Ammaar Bin Yaasir (رضي الله عنه)

'Amaar Bin Yaasir (Radhwiya Allaahu 'anhu)

 

Muhammad Faraj Salem As-Saiy (Rahimahu Allaah)

 

 

 

Ukoo wote wa Yaasir baba yake 'Ammaar (Radhwiya Allaahu 'anhum) ulipata bahati ya kubashiriwa na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuingiia Peponi.

 

Yaasir (Radhwiya Allaahu 'anhu) alisafiri kutoka kwao Yemen kwa ajili ya kumtafuta ndugu yake aliyepotea miaka mingi. Alipofika Makkah akaamua kuishi hapo chini ya Himaya ya Abu Hudhayfah aliyemwozesha mmoja katika vijakazi wake aitwae Summayyah binti Khayat (Radhwiya Allaahu 'anhaa), na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) akawaruzuku mtoto mwema waliyempa jina la 'Ammaar.
Ukoo huu uliingia katika dini ya Kiislaam mapema sana na kwa ajili hiyo waliteswa sana na Makafiri wa Makkah.

Walikuwa wakitolewa nje wote watatu - Yaasir, 'Ammaar na Sumayyah (Radhwiya Allaahu 'anhum) wakati wa jua kali sana, wakipelekwa jangwani na kupewa kila aina ya adhabu, na wakati huo Waislaam walikuwa bado wachache sana na hawakuwa na nguvu za kuweza kujitetea.
Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) alikuwa akipita nyumbani kwao kwa ajili ya kuwaliwaza kutokana na adhabu waliyokuwa wakiipata mikononi mwa Makureshi. Siku moja 'Ammaar (Radhwiya Allaahu 'anhu) akamwambia Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam);

 

يا رسول الله، لقد بلغ منا العذاب كُلَّ مبلغ

"Ee Rasuli wa Allaah adhabu tunayoipata hivi sasa imepindukia mipaka".

Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akamwambia;

 

صبرا آل ياسر فإن موعـدكم الجنة

"Kuweni na subira enyi aila (familia) ya Yaasir, hakika ahadi yenu (jazaa yenu) ni Pepo".

'Amru bin Maymun (Radhwiya Allaahu 'anhu) anasema;
"Washirikina walikuwa wakiuunguza mkono wa Yaasir, na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akipita kila siku na kuushika mkono huo huku akisema;
"Ewe moto kuwa baridi na wa salama juu ya Yaasir, kama ulivyokuwa baridi na salama juu ya Ibrahim".

 

Siku moja Abu Jahal alimuingilia Sumayyah, mama yake 'Ammaar (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) na kuanza kumpiga kwa mateke na magumi huku akimtaka amtukane Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kuwatukuza miungu yao. Sumayyah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) alistahamili adhabu yote hiyo huku akisema;
"Ahadun ahad",

 

Neno lililozidi kumtia uchungu Abu Jahal, akawa anaendelea kumpiga Bi Sumayyah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) mpaka akafariki dunia, na kwa ajili hiyo akawa mtu wa mwanzo kufa kifo cha Shaahid katika Uislaam.

 

 

Baada ya kifo cha baba na mama yake, 'Ammaar alizidishiwa adhabu maradufu. Wakati walimuadhibu kwa kumlaza katika mchanga wa jangwani na kumuwekea jiwe kubwa kifuani, mara nyingine wakimuunguza kwa moto na huku wakimuambia : Hatutakuachilia mpaka umtukane Muhammad na uwataje kwa wema lata na uzzah (Waungu wa kisanamu wa Maquraysh wakati huo). Akafanya kama wanavyotaka kutokana na adhabu kali. Na ‘Ammaar, bila ya kujijua, akawa akiyakariri haya maneno anayoambiwa.

Adhabu ilifikia hadi mpaka ‘Ammaar alikuwa akipoteza fahamu na wakati mmoja walimuadhibu mpaka hakujijua . Alipozinduka na kukumbuka aliyokuwa akiyasema aliingiwa na majuto huku akijua ni kosa kubwa kuyatamka na alipokutana na Rasuli alikuwa akilia kwa majuto na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalhi wa sallam) alikuwa akimfuta machozi na kumwambia usiwe na wasiwasi. Wakija tena na kukutaka utamke wanayokutaka uyatamke wakubalie kisha akamsomea aya ya Qur-aan katika Suuwratul An-Nahl:106

 

مَن كَفَرَ بِاللَّـهِ مِن بَعْدِ إِيمَانِهِ إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ وَلَـٰكِن مَّن شَرَحَ بِالْكُفْرِ صَدْرًا فَعَلَيْهِمْ غَضَبٌ مِّنَ اللَّـهِ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ

 

Atakayemkufuru Allaah baada ya iymaan yake (atapata adhabu) isipokuwa yule aliyekirihishwa (kukanusha Dini ya Kiislamu) na huku moyo wake umetua juu ya iymaan. Lakini aliyekifungulia ukafiri kifua chake, basi hao juu yao ni ghadhabu kutoka kwa Allaah na watapata adhabu kuu.

 

Tokea wakati huo ‘Ammaar hakuhuzunishwa wala kujutia kwani alijua kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa)Amemhakikishia kwamba ataziangalia nyoyo na si matamshi yanayotoka vinywani wakati moyo unayasuta.

 

Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi sallam) aliposikia juu ya kifo hicho aliona uchungu sana, lakini hakuwa na uwezo wa kufanya lolote mbele ya nguvu ya makafiri hao, na kwa ajili hiyo akawataka watu wake wahamie nchi ya Uhabeshi (Ethiopia).

 

Siku ile Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipohamia Madiynah, walipokuwa wakiujenga msikiti wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), watu wote walikuwa wakinyanyua tufali moja moja, isipokuwa 'Ammaar (Radhwiya Allaahu 'anhu), yeye alikuwa akinyanyua matufali mawili mawili, na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam ) alipomuona katika hali ile akawa anakitikisa kichwa chake huku akisema;

"Masikini 'Ammaar utauliwa na kundi lenye makosa".

Muslim na Ahmad

 

 

Baada ya waislamu kuhamia Madiynah na dola la kiislaam kuasisiwa, ‘Ammaar alikuwa ni miongoni mwa maswahaba waliokuwa na hadhi kubwa kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwani alikuwa akipendwa na Rasuli huku Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hukaa na kumsifia juu ya iymaan yake na uongofu wake. Mpaka siku moja palipotokea kutoelewana kati yake na Khaalid ibn Waliyd, Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema :

 

   من عادى عمارا، عاداه الله، ومن أبغض عمارا أبغضه الله"

  

                
"Yeyote mwenye kumfanyia uadui ‘Ammaar basi  Allaah Atamfanyia  uadui na yeyote mwenye kumbughudhi ‘Ammaar basi  Allaah Atambughudhi.

 

 

 

Ilimbidi Khaalid bin Waliyd (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwenda kumuomba radhi ‘Ammaar (Radhwiya Allaahu 'anhu).

Mapenzi haya ya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ‘Ammaar hayakuja kwa bahati bali ni jinsi ya iymaan yake, uongofu wake , mateso aliyoyapata kwa ajili ya dini. Mitihani aliyoipata ya kujaribiwa katika iymaan yake ni mambo yaliyoifanya itikadi yake kuwa thabiti isiyo na shaka wala kutetereka. Uongofu huu alikuwa akiuusia Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kusema :

" اقتدوا بالذين من بعدي أبي بكر وعمر, واهتدوا بهدي عمّار "           
 

“Wafuateni baada yangu kina Abu Bakr na ‘Umar, na igeni uongofu wa ‘Ammaar”

Imani ya ‘Ammaar haikumalizika kwa kufariki kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) bali alikuwa mstari wa mbele katika kupigana  Jihaad na kuzidi kutangaza kalimah yake Allaah (Subhaahu Wa Ta'aalaa) kuwa juu. Alikuwa ni mwanajihadi shujaa, asiyeogopa wala kubadilisha msimamo.

 

Mwandishi wa kitabu cha Siyra za Maswahaba anasema;
"Na hii ni dalili kuwa waliomuuwa 'Ammaar si makafiri wala si washirikina, bali ni upande uliofanya ijtihad lakini ukakosea katika jitihadi yao.

Baada ya kupita siku nyingi tokea umalizike kujengwa msikiti wa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), zikaenea habari kuwa 'Ammaar ameangukiwa na ukuta. Rasuli (Swala Allaahu 'alayji wa sallam) aliposikia habari hizo akasema;
"Hakufa 'Ammaar".

Ammaar (Radhwiya Allaahu 'anhu) alishiriki katika vita vingi sana pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam), alikuwa miongoni mwa watu waliochimba handaki siku ya vita vya Ahzab, na alikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kufungamana na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) chini ya mti wa Ridhwaan.

 

Enzi za Ukhalifa wa ‘Umar Ibn Al-Khattwaab aliteuliwa kuwa Amiyr katika mji wa Kufah na ‘AbduLLaah ibn Mas'uwd kuwa  waziri wake na mwalimu wa kuwafundisha waislaamu dini yao. Wakati watu wakiteuliwa Maamiri huzidi kuwa na nguvu au kuzidiwa na kibri lakini kwa ’Ammaar ilikuwa kinyume chake kwani alikuwa dhalili mpaka watu wakashangazwa na Amiyr walieletewa. Anasema Ibn Abu Huzayl ambae alikuwepo Kufah wakati ‘Ammaar bin yaasir ni Amiyr:

        "رأيت عمّار بن ياسر وهو أمير الكوفة يشتري من قثائها، ثم يربطها بحبل ويحملها فوق ظهره، ويمضي بها الى داره" 

 

                                                                           

“Nilikuwa nikumuona ‘Ammaar bin Yaasir wakati akiwa Amiyr wa Kufah akinunua vitu vyake akivifunga kwa kamba na kisha kuibeba mgongoni mwake akielekea nyumbani kwake”
 

Baada ya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kufariki dunia, 'Ammaar (Radhwiya Allaahu 'anhu) alipigana dhidi ya walortadi katika vita vya Al-Yamaamah chini ya uongozi wa Abu Bakar As- Swidiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu), na watu walipokuwa wakirudi nyuma baada ya vita kuwa vikali, 'Ammaar (Radhwiua Allaahu 'anhu) alisimama juu ya jabali dogo huku akiita kwa sauti kubwa;
"Enyi Waislaam, mnaikimbia Pepo? Mimi hapa 'Ammaar bin Yaasir, njooni kwangu". Alikuwa akisema maneno hayo huku akipigana kwa ujasiri mkubwa kabisa na wakati huo sikio lake lilikuwa limekatika katika vita hivyo.
'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) alipotawala, alimpa 'Ammaar ugavana wa mji wa Al-Kuufah na akawaandikia barua watu wa nchi hiyo akiwaambia;
"Enyi watu! Mimi nimekuleteeni 'Ammaar awe amiri wenu na 'AbduLLaah bin Mas'uud mwalimu wenu na msaidizi wake. Hawa ni katika Maswahaba wa Rasuli walio wema, kwa hivyo watiini na mfuate mwenendo wao".
Katika vita vya Siffiyn, vita vilivyopiganwa baina ya majeshi ya Alliy (Radhwiya Allaahu 'anhu) na Muawiyya (Radhwiya Allaahu 'anhu), Maswahaba wa Rasuli walioshiriki katika vita hivyo walikuwa wakimfuata 'Ammaar kama kwamba yeye ndiye bendera yao.

 

Hakuwa mtu mwenye mambo makubwa kwani hata siku moja alijiwa na mmoja katika wenye hadhi na jina katika mji wa Kufa ili kuomba jambo kwa Amiyr na kutokana na nafasi yake alikuwa na hakika kwamba Amiyr angelimkubalia. Hata hivyo ‘Ammaar alimkatalia na kukasirika mpaka kudiriki kumrushia shutuma na matusi Amiyr kwa kumwambia:

                                                    :" يا أجدع الأذن
 

“Mtizame aliekatika sikio!”

Sikio moja la ‘Ammaar lilikuwa limekatika alipopigana vita vya Al-Yamaamah ambavyo ushujaa wake ulikuwa ni changamoto ya kuweza kuwatia morali waislaamu na hatimaye kushinda. Mpaka ilifikia kusimama wakati tayari ameshakatwa sikio na kusema kwa sauti ya ukali “Mnaikimbia pepo? Niangalieni mimi ni ‘Ammaar bin Yaasir nifuateni nifuateni”

Amiri hakukasirishwa na kauli ile bali alijibu tu kwa kusema:

 

 

خير أذنيّ سببت.. لقد أصيبت في سبيل الله

 

“Umelitukana sikio langu lililo bora kwani lilikatwa (wakati nnapigana) kwa ajili ya Allaah”

Uadilifu wa ‘Ammaar ulikuja dhihirika zaidi wakati ilipokuja fitna kubwa katika Uislaamu na huku tayari akiwa ni mzee wa miaka zaidi ya tisini. Naam mzee wa miaka tisini aliweza kuikamata na kuibeba bendera ya vita ambavyo viliwagawa waislaamu wasijue nani aliye kwenye haki kati ya  ‘Aliy bin Abi Twwalib akiwa kama ni khaliyfah na Mu’awiyah ibn Abi Sufyaan. Siku hiyo alisimama na bendera na kusema :

" والذي نفسي بيده.. لقد قاتلت بهذه الراية مع رسول الله صلى الله عليه وسلم، وهأنذا أقاتل بها اليوم..

والذي نفسي بيده. لو هزمونا، لعلمت أننا على الحق، وأنهم على الباطل".                              .
 

“Kwa Yule ambae nafsi yangu iko kwenye mikono Mwake, nilipigana kwa ajili ya bendera hii pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na hivi leo nnapigana tena kwa ajili ya bendera hii.

 

Hii ndiyo siku aliyopigana ‘Ammaar kwa ajili ya haki na watu kumfuata mpaka akauwawa shahidi kama walivyokufa mashahidi wazazi wake wawili ambao walisiimamia haki.
 

Katika kitabu kiitwacho 'Al Istiy-aab' imenukuliwa kuwa AbdurRahmaan As-Sulamy amesema;
"Nilimsikia 'Ammaar akisema; 'Ewe Haashim tangulia, leo ndiyo siku ya kukutana na wapenzi, Muhammad na Swahibu zake".
WaLLaahi hata kama wangetushinda siku hiyo, tungekuwa na uhakika mmoja, nao ni kuwa sisi tuko katika upande wa Haki".
Inasemekana kuwa 'Ammaar (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikufa na miaka zaidi ya tisini aliuliwa katika vita vya Siffiyn katika Ukhaliyfah wa 'Alliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu 'anhu), Alikufa Shaahid katika kuisimamia haki ambayo ndiyo msimamo wa kila muislaamu. Alizikwa katika eneo pamoja na mashahidi, maiti yake ilibebwa na 'Alliy bin Abi Twaalib (Radhwiya Allaahu 'anhu) na kumswalia pamoja na Waislaam wenzake, kisha akamzika na nguo zake. Ulihifadhiwa mwili wake na huku Pepo ikiwa tayari ikimsubiri na kama alivyowahi kusimulia Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika moja ya hadiyth zake kwamba: "Pepo ilikuwa na hamu sana na ’Ammaar (Radhwiya Allaahu 'anhu)".
 

 

 

 

Share