Kisa Cha Nabiy Ibraahiym (عليه السلام) - 4

 

Imeandikwa na www.alhidaaya.com

 

KUJENGA KA'ABAH

 

Allaah سبحانه وتعالى  Akamuamrisha Ibraahiym عليه السلام ajenge Ka'abah.  Ibraahiym عليه السلام na Ismaa'iyl عليه السلام wakapandisha msingi wa nyumba (yaani Ka'abah). Ismaa'iyl عليه السلام akawa analeta mawe huku Ibraahiym عليه السلام anajenga.  Kuta za nyumba ziliponyanyuka juu, Ismaa'iyl عليه السلام alileta jiwe na kumpa Ibraahiym عليه السلام ili asimamie kuendelea kujenga huku Ismaa'iyl عليه السلام anamletea mawe. 

Ibraahiym عليه السلام alikuwa akisimama juu ya jiwe hilo na kila alipomaliza kujenga upande mmoja alisogea upande mwingine kumalizia kujenga Ka'abah.

Jiwe hilo liliweka alama ya miguu yake Ibraahiym عليه السلام.  Alipomaliza kujenga aliliweka jiwe karibu na ukuta wa Ka'abah na hapo ndipo mahali lilipokuwa miaka yote hiyo hadi ilipofika zama za ukhalifa wa 'Umar رضي الله عنه ndiye aliyelisogeza kutoka kuta za Ka'abah. 'Umar  رضي الله عنه ni mmoja wa wawili ambao Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema:

((اقتدوا باللَّذَين من بعدي أبي بكر وعمر

((Wafuateni watakaokuwa baada yangu, Abu Bakar na 'Umar)) [Tuhfat Al-Ahwadhiy: 569]

Na hii ndio  sehemu inayoitwa  'Maqaam Ibraahiym' (Kisimamo cha Ibraahiym) ambako anatakiwa mwenye kufanya Hajj au 'Umrah aswali Raka'ah mbili baada ya kufanya twawwaaf.

Na amri ya kuswali Raka'ah mbili ilikuwa ni kutoka kwa Allaah سبحانه وتعالى kwa sababu ya 'Umar ibnul-Khatwaab رضي الله عنه .

Ibn Abi Haatim ameripoti kuwa Jaabir alipokuwa akisimulia Hajj ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  amesema: "Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alipofanya Twawwaaf, 'Umar alimuuliza: "Hii ndio Maqaam ya baba yetu?" akasema: "Ndio". 'Umar akasema: "Je, tuifanye sehemu ya kuswalia?". Ikawa ndio sababu ya Allaah سبحانه وتعالى Kuteremsha aya hii:

   ((وَاتَّخِذُواْ مِن مَّقَامِ إِبْرَاهِيمَ مُصَلًّى))

((Na alipokuwa akisimama Ibraahiym pafanyeni pawe pa kuswalia)) [Al-Baqarah:125]

 

UTUKUFU WA KA'ABA

Mahali pa salama na amani

Anasema Allaah سبحانه وتعالى  kuhusu utukufu wa Ka'abah:

((وَإِذْ جَعَلْنَا الْبَيْتَ مَثَابَةً لِّلنَّاسِ وَأَمْناً وَاتَّخِذُواْ مِن مَّقَامِ إِبْرَاهِيمَ مُصَلًّى وَعَهِدْنَا إِلَى إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ أَن طَهِّرَا بَيْتِيَ لِلطَّائِفِينَ وَالْعَاكِفِينَ وَالرُّكَّعِ السُّجُود))

((Na kumbukeni Tulipoifanya ile Nyumba (ya Al-Ka'abah) iwe pahala pa kukusanyikia watu na pahala pa amani. Na alipokuwa akisimama Ibraahiym pafanyeni pawe pa kuswalia. Na Tuliagana na Ibraahiym na Ismaa'yil: Itakaseni Nyumba Yangu kwa ajili ya wanaoizunguka kwa kutufu na wanaojitenga huko kwa ibada, na wanaoinama na kusujudu))

[Al-Baqarah:125]

Maana ya 'pahala pa amani' ina maana kwamba amani  kutokana na maadui. Na ikaendelea Ka'abah kuwa mahali patukufu tokea siku hizo mpaka hii leo inajulikana kwa utukufu wake. Hata zama za ujaahiliyyah watu mara nyingi walikuwa ni waathirika wa uvamizi na watekwa nyara, ila waliokuwa katika eneo la Ka'abah (Al-Masjidul-Haraam) ndio walikuwa salama kutokana na kutekwa nyara. [At-Twabariy 3:29]

Vile vile Mujaahid, 'Atwaa' As-Suddiy, Qataadah na Ar-Rabi' bin Anas wameripotiwa wakisema kwamba Aya hiyo ina maana: "Yeyote atakayeingia humo atakuwa salama". [Ibn-Abi Haatim 1:370].

Aya hii ina inaonyesha kwamba Allaah سبحانه وتعالى Ameitukuza nyumba hii tukufu ambayo Ameifanya iwe kimbilio na bandari ya salama. Kwa hiyo nafsi za watu huwa zina hamu kubwa ya kuweko hapo na hawachoshwi kutembelea kila mara au kila mwaka. Hii ni kwa sababu Allaah سبحانه وتعالى Aliikubali Du'aa ya Ibraahiym عليه السلام alipomuomba Allaah سبحانه وتعالى Ajaaliye nyoyo za watu zipende kuelekea huko wakati alipomuacha mkewe Haajar na mwanawe Ismaa'iyl عليه السلام mwanzo alipofika hapo.   [Al-Bukhaariy 3364]

Aliomba:

((رَّبَّنَا إِنِّي أَسْكَنتُ مِن ذُرِّيَّتِي بِوَادٍ غَيْرِ ذِي زَرْعٍ عِندَ بَيْتِكَ الْمُحَرَّمِ رَبَّنَا لِيُقِيمُواْ الصَّلاَةَ فَاجْعَلْ أَفْئِدَةً مِّنَ النَّاسِ تَهْوِي إِلَيْهِمْ وَارْزُقْهُم مِّنَ الثَّمَرَاتِ لَعَلَّهُمْ يَشْكُرُونَ))

((Mola wetu! Hakika mimi nimewaweka baadhi ya dhuriya zangu katika bonde lisilokuwa na mimea, kwenye Nyumba Yako Takatifu, ewe Mola wetu, ili wasimamishe Swalah. Basi Zijaalie nyoyo za watu zielekee kwao, na Waruzuku matunda, ili wapate kushukuru)) [Ibraahiym :37]

 

Mahali patukufu pa kuswaliwa

Heshima ya mwanzo inamfikia Ibraahiym عليه السلام kwa kufanywa sehemu aliyosimama kujenga Ka'abah kuwa mahali patukufu pa kuswaliwa.

((وَاتَّخِذُواْ مِن مَّقَامِ إِبْرَاهِيمَ مُصَلًّى))

((Na alipokuwa akisimama Ibraahiym pafanyeni pawe pa kuswalia))

[Al-Baqarah:125]

 

Nyumba iliyotakaswa

Vile vile ilikuwa ni amri kwa Ibraahiym عليه السلام na mwanawe Ismaa'iyl عليه السلام kwamba waitakase Ka'abah.

((وَعَهِدْنَا إِلَى إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ أَن طَهِّرَا بَيْتِيَ لِلطَّائِفِينَ وَالْعَاكِفِينَ وَالرُّكَّعِ السُّجُودِ))

((Na Tuliagana na Ibraahiym na Ismaa'iyl: Itakaseni Nyumba Yangu kwa ajili ya wanaoizunguka kwa kutufu na wanaojitenga huko kwa ibada, na wanaoinama na kusujudu)) [Al-Baqarah:125]

Hali kadhalika ilikuwa ni amri ya kuitakasa na shirki :

((وَإِذْ بَوَّأْنَا لِإِبْرَاهِيمَ مَكَانَ الْبَيْتِ أَن لَّا تُشْرِكْ بِي شَيْئًا وَطَهِّرْ بَيْتِيَ لِلطَّائِفِينَ وَالْقَائِمِينَ وَالرُّكَّعِ السُّجُودِ))

((Na pale Tulipomweka Ibraahiym pahala penye ile Nyumba Tukamwambia: Usinishirikishe na chochote; na isafishe Nyumba Yangu kwa ajili ya wanaoizunguka kwa kutufu, na wanaokaa hapo kwa ibada, na wanaorukuu, na wanaosujudu)) [Al-Hajj:26]

Maana: Ifanye iwe safi  kwa wale wanaomuabudu Allaah Pekee bila ya kumshikirikisha na mtu au msaidizi.

 

Nyumba ya pekee inayozungukwa kama ibada

Ni nyumba pekee katika ulimwengu wa Waislamu inayozungukwa kama ni kitendo cha ibada. Twawwaaf na Swalah zimetajwa pamoja katika aya hiyo, kwa sababu hakuna mahali popote kwengine kulikofaradhishwa ibada hizi mbili pamoja isipokuwa hapa katika Ka'abah.     

 

Ni Msikiti wa mwanzo ulimwenguni

Ni Msikiti wenye baraka na uongofu

Nayo ni nyumba ya mwanzo kabisa duniani iliyofanywa kuwa ya ibada, yenye baraka, uongofu kwa watu wote, na ndipo Waislamu huenda kutekeleza nguzo yao ya tano ya fardhi.

((إِنَّ أَوَّلَ بَيْتٍ وُضِعَ لِلنَّاسِ لَلَّذِي بِبَكَّةَ مُبَارَكًا وَهُدًى لِّلْعَالَمِينَ))

((Hakika Nyumba ya kwanza waliowekewa watu kwa ibada ni ile iliyoko Bakkah,(Makkah), iliyobarikiwa na yenye uongofu kwa walimwengu wote)) [Al'Imraan:96]

عن أبي ذَر، رضي الله عنه، قال قلتُ: يا رسولَ الله، أيُّ مَسجِد وُضِع في الأرض أوَّلُ؟ قال: ))الْمسْجِدُ الْحَرَامُ((. قلت: ثم أَيُّ؟ قال: ))الْمسجِدُ الأقْصَى(( قلت: كم بينهما؟ قال: ))أرْبَعُونَ سَنَةً((. قلتُ: ثم أَيُّ؟ قال (( ثُم حَيْثُ أدْرَكْت الصَلاةَ فَصَلِّ، فَكُلُّهَا مَسْجِدٌ)).  أخرجه البخاري، ومسلم، وأحمد

Imetoka kwa Abu Dharr amesema: "Nilisema Ewe Mjumbe wa Allaah, msikiti gani ulikuwa wa mwanzo kabisa kujengwa duniani?" Akasema: ((Al-Masjidul-Haraam)) (Ulioko Makkah).  Nikasema: Kisha upi? Akasema: ((Al-Masjidul-Aqswaa)) (Palestina). Nikasema: Ilikuwa muda gani kujengwa baina yao? Akasema: ((Miaka arubaini)) Akaongeza: ((Popote (mtakapokuwa) na Swalah ikawakuta, Swalini humo, kwani ardhi yote imefanywa kuwa ni msikiti)) [Al-Bukhaariy, Muslim na Imaam Ahmad]

Usemi mwingine kutoka kwa wataalamu wanaofasiri, wamesema kuwa kwa vile Adam عليه السلام ni kiumbe cha mwanzo katika ardhi, alipewa heshima kujenga nyumba ya mwanzo ya ibada. Aliijenga kisha akaizunguka kama Malaika wanvyozunguka juu katika Baytul-Ma'amuur huko juu katika 'Arshi ya Allaah سبحانه وتعالى iliyoko katika mbingu ya saba.  Na inasemekana alijenga hema akawa anafanya ibada yake hapo, lakini baada ya kufariki na karne nyingi kupia, ikapotea alama ya sehemu hiyo. 

 

Nguzo ya tano ya Kiislamu inatimizwa hapo

 (( فِيهِ آيَاتٌ بَيِّنَاتٌ مَّقَامُ إِبْرَاهِيمَ وَمَن دَخَلَهُ كَانَ آمِنًا وَلِلّهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلاً وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ الله غَنِيٌّ عَنِ الْعَالَمِينَ)) 

((Ndani yake zipo Ishara zilizo wazi - masimamio ya Ibraahiym, na mwenye kuingia humo anakuwa katika amani. Na kwa ajili ya Allaah imewajibikia watu wahiji kwenye Nyumba hiyo, kwa yule awezae njia ya kwendea. Na atakayekanusha basi Allaah si mhitaji kwa walimwengu))  [Al-'Imraan: 97]

 

 

DU'AA ZA IBRAAHIYM عليه السلام BAADA YA KUJENGA KA'ABAH

Anasema Allaah سبحانه وتعالى :

((وَإِذْ يَرْفَعُ إِبْرَاهِيمُ الْقَوَاعِدَ مِنَ الْبَيْتِ وَإِسْمَاعِيلُ رَبَّنَا تَقَبَّلْ مِنَّا إِنَّكَ أَنتَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ))

((Na kumbukeni Ibraahiym na Ismaa'iyl walipoinyanyua misingi ya ile Nyumba wakaomba: Ewe Mola wetu! Tutakabalie! Hakika Wewe Ndiye Msikizi Mjuzi)) [Al-Baqarah:127]

Hapa tunapata fundisho kubwa kutoka kwa baba yetu Nabii Ibraahiym عليه السلام kwamba ingawa yeye na Ismaa'iyl عليه السلام wamejenga Ka'abah, nyumba ambayo inayozungukwa na mamilioni ya Waislamu kama ni ibada tukufu mpaka siku ya Qiyaamah, lakini hawakutegemea kwamba Allaah سبحانه وتعالى Atawapokelea amali hii moja kwa moja, bali kwanza wamemuomba Mola Awatakabalie. Hii ni tabia ya waumini wenye ikhlaas ambao wako baina ya khofu na matumaini wanapofanya vitendo vyema. Na sisi tunatakiwa tuwe tunaiomba Du'aa hii kila mara tunapomaliza kitendo au vitendo vyovyote vyema kwani vile vile hatujui kama vitendo hivyo vitakubaliwa na Mola wetu au havitakubaliwa. 

Akaendelea Ibraahiym عليه السلام kuomba pamoja na mwanawe Ismaa'iyl عليه السلام,

(( رَبَّنَا وَاجْعَلْنَا مُسْلِمَيْنِ لَكَ وَمِن ذُرِّيَّتِنَا أُمَّةً مُّسْلِمَةً لَّكَ وَأَرِنَا مَنَاسِكَنَا وَتُبْ عَلَيْنَآ إِنَّكَ أَنتَ التَّوَّابُ الرَّحِيمُ))

((Ewe Mola wetu! Tujaalie tuwe ni wenye kusilimu Kwako, na pia miongoni mwa vizazi vyetu wawe umma uliosilimu Kwako. Na Utuonyeshe njia za ibada yetu na Utusamehe. Bila shaka Wewe Ndiye Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu)) [Al-Baqarah: 128]

((وَأَرِنَا مَنَاسِكَنَا))

((utuonyeshe njia za ibada yetu))

Ina maana ni Taratibu za Hajj na 'Umrah ambazo Waislamu wanazifuata kutekelea nguzo ya  tano ya Kiislamu.

  ((رَبَّنَا وَابْعَثْ فِيهِمْ رَسُولاً مِّنْهُمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِكَ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَيُزَكِّيهِمْ إِنَّكَ أَنتَ العَزِيزُ الحَكِيمُ))    

((Ewe Mola wetu! Waletee Mtume anayetokana na wao, awasomee Aayah Zako, na awafundishe Kitabu na hikima na awatakase. Hakika Wewe Ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima)) [Al-Baqarah:129]

Du'aa hii: ((Waletee Mtume anayetokana na wao)) ndio sababu ya kutoka Mtume wa mwisho kutoka kizazi cha Ismaa'iyl عليه السلام naye ndiye Mtume bora kabisa kuliko mitume yote naye ni kipenzi cha Umma wa Kiislamu, Muhammad  صلى الله عليه وآله وسلم .

Vile vile maana ya ((awasomee Aya Zako, na awafundishe Kitabu na hikima)) ndio kitabu cha mwisho nacho ni Qur'aan aliyopewa Mtume Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم  ambayo ni uongofu kamili kwa watu wote ulimwenguni Waarabu na wasio Waarabu. 

Du'aa nyingine alizoomba Ibraahiym عليه السلام :

 

وَإِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ رَبِّ اجْعَلْ هَذَا الْبَلَدَ آمِنًا وَاجْنُبْنِي وَبَنِيَّ أَن نَّعْبُدَ الأَصْنَامَ ﴿35﴾ رَبِّ إِنَّهُنَّ أَضْلَلْنَ كَثِيرًا مِّنَ النَّاسِ فَمَن تَبِعَنِي فَإِنَّهُ مِنِّي وَمَنْ عَصَانِي فَإِنَّكَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿36﴾ رَّبَّنَا إِنِّي أَسْكَنتُ مِن ذُرِّيَّتِي بِوَادٍ غَيْرِ ذِي زَرْعٍ عِندَ بَيْتِكَ الْمُحَرَّمِ رَبَّنَا لِيُقِيمُواْ الصَّلاَةَ فَاجْعَلْ أَفْئِدَةً مِّنَ النَّاسِ تَهْوِي إِلَيْهِمْ وَارْزُقْهُم مِّنَ الثَّمَرَاتِ لَعَلَّهُمْ يَشْكُرُونَ ﴿37﴾ رَبَّنَا إِنَّكَ تَعْلَمُ مَا نُخْفِي وَمَا نُعْلِنُ وَمَا يَخْفَى عَلَى اللّهِ مِن شَيْءٍ فَي الأَرْضِ وَلاَ فِي السَّمَاء ﴿38﴾ الْحَمْدُ لِلّهِ الَّذِي وَهَبَ لِي عَلَى الْكِبَرِ إِسْمَاعِيلَ وَإِسْحَقَ إِنَّ رَبِّي لَسَمِيعُ الدُّعَاء ﴿39﴾ رَبِّ اجْعَلْنِي مُقِيمَ الصَّلاَةِ وَمِن ذُرِّيَّتِي رَبَّنَا وَتَقَبَّلْ دُعَاء ﴿40﴾ رَبَّنَا اغْفِرْ لِي وَلِوَالِدَيَّ وَلِلْمُؤْمِنِينَ يَوْمَ يَقُومُ الْحِسَابُ ﴿41﴾

 

 

((Na Ibraahiym aliposema: Ee Mola wangu! Ujaalie mji huu uwe wa amani, na Uniepushe mimi na wanangu na kuabudu masanamu))

((Ee Mola wangu! Hakika hayo yamewapoteza watu wengi. Basi aliyenifuata mimi huyo ni wangu, na aliyeniasi, hakika Wewe ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu)) 

((Mola wetu! Hakika mimi nimewaweka baadhi ya dhuriya zangu katika bonde lisilo kuwa na mimea, kwenye Nyumba Yako Takatifu, Ee Mola wetu , ili washike Swalah. Basi Zijaalie nyoyo za watu zielekee kwao, na waruzuku matunda, ili wapate kushukuru))

((Ee Mola wetu ! Hakika Wewe Unajua tunayoyaficha na tunayoyatangaza. Na hapana kitu kinachofichikana kwa Allaah katika ardhi wala katika mbingu)). 

((AlhamduliLLaah! Himdi zote ni za Allaah Aliyenipa juu ya uzee wangu Ismaa'iyl na Is-haaq. Hakika Mola wangu ni Mwenye kusikia maombi)) 

((Mola wangu! Nijaalie niwe mwenye kushika Swalah, na katika dhuriya zangu pia. Ewe Mola wetu , na Ipokee dua yangu)) 

((Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote wawili, na Waumini, siku ya kusimama hisabu))

[Ibraahiym: 35-41]

 

 

KUWAADHINIA WATU WAITIKIE KWENDA HAJJ

 

Alipomaliza kujenga Ka'abah Ibraahiym عليه السلام, Allaah سبحانه وتعالى Alimtaka awatangazie watu waje kuhiji kama ilivyo katika aya hii ifuatayo:

 

((وَأَذِّن فِي النَّاسِ بِالْحَجِّ يَأْتُوكَ رِجَالًا وَعَلَى كُلِّ ضَامِرٍ يَأْتِينَ مِن كُلِّ فَجٍّ عَمِيقٍ))

((Na watangazie watu Hajj; watakujia kwa miguu na juu ya kila ngamia aliyekonda, wakija kutoka katika kila njia ya mbali)) [Al-Hajj:27]

 

Ibraahiym عليه السلام alisema: "Mola wangu, vipi niwatangazie watu hivyo na hali sauti yangu haitawafikia?" Akaambiwa: "Waite (waadhinie) na Sisi Tutawafikishia". Ibraahiym عليه السلام akasimama na kusema: "Enyi watu, Mola wenu Ameanzisha  Nyumba ili mje kuhiji".

Imesemekana kuwa milima ilijiinamisha ili sauti ifikie pande zote za dunia, na ikawafikia watu wote mpaka waliokuwa matumboni mwa mama zao na migongo ya baba zao (yaani waliokuwa hawakuzaliwa bado).

Na majibu yakaja kutoka kwa kila mtu kutoka kila miji, majangwa na mashamba, na hao ndio ambao waliokwishajaaliwa kufika Makkah kutimiza Hijjah na vile vile wale ambao bado hawakufika, lakini watakaojaaliwa kufika kutimiza Hijjah mpaka siku ya Qiyaamah, waliokuwa hai na waliokuwa bado hawakuzaliwa, itakuwa ndio sauti ya Ibraahiym عليه السلام imewafikia.  Majibu  ya watu yalikuwa

"لبيك اللهم لبيك"

"Labbayka Allaahumma Labbayk"  

Nimekuitika Ee Allaah nimekuitika,

Na hivi ndivyo anavyosema mwenye kufanya Hijjah anapoingia katika Ihraam akiwa tayari kutekeleza taratibu za 'Umrah na Hijjah.

 

KUONDOKA MAKKAH BAADA YA KUJENGA KA'ABA

 

Ibraahiym عليه السلام akaondoka Makkah kwenda kuendelea na da'awa ya kuwaita watu katika Tawhiyd, akiwa na mkewe Sarah na akamuacha Ismaa'iyl عليه السلام pamoja na familia yake Makkah.  

Siku moja Ibraahiym عليه السلام alikuwa amekaa katika kambi yake akimfikiria mwanawe Ismaa'iyl عليه السلام, ndoto ya kumchinja na fidia Aliyomteremshia Allaah سبحانه وتعالى. Moyo wake ukazidi kujaa mapenzi ya Allaah سبحانه وتعالى kwa neema Zake zisizohesabika. Chozi kubwa likamdondoka alivyokuwa akimfikiria Ismaa'iyl عليه السلام na umbali alioko, jinsi alivyokuwa akimkosa na hamu ya kuwa naye.

Mara Malaika watatu wakateremka; Jibriyl, Israafiyl na Miykaaiyl. Walimjia kwa maumbo ya binaadamu wenye sura nzuri kabisa. Ibraahiym عليه السلام aliinuka na kuwakaribisha. Aliwaita ndani ya kambi huku akiwaza kuwa ni wageni asiowajua. Akawakaribisha vizuri na kuhakikisha kuwa wamestarehe, kisha akaomba idhini kwao ili aende kwa ahli yake. (kuagiza waletewe chakula).  

Sarah wakati huo ameshakuwa mzee, mvi zimemjaa kichwani. Ibraahiym عليه السلام akamuambia: "Tumepata wageni watatu".

Akamuuliza: "Ni nani hao?". Akamjibu: "Simjui hata mmoja wao". Akauliza Ibraahiym عليه السلام: "Tuna chakula gani?". Akajibu Sarah: "Tuna nusu kondoo". Ibraahiym عليه السلام akasema: "Nusu kondoo? Wachinjie nusu ndama, kwani wao ni wageni tusiowajua na hatujui pengine wana njaa".

Watumishi wakachinja nusu ndama na kumchoma vizuri. Kikaletwa chakula mbele ya hao wageni, Ibraahiym عليه السلام akawakaribisha wasogee kula. Akaona hawasogei kula, basi akaanza kula yeye ili awatie moyo nao watake kula lakini aliona kuwa hakuna hata mmoja wao aliyegusa chakula. Akawauliza: "Kwa nini hamli?". Akaendelea yeye kula, lakini wao walibakia vile vile bila ya kukaribisha mikono yao katika chakula. Ibraahiym عليه السلام akaanza kuogopa.

Khofu ya Ibraahiym عليه السلام ikazidi na Malaika wakawa wanamsoma mawazo yake, kisha mmoja wao akasema: "Usikhofu". Ibraahiym عليه السلام akasema: "Hakika nina khofu, kwani nimekukaribisheni mle lakini naona hamjanyoosha mikono yenu kutaka kula. Je, mmekusudia uovu?".

Malaika mmoja akatabasamu na kusema: "Sisi hatuli, kwani sisi ni Malaika wa Allaah". Mmoja wao akageuka kwa mkewe Ibraahiym عليه السلام na kumbashiria bishara njema ya mwana Is-haaq. 

Ibraahiym عليه السلام na Sarah walishtuka kubashiriwa mtoto katika umri huo walionao. Lakini juu ya mshtuko huo, Sarah aliingiwa na furaha kubwa kuwa atapata mtoto ambaye alimtamani miaka mingi sana! Na furaha ilizidi alipoambiwa kuwa mtoto huyo atakuwa ni mtoto mwenye ujuzi.  

Allaah سبحانه وتعالى Ametuelezea matukio haya kwa kirefu katika Aya zifuatazo:

 

 وَنَبِّئْهُمْ عَن ضَيْفِ إِبْراَهِيمَ ﴿51﴾ إِذْ دَخَلُواْ عَلَيْهِ فَقَالُواْ سَلامًا قَالَ إِنَّا مِنكُمْ وَجِلُونَ ﴿52﴾ قَالُواْ لاَ تَوْجَلْ إِنَّا نُبَشِّرُكَ بِغُلامٍ عَلِيمٍ ﴿53﴾ قَالَ أَبَشَّرْتُمُونِي عَلَى أَن مَّسَّنِيَ الْكِبَرُ فَبِمَ تُبَشِّرُونَ ﴿54﴾ قَالُواْ بَشَّرْنَاكَ بِالْحَقِّ فَلاَ تَكُن مِّنَ الْقَانِطِينَ ﴿55﴾ قَالَ وَمَن يَقْنَطُ مِن رَّحْمَةِ رَبِّهِ إِلاَّ الضَّآلُّونَ ﴿56﴾ قَالَ فَمَا خَطْبُكُمْ أَيُّهَا الْمُرْسَلُونَ ﴿57﴾ قَالُواْ إِنَّا أُرْسِلْنَا إِلَى قَوْمٍ مُّجْرِمِينَ ﴿58﴾ إِلاَّ آلَ لُوطٍ إِنَّا لَمُنَجُّوهُمْ أَجْمَعِينَ ﴿59﴾ إِلاَّ امْرَأَتَهُ قَدَّرْنَا إِنَّهَا لَمِنَ الْغَابِرِينَ ﴿60﴾

((Na uwape khabari za wageni wa Ibraahiym)) 

((Walipoingia kwake na wakasema: Salama! Yeye akasema: Hakika sisi tunakuogopeni))

((Wakasema: Usiogope. Sisi tunakubashiria kijana mwenye ujuzi))   

((Akasema: Mnanibashiria nami uzee umenishika! Basi kwa njia gani mnanibashiria?)) 

((Wakasema: Tunakubashiria kwa haki; basi usiwe miongoni mwa wanaokata tamaa)) 

((Akasema: Na nani anaye kata tamaa na Rehema ya Mola wake ila wale waliopotea?)) 

((Akasema: Hebu nini amri yenu, enyi wajumbe?)) 

((Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwa kaumu ya wakosefu!)) 

((Isipo kuwa waliomfuata Luut. Bila ya shaka sisi tutawaokoa hao wote)) 

((Ila mkewe. Tunakadiria huyo atakuwa miongoni wa wataobakia nyuma))

[Al-Hijr: 51-60]

Waliposema kuwa wanakwenda kuangamiza mji wa Luut  عليه السلام Ibraahiym عليه السلام alikhofu kuwa vipi wataangamiza mji huo na hali yumo Luut عليه السلام? Majibu yao Malaika yamo katika aya zifuatazo:  

((وَلَمَّا جَاءتْ رُسُلُنَا إِبْرَاهِيمَ بِالْبُشْرَى قَالُوا إِنَّا مُهْلِكُو أَهْلِ هَذِهِ الْقَرْيَةِ إِنَّ أَهْلَهَا كَانُوا ظَالِمِينَ))

 ((قَالَ إِنَّ فِيهَا لُوطًا قَالُوا نَحْنُ أَعْلَمُ بِمَن فِيهَا لَنُنَجِّيَنَّهُ وَأَهْلَهُ إِلَّا امْرَأَتَهُ كَانَتْ مِنَ الْغَابِرِينَ))   

((Na wajumbe wetu walipomjia Ibraahiym na bishara, walisema: Hakika sisi hapana shaka tutawahiliki watu wa mji huu, kwani watu wake hakika wamekuwa madhaalimu)) 

((Akasema: Hakika humo yumo Luutw. Wao wakasema: Sisi tunajua zaidi nani yumo humo. Hapana shaka tutamwokoa yeye na ahli zake, isipokuwa mkewe aliye miongoni mwa wataokaa nyuma. [Al-'Ankabuut: 31-32]

 هَلْ أَتَاكَ حَدِيثُ ضَيْفِ إِبْرَاهِيمَ الْمُكْرَمِينَ ﴿24﴾ إِذْ دَخَلُوا عَلَيْهِ فَقَالُوا سَلَامًا قَالَ سَلَامٌ قَوْمٌ مُّنكَرُونَ ﴿25﴾ فَرَاغَ إِلَى أَهْلِهِ فَجَاء بِعِجْلٍ سَمِينٍ ﴿26﴾ فَقَرَّبَهُ إِلَيْهِمْ قَالَ أَلَا تَأْكُلُونَ ﴿27﴾ فَأَوْجَسَ مِنْهُمْ خِيفَةً قَالُوا لَا تَخَفْ وَبَشَّرُوهُ بِغُلَامٍ عَلِيمٍ ﴿28﴾ فَأَقْبَلَتِ امْرَأَتُهُ فِي صَرَّةٍ فَصَكَّتْ وَجْهَهَا وَقَالَتْ عَجُوزٌ عَقِيمٌ ﴿29﴾ قَالُوا كَذَلِكَ قَالَ رَبُّكِ إِنَّهُ هُوَ الْحَكِيمُ الْعَلِيمُ ﴿30﴾ قَالَ فَمَا خَطْبُكُمْ أَيُّهَا الْمُرْسَلُونَ ﴿31﴾ قَالُوا إِنَّا أُرْسِلْنَا إِلَى قَوْمٍ مُّجْرِمِينَ ﴿32﴾ لِنُرْسِلَ عَلَيْهِمْ حِجَارَةً مِّن طِينٍ ﴿33﴾ مُسَوَّمَةً عِندَ رَبِّكَ لِلْمُسْرِفِينَ ﴿34﴾

 

   

((Je! Imekufikia hadithi ya wageni wa Ibraahiym wanaohishimiwa?)) 

((Walipoingia kwake wakasema: Salama! Na yeye akasema: Salama! Nyinyi ni watu nisio kujueni)) 

((Akenda kwa ahali yake na akaja na ndama aliyenona)) 

((Akawakaribisha, akasema: Mbona hamli?)) 

((Akahisi kuwaogopa katika nafsi yake. Wakasema: Usiwe na khofu, nao wakambashiria kupata kijana mwenye ilimu.))

((Ndipo mkewe akawaelekea, na huku anasema na akijipiga usoni kwa mastaajabu, na kusema: Mimi ni kikongwe na tasa!)) 

((Wakasema: Ndivyo vivyo hivyo Alivyosema Mola wako. Hakika Yeye ni Mwenye Hiimah na Mwenye kujua)) 

((Akasema: Basi ujumbe wenu ni nini, enyi mliotumwa?)) 

((Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwa watu wakosefu,)) 

((Tuwatupie mawe ya udongo)) 

((Yaliyotiwa alama kutoka kwa Mola wako kwa ajili ya wanaopindukia mipaka))

[Adh-Dhaariyaat: 24-34]

Malaika hao walikuwa wanakwenda katika mji wa Nabii Luut عليه السلام kuwaangamiza watu wake ambao walikuwa katika maasi.

Baada ya hapo, na kutokana na kubashiriwa mtoto, Sarah akashika mimba na akamzaa Is-haaq عليه السلام.

Naye Is-haaq عليه السلام akamzaa Ya'aquub عليه السلامambaye amemzaa Yuusuf عليه السلام pamoja na ndugu zake wengine  kumi na mojo. Mmoja wa ndugu yake Yuusuf عليه السلام akiitwa Binyaamiyn ndiye aliyekuwa ni ndugu yake khalisa (ndugu kwa baba na mama).    

Ibraahiym عليه السلام amefariki katika umri wa miaka mia na sabini na tano. [Qwisasul-Anbiyaa- Ibnu Kathiyr] na amezikwa Falastina katika mji ulioitwa Khaliyl.

Na Allaah Anajua zaidi.

 

MWISHO WA KISA CHA NABII IBRAHIYM عليه السلام

 

 

Allaah سبحانه وتعالى Ametuelezea zaidi:

 

لَقَدْ كَانَ فِي قَصَصِهِمْ عِبْرَةٌ ِلأُوْلِي الأَلْبَابِ مَا كَانَ حَدِيثًا يُفْتَرَى وَلَكِن تَصْدِيقَ الَّذِي بَيْنَ يَدَيْهِ وَتَفْصِيلَ كُلَّ شَيْءٍ وَهُدًى وَرَحْمَةً لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ

Kwa hakika katika visa vyao yamo mazingatio kwa wenye akili. Si maneno yaliyo zuliwa, bali ni ya kusadikisha yaliyo kabla yake, na ufafanuzi wa kila kitu, na ni uwongofu na rehema kwa kaumu yenye kuamini.

[Yuusuf: 111]

 

 

 

Share