Kuna Siku Maalumu Ya Kumuingilia Mke?

 

SWALI:

 

Siku gani ni nzuri sana kumwingilia mkeo?

 
JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Hakuna siku maalumu iliyowekwa kwa mume na mke kufanya tendo la ndoa. Jambo la kueleweka ni kuwa ni lazima kwa wanandoa hao wajitayarishe kisaikolojia, kimwili kwa kujipamba, kuwa wasafi na mengineyo ambayo yatalifanya tendo hilo kufanikishwa na kuwaleta watu hao wawili karibu zaidi na kuongeza mapenzi kati yao. Haifai kabisa kwa mume kumtaka mkewe kwa tendo la ndoa kisha mke akatae. Mtume s.a.w.w. ametufundisha kuwa haifai kwa mke kufunga hata funga ya Sunnah ikiwa mume yupo mjini bila ya kupata idhini kutoka kwake. Na pia akasema ikiwa mume amemtaka mkewe basi na amtimizie hata ikiwa ameweka chungu motoni. Na ndio tendo hilo likawa ni ‘Ibadah na mume na mke hupata thawabu kwayo. Mtume s.a.w.w. amesema: “Na kujamiiana kwenu pia ni sadaka”. Wakasema: “Ewe Mtume wa Allah! mmoja wetu huyajia matamanio yake na akawa atapata thawabu?” Akasema: “Mwaonaje lau aliiweka (tupu yake) katika haramu, angekuwa na dhambi” (Muslim kutoka kwa Abu Dharr [r.a]).

      Na Allah Amesema:

Wakishatahirika basi waendeeni Alivyokuamrisheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu Huwapenda wanaotubu na huwapenda wanaojisafisha. Wake zenu ni kama konde zenu. Basi ziendeeni konde zenu mpendavyo. Lakini jitangulizieni kheri nafsi zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kuwa hakika nyinyi mtakutana naye. Na wape bishara njema Waumini(2: 222 – 223).

Na ijulikane kuwa ni haramu kumuingilia mke kwa nyuma na aya ya hapo juu (2: 223) ni dalili kwa hilo pamoja na Hadithi nyingi za Mtume wa Allah s.a.w.w. Au pia akiwa katika damu ya hedhi au nifasi (baada ya kuzaa) mpaka atwahirike kama Alivyosema Allah:

Na wanakuuliza juu ya hedhi. Waambie, huo ni uchafu. Basi jitengeni na wanawake wakati wa hedhi. Wala msiwaingilie mpaka watahirike(2: 222).

 

Share