Hadiyth Ya "Ee 'Aliy Fanya Mambo Matano Kabla Ya Kulala" Ni Sahihi?

 

Hadiyth Ya "Ee 'Aliy Fanya Mambo Matano Kabla Ya Kulala" Ni Sahihi?

 

Alhidaaya.com

SWALI:

 

Kwanza natoa shukrani zangu kwa wahusika wote wa al-hidaaya. Mimi maswali ni matano:- 

 

1.- Ukiwa uatsoma suratul ikhlas mara tatu utakua umesoma quran nzima?              

 

2.- Ukiwa utasoma suratul fatiha mara nne utakua kama umetoa dirham elfu nne?  

 

3.- Ikiwa utasema laa ilaha illa Allah wahdahula sharika lahu mulku wa lahu lhamdu yuhyi wayumi wahuwa ala kulli shaiin qadiir. mara kumi basi utakua umezuru al-kaaba?                          

4.- Ukiwa utasema lahaula wala quwata illa billahi al alliyyu aladhim. mara kumi utakua umehifazi pahala pako peponi?    

 

5- Ikiwa utasema: astaghafirullah adhiim alladhii la illaha illah huwa hayyu al-quyuum wa atubu alaihi. Mara kumi basi nitakua nimewaridhia niliohasimiana nao? 

 

Nitashukuru al-hidaaya kama mtanijibu maswala yangu haya. inshallah. yote haya nikutaka uhakika kutoka kwenu.

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Kwanza tunataka kukufahamisha kuwa maswali yako yametokana na Hadiyth iliyoenezwa sana kwenye mtandao iitwayo ‘Ee ‘Aliy Usilale Hadi Umefanya Mambo Matano’

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) Kamwambia

 

Sayyidina 'Aliy (Radhwiya Allaahu 'anhu):

 

Ya   Ibn Ammi usilale ila umefanya mambo matano nayo ni:-

 

*kusoma Qur-ani Yote

 

*kutoa Sadaka Ya Dirham Elfu Nne

 

*kuzuru Al-kaaba.

 

*kuhifadhi Pahala Pako Peponi.

 

*Ridhaa Ya Uliohasimiana Nao. Sayyidina  'Aliy (Radhwiya Allaahu 'anhu) Akasema vipi ya Rasulallah?

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)akamwambia:-

 

1.) Ikiwa utasoma suratul Ikhlas mara tatu basi utakuwa umesoma Quran yote.

2.) Ikiwa utasoma Suwrah Al-Fatiha mara nne basi utakuwa umetowa sadaka ya dirham elfu nne

3.) Ikiwa utasema: Laa Illa Allaah Wahdhu Laa Ilaha Illa Allah  Wahdahu  La  Sharika Lahu Al Mulku Wa Lahu Lhamdu Yuhyi Wayumitu Wahuwa Ala Kulli Shaiin Qadiir.Mara kumi basi utakuwa umezuru Al-Kaaba.

4.) Ikiwa utasema: Lahaula Wala Quwwata Illa Billahi Al Aliyyu Al Adhiim. Mara kumi,basi utakuwa umehifadhi pahala pako peponi.

5.) Ikiwa utasema: Lahaula Wala Quwwata Illa Billahi Al Aliyyu Al Adhiim. Mara kumi. Basi umewaridhia uliohasimiana nao.

 

Tunataka ufahamu kuwa hiyo ni Hadiyth ya kutungwa na haina uhusiano wowote na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na Wanachuoni wanasema ni mojawapo za Hadiyth za kutungwa na Mashia.

 

Hivyo, tunawanasihi wote wenye kushughulika na kueneza habari za uongo kama hizo, wamuogope Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na waogope kutumbukia katika maonyo aliyotoa Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth zifuatazo:

  1. Imepokewa na ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Msiniongopee kwani anayeniongopea kwa kukusudia ataingia motoni”.
  2. Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Atakayeniongopea kwa makusudi basi ajiandalie makazi yake motoni”.
  3. Imepokewa kwa Abu Hurayrah kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa amesema: “Anayeniongopea kwa makusudi basi ajiandalie makazi yake motoni”.

Hadiyth zote hizi zimenukuliwa na [al-Bukhaariy na Muslim].

 

Pia hapa chini kuna maelezo muhimu kuhusiana na masuala hayo:

 

Hatari Ya Kueneza Hadiyth Dhaifu Na Visa Vya Uongo

 

Ama tukitazama fadhila za Suwrah kama Suwrah Al-Ikhlaasw ni kuwa kweli Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Yeyote mwenye kusoma Suratul Ikhlaasw ni kama amesoma thuluthi (1/3) ya Qur-aan" [Ahmad na an-Nasaa'iy kutoka kwa Ubayy bin Ka'b [Radhwiya Allaahu 'anhu].

 

Wanachuoni wamesema makusudio ya Suwrah hiyo kuwa ni thuluthi ya Qur-aan ni: "Hiyo ni kwa ajili ya maana na elimu na ujuzi, kwani elimu ya Qur-aan imegawanyika mara tatu: Tawhiyd, Hukmu na Visa. Na Suwrah hii inatuelezea kuhusu Tawhiyd, hivyo kuifanya kuwa Suwrah hii kuwa thuluthi kwa njia hii".

 

Pia panasemwa: "Hilo ni kwa ile thawabu anayopata mwenye kuisoma. Hivyo anayoisoma huwa ni kama amesoma thuluthi ya Qur-aan kwa ujira". Kwa hiyo, mwenye kuisoma mara tatu ni kama amesoma Qur-aan nzima.

 

Ama kuhusu fadhila za Suwrah Al-Faatihah hatujapata hiyo uliyosema na kuiandika bali Hadiyth zilizo sahihi kuihusu ni kama zifuatazo:

 

  • Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia Abi Sa'iyd bin al-Mu'allaa: "Nitakufundisha Suwrah tukufu zaidi katika Qur-aan kabla hujatoka Msikitini". Akasema: "Akanishika mkono wangu, na alipotaka kutoka nikamuuliza: 'Ee Rusuli wa Allaah! Uliniambia utanifundisha Suwrah tukufu zaidi kabisa katika Qur-aan?" Akasema: "Ndio, 'Alhamdulillahi Rabbil 'Aalamiyn' …" [Ahmad na al-Bukhaariy].
  • Ubayy bin Ka'ab (Radhwiya Allaahu 'anhu) alimsomea Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Umm al-Qur-aan, akasema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Naapa kwa Yule ambaye nafsi yangu iko Mkononi Mwake, haijateremshwa katika Taurati wala Injili wala katika Zaburi wala hakuna mfano wake katika Qur-aan. Nayo ni Aayah saba zinazorudia sana na Qur-aan Tukufu ambayo nimepatiwa" [Ahmad].

Ama kuhusu suala la tatu ‘Laa Ilaaha Illa Allaah Wahdahu La Shariyka Lahu, Lahul Mulk Wa Lahul Hamd, Yuhyi Wa Yumiytu Wa Huwa ‘Alaa Kulli Shay-in Qadiyr’, itabidi turekebishe kwani katika Hadiyth iliyo sahihi fadhila zake ni kama zifuatazo:

Kuwa anayesoma hiyo "…Kila siku mara mia moja, zitakuwa kwake sawa na kuacha huru watumwa kumi, na ataandikiwa mema mia moja, na atafutiwa maovu mia moja. Na itakuwa kinga kwake kumkinga na Shetani, siku yake hiyo mpaka jioni. Hakuna yeyote atayelifanya lililo bora zaidi yake, isipokuwa atakayefanya zaidi ya alivyofanya" [al-Bukhaariy na Muslim kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu)].

 

Na katika riwaya nyingine inasema: "Mwenye kusoma mara kumi …atakuwa sawa na mwenye kuacha huru watumwa wanne katika watoto wa Ismaa'iyl" (al-Bukhaariy na Muslim kutoka kwa Abu Ayyuub al-Answaariy [Radhwiya Allaahu 'anhu]).

 

Ama kuhusu dhikri ya ‘Laa Hawla Wala Quwwata Illa Billaahi’ mpaka hapo au mwisho ikabadilika kidogo mara nyingi imejumlishwa na dhikri nyingine mwanzoni. Ama moja ya hiyo ni ile inayotuambia fadhila yake: "Atasemehewa makosa yake hata yakiwa ni kama povu la bahari" (at-Tirmidhiy na an-Nasaa'iy).

Na pia dhikri hiyo imejulishwa na nyingine katika kile kisomo pindi Muislamu anapoamka asubuhi, na fadhila zake ni: "Mwenye kusema hayo atasamehewa, akiomba atajibiwa na lau atasimama, akachukua wudhuu kisha akaswali, Swalah yake itakubaliwa" (al-Bukhaariy na Ibn Maajah).

Pia kusema ‘Laa Hawla Wala Quwwata Illa Billaahi’ ni hazina miongoni mwa hazina za Peponi [al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaa'iy na Ibn Maajah].

 

Pia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliuliza: "Je, siwaonyeshi nyinyi mlango miongoni mwa milango ya Peponi?" Akasema: "Na ni upi huo?" Akasema: “Laa Hawla Wala Quwwata Illa Billaahi" [Ahmad].

 

Dhikri ambayo tumeipata katika Hadiyth ni: “Astaghfirullaah Alladhiy Laa ilaaha illaa Huwa al-Hayyul Qayyuum wa Atuwbu ilayhi” bila neno Adhiym. Hizi riwaya zilizokuja kuhusu hii dhikr zinataja idadi ya kusema mara tatu au bila kutaja lakini zipo zilizo dhaifu, batili, nzuri na sahihi. Fadhila yake ni kusamehewa madhambi hata kama alikimbia kutoka katika jihadi au mfano wa povu la bahari. Nyingine ni “Astaghfirullaah Al-‘Aliyyul Adhiym Alladhiy Laa ilaaha illaa Huwa al-Hayyul Qayyuum”, mwenye kusema mara tatu kwa yakini madhambi yake husamehewa [al-Bukhaariy].

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share