Jukumu La Kulea Yatima

SWALI:

Mtoto yatima amelelewa na shangazi yake, na hakupewa malezi ya kiislam mpaka akapotea katika njia ya haki, jukumu la upotevu wa mtoto huyu litakuwa la nani kati ya mama na shangazi?.

 

JIBU:

Sifa zote njema anastahiki Allah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Suala la malezi ni jambo la wajibu katika Uislam, kwani mtu akosapo malezi ya sawa bila ya shaka atakengeuka na atapotea, na kwa maana hiyo ndiyo Uislam ukawapa wafuatao uwajibu wa kumhifadhi na kumlinda mtoto ili asiangamie:

1. Mama ana haki zaidi ya kuyasimamia malezi ya mtoto wake baada ya kuachwa kwa talaka, au kifo, au kwa kuolewa na mume mwingine, na atanyimwa haki hiyo pale tu patakapojitokeza vizuizi vitakavyolazimu kufanya hivyo;

2. Bibi upande wa mama, bibi upande wa baba, kisha madada, kisha mama wadogo, kisha wapwa, kisha mabint wa kaka, kisha mashangazi, na kufuatia ndugu wengine kama ilivyo kwenye utaratibu wa mirathi.

Ama jukumu la kuharibika kwa mtoto, litamhusu kwanza yule aliyekuwa ndiyo sababu ya mtoto kuharibika, pili litamhusu kila aliyeuona uharibifu huo unatokea na akaunyamazia. Tutambue kuwa kila mtu mwenye jukumu lazima atimize mas-uliya yake na kila mmoja wetu ataulizwa kuhusu jukumu hilo kama alivyotufundisha Mtume wetu (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((كلكم راع وكلكم مسئول عن رعيته الإمام راع ومسئول عن رعيته والرجل راع في أهله وهو مسئول عن رعيته والمرأة راعية في بيت زوجها ومسئولة عن رعيتها))  

((Kila mmoja kati yenu ni mchungaji, na kila mmoja kati yenu atapaswa kuulizwa ya juu ya kile anachokichunga. Imaam ni mchungaji na ataulizwa kwa anaowachunga. Mume ni mchungaji wa familia yake, naye atapaswa kuulizwa juu ya anaowachunga. Na mke ni mchungaji wa nyumba ya mumewe, naye pia atapaswa kuulizwa juu ya anachokichunga. (Al-Bukhaariy, Muslim)

Tukija katika Suala la kulea yatima tutambue kuwa hili ni jukumu zaidi kwani kulea yatima kuna fadhila nyingi na ujira wake ni mkubwa mno. Na kutomlea vizuri pia kuna hatari yake.

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ametaja fadhila za Yatima mara nyingi sana katika Qur-aan, tutazitaja hapa chache:

 

((وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْيَتَامَى قُلْ إِصْلاَحٌ لَّهُمْ خَيْرٌ وَإِنْ تُخَالِطُوهُمْ فَإِخْوَانُكُمْ وَاللّهُ يَعْلَمُ الْمُفْسِدَ مِنَ الْمُصْلِحِ وَلَوْ شَاء اللّهُ لأعْنَتَكُمْ إِنَّ اللّهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ))

((Na wanakuuliza juu ya mayatima. Sema: Kuwatengenezea ndio kheri. Na mkichanganyika nao basi ni ndugu zenu; na Allaah Anamjua mharibifu na mtengenezaji. Na Allaah Angelipenda Angelikutieni katika udhia. Hakika Allaah ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima)) [Al-Baqarah: 2:220]

((يَسْأَلُونَكَ مَاذَا يُنفِقُونَ قُلْ مَا أَنفَقْتُم مِّنْ خَيْرٍ فَلِلْوَالِدَيْنِ وَالأَقْرَبِينَ وَالْيَتَامَى وَالْمَسَاكِينِ وَابْنِ السَّبِيلِ وَمَا تَفْعَلُواْ مِنْ خَيْرٍ فَإِنَّ اللّهَ بِهِ عَلِيمٌ))

((Wanakuuliza watoe nini? Sema: Kheri mnayoitoa ni kwa ajili ya wazazi na jamaa na mayatima na masikini na wasafiri. Na kheri yoyote mnayoifanya Allaah Anaijua)) [Al-Baqarah 2:215]

Na khaswa kwa vile ni jamaa yake wa damu anayemlea Amesisitiza Allah:

((فَلَا اقْتَحَمَ الْعَقَبَةَ))   ((وَمَا أَدْرَاكَ مَا الْعَقَبَةُ))   ((فَكُّ رَقَبَةٍ))   ((أَوْ إِطْعَامٌ فِي يَوْمٍ ذِي مَسْغَبَة))   (( يَتِيمًا ذَا مَقْرَبَةٍ))

11. Hakuweza kuvikwea vikwazo vya milimani (njia nzito ya kukufikisha peponi)?  

 

12. Na nini kitakujuvya ni nini njia ya vikwazo vya milimani (njia ya kukufikisha peponi)? 

 

13. (Kuvikwea vikwazo vya mlima huo ni) Kumkomboa mtumwa

 

14. Au kumlisha siku ya njaa 

 

15. Yatima aliye jamaa  

[Al-Balad: 11-14]

Vile vile kasema Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

((أنا وكافل اليتيم في الجنة هكذا)) وأشار بالسبابة والوسطى وفرج بينهما ( رواه البخاري)

((Mimi na mwenye kumlea Yatima kama hivi)) Akaashiria kidole cha shahada na cha katikatikati pamoja na akaviachanisha baina yake [Al-Bukhaariy]

Vile vile kasema


 من وضع يده على رأس يتيم رحمة ، كتب الله له بكل شعرة مدت على يده حسنة.   رواه الإمام أحمد


((Mwenye kuweka mkono wake kwenye kichwa cha Yatima kwa upole, Allah Humuandikia jema kwa kila unywele aliougusa kwa mkono wake))
[Imaam Ahmad].

 

Na katika kuwafanyia maovu Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ametuonya:

((فَأَمَّا الْيَتِيمَ فَلَا تَقْهَرْ))

((Basi yatima usimwonee)) [Adh-Dhwuhaa: 9]

((كلاَّ بَل لَّا تُكْرِمُونَ الْيَتِيمَ))

((Sivyo hivyo! Bali nyinyi hamuwakirimu mayatima)) [Al-Fajr: 17]

 

Shangazi wa huyo Yatima anapaswa kupewa nasiha amche Allah na atimize jukumu lake.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 


Share