064 - At-Taghaabun

 

  التَّغَابُن

 

064-At-Taghaabun

 

 

 

 064-At-Taghaabun: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

 

يُسَبِّحُ لِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۖ لَهُ الْمُلْكُ وَلَهُ الْحَمْدُ ۖ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴿١﴾

1. Vinamsabbih Allaah Pekee vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi[1]. Ufalme ni Wake Pekee na Himidi ni Zake Pekee. Naye juu ya kila kitu Ni Muweza.

 

 

 

 

هُوَ الَّذِي خَلَقَكُمْ فَمِنكُمْ كَافِرٌ وَمِنكُم مُّؤْمِنٌ ۚ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ﴿٢﴾

2. Yeye Ndiye Ambaye Amekuumbeni, basi miongoni mwenu yuko aliye kafiri na miongoni mwenu yuko aliye Muumini. Na Allaah kwa yale myatendayo Ni Mwenye Kuona.

 

 

 

 

خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بِالْحَقِّ وَصَوَّرَكُمْ فَأَحْسَنَ صُوَرَكُمْ ۖ وَإِلَيْهِ الْمَصِيرُ﴿٣﴾

3. Ameumba mbingu na ardhi kwa haki, na Akakutengenezeni sura, kisha Akafanya nzuri zaidi sura zenu,[2] na Kwake ndio mahali pa kuishia.

 

 

 

 

يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَيَعْلَمُ مَا تُسِرُّونَ وَمَا تُعْلِنُونَ ۚ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ﴿٤﴾

4. Anajua yale yaliyomo mbinguni na ardhini, na Anayajua yale mnayofanya siri na mnayoyatangaza. Na Allaah Ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani.[3]

 

 

 

 

أَلَمْ يَأْتِكُمْ نَبَأُ الَّذِينَ كَفَرُوا مِن قَبْلُ فَذَاقُوا وَبَالَ أَمْرِهِمْ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ﴿٥﴾

5. Je, haijakufikieni habari ya wale waliokufuru kabla wakaonja matokeo ya uovu wao? Nao watapata adhabu iumizayo.

 

 

 

 

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُ كَانَت تَّأْتِيهِمْ رُسُلُهُم بِالْبَيِّنَاتِ فَقَالُوا أَبَشَرٌ يَهْدُونَنَا فَكَفَرُوا وَتَوَلَّوا ۚ وَّاسْتَغْنَى اللَّـهُ ۚ وَاللَّـهُ غَنِيٌّ حَمِيدٌ﴿٦﴾

6. Hivyo kwa sababu ilikuwa wakiwafikia Rusuli wao kwa hoja bayana wakisema: Ah! Binaadam ndio watuongoze? Basi wakakufuru na wakakengeuka, na Allaah Akawa Hana haja nao, na Allaah Ni Mkwasi, Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa kwa yote.

 

 

 

 

زَعَمَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَن لَّن يُبْعَثُوا ۚ قُلْ بَلَىٰ وَرَبِّي لَتُبْعَثُنَّ ثُمَّ لَتُنَبَّؤُنَّ بِمَا عَمِلْتُمْ ۚ وَذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ﴿٧﴾

7. Waliokufuru wamedai kwamba hawatofufuliwa kamwe. Sema: Sivyo hivyo! Naapa kwa Rabb wangu, bila shaka mtafufuliwa, kisha mtajulishwa yale mliyoyatenda, na hayo kwa Allaah ni mepesi.[4]

 

 

 

 

 

فَآمِنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَالنُّورِ الَّذِي أَنزَلْنَا ۚ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ﴿٨﴾

8. Basi muaminini Allaah, na Rasuli Wake, na Nuru (Qur-aan) Tuliyoiteremsha. Na Allaah kwa yale myatendayo Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri.

 

 

 

 

يَوْمَ يَجْمَعُكُمْ لِيَوْمِ الْجَمْعِ ۖ ذَٰلِكَ يَوْمُ التَّغَابُنِ ۗ وَمَن يُؤْمِن بِاللَّـهِ وَيَعْمَلْ صَالِحًا يُكَفِّرْ عَنْهُ سَيِّئَاتِهِ وَيُدْخِلْهُ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ﴿٩﴾

9. Siku Atakayokukusanyeni kwa ajili ya Siku ya mkusanyiko.[5] Hiyo ndio Siku ya kupata na kukosa.[6] Basi yeyote anayemuamini Allaah na akatenda mema, (Allaah) Atamfutia maovu yake na Atamuingiza Jannaat zipitazo chini yake mito wadumu humo abadi. Huko ndiko kufuzu adhimu.

 

 

 

 

 

وَالَّذِينَ كَفَرُوا وَكَذَّبُوا بِآيَاتِنَا أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ خَالِدِينَ فِيهَا ۖ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ﴿١٠﴾

10. Na wale waliokufuru na wakakadhibisha Aayaat (na Ishara, Dalili) Zetu, hao ndio watu wa motoni, watadumu humo. Ni ubaya ulioje mahali pa kuishia!

 

 

 

 

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ ۗ وَمَن يُؤْمِن بِاللَّـهِ يَهْدِ قَلْبَهُ ۚ وَاللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ﴿١١﴾

11. Hausibu msiba wowote isipokuwa kwa Idhini ya Allaah. Na yeyote   anayemuamini Allaah, (Allaah) Huuongoza moyo wake.[7] Na Allaah kwa kila kitu Ni Mjuzi.

 

 

 

 

وَأَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ ۚ فَإِن تَوَلَّيْتُمْ فَإِنَّمَا عَلَىٰ رَسُولِنَا الْبَلَاغُ الْمُبِينُ﴿١٢﴾

12. Na mtiini Allaah na mtiini Rasuli,[8] lakini mkikengeuka, basi hakika ni juu ya Rasuli Wetu kubalighisha (ujumbe) bayana.

 

 

 

 

اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۚ وَعَلَى اللَّـهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُؤْمِنُونَ﴿١٣﴾

13. Allaah, hakuna muabudiwa wa haki ila Yeye. Na kwa Allaah watawakali Waumini.

 

 

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ مِنْ أَزْوَاجِكُمْ وَأَوْلَادِكُمْ عَدُوًّا لَّكُمْ فَاحْذَرُوهُمْ ۚ وَإِن تَعْفُوا وَتَصْفَحُوا وَتَغْفِرُوا فَإِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴿١٤﴾

14. Enyi walioamini! Hakika miongoni mwa wake zenu na watoto wenu ni maadui kwenu, basi tahadharini nao. Na mkisamehe na mkapuuza na mkayafutilia mbali, basi hakika Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu.[9]

 

 

 

 

إِنَّمَا أَمْوَالُكُمْ وَأَوْلَادُكُمْ فِتْنَةٌ ۚ وَاللَّـهُ عِندَهُ أَجْرٌ عَظِيمٌ﴿١٥﴾

15. Hakika mali zenu na watoto wenu ni jaribio. Na kwa Allaah kuna ujira adhimu.

 

 

 

 

فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ وَاسْمَعُوا وَأَطِيعُوا وَأَنفِقُوا خَيْرًا لِّأَنفُسِكُمْ ۗ وَمَن يُوقَ شُحَّ نَفْسِهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ﴿١٦﴾

16. Basi mcheni Allaah muwezavyo. Na sikilizeni, na tiini na toeni (kwa ajili ya Allaah), itakuwa ni kheri kwa ajili ya nafsi zenu. Na yeyote anayeepushwa na ubakhili na tamaa ya uchu wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufaulu.

 

 

 

 

إِن تُقْرِضُوا اللَّـهَ قَرْضًا حَسَنًا يُضَاعِفْهُ لَكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ۚ وَاللَّـهُ شَكُورٌ حَلِيمٌ﴿١٧﴾

17. Mkimkopesha Allaah karadha mzuri, Atakuzidishieni maradufu, na Atakughufurieni.[10] Na Allaah Ni Mwenye Kupokea shukurani, Mpole na Mvumilivu.

 

 

 

 

عَالِمُ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ﴿١٨﴾

18. Mjuzi wa ghaibu na dhahiri, Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote.

 

 

[1] Kila Kitu Kinamsabbih Allaah (عزّ وجلّ):

 

Rejea Al-Hashr (57:1) kwenye rejea zinazotaja viumbe na vitu Alivyoviumba Allaah kuwa vinamsabbih Yeye Allaah (عزّ وجلّ).

 

[2] Allaah Amemuumba Binaadam Katika Sura Na Umbo Zuri Kabisa:

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Anataja hayo katika Kauli Zake nyenginezo. Rejea Aal-‘Imraan (3:6), Al-Muuminuwn (23:12-14), Ghaafir (40:64), Al-Infitwaar (82:6-8), At-Tiyn (95:4).

 

[3] Allaah Anajua Ya Siri Na Ya Dhahiri:

 

Rejea Ghaafir (40:19).

 

[4] Makafiri Hawakuamini Kuwa Watafufuliwa:

 

Rejea Al-Israa (17:49) kwenye maelezo bayana na rejea mbalimbali.

 

[5] Watu Wote Watakusanywa Siku Ya Qiyaamah:

 

Hiyo ni sawa na Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):

 

قُلْ إِنَّ الْأَوَّلِينَ وَالْآخِرِينَ ﴿٤٩﴾ لَمَجْمُوعُونَ إِلَىٰ مِيقَاتِ يَوْمٍ مَّعْلُومٍ ﴿٥٠﴾

“Sema: (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Hakika wa awali na wa mwishoni. Bila shaka watajumuishwa katika wakati na mahali pa siku maalumu.” [Al-Waaqi’ah (56:49-500]

 

[6] Majina Ya Siku Ya Qiyaamah:

 

Rejea Suwrah Al-Qiyaamah (75:1) kwenye uchambuzi wa majina ya/sifa za Siku ya Qiyaamah, na rejea zake. 

 

[7] Muumini Kuamini Qadar Ya Allaah Katika Mitihani Na Misiba:

 

Muumini anapopatwa na misiba, basi anapaswa avute subira na aamini Qadar ya Allaah (سبحانه وتعالى). Na kuamini huko na kuvumilia, ni mojawapo wa kuthibitisha imaan yake kama ilivyoelezewa katika Hadiyth ifuatayo:

 

عَنْ صُهَيْبٍ، قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏ ‏.‏ عَجَبًا لإَمْرِ الْمُؤْمِنِ إِنَّ أَمْرَهُ كُلَّهُ خَيْرٌ، وَلَيْسَ ذَاكَ لإَحَدٍ إلاَّ لِلْمُؤْمِنِ. إِنْ أَصَابَتْهُ سَرَّاءُ شَكَرَ فَكَانَ خَيْرًا لَهُ، وَإِنْ أَصَابَتْهُ ضَرَّاءُ صَبَرَ فَكَانَ خَيْرًا لَهُ  مسلم

Amesimulia Swuhayb (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Ajabu ya jambo la Muumin kwamba kila jambo lake ni kheri. Na halipatikani hili isipokuwa kwa Muumin. Anapofikwa na jambo zuri hushukuru nayo ni kheri kwake, na anapofikwa na jambo lenye madhara husubiri nayo ni kheri kwake.” [Muslim]

 

Rejea pia Al-Baqarah (2:155) na Al-Hadiyd (57:22-23) kwenye faida nyenginezo.

 

[8] Amri Ya Kumtii Allaah (عزّ وجلّ) Na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم):

 

Amri ya kumtii Allaah (عزّ وجلّ) na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) na maonyo ya kutowatii yametajwa katika Qur-aan katika Aayah nyingi. Mojawapo ni Aayah ifuatayo:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَلَا تَوَلَّوْا عَنْهُ وَأَنتُمْ تَسْمَعُونَ﴿٢٠﴾

“Enyi walioamini! Mtiini Allaah na Rasuli Wake, na wala msijiepushe nazo (amri za Rasuli) na hali nyinyi mnasikia.” [Al-Anfaal (8:20)]

 

Rejea pia katika Suwrah hii At-Taghaabun (64:16). Kisha rejea Aal-‘Imraan (3:32), (3:132), An-Nisaa (4:13),(4:59), (4:69), (4:80), Al-Maaidah (5:92), Al-Anfaal (8:1), (8:46), An-Nuwr (24:52), (24:54), (24:56), Al-Ahzaab (33:36), (33:71), Muhammad (47:33), Al-Fat-h (48:10), (48:17), Al-Mujaadalah (58:13),

 

Na mojawapo wa Hadiyth ni ifuatayo:

 

حَدَّثَنَا عَبْدَانُ، أَخْبَرَنَا عَبْدُ اللَّهِ، عَنْ يُونُسَ، عَنِ الزُّهْرِيِّ، أَخْبَرَنِي أَبُو سَلَمَةَ بْنُ عَبْدِ الرَّحْمَنِ، أَنَّهُ سَمِعَ أَبَا هُرَيْرَةَ ـ رضى الله عنه ـ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ ‏ "‏ مَنْ أَطَاعَنِي فَقَدْ أَطَاعَ اللَّهَ، وَمَنْ عَصَانِي فَقَدْ عَصَى اللَّهَ، وَمَنْ أَطَاعَ أَمِيرِي فَقَدْ أَطَاعَنِي، وَمَنْ عَصَى أَمِيرِي فَقَدْ عَصَانِي ‏"‏‏.‏

Amesimulia Abuu Salamah Bin ‘Abdirrahmaan (رضي الله عنه): Amemsikia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: Atakayenitii mimi basi hakika amemtii Allaah, na atakayeniasi, basi hakika amemuasi Allaah. Na atakayemtii liwali wangu basi hakika amenitii, na atakayemuasi liwali wangu basi hakika ameniasi mimi.” [Al-Bukhaariy na Muslim] Al-Bukhaariy katika Kitabu cha Ahkaam (93), Kitabu Cha Jihaad (56) (mna Hadiyth mbili).

 

[10] Fadhila Za Kutoa Mali Kwa Ajili Ya Allaah:

 

Rejea Al-Hadiyd (57:11) kwenye maelezo na rejea mbalimbali za maudhui hii.

 

 

Share