Nini Historia Ya Hajarul-Aswad (Jiwe Jeusi)?

Nini Historia Ya Hajarul-Aswad (Jiwe Jeusi)?

www.alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Asalamu aleikum namshukuru Allah kwa kuweza kutufikisha hatua hii ambayo tunaweza kuwasiliana na waislam wa nchi mbali mbali kuuliza masuala na kujibiwa ujira wenu upo kwa Allah Ishaallah  Suala langu nasikia kuna jiwe jeusi huko Maka limewekwa wapi na linahistoria gani unaweza kunielezea tafadhali Ahsante

 

JIBU:

 

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kuna riwaayah nyingi zilizotaja kuhusu Hajarul-Aswad (Jiwe jeusi) na asili yake, lakini nyingi kati ya hizo zina mashaka ya usahihi wake. Na katika Uislam hatutakiwi kutegemea marejeo ambayo hayajapatikana usahihi wake mia kwa mia. Kwa hiyo iliyo sahihi zaidi ni kuwa asili yake limewekwa na Nabii Ibraahiym ('alayhis-salaam) baada ya kumaliza kujenga Ka'abah na kutokana na amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Na sababu yake ni kuwa ni alama ya kuanzia kufanya twawaaf katika Ka'bah.

 

Kwa hiyo Muislamu hatakiwi kuambatanisha Utukufu wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  na jiwe hilo kama alivyosema 'Umar ibnil-Khatwaab (Radhwiya Allaahu 'anhu) alipolibusu:

 

 "إني أعلم أنك حجر لا تضر ولا تنفع ‏ ‏ولولا أني رأيت النبي ‏ ‏صلى الله عليه وسلم ‏ ‏يقبلك ما قبلتك"   البخاري

 

"Wewe ni jiwe tu ambalo halinufaishi wala kumdhuru mtu, na ingelikuwa sikumona Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  anakubusu basi nisingelikubusu". [Al-Bukhaariy]

 

Inavyompasa Muislamu anapojaaliwa kwenda 'Umrah au Hajj anapofanya twawaaf ni kulibusu akiweza, yaani ikiwa hakuna zahma ya watu katika Ka'bah, au kuligusa. Na ikiwa ni zahma kubwa ya watu basi haimpasi Muislamu kusukuma watu kulifikia kwa kujilazimisha hadi alibusu kwani si lazima, bali inatosha kunyanyua mkono wake wa kulia kwa mbali na kusema: “Allaahu Akbar.” Na hii pia ni kufuata Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  kama ilivyo dalili katika Hadiyth ifuatayo:

 

Imetoka kwa Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alifanya twawaaf akiwa amepanda ngamia wake, na kila mara alipofika kwenye pembe (iliyowekwa jiwe) aliashiria na kusema: “Allaahu Akbar.” [Al-Bukhaariy]

 

Lakini baadhi ya ‘Ulamaa wameona usimulizi wa Hadiyth nyingine kuhusu Hajarul-Aswad kuwa ni sahiyh na ambazo zimetaja umuhimu wa Hajarul-Aswad nazo ni zifuatazo:

Hadiyth ya kwanza:

 

(( الحجر الأسود من الجنة))  صحيح النسائي   

  ((Hajarul-Aswad ni kutoka Jannah (Peponi)) [Sahiyh An-Nasaaiy]

 

Hadiyth ya pili:

 

عن ‏ ‏ابن عباس ‏ ‏قال: ‏قال رسول الله ‏ ‏صلى الله عليه وسلم ‏ ((‏نزل الحجر الأسود من الجنة وهو أشد بياضا من اللبن فسودته خطايا بني ‏ ‏آدم)) الترمذي

Kutoka kwa Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Lilipoteremshwa Hajarul-Aswad kutoka Jannh lilikuwa jeupe kama maziwa, lakini dhambi za wana Aadam zimelifanya kuwa jeusi)) [At-Tirmidhiy]

 

Hadiyth ya tatu:

 

عن ابن عباس رضي الله عنهما قال : قال رسول الله صلى الله عليه وسلم في الحجر((والله ليبعثنه الله يوم القيامة له عينان يبصر بهما ولسان ينطق به يشهد على من استلمه بحق )) وروى الترمذي وقال : حديث حسن وابن خزيمة وابن حبان في صحيحيهما

 Kutoka kwa Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Naapa kwa Allaah, Allaah Atalileta (Hajarul-Aswad) siku ya Qiyaamah na litakuwa na macho mawili ambayo yataona, na ulimi ambao utazungumza na litashuhudia wale walioligusa kwa ikhlaas)) [At-Tirmidhiy na kasema ni Hadiyth Hasan na Ibn Khuzayma, Ibn Hibbaan katika vitabu vyao]

 

Jiwe hilo liko katika pembe moja upande wa  Mashariki/Kusini mwa Ka'bah.

 

Urefu wake kutoka ardhi na takriban mita moja na nusu.

 

Jiwe hilo limefunikwa na chuma cha fedha safi kabisa. Tunaloliona ni karibu na nusu ya jiwe tu, na zaidi ya nusu nyingine imefunikwa ndani hatuioni.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share