Kusherehekea Siku Ya Kuzaliwa (Birthday) Inafaa?

SWALI:

asalam alaikum warahma tullahi wabarakatum. suali langu hivi jee ni vibaya mtoto kufanyiwa birthday bila musik ni ya watoto tu wenzao kula  na kunywa tu, na jee nivibaya kupuliza au kuuzima mshumaa wa happy birthday ni kuwa eti anauabudu moto? inshallah mtanipa jibu  muafaka.

 


 

 

JIBU:

AlhamduliLLah,  Waswalaatu Was-salaam 'alaa Rasuli-Llah  صلى الله عليه وآله وسلم Amma ba'ad,

 

Tunamshukuru ndugu yetu kwa kuuliza swali hili muhimu ambalo lenye kuhusu jambo ambalo Waislamu wengi wanalitenda wakati jambo lenyewe halina msingi wa mafundisho ya dini, bali ni katika mambo ya kuigiza makafiri.

Amesema Allaah سبحانه وتعالى  

((وَلَن تَرْضَى عَنكَ الْيَهُودُ وَلاَ النَّصَارَى حَتَّى تَتَّبِعَ مِلَّتَهُمْ))

((Mayahudi hawawi radhi nawe, wala Wakristo, mpaka ufuate mila yao)) Al-Baqarah:120

Miongoni mwa mila zao makafiri ni hizo za kuwasha mishumaa na kupuliza, na kuweka muziki na kadhalika, yote hayo ni mafundisho ya baatil yasiyompasa Muislamu kuyafuata bali ni kufuata mwendo wa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم pamoja na Wema Waliotangulia (Salaf Swaalih)  ambao haijathibitika kuwa walikuwa wakishereheka siku zao za kuzaliwa  abadan.

Kwa hiyo haifai kabisa kusherehekea kwa aina yeyote hata kama ni kualika watoto wenzake kukusanyika kula na kunywa tu, kwani kufanya hivi itakuwa ni mafundisho kwa wengine kuwa jambo hili linafaa kwa vile eti halina  muziki au hupulizi mishumaa.  Na kusita kwako kufanya hivyo itakuwa ni mafundisho ya wenzako na kizazi chako  kuendelea kujiepusha na mila hizi na kila atakayewacha kufanya kwa mafundisho yako basi utapata thawabu zako kutoka kwa Allaah سبحانه وتعالى .   

Ili kupata maelezo zaidi kuhusu upotofu wa jambo hili tafadhali soma makala muhimu sana iliyokuweko katika ALHIDAAYA katika kiungo kifuatacho yanayohusiana na maudhuu hii, upate kuona madhara yake na uweze kujiepusha na mambo haya yasio na maana katika dini yetu bali ni ya kumuingiza mtu katika kufuru ya kuigiza makafiri.

Bonyeza hapa:

Historia Ya Keki Na Mishumaa Katika Kuadhimisha Siku Ya Kuzaliwa (Birthday)

Na Allaah Anajua Zaidi.

 

 

Share