Fadhila za Suwratul-Faatihah

 

Fadhila za Suwratul-Faatihah

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Hii ni Suwrah iliyokuwa Adhimu na bora, kuliko Suwrah zote za Qur-aan, nayo ni miongoni mwa Suwrah zenye majina mengi na miongoni mwa majina yake ni: Al-Faatihah, Ummul-Qur-aan, AlhamduliLLaah, Asw-Swalaah, Ash-Shifaa, Ar-Ruqyah, Sab‘ul-Mathaaniy, Ummul-Kitaab. Haijateremka katika Tawraat wala katika Injiyl wala katika Zaburi mfano wake.

 

Utukufu na Fadhila za Suwratul-Faatihah unaelezewa katika Hadiyth nyingi, baadhi yake ni hizi zifuatazo:

 

Suwratul-Faatihah Ni Suwrah Adhimu Kabisa:

 

عَنْ أَبِى سَعِيدِ بْنِ الْمُعَلَّى قَالَ: كُنْتُ أُصَلِّى فَدَعَانِى النَّبِىُّ صلى الله عليه وسلم فَلَمْ أُجِبْهُ، قُلْتُ: يَا رَسُولَ اللَّهِ إِنِّى كُنْتُ أُصَلِّى. قَالَ: ((أَلَمْ يَقُلِ اللَّهُ :اسْتَجِيبُوا لِلَّه وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ))  ثُمَّ قَالَ: ((أَلاَ أُعَلِّمُكَ أَعْظَمَ سُورَةٍ فِى الْقُرْآنِ قَبْلَ أَنْ تَخْرُجَ مِنَ الْمَسْجِدِ))  فَأَخَذَ بِيَدِى فَلَمَّا أَرَدْنَا أَنْ نَخْرُجَ قُلْتُ يَا رَسُولَ اللَّهِ إِنَّكَ قُلْتَ لأُعَلِّمَنَّكَ أَعْظَمَ سُورَةٍ مِنَ الْقُرْآنِ. قَالَ: ((الْحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ، هِىَ السَّبْعُ الْمَثَانِى وَالْقُرْآنُ الْعَظِيمُ الَّذِى أُوتِيتُهُ))   

Abuu Sa’iyd bin Al-Mu’allaa (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amehadithia kwamba:  Nilikuwa nikiswali, akaniita Rasulu-Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) nikawa sikumuitikia mpaka nilipomaliza kuswali. Kisha nikamwendea akaniambia: “Kimekuzuia nini usinijie?”  Nikasema:  Yaa Rasula-Allaah, nilikuwa naswali. Akasema: “Kwani Allaah Hakusema:

اسْتَجِيبُوا لِلَّه وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ

 

“Muitikieni Allaah na Rasuli Anapokuiteni” [Al-Anfaal: 24]. Kisha akasema: “Nitakufundisha Suwrah tukufu kabisa katika Qur-aan kabla hukutoka Msikitini.” Akanikamata mkono, alipotaka kutoka Msikitini, nikamwambia: Yaa Rasula-Allaah! Ulisema utanifundisha Suwrah tukufu kabisa katika Qur-aan. Akasema: “Naam, AlhamduliLLaahi Rabbil-‘Alaamiyn, hizo ni (Aayaat) Saba zinazokaririwa (kusomwa) na Qur-aan Adhimu niliyopewa.” [Al-Hijr: 87] [Al-Bukhaariy]

 

 

Suwaratul-Faatihah Ni Shifaa (Poza)

 

عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ رضى الله عنه أَنَّ نَاسًا مِنْ أَصْحَابِ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم أَتَوْا عَلَى حَىٍّ مِنْ أَحْيَاءِ الْعَرَبِ فَلَمْ يَقْرُوهُمْ، فَبَيْنَمَا هُمْ كَذَلِكَ إِذْ لُدِغَ سَيِّدُ أُولَئِكَ فَقَالُوا: هَلْ مَعَكُمْ مِنْ دَوَاءٍ أَوْ رَاقٍ؟ فَقَالُوا: إِنَّكُمْ لَمْ تَقْرُونَا، وَلاَ نَفْعَلُ حَتَّى تَجْعَلُوا لَنَا جُعْلاً‏.‏ فَجَعَلُوا لَهُمْ قَطِيعًا مِنَ الشَّاءِ، فَجَعَلَ يَقْرَأُ بِأُمِّ الْقُرْآنِ، وَيَجْمَعُ بُزَاقَهُ، وَيَتْفِلُ، فَبَرَأَ، فَأَتَوْا بِالشَّاءِ، فَقَالُوا: لاَ نَأْخُذُهُ حَتَّى نَسْأَلَ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم فَسَأَلُوهُ، فَضَحِكَ وَقَالَ ‏:‏ ((وَمَا أَدْرَاكَ أَنَّهَا رُقْيَةٌ، خُذُوهَا، وَاضْرِبُوا لِي بِسَهْمٍ))

Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amehadithia kwamba: Baadhi ya Maswahaaba (wakiwa safarini) walifika karibu na kabila fulani la Waarabu, wakakataa kuwapokea. Walipobakia katika hali hiyo, huku mkuu wao alitafunwa na nyoka (au nge). Wakasema: Je, mna dawa yoyote au tabibu? Wakajibu: Nyinyi mmekataa kutupokea kwa hiyo hatutamtibu mgonjwa wenu hadi mtulipe! Wakakubali kuwapa kundi la kondoo. Mmoja wa Swahaaba akaanza kumsomea Suwratul-Faatihah huku akikusanya mate na kumtemea (mahali alipotafunwa). Mgonjwa akapona kisha watu wake wakawaletea kondoo lakini wakasema. Tusiwachukue mpaka tumuulize Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Walipomuuliza alicheka akasema: “Mmejuaje kuwa Suwratul-Faatihah ni ruqya? Wachukueni na nigaieni sehemu yangu.”  [Al-Bukhaariy]

 

Suwratul-Faatihah Zimefunguliwa Mbingu Kuipokea

 

عن ابْنِ عَبَّاسٍ قَالَ : بَيْنَمَا جِبْرِيلُ قَاعِدٌ عِنْدَ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ سَمِعَ نَقِيضًا مِنْ فَوْقِهِ ، فَرَفَعَ رَأْسَهُ ، فَقَالَ : هَذَا بَابٌ مِنْ السَّمَاءِ فُتِحَ الْيَوْمَ لَمْ يُفْتَحْ قَطُّ إِلَّا الْيَوْمَ ، فَنَزَلَ مِنْهُ مَلَكٌ ، فَقَالَ : هَذَا مَلَكٌ نَزَلَ إِلَى الْأَرْضِ لَمْ يَنْزِلْ قَطُّ إِلَّا الْيَوْمَ ، فَسَلَّمَ وَقَالَ : أَبْشِرْ بِنُورَيْنِ أُوتِيتَهُمَا لَمْ يُؤْتَهُمَا نَبِيٌّ قَبْلَكَ ؛ فَاتِحَةُ الْكِتَابِ وَخَوَاتِيمُ سُورَةِ الْبَقَرَةِ لَنْ تَقْرَأَ بِحَرْفٍ مِنْهُمَا إِلَّا أُعْطِيتَهُ

Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) amehadithia kwamba: Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) alipokuwa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisikia sauti kutoka juu. Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) akatazama juu akasema: “Huu mlango wa mbinguni umefunguliwa na haujapatapo kufunguliwa isipokuwa leo.” Malaika akateremka humo akasema: “Huyu Malaika ameteremka ardhini, hajapatapo kuteremka kamwe isipokuwa leo.” Akasalimia kisha   akasema: “Pokea bishara ya nuru mbili ulizopewa ambazo hakuna Nabiy aliyepewa kabla yako; Ufunguo wa Kitabu (Al-Faatihah), na Aayah (mbili) za mwisho wa Suwratul-Baqarah.  Hutosoma herufi humo ila utapewa barakah zake ziliomo.” [Muslim]

 

 

Suwratul-Faatihah: Allaah Ameigawa Baina Yake

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((مَنْ صَلَّى صَلَاةً لَمْ يَقْرَأْ فِيهَا بِأُمِّ الْقُرْآنِ فَهِيَ خِدَاجٌ)) ثَلَاثًا غَيْرُ تَمَامٍ، فَقِيلَ لِأَبِي هُرَيْرَةَ : إِنَّا نَكُونُ وَرَاءَ الْإِمَامِ؟ فَقَالَ: اقْرَأْ بِهَا فِي نَفْسِكَ فَإِنِّي سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ: ((قَالَ اللَّهُ تَعَالَى قَسَمْتُ الصَّلَاةَ بَيْنِي وَبَيْنَ عَبْدِي نِصْفَيْنِ وَلِعَبْدِي مَا سَأَلَ، فَإِذَا قَالَ الْعَبْدُ (الْحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ) قَالَ اللَّهُ تَعَالَى حَمِدَنِي عَبْدِي، وَإِذَا قَالَ (الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ)  قَالَ اللَّهُ تَعَالَى أَثْنَى عَلَيَّ عَبْدِي ، وَإِذَا قَالَ (مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ) قَالَ مَجَّدَنِي عَبْدِي، وَقَالَ مَرَّةً فَوَّضَ إِلَيَّ عَبْدِي، فَإِذَا قَالَ (إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ) قَالَ هَذَا بَيْنِي وَبَيْنَ عَبْدِي وَلِعَبْدِي مَا سَأَلَ)) 

Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amehadithia kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Atakayeswali Swalaah bila ya kusoma humo mama wa Qur-aan (Suwratu Al-Faatihah) huwa haikutimia (ina kasoro).” Alikariri mara tatu: “Haikutimia.” Mtu mmoja alimwambia Abuu Hurayrah: (Hata) tukiwa nyuma ya Imaam? Akasema: Isome mwenyewe (kimya kimya) kwani nilimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Allaah Ta’aalaa Amesema: Nimeigawa Swalaah baina Yangu na mja Wangu nusu mbili, mja Wangu atapata yale aliyoyaomba. Mja anaposema: Himidi zote Anastahiki Allaah Mola wa walimwengu, Allaah Ta’aalaa Husema: Mja Wangu kanihimidi (kanisifu). Na anaposema: Mwingi wa Rahmah, Mwenye kurehemu, Allaah Ta’aalaa Husema: Mja wangu kanitukuza, na anaposema: Mfalme wa siku ya malipo, Allaah Ta’aalaa Husema: Mja wangu kanipa heshima. Na mara moja alisema: Mja wangu kazikubali nguvu Zangu. Na anaposema: Wewe Pekee tunakuabudu na Wewe Pekee tunakuomba msaada, Husema: Hii ni baina Yangu na mja Wangu na mja Wangu atapata kile alichokiomba. Na anaposema: Tuongoze njia iliyonyooka, njia ya wale Uliowaneemesha, si ya walioghadhibikiwa wala waliopotea, Husema: Hii ni ya mja Wangu na mja Wangu atapata kile alichokiomba.” [Muslim, Maalik, At-Tirmidhiy, Abu Daawuwd, An-Nasaaiy na Ibn Maajah]  

 

 

Suwratul-Faatihah: Swalaah Haitiimi Bila Kuisoma

 

عَنْ عُبَادَةَ بْنِ الصَّامِتِ رضي الله عنه أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((لَا صَلَاةَ لِمَنْ لَمْ يَقْرَأْ بِفَاتِحَةِ الْكِتَابِ))

 ‘Ubaadah bin Swaamit (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amehadithia kwamba  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakuna Swalaah kwa asiyesoma (ndani yake) Ufunguo wa Kitabu.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

Suwratul-Faatihah Ni Aayah Sabab Zinazokaririwa:

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَلَقَدْ آتَيْنَاكَ سَبْعًا مِّنَ الْمَثَانِي وَالْقُرْآنَ الْعَظِيمَ﴿٨٧﴾

 Na kwa yakini Tumekupa (Aayaat) Saba zinazokaririwa (kusomwa) na Qur-aan Adhimu.

 

 

‘Ulamaa wa Tafsiyr akiwemo Imaam As-Sa’diy na Ibn Kathiyr, wamenukuu kuwa hizo ni ima Suwrah Saba za mwanzoni au ni Aayat Saba za Suwratul-Faatihah kwa kuwa zinakaririwa kusomwa katika Swalaah.

  

 

 

Share