٢﴾

2 Enyi walioamini! Msipandishe sauti zenu juu ya sauti ya Nabiy, na wala msiseme naye kwa sauti ya juu, kama mnavyosemezana wenyewe kwa wenyewe kwa sauti za juu, zisije zikaporomoka amali zenu nanyi hamhisi.[2]

 

 

 

 

إِنَّ الَّذِينَ يَغُضُّونَ أَصْوَاتَهُمْ عِندَ رَسُولِ اللَّـهِ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ امْتَحَنَ اللَّـهُ قُلُوبَهُمْ لِلتَّقْوَىٰ ۚ لَهُم مَّغْفِرَةٌ وَأَجْرٌ عَظِيمٌ﴿٣﴾

3. Hakika wale wanaoteremsha sauti zao mbele ya Rasuli wa Allaah, hao ndio ambao Allaah Amezichuja nyoyo zao kwa ajili ya taqwa. Watapata maghfirah[3] na ujira adhimu.

 

 

 

 

إِنَّ الَّذِينَ يُنَادُونَكَ مِن وَرَاءِ الْحُجُرَاتِ أَكْثَرُهُمْ لَا يَعْقِلُونَ﴿٤﴾

4. Hakika wale wanaokuita (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) nyuma ya vyumba, wengi wao hawatii akilini.[4]

 

 

 

 

وَلَوْ أَنَّهُمْ صَبَرُوا حَتَّىٰ تَخْرُجَ إِلَيْهِمْ لَكَانَ خَيْرًا لَّهُمْ ۚ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴿٥﴾

5. Na lau kwamba wao wangelisubiri mpaka ukawatokea, bila shaka ingelikuwa ni kheri zaidi kwao. Na Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu.

 

 

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن جَاءَكُمْ فَاسِقٌ بِنَبَإٍ فَتَبَيَّنُوا أَن تُصِيبُوا قَوْمًا بِجَهَالَةٍ فَتُصْبِحُوا عَلَىٰ مَا فَعَلْتُمْ نَادِمِينَ﴿٦﴾

6. Enyi walioamini! Anapokujieni fasiki kwa habari yoyote, basi pelelezeni, msije mkawadhuru watu kwa ujahili, mkawa kuwa wenye kujuta juu ya ambayo mmeyafanya.

 

 

 

 

وَاعْلَمُوا أَنَّ فِيكُمْ رَسُولَ اللَّـهِ ۚ لَوْ يُطِيعُكُمْ فِي كَثِيرٍ مِّنَ الْأَمْرِ لَعَنِتُّمْ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ حَبَّبَ إِلَيْكُمُ الْإِيمَانَ وَزَيَّنَهُ فِي قُلُوبِكُمْ وَكَرَّهَ إِلَيْكُمُ الْكُفْرَ وَالْفُسُوقَ وَالْعِصْيَانَ ۚ أُولَـٰئِكَ هُمُ الرَّاشِدُونَ﴿٧﴾

7. Na jueni kwamba pamoja nanyi yuko Rasuli wa Allaah. Lau kama atakutiini katika mambo mengi bila shaka mngelitaabika, lakini Allaah Amekupendezesheeni imaan, na Akaipamba katika nyoyo zenu, na Akakuchukizisheni kufuru, na ufasiki na maasi. Hao ndio walioongoka sawasawa.[5]

 

 

 

 

فَضْلًا مِّنَ اللَّـهِ وَنِعْمَةً ۚ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ﴿٨﴾

8. Ni Fadhila kutoka kwa Allaah na Neema. Na Allaah Ni Mjuzi wa yote, Mwenye Hikmah wa yote.

 

 

 

 

وَإِن طَائِفَتَانِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ اقْتَتَلُوا فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا ۖ فَإِن بَغَتْ إِحْدَاهُمَا عَلَى الْأُخْرَىٰ فَقَاتِلُوا الَّتِي تَبْغِي حَتَّىٰ تَفِيءَ إِلَىٰ أَمْرِ اللَّـهِ ۚ فَإِن فَاءَتْ فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا بِالْعَدْلِ وَأَقْسِطُوا ۖ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ﴿٩﴾

9. Na ikiwa makundi mawili ya Waumini yatapigana, basi suluhisheni[6] baina yao. Lakini mojawapo likikandamiza[7] jengine, basi piganeni na ambalo linakandamiza mpaka lielemee kwenye Amri ya Allaah. Likishaelemea, basi suluhisheni baina yao kwa uadilifu, na tendeni haki. Hakika Allaah Anapenda wenye kutenda haki.[8]

 

 

 

 

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُمْ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ﴿١٠﴾

10. Hakika Waumini ni ndugu, basi suluhisheni baina ya ndugu zenu.[9] Na mcheni Allaah ili mpate kurehemewa.

 

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا يَسْخَرْ قَوْمٌ مِّن قَوْمٍ عَسَىٰ أَن يَكُونُوا خَيْرًا مِّنْهُمْ وَلَا نِسَاءٌ مِّن نِّسَاءٍ عَسَىٰ أَن يَكُنَّ خَيْرًا مِّنْهُنَّ ۖ وَلَا تَلْمِزُوا أَنفُسَكُمْ وَلَا تَنَابَزُوا بِالْأَلْقَابِ ۖ بِئْسَ الِاسْمُ الْفُسُوقُ بَعْدَ الْإِيمَانِ ۚ وَمَن لَّمْ يَتُبْ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ﴿١١﴾

11. Enyi walioamini! Wanaume wasiwafanyie dhihaka na kuwadharau wanaume wengineo asaa wakawa bora kuliko wao, wala wanawake kwa wanawake wengineo, asaa wakawa bora kuliko wao. Na wala msifedheheshane kwa kutukanana, na wala msiitane majina (mabaya) ya utani. Ubaya ulioje kuita jina la ufasiki baada ya imaan![10] Na yeyote asiyetubu, basi hao ndio madhalimu.[11]

 

 

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اجْتَنِبُوا كَثِيرًا مِّنَ الظَّنِّ إِنَّ بَعْضَ الظَّنِّ إِثْمٌ ۖ وَلَا تَجَسَّسُوا وَلَا يَغْتَب بَّعْضُكُم بَعْضًا ۚ أَيُحِبُّ أَحَدُكُمْ أَن يَأْكُلَ لَحْمَ أَخِيهِ مَيْتًا فَكَرِهْتُمُوهُ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ تَوَّابٌ رَّحِيمٌ﴿١٢﴾

12. Enyi walioamini! Jiepusheni sana na dhana, kwani hakika baadhi ya dhana ni dhambi. Na wala msichunguzane, na wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi.[12] Je, anapenda mmoja wenu kwamba ale nyama ya nduguye aliyekufa? Basi mmelichukia hilo! Na mcheni Allaah! Hakika Allaah Ni Mwingi wa Kupokea Tawbah, Mwenye Kurehemu.

 

 

 

 

يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّا خَلَقْنَاكُم مِّن ذَكَرٍ وَأُنثَىٰ وَجَعَلْنَاكُمْ شُعُوبًا وَقَبَائِلَ لِتَعَارَفُوا ۚ إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّـهِ أَتْقَاكُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ﴿١٣﴾

13. Enyi watu! Hakika Sisi Tumekuumbeni kutokana na mwanamme na mwanamke, na Tukakufanyeni mataifa na makabila ili mtambuane. Hakika aliye na hadhi zaidi miongoni mwenu mbele ya Allaah ni mwenye taqwa zaidi kati yenu.[13] Hakika Allaah Ni Mjuzi wa yote, Mwenye Khabari za dhahiri na siri.

 

 

 

قَالَتِ الْأَعْرَابُ آمَنَّا ۖ قُل لَّمْ تُؤْمِنُوا وَلَـٰكِن قُولُوا أَسْلَمْنَا وَلَمَّا يَدْخُلِ الْإِيمَانُ فِي قُلُوبِكُمْ ۖ وَإِن تُطِيعُوا اللَّـهَ وَرَسُولَهُ لَا يَلِتْكُم مِّنْ أَعْمَالِكُمْ شَيْئًا ۚ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴿١٤﴾

14. Mabedui walisema: Tumeamini! Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Hamkuamini, lakini semeni: Tumesilimu. Kwani imaan haijaingia bado nyoyoni mwenu. Na mtakapomtii Allaah na Rasuli Wake, Hatokupunguzieni katika amali zenu kitu chochote. Hakika Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu.

 

 

 

 

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ ثُمَّ لَمْ يَرْتَابُوا وَجَاهَدُوا بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ ۚ أُولَـٰئِكَ هُمُ الصَّادِقُونَ﴿١٥﴾

15. Hakika Waumini ni wale waliomwamini Allaah na Rasuli Wake, kisha wakawa si wenye shaka, na wakafanya Jihaad kwa mali zao na nafsi zao katika Njia ya Allaah. Hao ndio wakweli.[14]

 

 

 

 

قُلْ أَتُعَلِّمُونَ اللَّـهَ بِدِينِكُمْ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۚ وَاللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ﴿١٦﴾

16. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Je, ati ndio mnamjulisha Allaah kuhusu Dini yenu, na hali Allaah Anajua yale yaliyomo mbinguni na yale yaliyomo ardhini? Na Allaah Ni Mjuzi wa kila kitu.  

 

 

 

 

يَمُنُّونَ عَلَيْكَ أَنْ أَسْلَمُوا ۖ قُل لَّا تَمُنُّوا عَلَيَّ إِسْلَامَكُم ۖ بَلِ اللَّـهُ يَمُنُّ عَلَيْكُمْ أَنْ هَدَاكُمْ لِلْإِيمَانِ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ﴿١٧﴾

17. Wanadhani wamekufanyia fadhila kwamba wamesilimu? Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Msidhani mmenifanyia fadhila kusilimu kwenu. Bali Allaah Amekufanyieni fadhila kwamba Amekuongozeni kwenye imaan mkiwa ni wakweli.

 

 

 

 

إِنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ غَيْبَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ وَاللَّـهُ بَصِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ﴿١٨﴾

18. Hakika Allaah Anajua ghaibu ya mbingu na ardhi, na Allaah ni Mwenye Kuona myatendayo.

 

 

 

[1] Sababun-Nuzuwl (Sababu Ya Kuteremshwa) Aayah Au Suwrah:

 

Bonyeza kiungo kifuatacho:  

 

049-Asbaabun-Nuzuwl: Al-Hujuraat Aayah 01: يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُقَدِّمُوا بَيْنَ يَدَيِ اللَّـهِ وَرَسُولِهِ

 

Haramisho La Kutoa Rai Katika Mas-ala Ya Dini Baada Ya Kuthibiti Dalili Katika Qur-aan na Sunnah:

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Anaamrisha Waumini kufuata Amri Zake na Amri za Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) na Anaharamisha mtu kufuata vinginevyo pindi inapothibiti dalili katika Qur-aan na Sunnah. Hivyo basi, rai yoyote ile haipasi kupokelewa. Lakini rai katika Dini zinakubalika pindi inapokuwa haijapatikana dalili iliyo wazi katika mas-ala fulani. Rai hizo hujulikana huwa ni Ijtihaad na pia kama Qiyaas katika upande wa Uswuwl.  Dalili ni Hadiyth ifuatayo pale Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alipomtuma Mu’aadh Bin Jabal (رضي الله عنه) kwenda Yemen akamuuliza maswali ambayo majibu yake yalimridhisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):

 

عَنْ مُعَاذٍ  أَنَّ رَسُولَ اللهِ صلى الله عليه وسلم  حِينَ بَعَثَهُ إِلَى الْيَمَنِ ، فَقَالَ (( كَيْفَ تَصْنَعُ إِنْ عَرَضَ لَكَ قَضَاءٌ؟)) قَالَ : أَقْضِي بِمَا فِي كِتَابِ اللهِ ، قَالَ  (( فَإِنْ لَمْ يَكُنْ فِي كِتَابِ اللهِ؟)) قَالَ : فَسُنَّةُ رَسُولِ الله ، قَالَ : ((فَإِنْ لَمْ يَكُنْ فِي سُنَّةِ رَسُولِ الله؟)) قَالَ : أَجْتَهِدُ رَأْيِي لاَ آلُو ، قَالَ : فَضَرَبَ رَسُولُ اللهِ صلى الله عليه وسلم   صَدْرِي ، ثُمَّ قَالَ : ((الْحَمْدُ ِللهِ الَّذِي وَفَّقَ رَسُولَ رَسُولِ اللهِ لِمَا يُرْضِي رَسُولَ الله)) سنن أبي داود

Amesimulia Mu’aadh (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alipomtuma Yemen alimuuliza: “Utafanyaje yatakapokufikia mas-ala?” Akasema: Nitahukumu kwa Kitabu cha Allaah. Akauliza: “Ikiwa hutopata katika Kitabu cha Allaah?” Akasema: Kwa Sunnah ya Rasuli wa Allaah. Akauliza: ”Ikiwa hukupata katika Sunnah ya Rasuli wa Allaah?” Akasema: Basi nitajitahidi rai yangu na sitovuka mipaka.  Kisha akasema:  Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akanipiga katika kifua changu akasema: “AlhamduliLLaah Ambaye Amemuwafikia mjumbe wa Rasuli wa Allaah katika yale aliyoyaridhia Rasuli wa Allaah.” [Sunan Abi Daawuwd]

 

Tanbihi: ‘Ulamaa wamekhitilafiana kuhusu usahihi wa Hadiyth hii, ila baadhi yao wamesema ni Swahiyh kwa njia zake nyingi zenye kuitilia nguvu.

 

Ama mtu au watu kutoa rai zao, au kupinga jambo la Dini lenye dalili, hii haijuzu na inakuwa ni kama kumkosoa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) katika Sunnah zake. Mfano utasikia baadhi ya watu hawaoni sawa kupangusa juu ya soksi au viatu katika suala la kupangusa juu ya khufu mbili (Al-mas-hu ‘alal khuffayn), wanasema kuwa si mantiki au haingii akilini kupangusa juu ya soksi (khufu), bali ipanguswe katika nyayo kwa sababu ndipo mtu anapokanyagia ardhini. Basi na itosheleze kauli ya ‘Aliy Bin Abiy Twaalib (رضي الله عنه):

  لو كان الدِّيْنُ بالرأي لكان أسفل الخُفِّ أوْلَى بالمَسْح من أعلاه، وقد رأيت رسول الله صلى الله عليه وسلم يمسح على ظاهر خُفَّيْه.  رواه أبو داود والدارقطني

Ingelikuwa Dini inakwenda kwa rai, basi ingelikuwa kupangusa chini ya khuff (soksi za ngozi) ni bora zaidi kuliko juu, na ilhali nimemuona Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) anapangusa juu ya khuff.” [Imepokelewa na Abu Daawuwd na Ad-Daaraqutwniy]

 

[3] Maana Ya Maghfirah:

 

Maana ya maghfirah ni kughufuriwa madhambi au kusitiriwa madhambi, yaani kutokuhesabiwa madhambi au makosa pindi mja akirudi kumuomba Rabb Wake maghfirah. Na hakuna yeyote awezaye kumghufuria mtu madhambi isipokuwa Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) kama Anavyosema:    

 

وَالَّذِينَ إِذَا فَعَلُوا فَاحِشَةً أَوْ ظَلَمُوا أَنفُسَهُمْ ذَكَرُوا اللَّـهَ فَاسْتَغْفَرُوا لِذُنُوبِهِمْ وَمَن يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلَّا اللَّـهُ

Na ambao wanapofanya machafu au wakajidhulumu nafsi zao (kwa maasi), humdhukuru Allaah wakaomba Maghfirah kwa madhambi yao. Na nani anayeghufuria madhambi isipokuwa Allaah. [Aal-‘Imraan (3:135)]

 

[4] Adabu Ya Kumwita Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم):

 

Aayah hizi tukufu ziliteremshwa kuhusu watu katika mabedui ambao Allaah (سبحانه وتعالى) Amewaeleza kuwa ni wenye hisia na tabia kavu na kwamba wao:

 

وَأَجْدَرُ أَلَّا يَعْلَمُوا حُدُودَ مَا أَنزَلَ اللَّـهُ عَلَىٰ رَسُولِهِ

Wameelekea zaidi kwamba wasijue mipaka ya (sharia) Alizoteremsha Allaah juu ya Rasuli Wake. [At-Tawbah (9:97)]

 

Makundi mawili (ya mabedui) walifika kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) wakamkuta katika nyumba yake na vyumba vya wake zake.  Hawakuweza kusubiri na hawakufahamu adabu na heshima ya kumwita na kumngojea hadi atoke bali walimwita: Yaa Muhammad! Yaa Muhammad!  Yaani: Toka utujie! Basi Allaah Akawalaumu kwa kukosa kwao akili, kwani hawakufahamu amri ya Allaah ya kuzingatia adabu za kuamiliana na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) na kumheshimu, kwani kuwa na akhlaaq njema ni ishara tosha juu ya akili ya mtu. [Tafsiyr Imaam As-Sa’diy]

 

[5] Duaa Ya Kuomba Imaan, Kinga Ya Kufru, Ufasiki, Uasi:

 

Katika Aayah hii, kuna duaa ifuatayo ambayo ni mojawapo wa duaa za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):

 

اللَّهُمَّ حَبِّبْ إِلَيْنَا الإِيمَانَ وَزَيِّنْهُ فِي قُلُوبِنَا وَكَرِّهْ إِلَيْنَا الْكُفْرَ وَالْفُسُوقَ وَالْعِصْيَانَ وَاجْعَلْنَا مِنَ الرَّاشِدِينَ.

 

Ee Allaah, Pendezesha kwetu imaan na Ipambe katika nyoyo zetu, na Chukiza kwetu kufru, ufasiki na uasi, na Tujaalie miongoni mwa waongofu.

 

[Ahmad, na Al-Bukhaariy ameitoa katika Al-Adabul-Mufrad (699), na Al-Albaaniy ameipa daraja ya Swahiyh katika Takhriyj Fiqhus-Siyrah (348), Swahiyh Al-Adabil-Mufrad lil-Bukhaariy (538/259), na Majma’u Az-Zawaaid (6/124)]

 

[6]  Fadhila Za Kusuluhisha Waliogombana:

 

Kusuluhisha waliogombana ni katika Amri za Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea An-Nisaa (4:114). Na kuna fadhila kubwa katika kutekeleza amri hii. Bonyeza viungo vifuatavyo upate faida:

 

Fadhila Za Kusuluhisha Waliokhasimiana -1

Fadhila Za Kusuluhisha Waliokhasimiana -2

 

[7] Maana Ya Baghyun Katika  Qur-aan:

 

Rejea Ash-Shuwraa (42:14) kupata maana zake mbalimbali.

 

[9] Waumini Kwa Waumini Ni Ndugu:

 

Kuna dalili nyingi katika Qur-aan na Sunnah zinazoashiria undugu wa Waumini. Na undugu huu, huwa ni mkubwa zaidi kuliko undugu wa uhusiano wa damu pindi anapokuwa ndugu wa uhusiano wa damu ni kafiri, au mwenye kuasi.  Na hii ndio inayoitwa al-walaa wal baraa (kupenda kwa ajili ya Allaah na kutengana kwa ajili ya Allaah).

 

Mifano kadhaa imo katika Siyrah ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم). Yeye mwenyewe alitengana na jamaa zake kama ammi yake Abuu Lahab. Swahaba pia walitengana na jamaa zao, kama mfano wa Sa’ad bin Abiy Waqaasw (رضي الله عنه)  ambaye aliposilimu, alitengana na mama yake ambaye alimtaka arudi ukafirini.

 

Baadhi ya Aayah zinazohimiza undugu wa Kiislamu, rejea At-Tawbah (9:71). Na katika kuombeana duaa, rejea Al-Hashr (59:10).

 

Na zifuatazo ni baadhi ya Hadiyth za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) zinazoamrisha undugu wa Kiislamu:

 

 عن النعمان بن بشير رضي الله عنهما قَالَ: قَالَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم: ((مَثَلُ المُؤْمِنينَ في تَوَادِّهِمْ وتَرَاحُمهمْ وَتَعَاطُفِهمْ، مَثَلُ الجَسَدِ إِذَا اشْتَكَى مِنْهُ عُضْوٌ تَدَاعَى لَهُ سَائِرُ الجَسَدِ بِالسَّهَرِ والحُمَّى)). مُتَّفَقٌ عَلَيهِ.

Amesimulia An-Nu’maan bin Bashiyr (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mfano wa Waumini katika kupendana kwao, kuhurumiana kwao na kusaidiana kwao, ni mfano wa mwili, kiungo kimoja kikiumwa basi mwili mzima hukesha kwa homa.” [Al-Bukhaariy, Muslim na Ahmad]

 

عَنْ أَبِي مُوسَى (رضي الله عنه) قال: قال رَسُولُ الله (صلى الله عليه و آله وسلم): ((الْمُؤْمِنَ لِلْمُؤْمِنِ كَالْبُنْيَانِ يَشُدُّ بَعْضُهُ بَعْضاً)) وَشَبَّكَ أَصَابِعَهُ - متفق عليه

Amesimulia Abuu Muwsa (رضي الله عنه):  Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Muumin kwa Muumin mwenziwe ni kama jengo, baadhi yake hutilia nguvu baadhi nyingine.” Akaviumanisha vidole vyake.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

عَنْ أَنَسٍ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ (صلى الله عليه و آله وسلم) قَالَ: ((لاَ يُؤْمِنُ أَحَدُكُمْ حَتَّى يُحِبَّ لإِخِيهِ مَا يُحِبُّ لِنَفْسِهِ)) متفق عليه

Amesimulia Anas (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hatoamini mmoja wenu mpaka ampendelee nduguye anayojipendelea nafsi yake.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Rejea pia Al-Fat-h (48:29) kwenye faida nyenginezo.

 

Na baadhi ya Hadiyth zinazoharamisha kutengana, kuchukiana, kuvunjiana heshima na kadhaalika. Na hii inahusiana na maamrisho ya Aayah namba (11) inayofuatia ya Suwrah hii Al-Hujuraat.

 

عن أبي أيوب الأنصاري رضي الله عنه قال : قال النبي صلى الله عليه وسلم: ((لا يَحِلُّ لِمُسْلِمٍ أَنْ يَهْجُرَ أَخَاهُ فَوْقَ ثَلَاثِ لَيَالٍ، يَلْتَقِيَانِ فَيُعْرِضُ هَذَا وَيُعْرِضُ هَذَا، وَخَيْرُهُمَا الَّذِي يَبْدَأُ بِالسَّلام))  

Amesimulia Abuu Ayyuwb Al-Answaariy (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Haimpasi Muislamu amhame ndugu yake kwa zaidi ya siku tatu hata wanapokutana huyu anamgeuzia (uso) huyu na huyu anamgeuzia (uso) huyu. Na aliye mbora wao kati ya hao wawili ni yule anayeanza kutoa salaam.” [Al-Bukhaariy na Muslim] 

 

 عن ابن عمر رضي الله عنهما أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال‏:‏ ‏ ((‏المُسْلِمُ أخُو المُسْلِمِ ، لاَ يَظْلِمُهُ  وَلاَ يُسْلِمُهُ . مَنْ كَانَ في حَاجَة أخِيه ، كَانَ اللهُ في حَاجَتِهِ، وَمَنْ فَرَّجَ عَنْ مُسْلِمٍ كُرْبَةً، فَرَّجَ اللهُ عَنْهُ بِهَا كُرْبَةً مِنْ كرَبِ يَومِ القِيَامَةِ ، وَمَنْ سَتَرَ مُسْلِماً سَتَرَهُ اللهُ يَومَ القِيَامَةِ )).‏ ‏متفق عليه‏ ‏.‏

Amesimulia Ibn ‘Umar (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Muislamu ni ndugu yake Muislamu, hamdhulumu wala hamsalimishi (kwa adui).  Mwenye kumtekelezea haja nduguye Allaah Atamtekelezea haja yake. Na mwenye kumwondolea Muislamu dhiki, Allaah Atamwondolea dhiki miongoni mwa dhiki za Siku ya Qiyaamah. Na mwenye kumsitiri Muislamu yeyote, Allaah Atamsitiri Siku ya Qiyaamah." [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

عَنْ أَنَسُ (رضي الله عنه) أنّ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((لاَ تَبَاغَضُوا، وَلاَ تَحَاسَدُوا، وَلاَ تَدَابَرُوا، وَلاَ تَقَاطَعوا، وَكُونُوا عِبَادَ اللَّهِ إِخْوَانًا، وَلاَ يَحِلُّ لِمُسْلِمٍ أَنْ يَهْجُرَ أَخَاهُ فَوْقَ ثَلاَثَةِ أَيَّامٍ)) متفق عليه

Amesimulia Anas (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Msibughudhiane (msichukiane), wala msihusudiane, wala msipeane mgongo, wala msikatane, bali kuweni ndugu, waja wa Allaah, wala haifai kwa Muislamu kumhama nduguye kwa zaidi ya siku tatu (asiseme naye).” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

[11] Amri Ya Kuheshimiana Na Katazo La Kufedheheshana:

 

Rejea Tanbihi ya Aayah namba (10) iliyotangulia ya Suwrah hii ya Al-Hujuraat.

 

[12] Madhara Ya Ghiybah (Kusengenya):

 

Bonyeza kiungo kifuatacho ambacho ndani yake mna makala zenye faida tele kuhusu maudhui hiyo pamoja na madhara ya An-Namiymah (kufitnisha):

 

Madhara Ya Ghiybah (Kusengenya) Na An-Namiymah (Kufitinisha)

 

[13] Taqwa Iko Moyoni Na Ndio Kipimo Pekee Cha Utukufu Na Hadhi Ya Mtu Kwa Allaah:

 

 

Taqwa ni katika mambo ya ghaibu ambayo hakuna ajuaye uhalisi wake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Kwa sababu, ingawa mtu anaweza kuonekana kuwa ana mandhari ya taqwa, au ya uswalihina, au ya utendaji ibaada na amali za kheri kwa wingi, lakini uhalisi wake umo moyoni mwake, na Allaah (سبحانه وتعالى) Pekee Ndiye Mwenye kujua. Hadiyth zifuatazo zimethibitisha:  

 

Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Taqwa iko hapa!” Akaashiria mara tatu kifuani mwake. [Muslim]

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه)  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ  (صلى الله عليه و آله وسلم): ((إِنَّ اللَّهَ لاَ يَنْظُرُ إِلى أجْسَامِكُمْ  وَلاَ إِلَى صُوَرِكُمْ وَلَكِنْ يَنْظُرُ إِلَى قُلُوبِكُمْ)) رواه مسلم

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah Hatazami viwiliwili vyenu wala sura zenu, lakini Anatazama nyoyo zenu.” [Muslim]

 

Na mtu kuwa na hadhi mbele ya Allaah au utukufu, hakutokani na kabila lake au nasaba yake, bali kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى) katika Aayah hii tukufu kuwa:

 

إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّـهِ أَتْقَاكُمْ ۚ

Aliye na hadhi zaidi miongoni mwenu mbele ya Allaah ni mwenye taqwa.

 

Na ingelikuwa uhusiano wa damu wa mtu mtukufu unaweza kumfanya jamaa yake awe na hadhi au utukufu, basi Abu Twaalib ambaye ni ammi yake Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), angekuwa na hadhi na utukufu mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى), lakini amefariki katika ukafiri. Rejea Al-Qaswasw (28:56). Na adhabu yake ni kama alivyosema Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) katika Hadiyth ifuatayo:

 

عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ، أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ ‏ "‏ أَهْوَنُ أَهْلِ النَّارِ عَذَابًا أَبُو طَالِبٍ وَهُوَ مُنْتَعِلٌ بِنَعْلَيْنِ يَغْلِي مِنْهُمَا دِمَاغُهُ ‏"‏ ‏.‏  مسلم

 

Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atakayepata adhabu ndogo kabisa katika watu wa motoni ni Abuu Twaalib. Ubongo wake utachemka kutokana na viatu viwili atakavyovivaa humo.” [Muslim Kitaab Cha Imaan]

 

Basi tofauti iliyoje ya hali ya Abuu Twaalib ammi wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na Swahaba mtukufu Bilaal (رضي الله عنه) ambaye alikuwa ni mtumwa, lakini alibashiriwa Jannah (Pepo) na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)  kama ilivyothibiti katika Hadiyth ifuatayo?!:

 

عن أَبي هريرة رضي اللهُ عنه : أنَّ رسول الله صلى الله عليه وسلم قَالَ لِبِلاَلٍ : (( يَا بِلاَلُ ، حَدِّثْنِي بِأَرْجَى عَمَلٍ عَمِلْتَهُ فِي الإسْلاَمِ ، فَإنِّي سَمِعْتُ دَفَّ نَعْلَيْكَ بَيْنَ يَدَيَّ في الجَنَّةِ )) قَالَ : مَا عَمِلْتُ عَمَلاً أرْجَى عِنْدي مِنْ أَنِّي لَمْ أتَطَهَّرْ طُهُوراً فِي سَاعَةٍ مِنْ لَيْلٍ أَوْ نَهَارٍ إِلاَّ صَلَّيْتُ بِذَلِكَ الطُّهُورِ مَا كُتِبَ لِي أنْ أُصَلِّي . متفقٌ عَلَيْهِ ، وهذا لفظ البخاري .

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuuliza Bilaal (رضي الله عنه): "Ee Bilaal! Niambie amali uliyoifanya katika Uislamu, kwani mimi nimesikia sauti ya viatu vyako ukiwa mbele yangu Peponi." (Bilaal) akasema: Sijafanya amali yoyote ambayo kwayo natarajia hayo, isipokuwa ninapojitwahirisha katika wakati wowote wa usiku au mchana, huswali kwa twahaara hiyo zile Alizoniandikia Allaah kuziswali. [Al-Bukhaariy na Muslim, na hii ni lafdhi ya Al-Bukhaariy]

 

Na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)  aliwatahadharisha ahli wake kutomtegemea yeye kwamba ataweza kuwafaa kwa lolote Siku ya Qiyaamah kwa sababu ya uhusiano wao wa damu. Hadiyth ifuatayo inahusiana na kuteremshwa kwa Aayah ya Suwrah Ash-Shu’araa (26:214):

 

عن أبي هُريرةَ (رضىِ الله عنه) قال: قام رسوِل الله  (صلى الله عليه وسلم) حين أُنزل عليه ((وَأَنذِرْ عَشِيرَتَكَ الْأَقْرَبِينَ )) فقال: ((يا مَعْشَرَ قُرَيش!)) - أو كلمة نحوها: ((اشتَرُوا أنفُسَكُم، لا أُغْنِي عَنْكُم مِنَ الله شيئاً، ويا عبَّاسُ بن عَبْدِ المُطَّلِبِ لا أُغْنِي عَنْكَ مِنَ الله شيئاً، وَيا صَفِيَّةُ عَمَّةَ رسولِ الله، لا أُغْنِى عَنْكِ مِن الله شيئاً، ويا فَاطِمَةُ بِنْتَ مُحمدٍ سَلِينِي مِنْ مَالِي مَا شِئْتِ، لا أُغْنِي عَنْكِ مِنَ الله شيئاً))

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضىِ الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alisimama ilipoteremshwa: 

وَأَنذِرْ عَشِيرَتَكَ الْأَقْرَبِينَ ﴿٢١٤﴾

Na onya (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) jamaa zako wa karibu. [Ash-Shu’araa (26:214)]

 

Akasema: “Enyi hadhara ya Quraysh!” - au maneno kama hayo – “Okoeni nafsi zenu, kwani sitowafaeni kwa chochote mbele ya Allaah!  Ee ‘Abbaas bin ‘Abdil-Muttwalib! Sitokufaa chochote mbele ya Allaah!  Ee Swafiyyah shangazi yake Rasuli wa Allaah! Sitokufaa chochote mbele ya Allaah! Ee Faatwimah bint Muhammad! Niombe mali utakayo, (lakini) sitokufaa chochote mbele ya Allaah.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

Rejea pia ‘Abasa (80:34-37) kwenye maudhui kama hii na rejea mbalimbali Rejea pia Al-Muuminuwn (23:101), Luqmaan (31:33), Faatwir (35:18), Al-Infitwaar (82:19).

 

[14] Kutangulizwa Mali Kabla Ya Nafsi Katika Aayah Za Jihaad:

 

Aayah zinazotaja kuhusu kufanya Jihaad kwa mali na nafsi zinafikia tisa, na zote zimetanguliza mali kabla ya nafsi isipokuwa Aayah moja katika Suwrah At-Tawbah (9:111).

 

Na katika Sunnah Hadiyth ifuatayo imethibitisha pia:

 

عَنْ أَنَسٍ ‏ رضى الله عنه ‏ أَنَّ اَلنَّبِيَّ ‏ صلى الله عليه وسلم ‏قَالَ: "جَاهِدُوا اَلْمُشْرِكِينَ بِأَمْوَالِكُمْ، وَأَنْفُسِكُمْ، وَأَلْسِنَتِكُمْ" رَوَاهُ أَحْمَدُ، وَالنَّسَائِيُّ، وَصَحَّحَهُ اَلْحَاكِمُ

Amesimulia Anas (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Piganeni na washirikina kwa mali yenu, nafsi zenu na ndimi zenu.” [Abuu Daawuwd, Ahmad na An-Nasaaiy na Al-Haakim ameisahihisha]

 

‘Ulamaa wakaelezea ifuatavyo kuhusu hikma au sababu ya kutangulizwa mali kabla ya nafsi:

 

Ibn Hibaan (رحمه الله):  Mali imetangulizwa kabla ya nafsi, kwa sababu Mujaahid ni muuzaji (anamuuzia Allaah mali yake na nafsi yake). Na nafsi imetajwa baada ya mali ili Allaah Atuzindushe kuwa nafsi ndiyo inayokabiliana na maumivu zaidi na majanga (ya vita), na mtu hayuko tayari kuitoa ila katika hatua ya mwisho (isiyo na budi). Na mnunuzi (Ambaye ni Allaah), nafsi imesogezwa Kwake ili kutuzindusha kwamba Yeye Anaitaka zaidi (kuliko mali), na Yeye Anachokitaka kwanza, ni kile kilicho ghali chenye thamani kubwa. [Al-Bahr Al-Muhiytw (2/242)]

 

Na zifuatazo ni baadhi ya Fataawa za ‘Ulamaa:

 

Shaykh ‘Abdur-Rahmaan Naaswir Al-Barraak:

 

Swali: Jihaad ya mali imetangulizwa kabla ya nafsi katika hali nyingi, lakini nafsi (katika Jihaad) haikutangulizwa isipokuwa sehemu moja tu. Basi  kuna hikma gani ya kutangulizwa mali kabla ya nafsi juu ya (kuwa kuna) utukufu (fadhila) wa Jihaad ya nafsi?

 

Jibu: ‘Ulamaa wamesema kwa sababu mali ndiyo nyenzo ya kwanza wezeshi inayoandaliwa, na kwa hivyo Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:

وَأَعِدُّوا لَهُم مَّا اسْتَطَعْتُم مِّن قُوَّةٍ وَمِن رِّبَاطِ الْخَيْلِ   

Na waandalieni nguvu (za kiakili na kila aina za silaha) na farasi waliofungwa tayari kwa vita. [Al-Anfaal 8:60)]

 

Bila mali Mujaahid hawezi kupigana Jihaad kwa nafsi yake isipokuwa kwa mali. Hivyo mali imepewa kipaumbele kutokana na uhalisia kwamba ni lazima iwepo kwanza kabla ya chochote. Jihaad ni lazima iandaliwe kwa zana na nyenzo zinazotumika katika mapambano, na vyote hivyo vinategemea mali. Jihaad  haiwezi kufanyika bila silaha, na silaha haipatikani bila mali. [Al-Mawqi’ Ar-Rasmiy li-Fadhwilah Ash-Shayh ‘Abir-Rahmaan Naasiwr Al-Baraak – Fataawaa Wa Duruws]

 

Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (رحمه الله):

 

Swali: Tunaona kwamba katika Aayah nyingi za Jihaad, Allaah (عزّ وجلّ) Anatanguliza Jihaad kwa mali kabla ya Jihaad ya nafsi. Kuna hikma gani katika hilo?

 

Jibu: “Ni dhahiri- na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi- kwamba jeshi la Kiislamu linahitaji mali zaidi kuliko watu, na kwa sababu pia Jihaad kwa mali ni nyepesi zaidi kuliko Jihaad ya nafsi.” [Majmuw’ Fataawaa Wa Rasaail Ibn ‘Uthaymiyn (25/312)]

 

Imaam Ibn Baaz (رحمه الله):

 

Swali: Kuhusu Hadiyth ya Anas: “Piganeni na washirikina kwa mali zenu, nafsi zenu na ndimi zenu.” Nini hikma ya utaratibu wa kutangulizwa mali (kabla ya nafsi) katika Jihaad?

 

Jibu: Mali imetangulizwa katika aghalabu ya Aayaat kwa sababu manufaa yake kiujumla ni mengi. Silaha za vita hununuliwa kwa mali, vifaa na zana za kuliandaa jeshi huhitajia mali, familia za wapiganaji hupewa pia (kwa masurufu) na mengineyo. Hivyo basi maslahi yake ni mengi, na ndio maana Allaah Ameitanguliza kabla ya nafsi katika sehemu nyingi isipokuwa katika Aayah ya Suwrah At-Tawbah:

 

إِنَّ اللَّـهَ اشْتَرَىٰ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ أَنفُسَهُمْ وَأَمْوَالَهُم بِأَنَّ لَهُمُ الْجَنَّةَ ۚ ي

Hakika Allaah Amenunua kwa Waumini nafsi zao na mali zao kwamba watapata Jannah. [At-Tawbah (9:111)]

 

Basi kinachokusudiwa ni kwamba Jihaad kwa mali inagusa maeneo mengi zaidi na kwa manufaa makubwa zaidi, kwani inaweza kuhitajika mali lakini wasihitajike watu (wengi). [Al-Mawqi' Ar-Rasmiy li-Samaahat Ash-Shaykh Al-Imaam Ibn Baaz]

 

 

 

Share