Kujichua Sehemu Za Siri Au Kujisaga Nini Hukmu Yake?

 

Kujichua Sehemu Za Siri Au Kujisaga Nini Hukmu Yake?

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali La Kwanza:

 

Nauliza Kwamba.... Dini Inasemaje Kuhusu Kupiga Punyeto Kwa Kijana Amabye Bado Hajaoa; Na Hanauwezo Wakuoa Bado?

 

 

Swali La Pili:

 

Asalam Alaykum,  naomba kuuliza juu ya baadhi ya vijana wa kike na wa kiume,wanapofikia umri fulani au baada ya kubaleghe hujiwa na matamanio ya kujamii (sexual desires) hivyo wengine huamua kutoa manii kwa kutumia mikono yao na kwa wanawake huamua kujitia kitu chochote kinachoweza kuleta hisia na kupunguza matamanio yao.
 

Swali ni kwamba,je hadiyth na quran inalizungumziaje swali hili.  natumai majibu mazuri.

 

 

Swali La Tatu:

 

Assalam aleikum!                                  

 

Swali ni kuwa kujitoa manii(nyeto) ni haramu au ni makuruu?kwani kwa fikra zangu naona ni vizuri kwani unapunguza matatamanio kwa wanawake na hasa kufanya tendo la zinaa kabla ya ndoa.

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Hili ni swali muhimu kwa kuwa linagusa tatizo sugu linalowakabili vijana wengi wa Kiislam, ambao bado hawajaoa, na wanaokabiliana kwa hali ya juu kabisa na vishawishi vilivyowazunguka katika jamii mbalimbali wanazoishi ndani yake. Kujichua wanaume au kujisaga wanawake ni jambo linalokubalika na kufanyika sana katika jamii zisizo za Kiislam kwa idadi kubwa ya watu: vijana wa kiume na kike, makapera, wazee na hata waliooa/kuolewa.

 

Lakini hali hiyo katika Uislam ni kinyume. Kwani katika Uislam kujichua au kujisaga (punyeto) ni haraam kwa mwanamme na mwanamke, kwa dalili zifuatazo:

 

Kwanza, dalili kutoka katika Qur’aan:

 

وَالَّذِينَ هُمْ لِفُرُوجِهِمْ حَافِظُونَ ﴿٥﴾إِلَّا عَلَىٰ أَزْوَاجِهِمْ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَإِنَّهُمْ غَيْرُ مَلُومِينَ ﴿٦﴾فَمَنِ ابْتَغَىٰ وَرَاءَ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْعَادُونَ ﴿٧﴾

Na ambao wanazihifadhi tupu zao. Isipokuwa kwa wake zao, au kwa iliyowamiliki mikono yao ya kuume basi hao hawalaumiwi. Lakini atakayetaka kinyume ya hayo; basi hao ndio wapindukao mipaka. [Al-Muuminuwn: 5-7]

 

Aayah hii inakataza waziwazi vitendo vyote vya tendo la ndoa (ikijumuisha punyeto) isipokuwa kwa wake, na yeyote anayejipelekea kwenye matendo kinyume na hayo yaliyoruhusiwa, basi ni katika warukao mipaka.

وَلْيَسْتَعْفِفِ الَّذِينَ لَا يَجِدُونَ نِكَاحًا حَتَّىٰ يُغْنِيَهُمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ ۗ 

Na wajisitiri (yaliyoharamishwa) wale ambao hawapati uwezo wa ndoa mpaka Allaah Awatajirishe katika fadhila Zake. [An-Nuwr: 33]

 

Aayah hii vilevile inaamrisha wazi kwa yule asiye na uwezo wa kimali kwa ajili ya kuoa, basi anatakiwa ajiweke katika hali ya kujidhibiti  na machafu na kujihifadhi kimwili na awe na subira ya kuweza kukabiliana na vishawishi mbalimbali ikiwemo kupiga punyeto, hadi Allaah Atakapomruzuku kwa fadhila Zake.

 

Vilevile Wanachoni wa Fiqh (Fuqahaa) wamechukulia hukumu kutoka katika ayah hii kuwa ni haraam kupiga punyeto kwa sababu mbili: Ya kwanza: Katika ayah hii, Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa  Anaamrisha kujizuia na machafu, na kutokana na kanuni za ki-Fiqh, maamrisho  yanaashiria ulazima (uwajibu) wa jambo. Hivyo kubaki katika hali ya usafi (kujizuia na machafu) ni wajibu na panapokuwa kujizuia na machafu ni wajibu, basi kujizuia na yale yote yanayopelekea kufanya machafu ni wajibu zaidi. Hii inatokana na ukweli kwamba kujizuia na machafu au kubaki safi kutapatikana pale mtu anapojizuia na vile vyenye kusababisha hayo machafu.

 

Sababu ya pili, kwamba katika ayah hiyo Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa  Ameamrisha Usafi (kutofanya machafu) kwa wale wasio na uwezo wa kuoa. Hapa Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa Hajadhihirisha uhusiano wa kujizua na machafu na ule wa kuoa. Hivyo kunahesabika kuwa kujichua ni haraam. Na kama kungekuwa ni halaal, basi hapa ndipo pahala pake palipokuwa panatakikana kutajwa. Kwa kutotajwa uhalali wa kujichua katika ayah hii ambapo ndipo pahali muwafaka wa kuelezwa hilo, kunadhihirisha kuwa jambo hilo ni haraam, Kwani ‘kunyamazwa katika sehemu ya kuelezwa kunaashiria makatazo.’ Tazama pia tafsiri ya Imaam Qurtubiy katika aayah hiyo.

 

Pili, dalili kutoka katika Sunnah:

 

Anasema ‘Abdullaah ibn Mas’uud (Radhwiya 'anhu), “Tulikuwa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa salaam) na hali bado ni vijana na hatuna uwezo wa mali. Basi Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa salaam)  akatuambia: (Enyi vijana! Mwenye kuweza kuoa na aoe, kwani kuoa kunamsaidia yeye kuinamisha macho yake (kutotazama ya haraam) na kuhifadhi tupu yake (kutofanya zinaa na uchafu mwingine), na yule asiye na uwezo wa kuoa, afunge, maana funga hupunguza matamanio ya kimwili)) [Al Bukhaariy]

 

Hadiyth hii inamuamrisha mtu asiye na uwezo wa kuoa, afunge, japokuwa kuna ugumu wa kufanya hivyo kila wakati anapozidiwa na matamanio, ili asitumbukie katika vitumbukizo vikiwemo punyeto, pamoja na urahisi na mvuto wa kulifanya jambo hilo. Na kama kungekuwa ni halali kupiga punyeto, basi hapa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa salaam)  angeliruhusu kwa sababu ni jambo rahisi na lenye kustarehesha na asingesema watu wafunge kwani hilo ni jambo gumu na zito kulifanya. Na kama tunavyofahamu, Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa salaam) hakuletwa kutufanyia ugumu na uzito.

 

Wema waliopita kama Sa’iyd ibn Jubayr (Radhwiya Allaahu 'anhu) anasema kuhusiana na punyeto, "Allaah Atawaadhibu watu kwa sababu walikuwa wakichezea sehemu zao za siri." Naye ‘Atwaa  Rahimahu Allaahu  anasema, "Baadhi ya watu watafufuliwa na hali mikono yao ina mimba, Nadhani ni wale waliokuwa wakipiga punyeto."

 

Ingawa baadhi ya Maimam wanalijuzisha jambo hilo kwa sababu mbalimbali, kama; ikiwa mtu anaogopa kutumbukia katika zinaa, au kufanya huko ni kwa sababu tu ya kutoa matamanio yaliyozidi na wala si kwa ajili ya kujistarehesha n.k.. Hata hivyo, rai hizo hazina dalili yoyote zilizoambatana nazo, kwa hivyo ni bora mtu kujiepusha na tendo hilo kutokana na dalili zilizotangulia kutajwa.

 

Tunawanasihi ndugu zetu wenye kukabiliwa na vishawishi hivyo, wafuate nukta hizi ili ziwasaidie kupambana na hali hiyo inayowasumbua wale walio katika hali ya ukapera (kutokua na mke/mume):

 

 

1-    Jambo la mwanzo na muhimu kuliko yote ili kuepukana na mtihani huu wa kutumbukia katika tabia hiyo, ni kujitahidi kufuata maamrisho ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kuogopa  adhabu Zake.

 

2-      Kuwa safi na machafu (Kujizuia na machafu), kwa kujiweka daima katika hali ya kufikiria adhabu ya moto, na kuamini kuwa kujihifadhi huko kwa kufanya machafu ni sababu ya kuipata pepo.

 

3-    Kuinamisha macho yako (kutotazama yale ya haraam kama picha za uchi, sinema, au kukaa majiani na kutazama maumbo ya wanawake wapitao). Kujizuia huko kutazama ya haraam, kutakusaidia sana kutoamsha hamu zilizorundikana ambazo zikishaamka, basi kufanyika haraam kunakuwa ni jambo lisiloepukika kirahisi. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameamrisha wanaume na wanawake katika ayah mbili zifuatazo:

 

قُل لِّلْمُؤْمِنِينَ يَغُضُّوا مِنْ أَبْصَارِهِمْ وَيَحْفَظُوا فُرُوجَهُمْ ۚ ذَٰلِكَ أَزْكَىٰ لَهُمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ خَبِيرٌ بِمَا يَصْنَعُونَ ﴿٣٠﴾وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ

Waambie Waumini wanaume wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao. Hivyo ni utakaso zaidi kwao. Hakika Allaah ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika kwa yale wayatendayo. Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao... [An-Nuwr: 30-31]

 

Naye Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa salaam)  anasema: ((Usifuatilize mtazamo (kuangalia kwa kutokusudia (vile vilivyoharamishwa) kwa mtazamo mwingine))[At-Tirmidhiy]

 

Huu ni mwongozo kutoka kwa Nabiy wetu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa salaam) wa kujizuia na yale yote yanayoweza kuchochea matamanio ya kimwili ambayo yanaweza kumpelekea mtu kufanya yaliyokatazwa.

 

4-    Ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hilo ni kukimbilia kuoa haraka pale tu unapokuwa tayari kiuwezo, kama tulivyoona katika hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa salaam).

 

5-   Kufunga. Jizoeshe kufunga kila unapohisi matamanio yanaanza kufumuka. Nako huko kufunga kunasaidia sana kwa mengi zaidi ya hilo. Jizoeshe kufunga kila Jumatatu na Alkhamiys, masiku meupe (tarehe 13, 14 na 15 za Kiislam, kila mwezi), na ukiona matamanio yako ni mengi na ya mara kwa mara basi funga Swawm ya Nabiy Dawuud  ('Alayhi wa Salaam)  ya kila baada ya siku moja.

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa salaam)   amesema:

 

((يَا مَعْشَرَ الشَّبَابِ مَنْ اسْتَطَاعَ الْبَاءَةَ فَلْيَتَزَوَّجْ فَإِنَّهُ أَغَضُّ لِلْبَصَرِ وَأَحْصَنُ لِلْفَرْجِ وَمَنْ لَمْ يَسْتَطِعْ فَعَلَيْهِ بِالصَّوْمِ فَإِنَّهُ لَهُ وِجَاءٌ))  البخاري ومسلم

((Enyi vijana, anayeweza kuoa basi na aoe kwani ni kuinamisha macho na ni stara ya uchi, Na asiyeweza basi afunge (Swawm) kwani ni kinga (ya matamanio).[Al-Bukhaariy na Muslim]

 

6.    Kuutumia muda wako usio na la kufanya, kwa kufanya ibada zaidi na kujisomea na kutafuta elimu ya dini; kwa kusikiliza mawaidha au kutazama.

 

7.    Kujiepusha na kutumia baadhi ya vyakula, vinywaji n.k. ambavyo vinachochea hamu na kusababisha mshawasha na muibuko wa matamanio.

 

8.    Daima fikiria madhara yanayoweza kusababishwa na tendo hilo; kama ya kudhoofisha nguvu za macho, nguvu za mishipa, nguvu za uume (kwa mwanamme) au uti wa mgongo. Na muhimu zaidi, ni kule kuwa na hisia za dhambi na usumbufu utakaopatikana baada ya kufanya kitendo hicho kama vile, kuweza kupoteza Swaalah ya faradhi kwa kukubidi kuchukua muda wa kwenda kuoga kila baada ya tendo hilo.

 

9.   Fanya Tawbah, muombe Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  msamaha kila wakati, kufanya hivyo na pia kutenda matendo mema na kutokata tamaa na Rahma za Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa   kunaweka karibu zaidi na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kukufanya kumuogopa zaidi na kufikiria kila tendo unalotaka kulifanya kwanza.

 

10.   Jua kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni Mwingi wa Kusamehe na daima Humkubalia du’aa za yule anayemtaka msaada. Hivyo basi, kumuomba Allaah(Subhaanahu wa Ta'aalaa) msamaha ni jambo lenye kupokelewa Naye, na hilo linatupa nguvu kumuomba Yeye daima na kutaraji msamaha Wake.

 

11.  Kujishughulisha na mambo ya muhimu na ya faida; yakiwa ni ya akhera au ya kilimwengu ili usipate nafasi ya kuwa na faragha na ukaanza kufikiria kufanya tendo hilo ambalo hakika ni ada iliyo ngumu kuepukika.

 

12.   Fanya mazoezi mbalimbali ya kukuchosha, mwili ukishachoka matamanio yanazama.

 

13.  Usile sana, au kula kila wakati. Kwani unaposhiba mambo mengine yanachemka na kutaka haki zake.

 

 

Hayo ndio machache katika mengi ambayo yanaweza kumsaidia mtu kujiweka mbali na tendo hilo linalowasumbua wengi haswa vijana na wajane.

 

 

Na Allaah Anajua Zaidi

 

Share