052 - Atw-Twuur

 

  الطُّور

 

052-Atw-Twuur

 

 052-Atw-Twuur: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

 

وَالطُّورِ ﴿١﴾

1. Naapa kwa mlima.[1]

 

 

وَكِتَابٍ مَّسْطُورٍ ﴿٢﴾

2. Na Naapa kwa Kitabu kilichoandikwa.[2]

 

 

فِي رَقٍّ مَّنشُورٍ ﴿٣﴾

3. Katika karatasi nyembamba ya ngozi iliyokunjuliwa.

 

 

وَالْبَيْتِ الْمَعْمُورِ ﴿٤﴾

4. Na Naapa kwa Nyumba yenye kuamiriwa mara kwa mara (na Malaika).[3] 

 

 

 

وَالسَّقْفِ الْمَرْفُوعِ ﴿٥﴾

5. Na Naapa kwa dari iliyonyanyuliwa (mbingu).

 

 

 

وَالْبَحْرِ الْمَسْجُورِ ﴿٦﴾

6. Na Naapa kwa bahari iliyojazwa (maji au itakayowashwa moto).  

 

 

 

إِنَّ عَذَابَ رَبِّكَ لَوَاقِعٌ ﴿٧﴾

7. Hakika adhabu ya Rabb wako bila shaka itatokea.

 

 

 

 

مَّا لَهُ مِن دَافِعٍ ﴿٨﴾

8. Hakuna mzuiaji.

 

 

 

يَوْمَ تَمُورُ السَّمَاءُ مَوْرًا ﴿٩﴾

9. Siku zitakapotaharaki mbingu na kutikisika kikweli.

 

 

 

 

وَتَسِيرُ الْجِبَالُ سَيْرًا ﴿١٠﴾

10. Na milima ikatembea mwendo wa kasi.

 

 

 

فَوَيْلٌ يَوْمَئِذٍ لِّلْمُكَذِّبِينَ ﴿١١﴾

11. Basi ole Siku hiyo kwa wakadhibishao.

 

 

 

الَّذِينَ هُمْ فِي خَوْضٍ يَلْعَبُونَ ﴿١٢﴾

12. Ambao wamo katika kushughulika na upuuzi wakicheza.

 

 

 

 

يَوْمَ يُدَعُّونَ إِلَىٰ نَارِ جَهَنَّمَ دَعًّا ﴿١٣﴾

13. Siku watakayovurumishwa katika Moto wa Jahannam kwa msukumo wa nguvu.

 

 

 

هَـٰذِهِ النَّارُ الَّتِي كُنتُم بِهَا تُكَذِّبُونَ ﴿١٤﴾

14. Huu ndio ule moto ambao mlikuwa mkiukadhibisha.

 

 

 

 

أَفَسِحْرٌ هَـٰذَا أَمْ أَنتُمْ لَا تُبْصِرُونَ ﴿١٥﴾

15. Je, ni sihiri hii au nyinyi hamuoni?

 

 

 

 

اصْلَوْهَا فَاصْبِرُوا أَوْ لَا تَصْبِرُوا سَوَاءٌ عَلَيْكُمْ ۖ إِنَّمَا تُجْزَوْنَ مَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿١٦﴾

16. Ingieni muungue humo, mkistahmili au msistahmili ni sawasawa kwenu, hakika hapana ila mnalipwa yale mliyokuwa mkiyatenda.

 

 

 

 

إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَنَعِيمٍ ﴿١٧﴾

17. Hakika wenye taqwa watakuwa katika Jannaat na Neema.[4]

 

 

 

فَاكِهِينَ بِمَا آتَاهُمْ رَبُّهُمْ وَوَقَاهُمْ رَبُّهُمْ عَذَابَ الْجَحِيمِ ﴿١٨﴾

18. Wakifurahia kwa ambayo Amewapa Rabb wao, na Atawalinda na adhabu ya moto uwakao vikali mno.

 

 

 

كُلُوا وَاشْرَبُوا هَنِيئًا بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿١٩﴾

19. Kuleni na kunyweni kwa raha kwa sababu ya mliyokuwa mnatenda.

 

 

 

مُتَّكِئِينَ عَلَىٰ سُرُرٍ مَّصْفُوفَةٍ ۖ وَزَوَّجْنَاهُم بِحُورٍ عِينٍ ﴿٢٠﴾

20. Wakiegemea juu ya makochi ya fakhari yaliyopangwa safusafu, na Tutawaozesha hurulaini: wanawake weupe wazuri wa Jannah wenye macho makubwa ya kupendeza.

 

 

 

 

وَالَّذِينَ آمَنُوا وَاتَّبَعَتْهُمْ ذُرِّيَّتُهُم بِإِيمَانٍ أَلْحَقْنَا بِهِمْ ذُرِّيَّتَهُمْ وَمَا أَلَتْنَاهُم مِّنْ عَمَلِهِم مِّن شَيْءٍ ۚ كُلُّ امْرِئٍ بِمَا كَسَبَ رَهِينٌ ﴿٢١﴾

21. Na wale walioamini na wakafuatwa na dhuriya wao kwa imaan, Tutawakutanisha nao dhuriya wao na Hatutawapunguzia katika ‘amali zao kitu chochote. Kila mtu atafungika kwa yale aliyoyachuma.[5]

 

 

 

وَأَمْدَدْنَاهُم بِفَاكِهَةٍ وَلَحْمٍ مِّمَّا يَشْتَهُونَ ﴿٢٢﴾

22. Na Tutawapa matunda na nyama katika ambavyo wanatamani.

 

 

 

 

يَتَنَازَعُونَ فِيهَا كَأْسًا لَّا لَغْوٌ فِيهَا وَلَا تَأْثِيمٌ ﴿٢٣﴾

23. Watabadilishana humo gilasi za mvinyo usiosababisha maneno ya upuuzi wala ya dhambi.

 

 

 

وَيَطُوفُ عَلَيْهِمْ غِلْمَانٌ لَّهُمْ كَأَنَّهُمْ لُؤْلُؤٌ مَّكْنُونٌ ﴿٢٤﴾

24. Na watawazungukia watumishi vijana kwa ajili yao kama kwamba ni lulu zilizohifadhiwa.

 

 

وَأَقْبَلَ بَعْضُهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ يَتَسَاءَلُونَ ﴿٢٥﴾

25. Na wataelekeana wao kwa wao wakiulizana.[6]

 

 

 

قَالُوا إِنَّا كُنَّا قَبْلُ فِي أَهْلِنَا مُشْفِقِينَ ﴿٢٦﴾

26. Watasema: Hakika sisi tulikuwa kabla tukiishi baina ya ahli zetu huku tukiogopa.

 

 

 

فَمَنَّ اللَّـهُ عَلَيْنَا وَوَقَانَا عَذَابَ السَّمُومِ ﴿٢٧﴾

27. Basi Allaah Akatuneemesha, na Akatuokoa na adhabu ya moto unaobabua.

 

 

 

إِنَّا كُنَّا مِن قَبْلُ نَدْعُوهُ ۖ إِنَّهُ هُوَ الْبَرُّ الرَّحِيمُ ﴿٢٨﴾

28. Hakika sisi tulikuwa kabla Tunamuomba Yeye Pekee. Hakika Yeye Ndiye Mwingi wa Ihsaan na Fadhila, Mwenye Kurehemu.

 

 

 

 

فَذَكِّرْ فَمَا أَنتَ بِنِعْمَتِ رَبِّكَ بِكَاهِنٍ وَلَا مَجْنُونٍ ﴿٢٩﴾

29. Basi kumbusha (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), kwani hakika wewe kwa Neema ya Rabb wako, si kahini wala si majnuni. 

 

 

 

 

 

أَمْ يَقُولُونَ شَاعِرٌ نَّتَرَبَّصُ بِهِ رَيْبَ الْمَنُونِ ﴿٣٠﴾

30. Au wanasema (huyu Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) ni mshairi, tunamtazamia kupatikana na maafa ya dahari.

 

 

 

 

قُلْ تَرَبَّصُوا فَإِنِّي مَعَكُم مِّنَ الْمُتَرَبِّصِينَ ﴿٣١﴾

31. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Ngojeeni kwani hakika na mimi ni pamoja nanyi ni miongoni mwa wenye kungojea.

 

 

 

 

أَمْ تَأْمُرُهُمْ أَحْلَامُهُم بِهَـٰذَا ۚ أَمْ هُمْ قَوْمٌ طَاغُونَ ﴿٣٢﴾

32. Au zinawaamrisha akili zao haya? Au basi tu wao ni watu wenye kupindukia mipaka kuasi?

 

 

 

 

أَمْ يَقُولُونَ تَقَوَّلَهُ ۚ بَل لَّا يُؤْمِنُونَ ﴿٣٣﴾

33. Au wanasema ameibuni (Qur-aan)? Bali hawaamini.[7]

 

 

 

 

فَلْيَأْتُوا بِحَدِيثٍ مِّثْلِهِ إِن كَانُوا صَادِقِينَ ﴿٣٤﴾

34. Basi walete kauli mfano wake wakiwa ni wakweli.[8]

 

 

 

 

أَمْ خُلِقُوا مِنْ غَيْرِ شَيْءٍ أَمْ هُمُ الْخَالِقُونَ ﴿٣٥﴾

35. Au wameumbwa pasipo na kitu chochote au wao ndio waumbaji?

 

 

 

 

أَمْ خَلَقُوا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ ۚ بَل لَّا يُوقِنُونَ ﴿٣٦﴾

36. Au wameumba mbingu na ardhi? Bali hawana yakini.

 

 

 

 

أَمْ عِندَهُمْ خَزَائِنُ رَبِّكَ أَمْ هُمُ الْمُصَيْطِرُونَ ﴿٣٧﴾

37. Au wanazo Hazina za Rabb wako, au wao ndio wenye madaraka?

 

 

 

 

أَمْ لَهُمْ سُلَّمٌ يَسْتَمِعُونَ فِيهِ ۖ فَلْيَأْتِ مُسْتَمِعُهُم بِسُلْطَانٍ مُّبِينٍ ﴿٣٨﴾

38. Au wanazo ngazi wanasikilizia kwa makini humo? Basi msikilizaji wao alete dalili bayana.

 

 

 

 

أَمْ لَهُ الْبَنَاتُ وَلَكُمُ الْبَنُونَ ﴿٣٩﴾

39. Au (Allaah) Ana mabanati, nanyi mna watoto wa kiume?[9]

 

 

 

 

أَمْ تَسْأَلُهُمْ أَجْرًا فَهُم مِّن مَّغْرَمٍ مُّثْقَلُونَ ﴿٤٠﴾

40. Au unawaomba ujira kwa hiyo wameelemewa na uzito wa gharama?

 

 

 

 

أَمْ عِندَهُمُ الْغَيْبُ فَهُمْ يَكْتُبُونَ ﴿٤١﴾

41. Au wanayo ilimu ya ghaibu kisha wao wanaandika?

 

 

 

 

أَمْ يُرِيدُونَ كَيْدًا ۖ فَالَّذِينَ كَفَرُوا هُمُ الْمَكِيدُونَ ﴿٤٢﴾

42. Au wanakusudia hila? Basi wale waliokufuru wao ndio watakaorudiwa na hila zao.

 

 

 

 

أَمْ لَهُمْ إِلَـٰهٌ غَيْرُ اللَّـهِ ۚ سُبْحَانَ اللَّـهِ عَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿٤٣﴾

43. Au wana ilaah asiyekuwa Allaah? Subhaana-Allaah! (Utakasifu ni wa Allaah) kutokana na ambayo wanafanya shirki.

 

 

 

 

وَإِن يَرَوْا كِسْفًا مِّنَ السَّمَاءِ سَاقِطًا يَقُولُوا سَحَابٌ مَّرْكُومٌ ﴿٤٤﴾

44. Na hata wangeliona pande kutoka mbinguni linaanguka wangelisema:  Mawingu yamerundikana.

 

 

 

 

فَذَرْهُمْ حَتَّىٰ يُلَاقُوا يَوْمَهُمُ الَّذِي فِيهِ يُصْعَقُونَ ﴿٤٥﴾

45. Basi waachilie mbali mpaka wakutane na Siku yao ambayo humo watapigwa na mngurumo na mwako wa umeme waangamizwe.

 

 

 

 

يَوْمَ لَا يُغْنِي عَنْهُمْ كَيْدُهُمْ شَيْئًا وَلَا هُمْ يُنصَرُونَ ﴿٤٦﴾

46. Siku ambayo hila zao hazitowafaa kitu chochote, na wala wao hawatonusuriwa.

 

 

 

 

وَإِنَّ لِلَّذِينَ ظَلَمُوا عَذَابًا دُونَ ذَٰلِكَ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٤٧﴾

47. Na hakika wale waliodhulumu watapata adhabu nyingine isiyokuwa hiyo, lakini wengi wao hawajui.

 

 

 

 

وَاصْبِرْ لِحُكْمِ رَبِّكَ فَإِنَّكَ بِأَعْيُنِنَا ۖ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ حِينَ تَقُومُ ﴿٤٨﴾

48. Na vuta subira (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kwa hukumu ya Rabb wako, kwani hakika wewe uko chini ya Macho Yetu. Na Sabbih pamoja na kumhimidi Rabb wako, wakati unapoinuka (usiku).[10]

 

 

 

 

وَمِنَ اللَّيْلِ فَسَبِّحْهُ وَإِدْبَارَ النُّجُومِ ﴿٤٩﴾

49. Na katika usiku Msabbih na zinapokuchwa nyota.

 

            

 

 

[1] Mlima Ambao Mahali Hapo Allaah (سبحانه وتعالى) Aliongea Na Nabiy Muwsaa (عليه السّلام):

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Anaapa kwa vitu vikubwa vyenye hikma kubwa za ufufuo, malipo ya waja wema na waliokadhibisha. Anaapa kwa Mlima ambao hapo Aliongea na Nabiy Muwsaa Ibn ‘Imraan (عليه السّلام) , Akampa Wahy ya yale Aliyomfunulia katika hukmu mbalimbali. Na katika hayo, kuna fadhila kwake na kwa ummah wake ambazo ni miongoni mwa Aayaat Adhimu na Neema Zake ambazo waja hawawezi kuzihesabu au kuzitathmini ipasavyo kwa kuwa ni zaidi ya kipimo wanachokisia. [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

[2] Kitabu Kilichoandikwa

 

Ni Al-Lawh Al-Mahfuwdhw (Ubao Uliohifadhiwa) au Qur-aan. Rejea Al-An’aam (6:38), Ar-Ra’d (13:39), Al-Buruwj (85:22).

 

[3] Bayt Al-Ma’muwr:

 

Ni nyumba iliyoko juu ya mbingu ya saba ambayo inajaa Malaika watukufu wakati wote. Kila siku Malaika sabiini elfu wanaingia humo kumwabudu Rabb wao kisha hawarudi tena mpaka Siku ya Qiyaamah.  Na imesemekana kuwa Baytul-Ma’muwr ni Nyumba Tukufu ya Allaah na inajaa wanaoswali na wanaomdhukuru Allaah nyakati zote, pamoja na wanaoifikia kwa Hajj na ‘Umrah. [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

Na Ma’muwr iliyoko mbingu ya saba, ndiyo ambayo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alimkuta Nabiy Ibraahiym  (عليه السّلام) akiwa ameegemezea mgongo wake kwenye ukuta wake, na humo wanaingia Malaika elfu sabiini (kila siku).  (Haya yapo katika Hadiyth ndefu iliyopokelewa na Imaam Muslim katika Kitaab cha Al- Iymaan na wengineo). 

 

[4] Miongoni Mwa Neema Za Jannah:

 

Aayah hii kuanzia namba (17) hadi (24), zinatajwa baadhi ya neema za Jannah. Rejea Faatwir (35:33) kwenye neema nyenginezo zilizotajwa na rejea mbalimbali.

 

[5] Ahli Watakutanishwa Jannah (Peponi) Na Vizazi Vyao Ikiwa Watathibiti Katika Imaan:

 

Hii ni katika utimilifu wa neema za watu wa Jannah kwamba, Allaah (عزّ وجلّ) Atawakutanisha na vizazi vyao ambao wamewafuata katika imaan, yaani Allaah (عزّ وجلّ) Atawafanya vizazi vyao hao, kufikia daraja za wazazi huko Jannah hata kama matendo yao hayatatosha kufikia daraja za wazazi, kuwa kama ni ongezeko la thawabu kwa wazazi. Na hayo hayatapunguza chochote katika amali za wazazi. Kwa vile huenda watu wakadhania kwamba vivyo hivyo itakuwa hali ya watu wa motoni, na kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Atawafanya vizazi vyao au wazazi wao kuungana motoni, Allaah (سبحانه وتعالى) Anatujulisha kwamba hukmu za sehemu mbili hizi (wakaazi wa Jannah na motoni) hazilingani sawa.   Moto ni makazi ya uadilifu, na katika uadilifu wa Allaah ni kwamba Hamuadhibishi mtu isipokuwa kwa madhambi yake mwenyewe. Ndio maana Anasema:

 

 كُلُّ امْرِئٍ بِمَا كَسَبَ رَهِينٌ ﴿٢١﴾

“Kila mtu atafungika kwa yale aliyoyachuma.”

 

Yaani mbebaji hatobeba mzigo (wa dhambi) wa mwengine, na mtu hatabebeshwa dhambi za mwengine. Utofauti huo ni kwa ajili ya kuondosha utata kufahamu swala lilotajwa. [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

[6] Watu Wa Jannah Wataelekeana Kuulizana:

 

Aayah hii namba (25) hadi (28):

 

Wataelezeana kuhusu mambo ya dunia na yaliyojiri ambayo yamewafikisha katika hali hii waliyonayo ya neema (za Jannah) na furaha, na kwamba walikuwa wakikhofu adhabu wakajiepusha na madhambi kutokana na kukhofia adhabu. Basi Allaah Akawaneemesha kwa hidaaya na tawfiyq na Akawakinga na adhabu, nayo ni moto mkali mno. Na kwamba walikuwa wakimsabilia kumuomba Yeye Pekee bila ya kumshirikisha na chochote ili Awakinge na adhabu ya moto na Awajaalie wapate neema hiyo ya Jannah. Hii inajumuisha duaa za ibaada na duaa za kuomba mas-ala mengineyo. (Watasema watu wa Jannah):

 

Basi Rabb wetu Akatuneemesha na Akatuitikia duaa zetu, kwani hakika Yeye ni 

 

هُوَ الْبَرُّ الرَّحِيمُ

“Mwingi wa Ihsaan na Fadhila, Mwenye Kurehemu.”

 

Na katika Wema Wake na Rehma Zake (Allaah), Ametujaalia Radhi Zake na kuturuzuku Jannah, na Ametulinda na Ghadhabu Zake na moto.   [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

 

[7] Makafiri Kumsingizia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Kuwa Ameitunga Qur-aan:

 

Rejea Al-Furqaan (25:4) kwenye uchambuzi wa maudhui hii pamoja na rejea mbalimbali.

 

[8] Changamoto Ya Kuleta Mfano Wa Qur-aan Wala Hakuna Awezaye Kamwe!

 

Rejea Yuwnus (10:38), Al-Israa (17:88), Al-Baqarah (2:23-24). Rejea pia Al-An’aam (6:93) ambako kumetajwa waongo waliodai Unabii.

 

[9] Washirikina Kumsingizia Allaah Kuwa Ana Wana Wa Kike:

 

Rejea Asw-Swaaffaat (37:149) kwenye maelezo na rejea mbalimbali.

 

[10] Kumdhukuru Allaah (عزّ وجلّ)   Usiku Na Fadhila Zake:

 

Aayah hii namba (48) na inayomalizia Suwrah hii ya (49), inatajwa maamrisho ya kumdhukuru Allaah (سبحانه وتعالى) usiku. Na maamrisho kama hayo na mengineyo pamoja na fadhila zake yametajwa katika Aayah kadhaa. Rejea Adh-Dhaariyaat (51:15) kwenye faida na rejea mbalimbali. Na Aayah nyenginezo pia ni kwenye Aal-‘Imraan (3:113), Al-Israa (17:78-79), As-Sajdah (32:15-17), Az-Zumar (39:9),   Qaaf (50:39-40), Al- Muzzammil (73:1-7), (73:20).

 

Na miongoni mwa Hadiyth, ni hii ifuatayo ambayo inaelezea fadhila adhimu ya kumdhukuru Allaah usiku, kumwomba na kutakabaliwa duaa:

 

عَنْ عُبَادَةُ بْنُ الصَّامِتِ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) عَنْ رَسُولِ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ: ((مَنْ تَعَارَّ مِنْ اللَّيْلِ فَقَالَ: لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ وَحْدَهُ لاَ شَرِيكَ لَهُ لَهُ الْمُلْكُ وَلَهُ الْحَمْدُ وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ، وَسُبْحَانَ اللَّهِ وَالْحَمْدُ لِلَّهِ وَلاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ وَاللَّهُ أَكْبَرُ وَلاَ حَوْلَ ولاَ قُوَّةَ إِلاَّ بِاللَّهِ، ثُمَّ قَالَ رَبِّ اغْفِرْ لِي، أَوْ دَعَا اسْتُجِيبَ لَهُ، فَإِنْ عَزَمَ فَتَوَضَّأَ ثُمَّ صَلَّى قُبِلَتْ صَلَاتُهُ))

 

Amesimulia ‘Ubaadah bin Asw-Swaamit (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atakayeamka usiku akasema: 

 

: لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ وَحْدَهُ لاَ شَرِيكَ لَهُ لَهُ الْمُلْكُ وَلَهُ الْحَمْدُ وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ، وَسُبْحَانَ اللَّهِ وَالْحَمْدُ لِلَّهِ وَلاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ وَاللَّهُ أَكْبَرُ وَلاَ حَوْلَ ولاَ قُوَّةَ إِلاَّ بِاللَّهِ،  رَبِّ اغْفِرْ لِي

 

Laa ilaaha illa-Allaah Wahdahu laa shariyka Lahu, Lahul-Mulku wa-Lahul-Hamdu wa-Huwa ‘alaa kulli shay-in Qadiyr, wa Subhaana-Allaah wal-HamduliLLaah walaa ilaaha illa-Allaah wa-Allaahu Akbar walaa hawla walaa quwwata illa biLlaah (Hapana muabudiwa wa haki isipokuwa Allaah Pekee Hana mshirika, Ufalme ni Wake na Himdi ni Zake Naye ni Mweza wa kila kitu. Ametakasika Allaah, na Himdi ni za Allaah, na hapana muabudiwa wa haki isipokuwa Allaah, Allaah ni Mkubwa kabisa, na hapana uwezo wala nguvu ila za Allaah).

 

Kisha akasema: 

رَبِّ اغْفِرْ لِي

Rabbigh-fir-liy (Ee Allaah, nighufurie).

 

Au akaomba, ataitikiwa. Na akiazimia kutawadha na kuswali atatakabaliwa Swalaah yake.” [Al-Bukhaariy na wengineo] 

 

Bonyeza kiungo kifuatacho kwenye faida kadhaa:

 

028-Hiswnul-Muslim: Nyiradi Za Kulala

 

16-Umuhimu Wa Tawhiyd Na Fadhila Zake: Ukilala Ukiamka Utamke Neno La Tawhiyd

 

 

 

Share