Miezi Ya Kiislamu Na Makosa Yaliyozooleka Katika Jamii Kwa Kuitaja Kwa "Mfungo Kadhaa"

 

Miezi Ya Kiislamu Na Makosa Yaliyozooleka Katika Jamii Kwa Kuitaja Kwa "Mfungo Kadhaa" 

 

www.alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Naomba mnitajie miezi ya Kiislamuu kwa sababu tunasikia wazee wakitaja mfungo mosi, mfungo pili na sasa tunaona inatajwa kwa majina mengine kama muharam, rajab n.k.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kuyaita majina ya miezi ya Kiislamu mfungo mosi, mfungo pili, mfungo tatu n.k., hakika ni majina yaliyozoeleka lakini si sahihi kwani yanapoteza ufahamu wa majina sahihi na mpangilio wa hiyo miezi ya Kiislamu.
 

Miezi ya Kiislamu hujulikana mwezi wa kwanza kama ni Muharram lakini baadhi ya watu huo mwezi wa kwanza umeitwa ni mfungo nne, na mwezi wa Dhul-Hijjah ambao ni mwezi wa kumi na mbili, wao wanauita mfungo tatu! Hivyo Waislamu wengi hudhani kuwa mwezi wa 12 wa Dhul-Hijjah ni mwezi wa 3 badala ya 12.

 

Kutoka katika mpango uliowekwa na Uislamu na kufuata mipango na taratibu za kimila na kitamaduni, kunasababisha mafunzo ya Dini kutofahamika kamwe, au kusahaulika kabisa.

 

Leo hii, Waislamu wengi hawajui miezi ya Kiislamu kwa majina yake ingawa wengi wanaijua hiyo ‘mifungo’. Huo ni ukweli wenye kusikitisha. Na wengi huita kalenda na tarehe za Kiislamu kuwa ni tarehe za Kiarabu badala ya Kiislamu; ilihali kuna tofauti kubwa kati ya Uislamu na Uarabu.

 

Miezi ya Kiislamu ni hiyo tuliyozungumzia hapo juu na tutaweka chini kabisa mpangilio wake wa majina ya miezi yote ya mwaka mzima. Kalenda au tarehe za Kiarabu ni tofauti na za Kiislamu na mtu akitaka kujua atazame magazeti ya Kiarabu ataona tofauti.

 

Hivyo, Waislam wajizoeshe kuita tarehe za Kiislamu au miezi ya Kiislamu na si ya Kiarabu, maana kuna Wakristo Waarabu nao hawafuati kalenda yetu ya Kiislamu.

 

Miezi Ya Kiislamu (Kila Muislam Ajitahidi Kuijua Na Kuihifadhi:

 

1

Muharram

محرّم

2

Swafar

صفر

3

Rabiy’u Al-Awwal

ربيع الأول

4

Rabiy'u Al-Aakhir

ربيع الآخر  

5

Jumaadaa Al-Uwlaa

جمادى الأولى

6

Jumaadaa Al-Aakhirah

جمادى الآخرة 

7

Rajab

رجب

8

Sha’baan

شعبان

9

Ramadhwaan

رمضان

10.

Shawwaal

شوّال  

11.

Dhul-Qa’dah

ذو القعدة

12

Dhul-Hijjah

ذو الحجة

 

Inasikitisha sana kuona Muislam kahifadhi miezi yote isiyo ya Kiislamu, lakini hawezi kutaja hata miezi sita ya Kiislamu. Sana sana utakuta Muislam anajua ile miezi ya karibu na Ramadhwaan kama Rajab, Sha’baan na pia labda mwezi huu wa Dhul-Hijjah na wengine huujua Rabiy’ul al-Awwal kwa sababu ya kusherekea tu Mawlid na huenda asijue kuwa ni Rabiy’ul-Awwal, bali atakuwa anaujua kwa jina la kijamii ‘Mfungo sita’!

 

Huu ndio msiba tulionao Waislam, inatubidi tuamke hivi sasa na tuzindukane na ujinga wa miaka na miaka. Na silaha pekee ya kuzindukana na hayo, ni elimu sahihi ya Dini hii tukufu.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share