Kula Dawa Kubadilisha Umbo Inafaa?

SWALI:

Ukila chakula kimewekwa madawa yaku shape mwili wako (an asana tumbo), je hiyo inakubalika katika dini ya kiislam??

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani sana kwa swali lako hili zuri. Mas-ala hii imekuwa ni tatizo kubwa kwetu tulioko Afrika Mashariki japokuwa hapo awali tatizo hii ilikuwa zaidi nchi za Kimagharibi.

Katika vyakula Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Ametuhalishia vilivyo halali na vizuri. Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) naye akatubainishia kuwa “Halali iko wazi na pia haramu ni hali hiyo hiyo, lakini baina ya hivyo viwili kuna mambo yenye shaka. Haya ya shaka hayajulikani na wengi na mwenye kuepeukana nayo, bila shaka atakuwa amehifadhi Dini na heshima yake…” (al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na Ibn Maajah).

Mbali na hiyo Hadiyth ya juu, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakika Allaah ni Mzuri na Hakubali ila zuri. Na hakika Allaah Amewaamrisha Waumini yale Aliyowaamrisha Mitume. Akasema: ‘Enyi Mitume! Kuleni vizuri na fanyeni mema’ (). Na akasema tena Allaah Aliyetukuka: ‘Enyi mlioamini! Kuleni vizuri Tulivyowaruzuku’ (2: 172)” (Muslim).

Vyakula vilivyo vizuri vinakuwa ni maslahi yetu ya afya na siha nzuri. Chakula chochote ambacho kinatiwa madawa ambayo tena mengi hayajulikani vinakuwa na madhara kwa mwili wa mwanadamu. Unapotumia tu dawa ya kuuweka mwili wako uwe na umbo zuri basi umbo hilo ili kubaki katika hali hiyo ni lazima uwe ni mwenye kutumia vyakula vyenye madawa hayo.

Hali hii itakuwa wewe ni mwenye kutumia vyakula hivyo, na utambue kuwa pindi utakapoacha basi madhara yako yatakuwa makubwa. Uislamu kwa kuwa unajali maslahi ya mwanaadamu hautaki yeye adhurike kwa njia yoyote ile. Kwa Uislamu una msingi kwa Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Haifai kudhuru wala kulipana madhara” (Maalik, Ibn Maajah na ad-Daraqutniy).

Na Allaah Aliyetukuka Ameliweka hili wazi pale Alitueleza kuhusu madhara ya vileo: “Katika hivyo mna madhara makuu na baadhi ya manufaa kwa watu, lakini madhara yake ni makubwa zaidi kuliko manufaa” (2: 219).

Hakika ni kuwa madhara ya vitu hivi ni kubwa hivyo kufanya kuwa haramu. Tutahadhari sana na kudangaywa kuhusu mambo haya kwani huenda tukadhurika na kukosa dawa na magonjwa yatatuvaa. Leo Bara Ulaya na Marekani inapiga kelele kuhusu vyakula vinavyokuzwa kwa kutumia teknojia ya jeni na kuitwa GMO’s kuwa zina madhara lakini hapo hapo teknolojia hiyo hiyo inaletwa Afrika ili kuondoa uhaba wa vyakula.

Vyakula vile vyenye rutuba ni vile vinavyokuuzwa kwa njia ya kawaida. Leo wageni wanaofika katika sehemu vyakula hivyo vinavyopatikana wanafurahi sana kwa ladha wanayoiona. Hakuna njia nzuri ya kuweka mwili wako uwezo kabambe kama kufanya mazoezi. Yapo mazoezi ya tumbo, misuli, miguu, kichwa ambayo unaweza kufanya nawe ukawa barabara kabisa. Na vyakula ni wewe kufunzwa au kununua vijitabu vinavyoeleza kuhusu lishe bora na kutizama utakuwa unakula nini na kiasi gani. Kufanya hivyo kitumbo hicho kitakuwa na umbile utakalo na madhara yatakuwa hayapo inshaAllaah.

Tukumbuke kuwa Allaah aliyetukuka Ametuambia: “Wala msijitie kwa mikono yenu katika maangamizo” (2: 195).

Kujibadilisha umbo Alilokuumba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) ni katika hila za shaytwaan ambaye hamuachi binaadamu kwa lolote ila kutaka kuwapotoa wapate ghadhabu za Mola wao, alisema shaytwaan:

((إِن يَدْعُونَ مِن دُونِهِ إِلاَّ إِنَاثًا وَإِن يَدْعُونَ إِلاَّ شَيْطَانًا مَّرِيدًا))

 

  (( لَّعَنَهُ اللّهُ وَقَالَ لَأَتَّخِذَنَّ مِنْ عِبَادِكَ نَصِيبًا مَّفْرُوضًا ((

 

 (( وَلأُضِلَّنَّهُمْ وَلأُمَنِّيَنَّهُمْ وَلآمُرَنَّهُمْ فَلَيُبَتِّكُنَّ آذَانَ الأَنْعَامِ وَلآمُرَنَّهُمْ فَلَيُغَيِّرُنَّ خَلْقَ اللّهِ وَمَن يَتَّخِذِ الشَّيْطَانَ وَلِيًّا مِّن دُونِ اللّهِ فَقَدْ خَسِرَ خُسْرَانًا مُّبِينًا ((

 

 )) يَعِدُهُمْ وَيُمَنِّيهِمْ وَمَا يَعِدُهُمُ الشَّيْطَانُ إِلاَّ غُرُورًا ))

 

 (( أُوْلَئِكَ مَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ وَلاَ يَجِدُونَ عَنْهَا مَحِيصًا ))

((Wao hawawaombi badala yake Yeye ila wanawake, wala hawamuombi ila Shaytwaan aliye asi))  

((Allaah Amemlaani. Naye Shaytwaan alisema: Kwa yakini nitawachukua sehemu maalumu katika waja Wako))   

 ((Na hakika nitawapoteza na nitawatia matamanio, na nitawaamrisha, basi watakata masikio ya wanyama, na nitawaamrisha, basi watabadili aliyo umba Allaah. Na mwenye kumfanya Shaytwaan kuwa ni mlinzi wake badala ya Allaah, basi huyo amekhasiri khasara ya dhaahiri))

 ((Anawaahidi na anawatia tamaa. Na Shaytwaan hawaahidi ila udanganyifu)) 

 ((Hao makao yao ni Jahannamu, na wala hawapati makimbilio kutoka humo))  [An-Nisaa: 117 – 121]

Kwa hiyo inakupasa kujiepusha na maouvu hayo.  

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share