Naingiliwa Kwa Kitendo Cha Ndoa Na Majini

 

 

SWALI:

asalaam aleikum warahmatullahi wabarakatu.

Kama kilivyo kichwa cha habari hapo juu ndugu zangu naomba munisaidie na jibu la hili swali langu. Toka niolewe inapata miaka 18 lakini daima napata hizi ndoto na nahisi pia kuwa daima kuna mtu analala na mimi wanaume na wanawake pia hata sijui nifanyeje. Nimemuhadithia mume wangu yote haya na yeye kanambia nizidishe ibada lakini hakuna faida. Bado haya yanatokea. Naomba munipe nasiha nini la kufanya.

 Asanteni sana

 

 



JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani dada yetu kwa swali lako hilo muhimu kuhusu mas-ala hayo uliyoyataja hapo juu. Tunatumai kuwa kwa nasaha na majibu yetu yatakusaidia katika kukuondolea shida hiyo ya muda mrefu sana. Tufahamu kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Allaah Hakuteremsha ugonjwa isipokuwa Ameweka na dawa yake”.

Hili ni jambo hutokea kwa wanaume na pia wanawake kwa sababu moja au nyingine. Kuna wakati mwanamume atajihisi kuwa anaingiliwa na mwanamke katika tendo la ndoa na wakati mwingine wanawake hupata hisia kama hizo kwa kuingiliwa kimwili na mtu mwengine ambaye hamuoni. Kwa hili inafaa sisi tujihifadhi na kuchukua kinga ambazo tumepatiwa na Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika hilo ili tusiwe ni wenye kupata mambo hayo.

Du’aa katika hili ni usaidizi mkubwa sana kwani mara nyingi huwa tunaingia sehemu ambazo ni mapito au makazi ya majini au mashetani. Hasa chooni, hivyo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatufundisha Du’aa ifuatayo tunapoingia humo: Bismillahi Allaahumma inniy A‘udhubika minal khubuthi wal khabaa’ith (Kwa jina Allaah! Ewe Allaah! Najilinda Kwako kutokana na mashetani wa kiume na wa kike)” (al-Bukhaariy na Muslim).

Na unapotoka unatakiwa useme: “Ghufraanaka – Nakuomba msamaha” (Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na Ibn Maajah).

Ipo pia Du’aa ya kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) pindi mume na mke wanapokutana katika tendo la ndoa. Kufanya hivyo kunamlinda mtoto asiwe ni mwenye kukumbwa na jinni kama alivyotuelezea Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth ya al-Bukhaariy.

Na hivyo hivyo kipo kisomo cha Qur-aan pamoja na Du’aa alizotufundisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambazo zinamlinda mja na wasiwasi au kuchezewa na shetani. Mojowapo ni zile Du’aa za kumfukuza shetani na za kuondoa wasiwasi wake. Linapokutokea hilo basi unafaa ufanye yafuatayo pindi unapohisi hilo linakutokea:

-      Kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akuhifadhi nae (Abu Daawuud na at-Tirmidhiy). Huko ni kusema A‘udhu Billahi minash shaytwaanir Rajiim.

-      Kumuadhinia (al-Bukhaariy na Muslim).

-     Kusoma nyiradi zilizopokewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kusoma Qur-aan.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuhimiza sana kusoma Suratul Baqarah na hasa zile ayah kumi ambazo ni kinga kubwa sana dhidi ya shetani pamoja na wasiwasi wake. Hizi ni 2: 1 – 5, 255 – 257 na 284 – 286. Pia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amehimiza tuwe ni wenye kusoma Suratul Ikhlaas, al-Falaq na an-Naas mara tatu tatu asubuhi na jioni na wakati wa kulala. Zote hizi ni kinga kwa Muislamu dhidi ya viumbe hao wasioonekana. Hii ni njia ya haraka ya kupata utulivu na nafuu kwa maradhi hayo.

Pia kinga iliyo muhimu zaidi na imejaribiwa na wengi na kuleta manufaa makubwa ya kuponyesha maradhi kama hayo ya jini n.k, ni kusoma Adhkaar (nyiradi) za asubuhi na jioni ambazo zimo katika kitabu cha Hiswnul Muslim tunachokuwekea kiungo chake chini. Lakini aghlabu watu huwa wanadharau na hawafuati kudumisha hizi Adhkaar ambazo hakika ni kinga na ponyesho kubwa la matatizo kama haya. Hivyo tunakupa nasaha ufululize kuzisoma bila ya kuacha hata siku moja na Insha Allaah kwa uwezo wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  itakuwa ni dawa yako, na tutafurahi sana utakapotujulisha kufanikiwa kwako katika hili.

Pia hakikisha unatawadha kabla hujalala na kusoma Du’aa za kulalalia.

Njia nyingine pia ni kwenda kwa Shaykh ambaye ni mcha Mngu na mwenye kufuata Sunnah vilivyo na mjuzi katika mas-ala ya kutoa majini kutumia Qur-aan na Sunnah. Tufahamu kuwa haifai kwetu tukiwa na shida kama hizo kwenda kwa waganga au wenye kuangalilia ili watoe majini kwani njia hizo ni kufuru.

Ingia katika kiungo hichi, utapata Du’aa mbalimbali zitakazokusaidia inshaAllaah.

HISWNUL MUSLIM

Nasi hapa tunakutakia kila la kheri ili upate dawa ya kudumu katika tatizo lako hilo. Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akuondoshee shida hiyo na Akuzidishie Imani ya kuweza kumtambua na kumuabudu Yeye peke Yake.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share