280-Aayah Na Mafunzo: Fadhila Za Anayempa Muda Mdaiwa Au Kusamehe Deni

Aayah Na Mafunzo

Al-Baqarah

Fadhila Za Anayempa Muda Mdaiwa Au Kusamehe Deni

 

 

 

 وَإِن كَانَ ذُو عُسْرَةٍ فَنَظِرَةٌ إِلَىٰ مَيْسَرَةٍ ۚ وَأَن تَصَدَّقُوا خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿٢٨٠﴾

280. Na ikiwa (mdaiwa) ni mwenye hali ngumu, basi (mdai) angoje mpaka afarijike. Na mkifanya deni kuwa ni swadaqah basi ni kheri kwenu mkiwa mnajua.

 

 

Mafunzo:

 

 

Ubaydullaah bin ‘Abdillaah alimsikia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kutoka kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Kulikuwa na tajiri anawakopesha watu, basi akiona mtu hawezi kumlipa deni kwa hali mbaya aliyokuwa nayo anawaambia vijana wake: Msameheni huenda Allaah Atatusamehe. Basi Allaah Akamsamehe.” [Al-Bukhaariy]

 

Abuu Hurayrah amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atakayemuakhirishia mwenye usiri (wa kulipa deni) au akamsamehe, Allaah Atamfunika kivuli Siku ya Qiyaamah chini ya kivuli cha ‘Arshi Yake, Siku ambayo hakutokuwa na kivuli isipokuwa kivuli Chake.” [At-Tirmdihy]

 

Sulaymaan bin Buraydah amehadithia kwamba baba yake alisema: Nilimsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Yeyote anayempa muda mdaiwa anayekabiliwa na matatizo, basi kila siku atalipwa sawa na kutoa swadaqah.” [Ahmad]

 

Hudhayfah (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Siku ya Qiyaamah, mmoja wa waja wa Allaah ataitwa mbele Yake na Atamuuliza: Umefanya ‘amali gani kwa ajili yangu katika maisha yako? Atajibu: Ee Rabb wangu! Sikuwahi katika uhai wangu kufanya ‘amali kwa ajili Yako iliyo sawa na chembe ndogo! (Ataulizwa na atajibu) Mara tatu, kisha mara ya tatu atasema: Ee Rabb wangu! Ulinijaalia mali na nilikuwa nafanya biashara. Nilikuwa mpole, nikiwapa masharti mepesi wenye uwezo na nikiwapa muda wa kulipa wadaiwa. Allaah Atamwambia: Mimi Ndiye Mwenye haki zaidi ya kutoa masharti mepesi kwa hiyo, ingia Jannah!.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Share