Pesa Alizozichuma Kusema Uongo Azifanye Nini?

 


SWALI:

Pesa zlilizopatikana kwa jili ya kusema uongo (income support) nizifanye nin ili nipate salama mbele ya mwenyezi mungu. Siwezi kuziregesha kwa njia yoyote ile. Kwa ajili ya kukhofia matatizo zaidi. wala siwezi kuwambia kua nilisema kua sina mume mkanipatia pesa na sasa nasema kua ninaye mume. Isipokua nataka kujitowa katika mambo hayo kwa njia ya salam. Lakini pesa nilizokua nazo kama akiba yangu niliyoiweka hapo mlipokua mkichukua hizo pesa nizifanye nini?

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa dada yetu katika Iymaan kuhusu suala hili nyeti katika maisha yetu ya kuishi nje ya nchi zetu.

Hakika hili ni tatizo sugu kwa ndugu zetu ambao wanakimbilia nchi za ng’ambo kwa sababu moja au nyingine. Ukweli ni sifa ambayo kila Muislamu anafaa ajipambe nayo na wazazi wawalee watoto wao juu ya sifa hiyo. Ndio Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akafundisha wazazi wasiwe ni wenye hata kuwaita watoto wao, njoo nitakupatia kitu fulani kisha usimpatie. Ukifanya hivyo utakuwa umesema uongo.

Uongo katika mzungumzo ni sifa mojawapo ya alama ya unafiki, hivyo inabidi tung’ang’ane ili tuondoe sifa hiyo katika maisha yetu. Allaah Aliyetukuka Amehimiza sana sifa hiyo pale Aliposema: “Enyi mlioamini! Mcheni Allaah na kuweni pamoja na wakweli” (9: 119). Hii ni sifa ambayo inamwingizaa sahibu wake Peponi: “…na wanaume wasemao kweli na wanawake wasemao kweli…Allaah Amewaandalia msamaha na ujira mkubwa” (33: 35).

Naye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Bila shaka, ukweli ni wema, na wema unampeleka (mtu) Peponi. Hakika uongo ni uovu, na uovu unampeleka (mtu) motoni” (Muslim).

Amesema tena: “Chungeni sana kuhusu ukweli na ikhlasi, kwani ukweli na ikhlasi inaongoza kwenye wema, na wema unaongoza Peponi” (al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na Maalik).

Ni hakika isiyopingika kuwa pindi tu unapokengeuka na kupotoka katika msimamo wa sawa utajiingiza katika matatizo. Shida ambayo mara nyengine inakuwa ni tatizo kujikomboa au unakuwa umechelewa sana katika hilo. Bila shaka yoyote pindi mwanadamu anapopuuza maagizo ya Allaah Aliyetukuka au Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ataingia katika matatizo na usumbufu. Hakika ni kuwa lile ambalo Allaah Aliyetukuka Anatuambia tufanye huwa lina maslahi nasi na lile Analotuambia tusifanye basi huwa lina madhara makubwa nasi.

Na hivyo hivyo maagizo na makatazo ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mfano mzuri katika uhai wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni Vita vya Uhud, ambapo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaangiza Maswahaba hamsini (50) wakae kwenye mlima na wasiondoke hata kukatokea nini mpaka awapatie agizo hilo. Pindi walipoona Waumini wanaokota ngawira walishuka kwenye kilima na hapo ushindi uliokuwa wazi ukageuka ikawa ni kushindwa na Maswahaba wengi kuuliwa. Hawa ni Maswahaba wakiwa pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walipata dhara hilo kubwa na zito seuze sisi.

Hivyo tunatoa nasaha kwa ndugu zetu wenye kukimbilia katika nchi za kikafiri wawe ni wenye kusema ukweli na hiyo itakuwa ni njia moja ya kufanya Da‘wah. Tusiwe sisi tunaangalia maslahi ya hapa duniani huku tukisahau au kujisahaulisha kuwa ipo siku ya kufa, kufufuliwa na kusimama mbele ya Hakimu Muadilifu, Allaah Mtukufu. Huenda ukapata madhara makubwa kwa kujulikana na hivyo kuwavunja moyo wale waliokuwa wana niya ya kuingia katika Dini wakifikiria kuwa Dini hii ni ya watu waongo. Huenda pia ukapata adhabu ukijulikana ima kulipishwa faini kubwa, kufukuzwa nchi au kufungwa gerezani.

Kwa kuwa jambo hili lishatokea ikiwa ni kwa kujua au kutojua. Ikiwa ni kwa kutojua inakuwa sahali kwani Allaah Aliyetukuka Anasema: “Toba inayokubaliwa na Allaah ni ya wale wanaofanya uovu kwa ujinga, kisha wakatubia kwa upesi. Hao ndio Allaah huipokea toba yao. Na Allaah ni Mjuzi na Mwenye hikima” ().

Toba isiyo kubaliwa ni ile ya mtu anayefanya maovu mpaka mauti yakakaribia, hapo ndipo akasema: Mimi nimetubia sasa. Hali hii ya pili inamfikisha mtu huyo pabaya sana.

Lakini katika hili swali inaonyesha raghba na azma kubwa ya dada yetu kutaka kurudi kwa Mola wake. Hiyo ndio njia ya kuwa na azma ya kutorudia tena kosa, kujuta na kurudi kwa Mola kwa kufanya mambo mema. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Hakika mema hufuta maovu. Huu ni ukumbusho kwa wanaokumbuka” (11: 114).

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mche Allaah popote ulipo, na ufuatilize jambo baya kwa jema litafuta hilo baya na utangamane na watu kwa tabia nzuri” (Ahmad, at-Tirmidhiy na ad-Daarimiy, nayo ni Hadiyth Sahihi).

Jambo ambalo unafaa ufanye sasa, wakati huu ukiwa mzima, mwenye siha na nguvu ni kufanya mambo ya kheri mengi zaidi. Jitoe katika jambo hilo la kuchukua hizo pesa kuanzia wakati huu kwa njia ambayo hawatashuku lolote wala chochote. Ikiwa hiyo akiba uko nayo basi unaweza kuitoa sadaka kwa njia moja au nyengine hasa kwa wale walioko sehemu ya nyumbani Afrika Mashariki ambao wapo katika hali mbaya. Unaweza kuwasaidia wasiojiweza kwa kulipa karo zao za shule, kusaidia masikini au waliosilimu na wako katika shida.  

Allaah Aliyetukuka kwa kuwa Anatuonea huruma sana sisi hutufutia yaliyopita, hivyo ni juu yetu kuganga yajao. Anasema: “Allaah Amekwishayafuta yaliyopita; lakini atakayefanya tena Allaah Atamuadhibu. Na Allaah ndiye Mwenye nguvu na Mwenye kuadhibu” (5: 95).

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka kwa majina Yake Matukufu Akusamehe na Akupe moyo na taufiki ya kutorudia hayo tena katika maisha yako.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share