Kisa Cha Nabiy Swaalih (عليه السلام) - 2

 

 

Kisa Cha Nabiy Swaalih ('alayhis-salaam)

 

Sehemu Ya 2

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Muujiza Wa Ngamia:

 

 

Wafasiri wa Qur-aan wamesema kwamba siku moja watu wa Thamuwd walikusanyika katika baraza lao akaja   Nabiy Swaalih (‘alayhis-salaam) kuwalingania katika Tawhiyd ya Allaah (Kumpwekesha Allaah), na akawapa mawaidha na kuwaonya. Wakadai dalili kuhusu ujumbe wake aliokuja nao kama kweli umetoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).        

 

 

Wakamwambia: “Ewe Swaalih! Tutolee katika jabali lile (wakaashiria jabali lililokuwepo) ngamia wa kike, ambaye ana mimba ya miezi kumi.” (Na wakataja sifa nyingine kadha)  

 

 

Nabiy Swaalih ('alayhis-salaam) akawauliza:  "Je, mkiletewa hiyo miujiza mliyoomba na mliyotaka iwe vile vile, mtaniamini na kuamini  ujumbe niliotumwa nao kwenu?" Wakajibu: "Ndio tutakuamini na kukusadiki yote utakayotuambia."  Nabiy Swaalih ('alayhis-salaam) akachukua ahadi hiyo kwa watu wake kisha akamuelekea Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kumuomba awaletee miujiza hiyo waliyotaka.

 

 

Kama tunavyojua na kuamini kuwa hakuna jambo lolote linalomshinda   Allaah ('Azza wa Jalla) kulifanya kama Anavyosema Mwenyewe:

 

إِنَّمَا أَمْرُهُ إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَن يَقُولَ لَهُ كُن فَيَكُونُ ﴿٨٢﴾

Hakika amri Yake Anapotaka chochote hukiambia: Kun! (Kuwa), nacho huwa. [Yaasiyn: 82]

 

 

 

Basi watu wa Nabiy Swaalihi ('alayhis-salaam) wakakusanyika mbele ya jabali hilo na kusubiri waone kama ombi lao litatimizwa.  Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Aliamrisha jabali lipasuke na akatoka ngamia mwenye sifa zile zile walizozitaka; ngamia mwanamke, mwenye mimba ya miezi kumi, mweupe.  Akatokeza huyo ngamia kutoka kwenye hilo jabali akipita mbele yao wakimtazama.

 

Ulikuwa ni muujiza mkubwa wa kustaajabisha ambao ni  dalili za dhahiri ya uwezo wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).   Lakini juu ya hivyo wengi katika watu hao wa Nabiy Swaalih ('alayhis-salaam) hawakuamini!

 

Hali ya watu wa Nabiy Swaalih ('alayhis-salaam) imetajwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika Aayah zifuatazo:

 

قَالَ الْمَلَأُ الَّذِينَ اسْتَكْبَرُوا مِن قَوْمِهِ لِلَّذِينَ اسْتُضْعِفُوا لِمَنْ آمَنَ مِنْهُمْ أَتَعْلَمُونَ أَنَّ صَالِحًا مُّرْسَلٌ مِّن رَّبِّهِ ۚ قَالُوا إِنَّا بِمَا أُرْسِلَ بِهِ مُؤْمِنُونَ ﴿٧٥﴾

Wakasema wakuu waliotakabari katika kaumu yake kuwaambia wale waliokandamizwa ambao walioamini miongoni mwao: Je, mnajua kwamba Swaalih ametumwa kutoka kwa Rabb wake?  Wakasema: Hakika sisi kwa yale aliyotumwa nayo ni wenye kuyaamini. 

 

قَالَ الَّذِينَ اسْتَكْبَرُوا إِنَّا بِالَّذِي آمَنتُم بِهِ كَافِرُونَ ﴿٧٦﴾

Wakasema wale waliotakabari: Hakika sisi kwa yale mliyoyaamini tunayakanusha. [Al-A’raaf: 75-76]

 

Ngamia huyo wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   aliletwa na shuruti zake walizoombwa watu wa Nabiy Swaalih ('alayhis-salaam) wazitimize nazo ni: wamwache huru wala wasimdhuru, wala wasimuuwe kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَإِلَىٰ ثَمُودَ أَخَاهُمْ صَالِحًا ۗ قَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ ۖ قَدْ جَاءَتْكُم بَيِّنَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ ۖ هَـٰذِهِ نَاقَةُ اللَّـهِ لَكُمْ آيَةً ۖ فَذَرُوهَا تَأْكُلْ فِي أَرْضِ اللَّـهِ ۖ وَلَا تَمَسُّوهَا بِسُوءٍ فَيَأْخُذَكُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٧٣﴾

Na kwa Thamuwd (Tuliwapelekea) kaka yao Swaalih. Akasema: Enyi kaumu yangu! Mwabuduni Allaah, hamna mwabudiwa wa haki ghairi Yake. Kwa yakini imekujieni hoja bayana kutoka kwa Rabb wenu. Huyu ngamia jike wa Allaah ni Aayah (ishara, dalili) kwenu. Basi muacheni ale katika ardhi ya Allaah, na wala msimguse kwa uovu isije ikakuchukueni adhabu iumizayo. [Al-A’raaf: 73]

Na wakapewa mtihani mwengine ambao ulikuwa ni sharti la kufanya zamu ya kunywa maji baina yao na baina ya ngamia huyo. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

إِنَّا مُرْسِلُو النَّاقَةِ فِتْنَةً لَّهُمْ فَارْتَقِبْهُمْ وَاصْطَبِرْ ﴿٢٧﴾

Hakika Sisi Tutawapelekea ngamia jike awe jaribio kwao, basi (ee Nabiy Swaalih   عليه السلام) watazame na vuta subira.

وَنَبِّئْهُمْ أَنَّ الْمَاءَ قِسْمَةٌ بَيْنَهُمْ ۖ كُلُّ شِرْبٍ مُّحْتَضَرٌ ﴿٢٨﴾

Na wajulishe kwamba maji ni mgawanyo baina yao (ngamia na wao), kila sehemu ya maji itahudhuriwa (kwa zamu). [Al-Qamar: 27]

 

 

Alikuwa ni ngamia mwenye baraka nyingi, maziwa yake yaliyokamuliwa siku moja yaliwatosheleza watu wa mji mzima! Alikuwa akilala mahali ambapo wanyama wengine walikuwa hawapakaribii pahali hapo. Kwa hiyo walijua kuwa huyo hakuwa ngamia wa kawaida, bali alikuwa ni ishara kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).   Wakatakiwa wamwache atembee anapotaka katika mji huo, ale anavyotaka, na zamu ya kunywa maji iwe siku moja anywe ngamia na siku ya pili wanywe wao. Na siku ya zamu ya watu wa Thamuwd, walijichotea maji ya kutosha na kuyaweka ili kuyatumia kwa haja zao ya siku ya pili. Na ile siku ya zamu ya ngamia, watu wa Thamwud  walikuwa wakinywa maziwa yake huyo ngamia. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

  

 قَالَ هَـٰذِهِ نَاقَةٌ لَّهَا شِرْبٌ وَلَكُمْ شِرْبُ يَوْمٍ مَّعْلُومٍ ﴿١٥٥﴾

Akasema: Huyu hapa ngamia jike ana zamu ya kinywaji, nanyi mna zamu ya kinywaji siku maalumu. [Ash- Shu’araa: 155]

 

 

Tena wakaonywa kuwa wasimdhuru wasije kupata adhabu.

 

 

وَلَا تَمَسُّوهَا بِسُوءٍ فَيَأْخُذَكُمْ عَذَابُ يَوْمٍ عَظِيمٍ ﴿١٥٦﴾

Na wala msimguse kwa uovu, ikaja kukuchukueni adhabu ya Siku adhimu. [Ash-Shua’raa: 156]

 

Na pia katika Suwrah nyengine:

 

وَيَا قَوْمِ هَـٰذِهِ نَاقَةُ اللَّـهِ لَكُمْ آيَةً فَذَرُوهَا تَأْكُلْ فِي أَرْضِ اللَّـهِ وَلَا تَمَسُّوهَا بِسُوءٍ فَيَأْخُذَكُمْ عَذَابٌ قَرِيبٌ﴿٦٤﴾

  Enyi kaumu yangu! Huyu ni ngamia jike wa Allaah, ni Aayah (miujiza, ishara) kwenu, basi mwacheni ale katika ardhi ya Allaah, na wala msimguse kwa uovu ikakupateni adhabu iliyo karibu. [Huwd: 64]

 

Lakini hawakutaka kutii amri ya mwanzo ya kuacha kuabudu masanamu wala hawakutaka kutii amri ya kumtunza huyo ngamia, bali walimuua na wakakusudia kumua pia Nabiy Swaalih ('alayhis-salaam). Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَمَا مَنَعَنَا أَن نُّرْسِلَ بِالْآيَاتِ إِلَّا أَن كَذَّبَ بِهَا الْأَوَّلُونَ ۚ وَآتَيْنَا ثَمُودَ النَّاقَةَ مُبْصِرَةً فَظَلَمُوا بِهَا ۚ وَمَا نُرْسِلُ بِالْآيَاتِ إِلَّا تَخْوِيفًا ﴿٥٩﴾

Na hakuna kinachotuzuia kuleta Aayaat (muujiza) isipokuwa ni kuwa watu wa awali waliikadhibisha. Na Tuliwapa kina Thamuwd ngamia jike kuwa dalili dhahiri lakini wakamdhulumu. Na Hatupeleki Aayaat (miujiza, maonyo) isipokuwa kwa ajili ya kukhofisha. [Al-Israa: 59]

 

Kwa maana:  walikanusha na wakamdhuru.  

 

Basi haukupita muda, na hawakuweza  kustahmili hali hiyo ya ngamia na masharti waliyopewa. Na chuki  zao juu ya Nabiy Swaalih ('alayhis-salaam) wakazigeuza kumchukia ngamia. Wakuu katika watu wa Thamwud  wakakutana kupanga njama ya  kumuua ngamia ili wapate uhuru wa maji yao. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

  

فَعَقَرُوا النَّاقَةَ وَعَتَوْا عَنْ أَمْرِ رَبِّهِمْ وَقَالُوا يَا صَالِحُ ائْتِنَا بِمَا تَعِدُنَا إِن كُنتَ مِنَ الْمُرْسَلِينَ ﴿٧٧﴾

Wakamuua yule ngamia jike na wakaasi amri ya Rabb wao; na wakasema: Ee Swaalih, tuletee hayo unayotutishia ukiwa ni miongoni mwa Rusuli. [Al-A’raaf: 77]

 

Kisha wakamhimiza Nabiy Swaalih ('alayhis-salaam) awaletee adhabu aliyowaonya nayo.  

 

Maasi yao yakwa ni kuhalifu amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli Wake kwa kumuua ngamia huyo. Na pia kufanya istihizai na kuhimiza adhabu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) iwateremkie.

 

 

Njama Za Kumuua Ngamia:

 

 

Walipopanga njama za kumuua ngami wa Allaah, walitafuta  usaidizi kutoka kwa  mwanamke Swaduwq bin Mahya aliyekuwa tajiri na ambaye alitokana na kabila la heshima   kabisa.    Akajitolea kujiuza kwa kijana aliyeitwa Masra'i ibn Mahraj kwa sharti amkate miguu ngamia. Mwanamke mwengine mtu mzima aliyeitwa ‘Aniza, alijitolea kumuuza mtoto wake wa kike kwa kijana aliyeitwa Qudaar ibn Saluf kwa sharti amuue ngamia. Vijana hao wawili walipata tamaa kwa hayo waliyoahidiwa wakatoka kutafuta watu wengine saba  kuwasaidia kufanya kazi hiyo. Vijana hao wawili wakaungana na wengine saba wakawa jumla ni watu tisa.

 

 

Wakawa wanamfuatilia ngamia na kumvizia, wakitazama nyendo zake zote. Alipokuja ngamia kunywa maji katika kisima, Masra'i akamdunga katika mguu wake kwa mshale. Ngamia aljaribu kukimbia lakini alishindwa kwani mshale ulishamwingia katika mguu na kumjeruhi. Qudaar akamfuata ngamia na kumdunga mshale katika mguu mwengine. Ngamia akaanguka chini, na kisha akamchoma na upanga.

 

Kauli za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَكَانَ فِي الْمَدِينَةِ تِسْعَةُ رَهْطٍ يُفْسِدُونَ فِي الْأَرْضِ وَلَا يُصْلِحُونَ ﴿٤٨﴾

Na kulikuweko katika mji ule watu tisa wakifanya ufisadi katika ardhi na wala hawatengenei.

 

قَالُوا تَقَاسَمُوا بِاللَّـهِ لَنُبَيِّتَنَّهُ وَأَهْلَهُ ثُمَّ لَنَقُولَنَّ لِوَلِيِّهِ مَا شَهِدْنَا مَهْلِكَ أَهْلِهِ وَإِنَّا لَصَادِقُونَ ﴿٤٩﴾

Wakasema: Apishaneni kwa Jina la Allaah kwamba tutamhujumu (Swaalih) kwa siri usiku na ahli yake, kisha tutasema kwa jamaa yake wa karibu: Hatukushuhudia maangamizi ya ahli yake; nasi hakika ni wa kweli.

 

وَمَكَرُوا مَكْرًا وَمَكَرْنَا مَكْرًا وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ ﴿٥٠﴾

Wakapanga njama Nasi Tukapanga mipango ya kuvurumisha njama nao huku hawatambui.   [An-Naml: 48-50]

 

 

Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

فَنَادَوْا صَاحِبَهُمْ فَتَعَاطَىٰ فَعَقَرَ ﴿٢٩﴾

Wakamwita swahibu wao, akakamata (upanga) akaua (ngamia). [Al-Qamar: 29]

 

Na Hadiyth ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu mtu muovu kabisa:

 

 عن عمار بن ياسر، قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم لعلي: "ألا أحدثك بأشقى الناس"؟ قال: بلى، قال: "رجلان: أحدهما أحيمر ثمود الذي عقر الناقة، والذي يضربك يا علي على هذا ـ يعني قرنه ـ حتى تبتل منه هذه ـ يعني لحيته    رواه ابن أبي حاتم

Kutoka kwa 'Ammaar bin Yaasir ambaye amesema:  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema (kumwambia 'Aliy)  ((Je, nikujulishe ni yupi mtu muovu kabisa?))  Akasema ndio: Akasema: ((Watu wawili; mmoja ni mpiga chuku wa Thamuwd aliyemuua ngamia na mwengine ni yule atakayekupiga ee 'Aliy hapa juu (yaani kichwani kwake) mpaka hizi (ndevu) zirowe damu))     [Imesimuliwa na ibn Haatim]

 

Maelezo zaidi yamo katika Kauli za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwenye Suwrah mbali mbali kuhusu kisa cha Nabiy Swaalih ('alayhis-salaam):  

 

كَذَّبَتْ ثَمُودُ بِطَغْوَاهَا ﴿١١﴾

Kina Thamuwd walikadhibisha (Rasuli wao) kwa upindukaji mipaka ya kuasi kwao.

 

إِذِ انبَعَثَ أَشْقَاهَا ﴿١٢﴾

Pale alipochomoka haraka muovu wao mkuu.

 

فَقَالَ لَهُمْ رَسُولُ اللَّـهِ نَاقَةَ اللَّـهِ وَسُقْيَاهَا ﴿١٣﴾

Rasuli wa Allaah (Swaalih عليه السلام) aliwaambia: (Msimdhuru) Ngamia jike wa Allaah, na kinywaji chake.

 

فَكَذَّبُوهُ فَعَقَرُوهَا فَدَمْدَمَ عَلَيْهِمْ رَبُّهُم بِذَنبِهِمْ فَسَوَّاهَا ﴿١٤﴾

Lakini walimkadhibisha na wakamuua; basi Rabb wao Akawaangamiza  kwa sababu ya dhambi zao, na Akayafanya mateketezi yao sawasawa kwa wote.

 

وَلَا يَخَافُ عُقْبَاهَا ﴿١٥﴾

Na wala (Allaah) Hakhofu hatima yake. [Ash-Shams: 11-15]

 

Na pia:

 

 وَإِلَىٰ ثَمُودَ أَخَاهُمْ صَالِحًا ۗ قَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ ۖ قَدْ جَاءَتْكُم بَيِّنَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ ۖ هَـٰذِهِ نَاقَةُ اللَّـهِ لَكُمْ آيَةً ۖ فَذَرُوهَا تَأْكُلْ فِي أَرْضِ اللَّـهِ ۖ وَلَا تَمَسُّوهَا بِسُوءٍ فَيَأْخُذَكُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٧٣﴾

Na kwa Thamuwd (Tuliwapelekea) kaka yao Swaalih. Akasema: Enyi kaumu yangu! Mwabuduni Allaah, hamna mwabudiwa wa haki ghairi Yake. Kwa yakini imekujieni hoja bayana kutoka kwa Rabb wenu. Huyu ngamia jike wa Allaah ni Aayah (ishara, dalili) kwenu. Basi muacheni ale katika ardhi ya Allaah, na wala msimguse kwa uovu isije ikakuchukueni adhabu iumizayo.

 

وَاذْكُرُوا إِذْ جَعَلَكُمْ خُلَفَاءَ مِن بَعْدِ عَادٍ وَبَوَّأَكُمْ فِي الْأَرْضِ تَتَّخِذُونَ مِن سُهُولِهَا قُصُورًا وَتَنْحِتُونَ الْجِبَالَ بُيُوتًا ۖ فَاذْكُرُوا آلَاءَ اللَّـهِ وَلَا تَعْثَوْا فِي الْأَرْضِ مُفْسِدِينَ ﴿٧٤﴾

Na kumbukeni Alipokujaalieni warithi baada ya ‘Aad, Akakufanyieni makazi katika ardhi mnachukua katika nyanda zake tambarare majumba ya fakhari na mnachonga majumba kutokana na majabali. Basi kumbukeni neema nyingi za Allaah na wala msifanye vitendo vya hujuma katika ardhi mkifisidi.

 

 

قَالَ الْمَلَأُ الَّذِينَ اسْتَكْبَرُوا مِن قَوْمِهِ لِلَّذِينَ اسْتُضْعِفُوا لِمَنْ آمَنَ مِنْهُمْ أَتَعْلَمُونَ أَنَّ صَالِحًا مُّرْسَلٌ مِّن رَّبِّهِ ۚ قَالُوا إِنَّا بِمَا أُرْسِلَ بِهِ مُؤْمِنُونَ ﴿٧٥﴾

Wakasema wakuu waliotakabari katika kaumu yake kuwaambia wale waliokandamizwa ambao walioamini miongoni mwao: Je, mnajua kwamba Swaalih ametumwa kutoka kwa Rabb wake?  Wakasema: Hakika sisi kwa yale aliyotumwa nayo ni wenye kuyaamini.

 

قَالَ الَّذِينَ اسْتَكْبَرُوا إِنَّا بِالَّذِي آمَنتُم بِهِ كَافِرُونَ ﴿٧٦﴾

Wakasema wale waliotakabari: Hakika sisi kwa yale mliyoyaamini tunayakanusha.

 

 

فَعَقَرُوا النَّاقَةَ وَعَتَوْا عَنْ أَمْرِ رَبِّهِمْ وَقَالُوا يَا صَالِحُ ائْتِنَا بِمَا تَعِدُنَا إِن كُنتَ مِنَ الْمُرْسَلِينَ ﴿٧٧﴾

Wakamuua yule ngamia jike na wakaasi amri ya Rabb wao; na wakasema: Ee Swaalih, tuletee hayo unayotutishia ukiwa ni miongoni mwa Rusuli

 

فَأَخَذَتْهُمُ الرَّجْفَةُ فَأَصْبَحُوا فِي دَارِهِمْ جَاثِمِينَ ﴿٧٨﴾

Basi ikawachukua tetemeko la ardhi wakawa majumbani mwao wenye kuanguka kifudifudi (wamekufa).

 

فَتَوَلَّىٰ عَنْهُمْ وَقَالَ يَا قَوْمِ لَقَدْ أَبْلَغْتُكُمْ رِسَالَةَ رَبِّي وَنَصَحْتُ لَكُمْ وَلَـٰكِن لَّا تُحِبُّونَ النَّاصِحِينَ ﴿٧٩﴾

 (Swaalih) akajitenga nao na akasema: Enyi kaumu yangu! Kwa yakini nilishakubalighishieni risala ya Rabb wangu na nilikunasihini, lakini nyinyi hamuwapendi wenye kunasihi. [Al-A’raaf: 73-79]

 

Wauaji hao wakapongezwa kwa uhodari wao  wa kumuua ngamia, wakashangiliwa kwa nyimbo na mashairi ya kuwasifu uhodari wao, na wakamkejeli Nabiy Swaalih ('alayhis-salaam) lakini akawatahadharisha adhabu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na hali ikawa kama ifuatavyo:

 

فَعَقَرُوهَا فَقَالَ تَمَتَّعُوا فِي دَارِكُمْ ثَلَاثَةَ أَيَّامٍ ۖ ذَٰلِكَ وَعْدٌ غَيْرُ مَكْذُوبٍ﴿٦٥﴾

Basi wakamuua; (Swaalih) akasema: Stareheni majumbani mwenu siku tatu. Hiyo ni ahadi isiyo ya uongo.

 

 

فَلَمَّا جَاءَ أَمْرُنَا نَجَّيْنَا صَالِحًا وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ بِرَحْمَةٍ مِّنَّا وَمِنْ خِزْيِ يَوْمِئِذٍ ۗ إِنَّ رَبَّكَ هُوَ الْقَوِيُّ الْعَزِيزُ﴿٦٦﴾

Basi ilipokuja amri Yetu, Tulimuokoa Swaalih na wale walioamini pamoja naye kwa rahmah kutoka Kwetu, na kutokana na hizaya ya Siku hiyo. Hakika Rabb wako Yeye Ndiye Mwenye nguvu, Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika.

 

وَأَخَذَ الَّذِينَ ظَلَمُوا الصَّيْحَةُ فَأَصْبَحُوا فِي دِيَارِهِمْ جَاثِمِينَ﴿٦٧﴾

Na wale waliodhulumu uliwachukuwa ukelele angamizi, wakapambazukiwa wameanguka kifudifudi majumbani mwao (wamekufa).

 

كَأَن لَّمْ يَغْنَوْا فِيهَا ۗ أَلَا إِنَّ ثَمُودَ كَفَرُوا رَبَّهُمْ ۗ أَلَا بُعْدًا لِّثَمُودَ﴿٦٨﴾

Kama kwamba hawakuishi wakineemeka humo. Tanabahi! Hakika kina Thamuwd walimkufuru Rabb wao. Tanabahi! Wameangamiziliwa mbali kina Thamuwd. [Huwd: 65-68]

 

 

Maelezo zaidi ya kisa hiki katika kauli za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) zifuatazo:

 

وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا إِلَىٰ ثَمُودَ أَخَاهُمْ صَالِحًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ فَإِذَا هُمْ فَرِيقَانِ يَخْتَصِمُونَ ﴿٤٥﴾

Na kwa yakini Tuliwapelekea kina Thamuwd ndugu yao Swaalih kwamba: Mwabuduni Allaah. Tahamaki wakawa makundi mawili yanayokhasimiana.

 

قَالَ يَا قَوْمِ لِمَ تَسْتَعْجِلُونَ بِالسَّيِّئَةِ قَبْلَ الْحَسَنَةِ ۖ لَوْلَا تَسْتَغْفِرُونَ اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ﴿٤٦﴾

 (Swaalih) Akasema: Enyi kaumu yangu! Kwa nini mnahimiza uovu kabla ya mema; kwa nini msimwombe Allaah maghfirah ili huenda mkarehemewa?

 

 

قَالُوا اطَّيَّرْنَا بِكَ وَبِمَن مَّعَكَ ۚ قَالَ طَائِرُكُمْ عِندَ اللَّـهِ ۖ بَلْ أَنتُمْ قَوْمٌ تُفْتَنُونَ ﴿٤٧﴾

Wakasema: Tumepata nuksi kwa sababu yako na kwa wale walio pamoja nawe. (Swaalih) Akasema: Nuksi yenu iko kwa Allaah. Bali nyinyi ni watu mliojaribiwa.

وَكَانَ فِي الْمَدِينَةِ تِسْعَةُ رَهْطٍ يُفْسِدُونَ فِي الْأَرْضِ وَلَا يُصْلِحُونَ ﴿٤٨﴾

Na kulikuweko katika mji ule watu tisa wakifanya ufisadi katika ardhi na wala hawatengenei.

 

 

قَالُوا تَقَاسَمُوا بِاللَّـهِ لَنُبَيِّتَنَّهُ وَأَهْلَهُ ثُمَّ لَنَقُولَنَّ لِوَلِيِّهِ مَا شَهِدْنَا مَهْلِكَ أَهْلِهِ وَإِنَّا لَصَادِقُونَ ﴿٤٩﴾

Wakasema: Apishaneni kwa Jina la Allaah kwamba tutamhujumu (Swaalih) kwa siri usiku na ahli yake, kisha tutasema kwa jamaa yake wa karibu: Hatukushuhudia maangamizi ya ahli yake; nasi hakika ni wa kweli.

 

وَمَكَرُوا مَكْرًا وَمَكَرْنَا مَكْرًا وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ ﴿٥٠﴾

Wakapanga njama Nasi Tukapanga mipango ya kuvurumisha njama nao huku hawatambui.

 

فَانظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ مَكْرِهِمْ أَنَّا دَمَّرْنَاهُمْ وَقَوْمَهُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٥١﴾

Basi tazama vipi ilikuwa hatima ya njama zao, kwamba Tuliwadamirisha na watu wao wote.

 

فَتِلْكَ بُيُوتُهُمْ خَاوِيَةً بِمَا ظَلَمُوا ۗ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لِّقَوْمٍ يَعْلَمُونَ ﴿٥٢﴾

Basi hizo ni nyumba ni magofu kwa sababu ya yale waliyodhulumu. Hakika katika hayo kuna Aayah (ishara, zingatio, funzo n.k.) kwa watu wanaojua. [an-Naml: 45-52]

 

 

…./3

 

  

 

 

 

 

Share