Taraawiyh: Swalaah Ya Taraawiyh Ni Sunnah Au Uzushi?

 

SWALI:

Asalam alaykum,

Mie pia naomba kuelimishwa vilevile kuhusu jambo hili kwa sababu nimesikia kuwa Mtume (s.a.w) hakuwahi kuisali alifundisha watu tu yeye hakuisali hata siku moja, hii ni kweli? kama kweli kwanini sie tunaisali jamaa na mtume hakufanya hivi?

Musione tabu kutuelimisha kwani tunakiu ya kuijuwa kwa uwazi dini yetu. JazakAllaahul kheir.

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukran kwa suala lako kuhusu Swalah hii ya taraawiyh. Naomba kabla ya kulijibu Swali hilo ili tufahamike vyema na vizuri kueleza ufahamu wa Sunnah kwa muono wa sharia yetu. Tunapozungumza kuhusu Sunnah huwa ina maana ya kauli za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), vitendo vyake na lililofanywa mbele yake asilikataze. Sasa tukitazama tu ibara yako tayari suala lako huwa limejibiwa: “Nimesikia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwahi kuisali alifundisha watu tu yeye hakuisali hata siku moja”.

Kule kufundisha watu tu inatosha kwa Waislamu kufuata agizo hilo. Mfano wake ni kama Swawm ya Sunnah ya Taasu‘aa (tarehe tisa Muharram) Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwahi kuifungwa kwa mujibu wa Hadiyth: “Nikibakia hadi mwakani basi nitafunga tarehe tisa (Muharram)” (Muslim).

 Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliaga dunia kabla ya kufika mwaka mwingine lakini hii inafahamika ni Sunnah ambayo Maswahaba na watangu wema wamekubaliana bila tatizo.

Sasa tukija katika suala lako ni kuwa huyo au hao waliokuambia hawakukuambia ukweli kwani Swalah ya taraawiyh ni Sunnah Muakkadah (iliyohimizwa sana) kwa kuafikina Waislamu wote kuanzia Maswahaba mpaka sisi leo. Na Sunnah ni kwa wanaume na wanawake kuitekeleza sawa sawa bila tofauti yoyote.

Ama Hadiyth kuhusiana na hilo ni ile ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mwenye kusimama kisimamo cha Ramadhaan (taraawiyh) kwa Imani na kutarajia malipo kutoka kwa Allaah husamehewa madhambi yake yaliyopita” (al-Bukhaariy na Muslim).

Haya tunaweza kusema ni maneno yake lakini umesema kuwa umesikia kuwa yeye mwenyewe (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuswali! Hilo si kweli. Hebu tutazame Hadiyth ya mama wa waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) ambaye anatueleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali Swalah (ya taraawiyh) Ramadhaan watu wakamfuata. Siku ya pili akaswali tena na watu wakamfuata, ama ilipofika siku ya tatu watu walikuwa wengi sana naye hakutoka kuswalisha. Ilipofika asubuhi aliwaambia kuwa hakutoka makusudi kuja kuswalisha Msikitini ili isije kufaradhiwa na hivyo shida kwa Ummah wake (al-Bukhaariy na Muslim).

Hali hiyo ya yeye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuswali peke yake na Maswahaba kufanya hivyo pia iliendelea mpaka katika ukhalifa wa ‘Umar bin al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipopita Msikitini usiku mmoja akawaona Waumini wanaswali mmoja mmoja au kwa vikundi vidogo vidogo. Hapo aliamuru wote waswali jamaa moja nyuma ya Imaam Ubayy bin Ka‘b (Radhiya Allaahu ‘anhu) (al-Bukhaariy na Maalik).

Kuanzia wakati huo Swalah ya taraawiyh ikawa inaswaliwa jamaa hadi leo. Hiyo alieleza ni kuwa hakuna uwezekano wa Swalah hiyo kufaradhishwa kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amefariki na wahyi umekatika. Hakuna Swahaba aliyepinga hilo kwani hoja ni nzito hiyo isiyoweza kupingika.

Kwa ufupi, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali Swalah ya taraawiyh kimatendo pamoja na kuhimiza watu wafanye hivyo. Na wale wanaosema ni bid’ah iliyoanzishwa na ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) ni watu waongo wasio na ushahidi na zaidi wanataka kuwafarakanisha Waislamu kwa kuwatia mashaka katika yale yaliyo sahihi na yaliyothibiti kwenye Hadiyth mbalimbali sahihi.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 
Share