Kumsaidia Mwenye Kudhulumu Watu

 

SWALI: 

Ikiwa mtu anamkandamiza Muislam na wewe ukamsaidia nini hukumu yake.
        

 


 

 

JIBU:

 Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Dhulma ni kitu kibaya sana katika Dini yetu na mwenye kusaidia katika maasiya naye anapata fungu lake la madhambi. Na katika Hadithi al–Qudsiy Allah Anasema: 

 “Enyi waja Wangu! Mimi Nimejiharimishia dhulma juu ya Nafsi Yangu na Nikaifanya ni haramu baina yenu basi msidhulumiane” (Muslim kutoka kwa Abu Dharr ).

Hii ni kwa kuwa Uislamu huwa unataka kuondoa maovu kutoka katika shina lake na sio kwa matawi yake ili madhambi yale yasiwe ni yenye kukua. Allaah Anasema:

“Madhalimu hawatakuwa na rafiki, wala mwombezi wa kuitikiwa” (40: 18).

Na Mtume (Swalla-Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  anatupatia mfano wa Riba ambayo ni dhulma anayefanyiwa yule anayekopa, hivyo mwenye kusaidia kwa njia yoyote anapata madhambi:

“Amelaaniwa anayechukua riba, mwenye kulipa, shahidi na mwenye kuandika”  (Abu Dawuud kutoka kwa Ibn Mas‘uud 

Na Hadiyth kama hiyo imenukuliwa na at-Tirmidhy na An-Nasaaiy kutoka kwa ‘Ali bin Abi Twaalib 

Hivyo, dhulma nyingine yoyote inachukua mfano wa dhulma ya riba, hivyo mwenye kusaidia kwa njia moja au nyingine atapata dhambi.

Inabidi ndugu yetu akatae kutumiwa katika kuwadhulumu watu wengine ikiwa ni Waislamu au si Waislamu, lakini wakiwa ni Waislamu uovu unakuwa mkubwa zaidi.

Tunamwambia ndugu yetu huyo arudi kwa Allah kwa kutaka msamaha na asirudie tena kosa hilo na afanye bidii katika kufanya mema.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share