La Kufanya Unapochelewa Swalaah Ya Jamaa’ah Ukamkuta Imaam Ameshamaliza Swalaah

 

La Kufanya Unapochelewa Swalaah Ya Jamaa’ah Ukamkuta Imaam Ameshamaliza Swalaah

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

A.aleykim warahamatullah wabarakatu.

Naomba kuuliza kuhusu swala. Kama umechelewa jamaa na umekuta Imamu ameshatoa salaam. Nini unapaswa kufanya ? Kabla ya kufumga swala? Kuleta Adhana na uqimu swala au unapaswa kunuia swala na kuanza kuswali ? Hapa pana mtihani, kila mtu ana ataili yake. Nielimishe na mimi nipate kuelimisha wengine.  

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwanza, tunakukumbusha kuandika salaam kwa urefu na ukamilifu bila kufupisha kama ulivyoandika. Soma hii Makala hapa chini upate faida kuhusu umuhimu wa salaam na namna ya kusalimiana kisawasawa pamoja na makatazo ya kufupisha salaam nk.

 

Maamkizi Ya Kiislaam: Maamrisho Na Fadhila Zake

 

Hukmu Ya Kufupisha Thanaa (Kumtukuza Allaah) Na Kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) Na Maamkizi Ya Kiislam

 

Ama kuhusu swali lako ni kwamba, unapomkuta Imaam kamaliza Swalaah Msikitini, basi unachopaswa kufanya ni kuswali sehemu yenye sutrah (kizuizi mbele yako) na tayari utakuwa umeshaweka niyyah kwa kudhamiria kuja kwenye Swalaah hiyo, huna haja ya kutamka niyyah kwa maneno bali niyyah mahali pake ni moyoni.

 

Kisha utafunga Swalaah na kuendelea kuswali. Adhana na Iqaamah ishatolewa Msikitini na hiyo inatosheleza, hivyo si lazima kwako kutoa Adhaana nyingine na kuqimu Swalaah. Lakini ikiwa mtu atatoa Iqaamah au Adhaan na Iqaamah, basi hakuna makatazo kwani hili ni jambo wametofautiana ‘Ulamaa; kuna wanaoona hakuna haja ya kutoa tena Adhaana wala Iqaamah kwa sababu tayari ilishatolewa Msikitini na hiyo inatosheleza.

 

Na kuna wanaoona ni vizuri kutoa Iqaamah pekee na kuna wanaoona ni vizuri kutoa Adhaana na Iqaamah.

Lakini pindi itakapoadhiniwa tena, basi isiwe kwa sauti kubwa bali iwe sauti tu ya kujisikia mwenyewe au wanaoswali naye.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share