053 - An-Najm

 

  النَّجْم

 

053-An-Najm

 

 

 053-An-Najm: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

 

وَالنَّجْمِ إِذَا هَوَىٰ ﴿١﴾

1. Naapa kwa nyota zinapotua.[1]

 

 

مَا ضَلَّ صَاحِبُكُمْ وَمَا غَوَىٰ ﴿٢﴾

2. Hakupotoka sahibu wenu na wala hakukosea.

 

 

وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ ﴿٣﴾

3. Na wala hatamki kwa hawaa.

 

 

إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ ﴿٤﴾

4. Hayo si chochote isipokuwa ni Wahy unaofunuliwa.

 

 

عَلَّمَهُ شَدِيدُ الْقُوَىٰ ﴿٥﴾

5. Amemfunza (Jibriyl) mwenye nguvu shadidi.

 

 

ذُو مِرَّةٍ فَاسْتَوَىٰ ﴿٦﴾

6. Mwenye muonekano jamili, muruwa na nguvu na kisha akalingamana sawasawa.

 

 

وَهُوَ بِالْأُفُقِ الْأَعْلَىٰ ﴿٧﴾

7. Naye yuko juu kabisa katika upeo wa macho.

 

 

ثُمَّ دَنَا فَتَدَلَّىٰ ﴿٨﴾

8. Kisha akakurubia na akashuka.

 

 

فَكَانَ قَابَ قَوْسَيْنِ أَوْ أَدْنَىٰ ﴿٩﴾

9. Kisha akawa kiasi cha umbali wa mipinde miwili au karibu zaidi.

 

 

 

 

فَأَوْحَىٰ إِلَىٰ عَبْدِهِ مَا أَوْحَىٰ ﴿١٠﴾

10. (Allaah) Akamfunulia Wahy Mja Wake yale Aliyomfunulia Wahy.

 

 

 

 

مَا كَذَبَ الْفُؤَادُ مَا رَأَىٰ ﴿١١﴾

11. Moyo haukukadhibisha yale aliyoyaona.

 

 

 

 

أَفَتُمَارُونَهُ عَلَىٰ مَا يَرَىٰ ﴿١٢﴾

12. Je, mnambishia kuhusu yale aliyoyaona?

 

 

 

وَلَقَدْ رَآهُ نَزْلَةً أُخْرَىٰ ﴿١٣﴾

13. Na kwa yakini amemuona (Jibriyl) katika uteremko mwingine.

 

 

 

عِندَ سِدْرَةِ الْمُنتَهَىٰ ﴿١٤﴾

14. Kwenye mkunazi wa mpaka wa mwisho kabisa.[2]  

 

 

عِندَهَا جَنَّةُ الْمَأْوَىٰ ﴿١٥﴾

15. Karibu yake kuna Jannah ya Al-Ma-waa.[3]

 

 

إِذْ يَغْشَى السِّدْرَةَ مَا يَغْشَىٰ ﴿١٦﴾

16. Ulipoufunika mkunazi huo unachokifunika.  

 

 

مَا زَاغَ الْبَصَرُ وَمَا طَغَىٰ ﴿١٧﴾

17. Jicho lake halikukengeuka wala halikupinduka mipaka.

 

 

 

 

لَقَدْ رَأَىٰ مِنْ آيَاتِ رَبِّهِ الْكُبْرَىٰ ﴿١٨﴾

18. Kwa yakini aliona miongoni mwa Aayaat (Ishara, Dalili) za Rabb wake kubwa kabisa.

 

 

 

أَفَرَأَيْتُمُ اللَّاتَ وَالْعُزَّىٰ ﴿١٩﴾

19. Je, mmemwona laata na ‘uzzaa?[4]

 

 

 

وَمَنَاةَ الثَّالِثَةَ الْأُخْرَىٰ ﴿٢٠﴾

20. Na manaata mwengine wa tatu?

 

 

 

 

أَلَكُمُ الذَّكَرُ وَلَهُ الْأُنثَىٰ ﴿٢١﴾

21. Je, nyinyi mna wana wa kiume Naye Ana wana wa kike?[5]

 

 

 

 

تِلْكَ إِذًا قِسْمَةٌ ضِيزَىٰ ﴿٢٢﴾

22. Hiyo basi hapo ni mgawanyo wa dhulma kubwa!

 

 

 

 

 

إِنْ هِيَ إِلَّا أَسْمَاءٌ سَمَّيْتُمُوهَا أَنتُمْ وَآبَاؤُكُم مَّا أَنزَلَ اللَّـهُ بِهَا مِن سُلْطَانٍ ۚ إِن يَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ وَمَا تَهْوَى الْأَنفُسُ ۖ وَلَقَدْ جَاءَهُم مِّن رَّبِّهِمُ الْهُدَىٰ ﴿٢٣﴾

23. Hayo si chochote isipokuwa ni majina mmeyaita nyinyi na baba zenu, wala Allaah Hakuyateremshia dalili yoyote. Hawafuati isipokuwa dhana na yale yanayotamani nafsi (zao), na hali umekwishawajia kutoka kwa Rabb wao Mwongozo.

 

 

أَمْ لِلْإِنسَانِ مَا تَمَنَّىٰ ﴿٢٤﴾

24. Kwani hivi binaadamu anapata yote anayoyatamani?

 

 

 

فَلِلَّـهِ الْآخِرَةُ وَالْأُولَىٰ ﴿٢٥﴾

25. Basi ni ya Allaah Pekee ya Aakhirah na ya mwanzo (ya dunia).

 

 

 

 

وَكَم مِّن مَّلَكٍ فِي السَّمَاوَاتِ لَا تُغْنِي شَفَاعَتُهُمْ شَيْئًا إِلَّا مِن بَعْدِ أَن يَأْذَنَ اللَّـهُ لِمَن يَشَاءُ وَيَرْضَىٰ ﴿٢٦﴾

26. Na Malaika wangapi mbinguni hautowafaa chochote uombezi wao isipokuwa baada ya kuwa Allaah Ametoa idhini kwa Amtakaye na Akaridhia.[6]

 

 

 

إِنَّ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ لَيُسَمُّونَ الْمَلَائِكَةَ تَسْمِيَةَ الْأُنثَىٰ ﴿٢٧﴾

27. Hakika wale wasioamini Aakhirah bila shaka wanawaita Malaika kwa majina ya kike.

 

 

 

 

وَمَا لَهُم بِهِ مِنْ عِلْمٍ ۖ إِن يَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ ۖ وَإِنَّ الظَّنَّ لَا يُغْنِي مِنَ الْحَقِّ شَيْئًا ﴿٢٨﴾

28. Na wala hawana ujuzi wowote ule wa hayo. Hawafuati isipokuwa dhana, na hakika dhana haifai kitu chochote mbele ya haki.

 

 

 

 

فَأَعْرِضْ عَن مَّن تَوَلَّىٰ عَن ذِكْرِنَا وَلَمْ يُرِدْ إِلَّا الْحَيَاةَ الدُّنْيَا ﴿٢٩﴾

29. Basi achana mbali na ambaye ameupa mgongo Ukumbusho Wetu na wala hataki isipokuwa uhai wa dunia.

 

 

 

 

ذَٰلِكَ مَبْلَغُهُم مِّنَ الْعِلْمِ ۚ إِنَّ رَبَّكَ هُوَ أَعْلَمُ بِمَن ضَلَّ عَن سَبِيلِهِ وَهُوَ أَعْلَمُ بِمَنِ اهْتَدَىٰ ﴿٣٠﴾

30. Huo ndio upeo wao wa ilimu. Hakika Rabb wako Anamjua zaidi aliyepotoka Njia Yake na Yeye Anamjua zaidi aliyehidika.

 

 

 

 

وَلِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ لِيَجْزِيَ الَّذِينَ أَسَاءُوا بِمَا عَمِلُوا وَيَجْزِيَ الَّذِينَ أَحْسَنُوا بِالْحُسْنَى ﴿٣١﴾

31. Na ni vya Allaah Pekee vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini ili Awalipe wale waliofanya uovu kwa yale waliyoyatenda, na Awalipe wale waliofanya mema kwa mema zaidi.

 

 

 

 

الَّذِينَ يَجْتَنِبُونَ كَبَائِرَ الْإِثْمِ وَالْفَوَاحِشَ إِلَّا اللَّمَمَ ۚ إِنَّ رَبَّكَ وَاسِعُ الْمَغْفِرَةِ ۚ هُوَ أَعْلَمُ بِكُمْ إِذْ أَنشَأَكُم مِّنَ الْأَرْضِ وَإِذْ أَنتُمْ أَجِنَّةٌ فِي بُطُونِ أُمَّهَاتِكُمْ ۖ فَلَا تُزَكُّوا أَنفُسَكُمْ ۖ هُوَ أَعْلَمُ بِمَنِ اتَّقَىٰ ﴿٣٢﴾

32. Wale wanaojiepusha na madhambi makubwa na machafu isipokuwa makosa madogo-madogo.[7] Hakika Rabb wako ni Mkunjufu wa Kughufuria. Yeye Anakujueni vyema, tangu Alipokuanzisheni kutoka katika ardhi, na pale mlipokuwa mimba changa matumboni mwa mama zenu. Basi msizitakase nafsi zenu. Yeye Anamjua zaidi aliyekuwa na taqwa.

 

 

 

 

أَفَرَأَيْتَ الَّذِي تَوَلَّىٰ ﴿٣٣﴾

33. Je, (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) umemuona yule aliyegeukia mbali?

 

 

 

 

وَأَعْطَىٰ قَلِيلًا وَأَكْدَىٰ ﴿٣٤﴾

34. Na akatoa kidogo, kisha akazuia.

 

 

 

 

أَعِندَهُ عِلْمُ الْغَيْبِ فَهُوَ يَرَىٰ ﴿٣٥﴾

35. Je, anayo ilimu ya ghaibu hivyo basi anaona?

 

 

 

 

 

أَمْ لَمْ يُنَبَّأْ بِمَا فِي صُحُفِ مُوسَىٰ ﴿٣٦﴾

36. Au hakujulishwa yale yaliyomo katika Suhuf za Muwsaa?[8] 

 

 

 

 

وَإِبْرَاهِيمَ الَّذِي وَفَّىٰ ﴿٣٧﴾

37. Na Ibraahiym aliyetimiza (ahadi).

 

 

 

 

أَلَّا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَىٰ ﴿٣٨﴾

38. Na kwamba mbebaji dhambi hatobeba mzigo wa mwenginewe.

 

 

 

 

وَأَن لَّيْسَ لِلْإِنسَانِ إِلَّا مَا سَعَىٰ ﴿٣٩﴾

39. Na kwamba binaadam hatopata (jazaa) isipokuwa yale aliyoyafanyia juhudi.

 

 

 

 

وَأَنَّ سَعْيَهُ سَوْفَ يُرَىٰ ﴿٤٠﴾

40. Na kwamba juhudi yake itakuja kuonekana.  

 

 

 

 

ثُمَّ يُجْزَاهُ الْجَزَاءَ الْأَوْفَىٰ ﴿٤١﴾

41. Kisha atalipwa jazaa kamilifu.

 

 

 

 

وَأَنَّ إِلَىٰ رَبِّكَ الْمُنتَهَىٰ ﴿٤٢﴾

42. Na kwamba kwa Rabb wako ndio kikomo.

 

 

 

 

وَأَنَّهُ هُوَ أَضْحَكَ وَأَبْكَىٰ ﴿٤٣﴾

43. Na kwamba Yeye Ndiye Anayesababisha kicheko na kilio.

 

 

 

 

وَأَنَّهُ هُوَ أَمَاتَ وَأَحْيَا ﴿٤٤﴾

44. Na kwamba Yeye Ndiye Anayefisha na Anayehuisha.

 

 

 

 

وَأَنَّهُ خَلَقَ الزَّوْجَيْنِ الذَّكَرَ وَالْأُنثَىٰ ﴿٤٥﴾

45. Na kwamba Yeye Ameumba jozi mbili; dume na jike.

 

 

 

 

مِن نُّطْفَةٍ إِذَا تُمْنَىٰ ﴿٤٦﴾

46. Kutokana na tone la manii linapomiminwa.  

 

 

 

 

وَأَنَّ عَلَيْهِ النَّشْأَةَ الْأُخْرَىٰ ﴿٤٧﴾

47. Na kwamba ni juu Yake uanzishaji mwengineo (kufufua).

 

 

 

 

وَأَنَّهُ هُوَ أَغْنَىٰ وَأَقْنَىٰ ﴿٤٨﴾

48. Na kwamba Yeye Ndiye Atoshelezaye na Akinaishaye.

 

 

 

 

وَأَنَّهُ هُوَ رَبُّ الشِّعْرَىٰ ﴿٤٩﴾

49. Na kwamba Yeye Ndiye Rabb wa nyota ya Ash-Shi’-raa[9] (inayoabudiwa).

 

 

 

 

وَأَنَّهُ أَهْلَكَ عَادًا الْأُولَىٰ ﴿٥٠﴾

50. Na kwamba Yeye Ndiye Aliyeangamiza kina ‘Aad wa awali.

 

 

 

 

وَثَمُودَ فَمَا أَبْقَىٰ ﴿٥١﴾

51. Na kina Thamuwd kisha Hakubakisha.

 

 

 

 

وَقَوْمَ نُوحٍ مِّن قَبْلُ ۖ إِنَّهُمْ كَانُوا هُمْ أَظْلَمَ وَأَطْغَىٰ ﴿٥٢﴾

52. Na kaumu ya Nuwh hapo kabla. Hakika wao walikuwa madhalimu zaidi na wapindukaji mipaka zaidi ya kuasi.

 

 

 

وَالْمُؤْتَفِكَةَ أَهْوَىٰ ﴿٥٣﴾

53. Na miji iliyopinduliwa.[10] Ameiporomosha mbali mbali.

 

 

 

 

فَغَشَّاهَا مَا غَشَّىٰ ﴿٥٤﴾

54. Vikaifunika vilivyofunika.

 

 

 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكَ تَتَمَارَىٰ ﴿٥٥﴾

55. Basi Neema gani za Rabb wako unazitilia shaka?

 

 

 

 

هَـٰذَا نَذِيرٌ مِّنَ النُّذُرِ الْأُولَىٰ ﴿٥٦﴾

56. Huyu (Rasuli صلى الله عليه وآله وسلم) ni mwonyaji wa yale maonyo ya awali.

 

 

 

 

أَزِفَتِ الْآزِفَةُ ﴿٥٧﴾

57. Kimekaribia kinachokaribia.

 

 

 

 

لَيْسَ لَهَا مِن دُونِ اللَّـهِ كَاشِفَةٌ ﴿٥٨﴾

58. Hakuna chenye uwezo wa kukifichua isipokuwa Allaah.

 

 

 

 

أَفَمِنْ هَـٰذَا الْحَدِيثِ تَعْجَبُونَ ﴿٥٩﴾

59. Je, mnastaajabu kwa Hadiyth hii (ya Qur-aan)?

 

 

 

وَتَضْحَكُونَ وَلَا تَبْكُونَ ﴿٦٠﴾

60. Na mnacheka na wala hamlii?

 

 

 

 

وَأَنتُمْ سَامِدُونَ ﴿٦١﴾

61. Na hali nyinyi mnaghafilika, mnadharau na kushughulika na anasa? 

 

 

 

فَاسْجُدُوا لِلَّـهِ وَاعْبُدُوا ۩﴿٦٢﴾

62. Basi msujudieni Allaah na mwabuduni Yeye.[11]

 

[1] Uthibitisho Wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), Ukweli Wake, Wahy, Na Safari Ya Israa Wal-Mi’raaj:

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Anaanza Aayah namba (1) ya Suwrah hii tukufu kwa kiapo cha nyota zinapotua. Kisha Anaendelea Aayah zinazofuatia hadi namba (18) kuthibitisha ukweli wa kumtuma Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), na kuwapinga waliomkadhibisha pamoja na kukadhibisha Safari yake ya muujiza ya Israa wal- Mi’raaj. Na pia Anathibitisha Wahy Aliomteremshia kupitia Jibriyl (عليه السّلام). Rejea Al-Israa (17:1) kwenye maelezo na faida kuhusu safari hiyo tukufu.  

 

[2] Sidratul-Muntahaa: (Mkunazi Wa Mwisho):

 

Sidr ni mkunazi, na Sidratul-Muntahaa imekusudiwa ni kituo cha mwisho wa Safari ya Al-Israa Wal-Mi’raaj.

 

Zifuatazo ni baadhi ya Hadiyth zinazoelezea kuhusu tukio hili adhimu:

 

Amesema ‘Abdullaah bin Mas’uwd: Wakati Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alipochukuliwa safari yake kwenda mbinguni, alifikishwa mpaka Sidratul-Muntahaa ambapo kila kitu kinachopanda kutoka ardhini hukomea  hapo, na na kile kinachoshuka kutoka juu hukomea hapo pia…” [Muslim 329]

 

Na pia,

 

Rasuli wa Allaah (سبحانه وتعالى) amesema: “Kisha nilichukuliwa hadi Sidratul-Muntahaa mti ambao majani yake ni kama masikio ya tembo na matunda yake makubwa kama mitungi. Na mti huu ulipogubikwa na amri za Allaah, basi ulibadilika kuwa katika hali ambayo hakuna kiumbe ambaye anaweza kumsabihi Allaah kwa uzuri wake.” [Muslim]

 

Katika riwaayah nyingine: “Kisha nilipandishwa mbinguni hadi kufikia Sidratul-Muntahaa. Matunda yake yalikuwa makubwa kama magudulia ya Hajr (sehemu ambayo ni karibu na Madiynah) na majani yake yalikuwa makubwa kama masikio ya tembo. Jibriyl (عليه السّلام) akasema: Huu ni mkunazi wa mbali kabisa. Kulikuwa na mito minne karibu yake, miwili ikiwa haionekani na miwili ikiwa wazi inaonekana. Nikauliza: Hii mito miwili ni mito gani ee Jibriyl? Basi akajibu: Ama kwa mito miwili isiyoonekana, ni mito miwili ya Peponi, na mito miwili inayoonekana, hiyo ni mto Naili (Nile) na mto Furati (Euphrates).”

 

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) pia alisema: “Jibriyl alinipandisha mbinguni hadi tukafika Sidratul-Muntahaa (mkunazi ambao una mpaka wa mwisho) ambao ulikuwa umepamba kwa rangi ambazo haziwezi kuelezeka. Kisha niliruhusiwa kuingia Peponi ambamo nilikuta mahema (madogo madogo) au kuta ambazo zimejengwa kwa lulu na ardhi yake ilikuwa ni ya miski.” [Al-Bukhaariy, Juzuu (1) Namba (345)]

 

Kwa faida nyenginezo bonyeza viungo vifuatavyo:

 

Tukio la Israa Na Mi'iraaj

 

Muujiza Wa Al-Israa Wal-Mi'raaj Na Mafunzo Yake

 

[3] Aina Na Sifa Jannah (Pepo), Na Makazi Ya Aakhirah: 

 

Baadhi ya Jannah zilizotajwa katika Qur-aan:

 

- جنة المأوى  Jannatul-Ma-awaa ambayo ni hii iliyotajwa katika Suwrah hii An-Najm Najm (53:15).

 

 

 

- الفردوس جنّة  Jannatul-Firdaws. Rejea Al-Muuminuwn (23:1-11) kwenye faida zake.

 

- جنّة النّعيم Jannatun-Na’iym (Pepo za neema ambazo jicho jicho lolote halijapata kuona, wala sikio lolote halijapata kusikia na wala haijapata kupita katika moyo au fikra ya  binaadam). Rejea Luqmaan (31:8).

 

- جنّة الخلد Jannatul-Khuld (Pepo za kudumu milele). Rejea Al-Furqaan (25:15).

 

- جنّات عدن Jannaat ‘Adn (Jannah au mabustani a kuishi humo milele bila ya kuhama). Rejea Maryam (19:61). Imesemwa kuwa, ‘Adn ni jina makhsusi la Jannah mojawapo. Na imesemwa ni jina la Jannah zote kwa sababu zote ni za kudumu milele. Na Allaah Mjuzi zaidi

 

Na Jannah nyenginezo zimetajwa kuwa ni makazi ya sifa fulani kama ifuatavyo: 

 

- دار السلام Daarus-Salaam (Nyumba ya amani). Rejea  Al-An’aam (6:127).

 

- مقام الأمين Maqaam Al-Amiyn (Makazi ya kusalimika na mauti, huzuni, uchovu, dhiki na kutokana na kila shari) Rejea Ad-Dukhaan (44:51).

 

- دار المقامة Daar Al-Muqaamah (Nyumba ya makazi ya kudumu, wakaazi wake hawaondoki humo). Rejea Faatwir (35:35).

 

- دار الحيوان Daar Al-Hayawaan (Nyumba ya hai wa kudumu milele). Rejea Al-‘Anakabuwt (29:64).

 

- دار القرار Daar Al-Qaraar  (Nyumba ya kustakiri, makazi yasiyotoweka wala uhamisho wala mabadiliko). Rejea Ghaafir (40:39).

 

Na milango ya Jannah ni minane kutokana na Hadiyth Swahiyh mbalimbali. Mojawapo wa Hadiyth hizo ni ile inayohusu fadhila za wudhuu ambayo pindi mtu akisoma duaa ya wudhuu, basi ataambiwa aingie Peponi kupitia mlango wowote aupendao kati ya milango minane:

 

Bonyeza kiungo kifuatacho chenye duaa hiyo kwa maandishi na kwa sauti, na Hadiyth inayotaja fadhila zake hizo:

 

009-Hiswnul-Muslim: Du’aa Baada Ya Kutawadha

 

[4] Laata, ‘Uzzaa, Manaata: Majina Ya Miungu Waliyokuwa Wakiyaabudu Washirikina:  

 

Imaam As-Sa’diy  (رحمه الله) amesema: Baada ya Allaah (سبحانه وتعالى) Kutaja aliyoletwa nayo Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) ya Hidaya na Dini ya haki, na   amri ya kumwabudu Allaah na Tawhiyd (kumpwekesha), Akataja ubatili wa washirikina kuwaabudu ambao hawana sifa za ukamilifu, wala manufaa wala madhara, bali ni majina yasiyo na maana waliyoyaita washirikina, wao na baba zao wapotovu. Wajinga waliwatengenezea majina ya uwongo wasiyostahiki. Kwa hivyo wakajidanganya nafsi zao na wengine kutokana na upotofu, kwani miungu iliyo katika hali hii haistahiki uzito wa chembe ya kuabudiwa. Na hawa waliowalinganisha (na Allaah) ambao waliwaita kwa majina haya, walidai kuwa sifa zao zina maana, kwa hivyo waliitwa “al-laata: kutokana na al-ilaah, al-‘uzzah: kutokana na ‘aziyz (azizi, adhimu, mwenye nguvu),  na manaata: kutokana na mannaan (fadhila).

 

Ni ukanushaji wa Majina ya Allaah (سبحانه وتعالى) na kumshirikisha. Na majina haya hayana maana yoyote ile, kila mtu ambaye ana ufahamu mdogo wa akili anajua ubatili wa sifa hizo.   [Tafsiyr Imaam As-Sa’diy]

 

[5] Washirikina Wamemsingizia Allaah (سبحانه وتعالى) Kuwa Ana Wana Wanawake.

 

Rejea Asw-Swaaffaat (37:149).

 

[6] Hakuna Atakayemiliki Ash-Shafaa (Uombezi) Ila Aridhie Allaah (سبحانه وتعالى):

 

Rejea Al-Baqarah (2:255), Twaahaa (20:109). Rejea pia Al-Israa (17:79) ambako kumetajwa kuwa Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) ni Nabii Pekee atakayeruhusiwa ash-shafaa’ah atakapokuwa katika Maqaaman Mahmuwdan (Cheo Cha Kuhimidiwa).  Rejea pia Az-Zukhruf (43:86) kwenye faida nyenginezo.

 

[7] Madhambi Makubwa Na Madogo:

 

Bonyeza kiungo kifuatacho:

 

Madhambi Makubwa Na Madogo

 

[8] Suhuf (Maandiko Matukufu) Na Tofauti Baina Yake Na Vitabu Vinginevyo Vya Mbinguni:

 

Rejea Al-A’laa (87:18-19) kwenye maelezo bayana. Na rejea pia  Al-Bayyinah (98:2).

 

[9] Nyota Ya Ash-Shi’-raa:

 

Ni nyota inayong’aa iliyoitwa Mirzam Al-Jawzaa (Sirius) ambayo kundi la Waarabu (katika Ujaahiliyyah) walikuwa wakiiabudu.  [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

[10] Miji Iliyopinduliwa:

 

Ni mji wa kaumu ya Nabiy Luutw (عليه السّلام).

 

[11] Sajdatut-Tilaawaa (Sijda Ya Kisomo:

 

Hii ni Sijdah ya mwanzo wa Risala ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kuwalingania makafiri wa Makkah. Basi aliposoma Suwrah hii akafikia hapo, alisujudu na washirikina wote walijisahau wakasujudu.  Hadiyth ifuatayo inataja:

 

حَدَّثَنَا مُسَدَّدٌ، قَالَ حَدَّثَنَا عَبْدُ الْوَارِثِ، قَالَ حَدَّثَنَا أَيُّوبُ، عَنْ عِكْرِمَةَ، عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ ـ رضى الله عنهما أَنَّ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم سَجَدَ بِالنَّجْمِ وَسَجَدَ مَعَهُ الْمُسْلِمُونَ وَالْمُشْرِكُونَ وَالْجِنُّ وَالإِنْسُ‏.‏ وَرَوَاهُ ابْنُ طَهْمَانَ عَنْ أَيُّوبَ‏.‏

 

Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alisujudu alipoisoma Suwrah An-Najm (53), wakasujudu pamoja naye Waislamu, washirikina, majini na watu wote. [Al-Bukhaariy Kitaab cha Kusujudu Inaposomwa Qur-aan (17)]

 

Duaa ya Sajdatut-Tilaawa ni ifuatayo:

 

سَجَـدَ وَجْهـي للَّـذي خَلَقَـهُ وَصَـوَّرَهُ وَشَقَّ سَمْـعَـهُ وَبَصَـرَهُ بِحَـوْلِـهِ وَقُـوَّتِهِ فَتَبَارَكَ اللَّـهُ أَحْسَنُ الْخَالِقِينَ

Sajada wajhiya liLLadhiy khalaqahu, wa swaw-warahu, wa shaqqa sam-’ahu wa baswarahu bihawlihi wa quwwatihi, fa-Tabaaraka-Allaahu Ahsanul-Khaaliqiyn.

 

Umesujudu uso wangu kumsujudia Ambaye Ameuumba na Akapasuwa masikio yake, na macho yake, kwa uwezo Wake na nguvu Zake, Amebarikika Allaah Mbora wa waumbaji.

 

Hadiyth ya ‘Aaishah (رضي الله عنها) - At-Tirmidhiy (2/474), Ahmad (6/30), na Al-Haakim na ameisahihisha Adh-Dhahabiy (1/220) kwa ziada yake na Aayah ni namba (14) ya Suwratul-Muu-minuwn.   

 

اللّهُـمَّ اكْتُـبْ لي بِهـا عِنْـدَكَ أَجْـراً، وَضَـعْ عَنِّـي بِهـا وِزْراً، وَاجْعَـلها لي عِنْـدَكَ ذُخْـراً، وَتَقَبَّـلها مِنِّـي كَمـا تَقَبَّلْتَـها مِنْ عَبْـدِكَ دَاوُد

Allaahummak-tubliy bihaa ’Indaka ajran, wa dhwa’ ’anniy bihaa wizran, waj-’alhaa liy ’Indaka dhukhran, wa taqabbalhaa minniy kamaa taqabbaltahaa min ’abdika Daawuwd

 

Ee Allaah Niandikie Kwako kwa sijdah hii malipo, na Nifutie kwayo madhambi, na Ijaalie kwangu mbele Yako ni akiba, na Nikubalie kama Ulivyomkubalia mja wako Daawuwd.

 

 Hadiyth ya ‘Abdullaah bin ‘Abbaas (رضي الله عنهما) At-Tirmidhiy (2/473), Al-Haakim, na Adh-Dhahabiy ameisahihisha (1/219).

 

Na katika kiungo kifuatacho kuna sauti inayosoma duaa hiyo:

 

021-Hiswnul-Muslim: Du’aa Za Sijdah Ya Kisomo

 

Bonyeza viungo vifuatavyo kupata faida nyenginezo

 

08-Sajdatut-Tilaawah (Sijda Ya Kisomo)

 

034-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Sijdah Ya Kisomo

 

 

 

Share