Vipi Nijiokoe na Ghiyba (Kusengenya) ?

 

Vipi Nijiokoe na Ghiyba  (Kusengenya) ?

 

Alhidaaya.com

 

Swali:

 

Assalamu Alaykum,

 

Mimi ni ndugu yenu wa kiislam ambae nafuatilia makala ya alhidaaya na pia nafuatilia sana makala ya Ghibya (kusengenya) ambayo ndiyo mada inayoendelea hivi sasa. 

 

Nashukuru sana ninafaidika sana na mtandao huu wa alhidaaya na kwa kweli ninapata mafunzo mengi ndani yake. Kwa vile ninafuatilia mada hii ya Ghibya nina mashaka kidogo na ibada zangu kutokana na hii ghibya kwani ninajitahidi sana kutokusengenya kwa njia yoyote ile lakini najikuta nina kasoro bado kutokana na sababu zangu zifuatazo:-

 

Mimi ninaishi nyumba moja na mke mwenzangu na kama mnavyojua ndugu zangu wa kiislam nafsi zetu binaadam zilivyo na hasa panapokuwa na uke wenza, pamoja na jitihada zangu zote za kuepusha ugomvi na mambo mengi kati ya mimi na mke mwenzangu lakini kuna mambo ambayo katika hali halisi ya kuishi pamoja na hasa wanawake na zaidi katika hali ya uke wenza inakuwa ni vigumu kuvumilia baadhi ya mambo ambayo huenda mwenzio anafanya kwa ajili ya mume wake kama mavazi, mapishi mazuri n.k mambo haya akiyaona mwenzio katika hali ambayo yeye pengine hafikii kiwango kama kile na yakawa hayamfurahishi hali hii inasababisha kuwa na vineno vidogo vidogo kati yetu sisi wawili na zaidi akitokea mtu wa tatu ndio Hadiyth na vijineno ndipo vinapoanza. Kutokana na yote haya najiona kila nikikimbia madhambi ya ghibya na kwa vile kusengenya kuna njia nyingi kwa kweli naona sijui nifanyeje.

 

Nakuombeni ndugu waislamu wenzangu mnisaidie ndugu yenu kuhusu hili nifanyeje hapa ili niepukane nayo hii Ghibya? Kwa kumalizia tu naomba jibu la suala hili mnitumie mimi mwenyewe tu kwani ni suala langu binafsi.

 

Wabilahi tawfig,

 

Assalam aleykum. 

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Tunamshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kuona kwamba ndugu zetu mnafuatilia Makala zetu mbali mbali na kufaidika nazo hadi kujitahidi kujiokoa katika maasi mbali mbali. 

 

 

Hakika uke wenza sio jambo jepesi kulikubali mwanamke yoyote khaswa kwa mke wa mwanzo ambaye kawaida ndiye mwenye kuhisi uzito wa jambo hili. Hisia hizi ni hulka za kimaumbile ambazo hata wake za Rusuli waliliona kuwa ni jambo gumu seuze wanawake wengine wowote. Mfano ni mke wake wa mwanzo Nabiy Ibraahiym ('alayhis-salaam) Bibi Saarah ambaye alikuwa tasa hivyo mwenyewe akamtaka Ibraahiym amuoe Bibi Haajar lakini baadaye ukamjia wivu naye. Vile vile wake wa Nabiy ((Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambao kwao pia uke wenza uliwapeleka kufanya mambo kadhaa ya kumuudhi Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hadi wakateremshiwa Aayah, baadhi yake ni hizi zifuatazo: 

 

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ لِمَ تُحَرِّمُ مَا أَحَلَّ اللَّـهُ لَكَ ۖ تَبْتَغِي مَرْضَاتَ أَزْوَاجِكَ ۚ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴿١﴾قَدْ فَرَضَ اللَّـهُ لَكُمْ تَحِلَّةَ أَيْمَانِكُمْ ۚ وَاللَّـهُ مَوْلَاكُمْ ۖ وَهُوَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ﴿٢﴾وَإِذْ أَسَرَّ النَّبِيُّ إِلَىٰ بَعْضِ أَزْوَاجِهِ حَدِيثًا فَلَمَّا نَبَّأَتْ بِهِ وَأَظْهَرَهُ اللَّـهُ عَلَيْهِ عَرَّفَ بَعْضَهُ وَأَعْرَضَ عَن بَعْضٍ ۖ فَلَمَّا نَبَّأَهَا بِهِ قَالَتْ مَنْ أَنبَأَكَ هَـٰذَا ۖ قَالَ نَبَّأَنِيَ الْعَلِيمُ الْخَبِيرُ﴿٣﴾إِن تَتُوبَا إِلَى اللَّـهِ فَقَدْ صَغَتْ قُلُوبُكُمَا ۖ وَإِن تَظَاهَرَا عَلَيْهِ فَإِنَّ اللَّـهَ هُوَ مَوْلَاهُ وَجِبْرِيلُ وَصَالِحُ الْمُؤْمِنِينَ ۖ وَالْمَلَائِكَةُ بَعْدَ ذَٰلِكَ ظَهِيرٌ﴿٤﴾عَسَىٰ رَبُّهُ إِن طَلَّقَكُنَّ أَن يُبْدِلَهُ أَزْوَاجًا خَيْرًا مِّنكُنَّ مُسْلِمَاتٍ مُّؤْمِنَاتٍ قَانِتَاتٍ تَائِبَاتٍ عَابِدَاتٍ سَائِحَاتٍ ثَيِّبَاتٍ وَأَبْكَارًا﴿٥﴾

Ee Nabiy! Kwanini unaharamisha kile Alichokuhalalishia Allaah? Unataka kuwaridhisha wake zako; na Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. Allaah  Amekwishakufaridhishieni ukomboaji kwa viapo vyenu, na Allaah ni Mola wenu Naye Ndiye Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote. Na pale Nabiy alipompa mmoja wa wake zake jambo la siri, na huyo mke alipoipasha habari na Allaah Akamdhihirishia (Nabiy صلى الله عليه وآله وسلم), akataarifu baadhi yake na akaacha nyingine. Basi alipomjulisha hayo, akasema: Nani aliyekujulisha haya? Akasema: Amenijulisha Mjuzi wa yote, Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. Ikiwa nyinyi wawili mtatubia kwa Allaah (ni kheri kwenu) kwani kwa hakika nyoyo zenu zimeelemea (yanayomchukiza Nabiy صلى الله عليه وآله وسلم). Na mkisaidiana dhidi yake, basi hakika Allaah Ndiye Mlinzi Msaidizi wake na Jibriyl na Waumini wema, na zaidi ya hayo, Malaika pia watasaidia. Akikutalikini, asaa Rabb Wake Akambadilishia wake bora kuliko nyinyi; Waislamu, Waumini, watiifu na wanyenyekevu, wanaotubia, wenye kufanya ‘ibaadah, wanaofunga Swiyaam au wanaohajiri kwa ajili ya Allaah, wajane, na walio bikra. [At-Tahriym: 1-5]

 

 

Nawe dada yetu tunakuona una moyo mkubwa wa kuwa unaishi nyumba moja na mke mwenzio na juu ya hivyo kujitahidi uwezavyo kuvumulia wivu na mengineyo, kwani sio wepesi kabisa wake wenza kuishi pamoja. Hii peke yake ni dalili kwamba umeridhika na majaaliwa hayo ya Rabb wako, maana wake wengine huwa kabisa hawalikubali jambo hili la kuishi nyumba moja na mke mwenza. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Azidi kukupa subira kwa hilo na mengineyo.

 

Nasaha yetu ya kwanza ni kwamba nawe ujitahidi umshinde mke mwenzio katika kumpendezesha mume wako kwa kila njia, usikubali kushindwa kwa jambo kama hili, ila jaribu usifanye kwa kukejeli au kusababisha aina yoyote ya ugomvi na mke mwenzio. Hivyo shindana naye kwa:

 

Kumpikia maakulaat mazuri mazuri, mengi mno yamo humu AL HIDAAYA bonyeza hapa:  Mapishi

 

 

Jipambe kwa nguo nzuri na kila aina ya mapambo akuone saa zote unang'ara na kupendeza, na kunukia vizuri. Pamba chumba chako kwa kila aina ya vitu vizuri, na kukiweka maridadi saa zote.

 

 

Soma mada ifuatayo ikusaidie kupata mbinu zaidi za kumfurahisha mumeo: Jinsi Ya Kumfurahisha Mumeo

 

 

Ama kuhusu hayo anayokushinda mke mwenzio katika kumpendeza mume hadi kukufanya utake kuyaelezea ni jambo ambalo bila shaka litakuingiza katika Ghiybah, na kujipeusha nalo ni waajib. Hivyo nasaha yetu ni kwamba uongeze subira kubwa kuvumilia kunyamaza kimya kuliko kumueleze yeyote, kwani kufanya hivyo utadiriki mambo mawili makuu; Kwanza, utajiepusha na Ghiybah hivyo ni kujiepusha na adhabu zake pamoja na kuhifadhi amali zako. Pili, utapata malipo makubwa ya kuvuta subira kwani subira ina fadhila nyingi mno zilizotajwa katika Qur-aan na Sunnah, mojawapo ni malipo yasiyo na hesabu:

نَّمَا يُوَفَّى الصَّابِرُونَ أَجْرَهُم بِغَيْرِ حِسَابٍ 

Hakika wanaosubiri watalipwa kikamilifu ujira wao bila ya hesabu. [Az-Zumar: 10]

 

 

Wivu unapokufikia au maudhi, muelekee Rabb wako na kumuomba na kumshtakia badala ya rafiki kwani rafiki leo unaye kesho huenda akageuka akakutangazia siri zako unazompa.

 

 

Vile vile huenda hayo unayomsengenya mke mwenzio yakamfikia mumeo, naye akaudhika nawe na kuzidi kuona upungufu wako na hapo ndipo utakapokosa mapenzi zaidi ya mume na kuzidi kuona uzito wa hali yako. Na wakati uko katika subira, tumia wakati wako kwa kuongeza ibada mbali mbali kama kusoma Qur-aan ambayo ni poza ya kila baya, fanya dhikr nyingi, sikiliza mawaidha, n.k., yote haya yatakuburudisha na mwisho utaridhika nafsi yako kuwa umetenda mema badala ya maovu ya Ghiybah.

 

 

Njia nyingine muhimu ya kukuondoshea uzito huo ni kuleta Adhkaar za asubuhi na jioni ambazo zimo katika kitabu cha Hiswnul-Muslim, tunakuwekea hapa viungo vyake:

 

Hiswnul-Muslim: Du’aa Na Adhkaar Kusoma Na Kwa Kusikiliza (Toleo Lilohaririwa)

 

027-Hiswnul-Muslim: Nyiradi Za Asubuhi Na Jioni

 

 

Vile vile soma du'aa ifuatayo kutoka katika Qur-aan:
 

رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ﴿١٠﴾

Rabb wetu! Tughufurie na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa iymaan na wala Usijaalie katika nyoyo zetu mafundo ya chuki kwa wale walioamini; Rabb wetu! Hakika Wewe ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu. [Al-Hashr: 10]

 

Faida nyingine ya kuweza kuvumilia yote hayo, ni mwishowe pia kupata ridhaa ya mumeo ambaye ni mojawapo ya sababu ya wewe kuingia peponi ikiwa utamtii kwa yale mema na ya halali. 

 

 

Tunatumai kwa nasaha hizi In shaa Allaah utaweza kujiepusha na maovu ya Ghiybah na tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akufanyie wepesi, Akupe subira na Aridhike na wewe.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share