Uhuru Wa Kubadili Dini Zanzibar

Uhuru Wa Kubadili Dini Zanzibar

 

Imekusanywa Na:  Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com 

 

 

 

I.            Muhtasari

II.           Utangulizi

III.          Uhuru Wa Kuabudu Ndani Ya Katiba Ya Zanzibar

IV.          Murtadi

V.            Aina Za Murtadi

VI.           Msimamo Wa Uislam Juu Ya Uhuru Wa Kutoka Katika Dini

VII.          Murtadi Na Uhaini

VIII.         Adhabu Kwa Murtadi

 IX.           Athari Ya Kurtadi Kwa Ndoa

 X.             Hitimisho

 XI.            Marejeo 

 

 

 

 

I.                    Muhtasari

 

Sifa zote njema ni zake Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), Muumbaji wa vilivyo dhahiri na vilivyofichikana, Bwana wa Ulimwengu. Rehma na Amani ziwe juu ya kipenzi chetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye ameletwa kwetu kuwa ni Rehma kwa walimwengu. Nashuhudia kwamba ameufikisha kwa ulimwengu ujumbe sahihi na muongozo wa haki kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

 

Tabia ya kubadili dini (kurtadi) kwa kisingizio cha uhuru wa kuabudu ni hatari sana, sio hatari tu kwa imani peke yake bali hata kwa ndoa. Kwani athari ya kurtadi haishii kwenye imani bali mpaka kwenye ndoa. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atuepushe.

 

Hivyo tunakumbushia na kuwanasihi, ili kuwahadharisha majahili wa dini wanaoingia katika sababu za kurtadi, kuacha kabisa mchezo huo muovu.

 

Tumeipa jina makala hii “Uhuru wa Kubadili Dini Zanzibar” ili kuelezea yale muhimu kwa Muislamu anayowajibika kuelewa kutokana na sheria za Zanzibar zinavyoeleza pamoja na kupambanisha hukmu za Kiislamu katika mas’ala ya uhuru wa kubadili dini. Mwisho wa makala hii, tutakubaliana pamoja kuwa sheria za nchi zinaeleza tofauti na ambavyo Uislamu unamtaka afahamu.

 

Makala ya “Uhuru wa Kubadili Dini Zanzibar” ni muhimu kwa kila Muislamu na kwa kila anayetaka kufahamu mafunzo sahihi ya Kiislamu. Makala hii tumeigawa kipengele baada ya kipengele, kuonesha kanuni muhimu zenye kufungamana na maudhui hii.

 

 

II. Utangulizi

 

Dunia inaweza kugawanywa kwenye sehemu kuu mbili kuhusiana na mgawanyiko wa Imani ya dini. Ya mwanzo, ni zile nchi zinazojitangaza kuwa ni zenye dini na ya pili ni zile nchi zisizokuwa na dini.

 

Nchi zinazoongozwa kwa misingi ya dini kama vile Uislamu haziruhusu uhuru wa kubadili dini. Mataifa ya Kiislamu yanaongozwa kwa kutumia Shariah ambapo Qur-aan na Sunnah inamzuia Muislamu kubadili dini kwa kuingia kwenye dini nyengine. Namna hiyo Murtadi (Muislamu aliyebadili dini) ndani ya Uislaam ana adhabu kali[1] kama lilivyo kosa la uhaini[2] (treason) katika Sheria za leo. Pia Abu Ala ameeleza kuwa adhabu kwa Murtadi ni kifo[3].

 

Mfano wa nchi zilizofuata hisia za dini ya Kikristo ni Zambia chini ya utawala wa Frederick Chiluba (1991-2001) ambapo alitangaza nchi yake kuwa ni ya Kikristo[4]. Baadhi ya nchi nyengine zenye kutambua Ukristo kuwa ni Dini kuu ya Taifa ni Argentina (Roman Catholic), Cyprus (Eastern Orthodox), Denmark (Lutheran) na England (Anglican)[5].

 

Israel inatambulika ndani ya sheria zake kuwa ni Taifa la Demokrasia ya Kiyahudi (Democratic Jewish State), hata hivyo neno Jewish (Uyahudi) lina maana mbili kwa wakati mmoja, linaashiria wananchi wa Kiyahudi au/na dini ya Kiyahudi[6].

 

Kwa njia yoyote, nchi za Kiislamu inapojitangaza kuongozwa kwa misingi ya Kiislamu, ni lazima itawaliwe na Shariah. Ndivyo ilivyo kwa mataifa ya Waislamu kama Saudi Arabia, Afghanistan, Pakistan, Maldives, Algeria, Bangladesh n. k. Katika nchi hizi, wananchi na viongozi wao wanafungwa kuvuka mpaka kwenye mafundisho, vitendo, mila, tamaduni za dini ya Kiislamu. Kwa mfano Muislamu atayebadili dini atastahili adhabu kwa mujibu wa Sheria za Kiislamu.

 

Itikadi ya pili ni Taifa lisilokuwa na msimamo wowote wa dini ambazo ni nyingi kwa ulimwengu wa leo ukilinganisha na zile nchi ambazo zinaongozwa kwa dini. Tanzania, India, Australia, Germany, Canada, n.k ni mifano ya nchi zisizo na misimamo ya dini.

 

Mataifa yasiyo na msimamo wa dini zinatambua idadi ya dini zinazofuatwa ndani ya nchi yake na katu haitakiwi kuingilia dini hizo kwani wananchi wote wana uhuru wa kuabudu chochote na dini moja haina ruhusa kuitendea vibaya dini nyengine, na wala itikadi au ibada hizo za dini yoyote zisiingilie Dola.

 

 

III. Uhuru Wa Kuabudu Ndani Ya Katiba Ya Zanzibar.

 

“Uhuru wa Kuabudu” ni haki ya kushikamana kwa muundo wowote wa dini au kutoabudu au kujizuia kufuata itikadi za dini, na kuwa huru kutoingiliwa na Serikali katika kukuza/kuitangaza dini yake kama ilivyodhaminiwa chini ya Katiba ya nchi husika[7].

 

Zanzibar kama ilivyo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejitawaza kuwa ni taifa lisilokuwa na msimamo wa dini chini ya Katiba yake Kifungu 19 kinachosomeka kama ifuatavyo:

 

(1) Kila mtu anastahili kuwa na uhuru wa mawazo, wa imani na wa uchaguzi katika mambo ya dini, pamoja na uhuru wa kubadilisha dini au imani yake.

 

(2) Bila ya kuathiri sheria zinazohusika za Jamhuri ya Muungano, kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kuendeleza dini itakuwa huru na jambo la hiari ya mtu binafsi; na shughuli na uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za Mamlaka ya Nchi.

(3) Kila palipotajwa neno “dini” katika kifungu hiki ifahamike maana yake ni pamoja na madhehebu ya dini, na maneno mengineyo yanayofanana au kuambatana na neno hilo nayo yatatafsiriwa kwa maana hiyo.”

Hivyo, kwa kuwa ni taifa lisilofungamana na dini yoyote, Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, zinatakiwa ziheshimu uhuru wa kuabudu na wananchi wana uhuru wa kubadili dini wakati wowote bila ya kuteswa/kuingiliwa.

 

Uhuru wa kuabudu unaopatikana ndani ya Katiba ya Zanzibar, umeunganishwa chini ya Tamko la Pamoja Kuhusiana na Haki Kuu za Binaadamu (Universal Declaration of Human Rights) zenye msingi na ulinzi wake kutoka Umoja wa Mataifa[8], ambapo Tanzania ni mwanachama na hivyo inalazimika kufuata na kusimamisha uhuru huu wa kuabudu.

 

Kifungu 19 cha Katiba ya Zanzibar sio tu kinatoa uhuru wa kuabudu bali pia unampatia mkaazi wa Zanzibar haki ya kubadili dini yoyote na haki ya kuitangazia imani yake bila ya kuathiri Serikali.

 

Uhuru wa kubadili dini ndani ya Katiba ya Zanzibar ni ile haki inayopatikana chini ya Taifa (lolote) lisilofungamana na dini. Kwa hivyo, Zanzibar haitawaliwi au kutezwa nguvu na hisia za dini yoyote.

 

Katiba ya Zanzibar inatawaza uhuru wa kuabudu, na Serikali ya Mapinguzi ya Zanzibar (SMZ) inatakiwa iheshimu haki hii kwa vitendo.

 

Kama tulivyoona Kifungu 19 cha Katiba ya Zanzibar, mkaazi wa Zanzibar ana uhuru wa kubadili dini kutoka au kuingia imani aitakayo. Lakini uhuru huu una mipaka yake kwa mujibu wa Sheria za nchi na hivyo SMZ ina uwezo wa kuingilia dini fulani pale inapoona sawa. Kwa mara kadhaa nguvu hizi zinatumika kuingilia dini bila ya sababu za msingi na uhakika imepelekea hadi Zanzibar kupitisha sheria ambayo kwa nje inaonekana kuwanufaisha Waislamu lakini ukweli ni kuwa inaingilia uhuru wa kuabudu kwa Muislamu. Kwa mfano mwaka 2001, Zanzibar iliikubali hati (bill) ya kuanzisha kiongozi wa Kiislamu kwa jina la Mufti[9], ambaye atakuwa ni muajiriwa wa SMZ.

 

Kwa upande mmoja wahusika walijibu kuwa wanahitaji Ofisi ya Mufti ili kuunganisha shughuli za Kiislamu na kukuza maelewano ya dini. Waislamu kwa upande wa pili wameibeza (wameikataa) Ofisi ya Mufti kwani inachupa mipaka ya Katiba na ni kinyume cha uhuru wa binaadamu[10].

 

 

IV. Murtadi

 

Murtadi ni mtu ambaye anakufuru baada ya Uislaam wake japo hata kwa kufanya masikhara, basi atakufuru kwa kila kinachomshirikisha Subhaanah, au kumfanyia ushirika au mtoto Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa), au kukataa ulinganio wa Utume, au kukataa ujio wa Nabiy yeyote ambaye ametajwa kwenye Qur-aan kama Adam, Idriys, Ilyaas, Ibraahiym, Muwsa, ‘Iysa, Muhammad (‘Alayhi Swalaat wa ssalaam Ajmaiyn).

 

Anakufuru kila ambae anamfanyia istihzai Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) au Nabiy wake, au Kitabu chake kwa kauli au akatunga kitabu chengine au kwa vitendo na akakufuru kwa mambo ya Muumba(Allaah). Hata kama mtu atakuwa na ghadhabu, hali hiyo sio udhuru wa kumpelekea mtu kutukana Qur-aan au kumsema vibaya Malaika.

 

Anakufuru yeyote anayechukia kuwepo Malaika na Majini, Aakhirah (kuwepo kwa Jannah na Moto, Hisabu, Mizani na Siraati). Anakufuru yeyote anayeitakidi kuwa Allaah yupo kwa umbo sehemu yoyote, akazikubali itikadi za watu washirikina.

Anakufuru kwa atakaeupaka matope Uislaam na akazikataa Sheria za Kiislamu kuwa hazifai kwa kuhukumia zama za leo. Akadharau Swahaba, akawasifu kwa ujinga/ubedui.

 

Basi ni juu ya Muislamu kujihadhari na kujiepusha kwa kitendo au kauli au itikadi inayopelekea kwenye ukafiri na itakapotokezea moja kati ya hayo. Analazimika kutubu kwa haraka sio kwa istighfari tu bali arejee kutamka shahada mbili kwa mdomo na aiyakinishe shahada ndani ya moyo wake kwa kutanguliza vitendo sahihi vya Kiislamu.

 

 

V. Aina Za Murtadi.

 

Kwa minajili ya makala hii, tunamgawa mkanushaji wa dini ya Kiislamu (Murtadi) katika sehemu mbili.

 

Aina ya kwanza ni yule wa binafsi, murtadi ambaye ameacha mafundisho muhimu kama kuswali na mfano wake hata kufikia kuingia kwenye shirki lakini bila ya kuiathiri jamii ya Kiislamu kwani ni msiri kupita mpaka.

 

Murtadi wa pili ni yule wa jamii, anayejitangazia kuingia kwenye shirki na kufurahia hatua yake hiyo kwa kuanza kuukejeli Uislaam na Waislamu. Anashiriki kuupiga vita Uislaam na kufanya vitendo vya ujasusi.

 

Bila ya shaka adhabu ya murtadi wa pili itakuwa kubwa zaidi kuliko murtadi wa kwanza.

 

 

VI.  Msimamo Wa Uislamu Juu Ya Uhuru Wa Kutoka Katika Dini.

 

 

i) - Uhuru wa Imani

 

 

Ndani ya Uislaam, binaadamu hana uhuru wa kuamini akitakacho, analazimika kuamini kuwa Mungu ni Mmoja, wala Hana mshirika, Muumba (Allaah) wa kila kitu na ndie Mlezi wake (kabla ya kuzaliwa, baada ya kuzaliwa na baada ya kufa).

 

Uislaam unafahamu kuwa jamii ya wanaadamu imepata mashaka katika historia yake kupitia kwa viongozi waovu wa nchi zao ambao wamewanyanyasa binaadamu bila ya hatia yoyote. Hivyo, Nabiy (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa ‘aalihi wa Sallam) ameletwa kwetu kuikomboa jamii kutokana na dhulma hizi. Haitakikani binaadamu kurudi na kuanza kudhulumu au kudhulumiwa.

 

Kwa mujibu wa mafundisho sahihi ya Kiislamu, kila mtoto anazaliwa Muislamu. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema ndani ya Qur-aan Tukufu:

 

 وَنَفْسٍ وَمَا سَوَّاهَا ﴿٧﴾ فَأَلْهَمَهَا فُجُورَهَا وَتَقْوَاهَا ﴿٨﴾ قَدْ أَفْلَحَ مَن زَكَّاهَا ﴿٩﴾ وَقَدْ خَابَ مَن دَسَّاهَا ﴿١٠﴾

Naapa kwa nafsi na Aliyeisawazisha. Kisha Akaitambulisha uovu wake na taqwa yake. Kwa yakini amefaulu yule aliyetakasa. Na kwa yakini ampita patupu aliyeifisidi. [Ash-Shams: 7-10]

 

Uislaam unatambua kuwa kila mtoto anazaliwa na akili ya kuweza kumtambua na kumuamini Mumba (Allaah) wake; anacho kipande hicho cha akili ambacho kimewekwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) tokea asili yake mtoto.

 

 

ii) - Kutumia Nguvu

 

Msimamo wa Uislaam kwa nadharia yake ni kuwa imani ya Allaah ipo katika asili yake binaadamu, hivyo ni wazee na jamii inayoipotosha roho (mtoto) na kuigeuza kutoka njia iliyo sahihi.

 

Kwa nadharia hii, Uislaam unampa nafasi binaadamu (aliyezaliwa nje ya Uislaam) anapokuwa na fahamu zake kumtafuta Allaah mmoja na ni wangapi waliosilimu kwa nadharia hii? Ni wajibu wa kila aliyezaliwa nje ya Uislaam kuutafuta ukweli na uhakika wa Uislaam. Hivyo Uislaam hauwezi kusimamishwa kwa kutumia njia za lazima kwa asiyekuwa Muislamu na Jihaad sio njia inayotumiwa kusimamisha imani ya Uislaam kwa wasokuwa Waislamu.

 

Kupigana vita kwa njia ya Jihaad kunaweza tu kuanzishwa kuondosha dhulma na uongozi uliojikita mizizi katika maasi unaofanywa na wasokuwa Waislamu.

 

Kupigana vita kwa njia ya Jihaad kunaweza pia kutumika kuondosha uongozi (wenye kukandamiza) na dhulma inayofanyiwa Taifa la Kiislamu au Waislamu. Pale inapoonekana kuwa hakuna njia nyengine ya kufikisha Risala ya Rabb na kutimiza uhuru kamili wa kuabudu, kupigana vita kwa njia ya Jihaad pia yaweza kutumika. Hivyo kupigana vita kwa njia ya Jihaad haiwezi kutumika kuulazimisha Uislaam kwa wengine[11] lakini inatumika kuondoa madhila na dhuluma.

 

 

 

iii) - Kubadili Dini.

 

Kuingia mtu katika Uislaam kwa kulazimishwa hakukubaliki ndani ya Uislaam. Hatotambuliwa kuwa ni Muislamu hadi pale atakapoukubali Uislaam kwa khiari na ridhaa yake.

 

Atakapoingia mmoja wao kwenye Uislaam, kanuni zinabadilika. Kuanzia hapo, aliyeingia katika Uislaam atawajibika kumtakasa Allaah kwa hali zote.

 

 يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا ادْخُلُوا فِي السِّلْمِ كَافَّةً وَلَا تَتَّبِعُوا خُطُوَاتِ الشَّيْطَانِ ۚ إِنَّهُ لَكُمْ عَدُوٌّ مُّبِينٌ ﴿٢٠٨﴾

 

Enyi walioamini! Ingieni katika Uislamu kikamilifu, na wala msifuate hatua za shaytwaan. Hakika yeye kwenu ni adui wa wazi. [Al-Baqarah:208]

 

Hivyo, suala la aliyebadili dini ndani ya Uislaam linakuwa ni la Kiislamu na linatawaliwa kwa Sheria za Kiislamu. Akishaingia ndani ya Uislaam, kuacha mambo ya msingi na kuanza kutukana Qur-aan au Sunnah hayatovumiliwa.

 

Kuuacha Uislaam, unatambulika kama kuacha utaratibu wa kila kitu, kwani Uislaam ni mfumo kamili wa maisha.

 

Pia tendo la kuukana Uislaam linatambulika kama kuacha utaratibu wa maisha kwa kumshusha hadhi yake mwanaadamu na Rabb wake na Waislamu wengine, kama vile mkewe, jamaa zake na kadhalika.

 

Uhuru wa kuikana dini ya Kiislamu hauruhusiwi kwani uhuru huu unazuiwa kwa sababu zifuatazo:

 

 

1)     Uhuru wa kutoka katika dini (Irtidaad au Ridda) hauruhusiwi kwani, utamruhusu mwanaadamu kuziacha taratibu za jamii, mila na kuleta mtafaruku kwa jamii.

 

 

2)     Murtadi anaweza kutumia nafasi hii kutaka kuliangusha Taifa la Kiislamu kwa kufanya ujasusi na unafiki kwa manufaa ya maadui wa Kiislamu.

 

 

3)     Murtadi anaweza kutawanya migongano (machafuko) kwa mapana na marefu ndani ya Taifa la Kiislamu na kuzifanyia masikhara sheria, mila na vikwazo vya Kiislamu.

 

 

VII.    Murtadi Na Haini

 

 

Kwa mujibu wa Sheria za Kiingereza[12] (Common Law) Uhaini ni uhalifu juu ya Serikali ya Mfalme. Sehemu hii tunamfasiri murtadi kuwa si yule tu anayeacha Uislaam na kuingia dini nyengine bali anafanyia kazi kwa madhumuni ya kuuangusha Uislaam.

 

Hapa murtadi ana maana sawa na haini kwa Sheria za Kiingereza, kwani kwa Uingereza anahusishwa na masuala ya siasa na jeshi. Ndivyo ilivyo kwa Uislaam kuhusu murtadi kwani hutaka kuleta mageuzi yasiyo sahihi kwenye anga za siasa na jeshi la Taifa la Kiislamu au Waislamu kwa jumla.

 

Kosa la uhaini ni sawa na murtadi ndani ya Uislaam kwani lina alama za uhaini. Haini ni mtu anayetaka kufanya uasi dhidi ya Serikali/Mfalme, ndivyo kwa Murtadi kujaribu kumfanyia uasi Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa).

 

Kama tulivyobainisha kabla kuwa tendo la kuuacha Uislaam na kuwa Murtadi lina hisia mbaya kwa Waislamu kwani litaleta mtafaruku baina ya Waislamu. Hivyo, ni kukariri maneno kwamba murtadi havumuliki kuachiwa huru.

 

 

VIII. Adhabu Kwa Murtadi

 

 

‘Ulamaa wa Kiislamu wametofautiana kuhusiana na adhabu ya Murtadi. Baadhi ya ‘ulamaa wanakubali Murtadi kuhukumiwa kifo na wengine wanaeleza kuwa Murtadi hafai kuuliwa. ‘Ulamaa wasiokubali adhabu ya kifo wanatoa hoja kuwa hakuwahi murtadi kuhukumiwa kifo kwenye kipindi cha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alyhi wa aalihi wa Sallam). Bila ya shaka kila ‘Ulamaa ametoa maelezo ya kutosha kuhusiana na Hukmu ya Murtadi ambapo sio lengo la makala hii kuyaweka wazi.

 

Ni vyema hapa kueleza kuwa Muislamu lazima aheshimu maisha, mali na heshima ya Muislam mwenzake kama alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hijjatul widaa (Hijja ya mwago): “Enyi watu damu zenu (kuua), mali zenu (kunyang’anya, kuiba) ni haraam kwenu hadi mtapokutana na Rabb wenu…”

 

 

Dini ya Uislaam ni dini tukufu yenye malengo na mipangilio bora kabisa ya hukumu zake. Na ndio maana Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) ameyapa heshima maisha (roho) ya mwanaadamu, lakini kwa hali nyingine, huenda akafanya uhalifu hadi ukamfanya kuwa hastahiki tena kuishi. Sasa cha kujiuliza kama haini ana adhabu ya kifo, kwanini Uislaam ambao ndio dini tukufu isiwe na adhabu ya kifo kwa murtadi?

 

 

Na hii ndiyo maana mtu atakayetoka katika dini, akinyamaza kimya asiseme kitu, hawezi kuhukumiwa kama ni murtadi. Na hii ni kwasababu Waislamu hawatakiwi kufuatilia na kuchunguza aibu na matendo ya watu yaliyotendwa kwa kujistiri au kwa kujificha. Bali wanahesabiwa kwa matendo yaliyofanywa kwa jahara tena pawe na ushahidi usio na shaka kuwa mtu huyo anajuwa analotenda na alilikusudia.

 

Hata hivyo, aya zifuatazo ndani ya Qur-aan ni muhimu kuzibainisha:

 

فَإِن تَابُوا وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ فَإِخْوَانُكُمْ فِي الدِّينِ ۗ وَنُفَصِّلُ الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَعْلَمُونَ﴿١١﴾ وَإِن نَّكَثُوا أَيْمَانَهُم مِّن بَعْدِ عَهْدِهِمْ وَطَعَنُوا فِي دِينِكُمْ فَقَاتِلُوا أَئِمَّةَ الْكُفْرِ ۙ إِنَّهُمْ لَا أَيْمَانَ لَهُمْ لَعَلَّهُمْ يَنتَهُونَ﴿١٢﴾

 

Wakitubu, na wakasimamisha Swalaah, na wakatoa Zakaah; basi ni ndugu zenu katika Dini. Na Tunafasili waziwazi Aayaat kwa watu wanaojua.Na wakivunja viapo vyao baada ya ahadi yao, na wakatukana Dini yenu, basi wapigeni vita viongozi wa ukafiri. Hakika viapo vyao havina maana. (Piganeni nao) ili wapate kukoma. [At-Tawbah: 11-12]

 

 

 

Pia katika Hadithi ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Aalihi wa Sallam).

 

Kutoka kwa Ibn Mas'uud (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye alisema: Nabiy (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa Aalihi wa sallam) kasema: “Damu ya Muislamu haiwezi kwa haki kumwagwa isipokuwa katika hali tatu:  Mzinzi Muolewa (Mtu  mzima aliyeoa/olewa), uhai kwa uhai (nafsi kwa nafsi) na kwa yule anayeacha dini  na akajifarikisha na  jama’ah (kundi) (amejitenga na watu wa dini yake” [Imesimuliwa na Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Katika Siyrah ya Sayyidna Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) yaonesha kuwa aliamua kuingia vitani na waasi wa makabila yanayoishi mbali na mji wa Madina baada ya kukataa kumpa Khalifa (huyu) mpya wa Waislamu mali ya Zaka kama walivyokuwa wakimpa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Sayyidna Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliamua kuingia vitani na waasi hao kutokana na sababu kuu mbili:

 

 

i)  Aliona kuwa huko ni kuasi, kwa sababu Zaka ni nguzo ya tatu ya Kiislamu na kukataa kuitoa ni kuikataa nguzo hiyo.

 

 

ii)  Aliona pia kuwa kunyamazia mambo hayo kutasababisha kutokea uasi wa aina nyengine, maana watu watakapoona kuwa pana udhaifu katika uongozi, kila mmoja atataka kuiweka sheria mikononi mwake.

 

Makala hii, haina lengo la kueleza kwa undani adhabu ya Murtadi ila tu kueleza kuwa huko kuasi Uislaam ni kosa kubwa kama Siyrah ya Sayyidna Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) inaonesha kupigana vita na Waasi walioacha tu kulipa Zaka seuze atakayertadi na kuanza kumtukana Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Mifano ni mingi tu ya watu waliortadi ambao wameleta athari mbaya kwa Uislaam na Waislamu. Jee, Uislaam uwaachie tu watu hawa ambao wanajulikana kuleta fitna kubwa ndani ya jamii hii tukufu? Salman Rushdie ni kinara wa Murtadi katika karne ya 20. Kitabu chake cha Satanic Verses (Aayah za Shetani) kilichochapishwa mwaka 1988 kilizua mtafaruku mkubwa. Ameeleza ndani ya kitabu hicho kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliongeza aayah ndani ya Qur-aan zinazokubali kuwa kuna Miungu watatu ambao walikuwa wakiabudiwa Makkah (Astaghfiru Allaah).

 

Sasa cha kujiuliza, mtu kama huyu aliyekuwa Muislamu aachiwe tu hivi hivi kama vile hakufanya kosa? Ukweli ni kuwa haiwezekani, ni lazima tu aadhibiwe. Uhakika ni kuwa Salman anaufahamu ukweli upo wapi ila ametaka kuipotosha jamii pamoja na kuzua mtafaruku kwa Waislamu.

 

Bila ya shaka Murtadi anayejiingiza kwenye ujasusi na kuupiga vita Uislaam kwa kuitukana Qur-aan, kumtukana Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi aalihi wa sallam) atakuwa na adhabu kali zaidi kuliko yule aasi atakaeacha kuswali, kufunga n.k.

 

 

Kwa lugha nyepesi wote hapo juu wanaangukia kundi la Waasi na kuukana Uislaam kwa kurtadi ni kosa kwa misingi ya Sheria ya Kiislamu tofauti kabisa inavyoeleza Katiba ya Zanzibar.

 

 

IX. Athari Ya Kurtadi Kwa Ndoa

 

 

Yafuatayo ni maelezo ya Sheikh Ahmad Kan’ani kutoka kitabu chake cha Usulul Al Ma’ashirati Al-Zawjiyah (Misingi Ya Maisha Ya Ndoa):

 

Wamekubaliana ‘Ulamaa walio wengi kuwa ikiwa mume au mke aliyeritadi, zinaondoka halali zote baina ya mume na mke. Walichotofautiana ‘Ulamaa ni muda gani hiyo ndoa inaharibika (baada ya kurtadi) na namna gani inaharibika, ama kwa muda (temporary) au moja kwa moja (permanent).

 

 

Imamu Wakuu Wanne Wanaeleza Kama Ifuatavyo:

 

Imam Shafi’iy na Hanbali wameafikiana kuwa murtadi anapotubu, anamrudia mwenza bila ya akdi mpya ikiwa kwa mke aliyeingiliwa. Kwa yule mke aliyekuwa hajawahi kuingiliwa na akaachika kwa sababu ya murtadi, talaka yake imebainika wazi (dumu milele). Ama mke aliyeachika kwa murtadi na akamaliza edda, basi akdi mpya itakuwa lazima.

 

 

Kwa upande wa Imam Abu Haniyfah anasema kuwa anaportadi mmoja wao, huharibika ndoa pale pale na inatokea haraka bila ya kuhukumu Qadhi kwa jambo hilo. Anapotubu murtadi na akataka kumrejea mkewe, hamna budi kufunga ndoa mpya.

 

 

Kwa kumalizia na Imam Maalik anaeleza kuwa, kurtadi inabainisha talaka moja iliyo wazi na yenye kudumu haraka. Hamna budi baada ya hapo kufunga ndoa mpya.

 

 

X.  Hitimisho

 

Uislaam haukubaliani kutumia nguvu (Jihaad) kumlazimisha mtu kuingia kwenye Uislaam. Njia zote za udanganyifu, uongo na hata hiyo nguvu hazina nafasi katika kulingania Uislam kama Qur-aan inavyoeleza kuwa:

لَا إِكْرَاهَ فِي الدِّينِ ۖ 

 Hapana kulazimisha katika Dini[13], [Al-Baqara:256]

 

 

Kwani kila kitu kipo wazi, anayeasi ni yeye na Rabb wake, tunamshukuru Allaah (Subhanaahu wa Ta’aalaa) kutupa neema ya kuwa Waislamu kwani Mushrikuun wote wataulizwa kuhusiana na upotovu wao.

 

 

Tufahamu kuwa kutolazimishana huku ni kwa Washirikina tu, ama baina ya Waislamu ni lazima kulazimishana katika kuswali, kutoa Zakah n.k. kwani ni wajibu wa kila Muislamu aliye mukallaf (aliyelazimika).

 

 

Vikwazo hivyo hivyo ndivyo vinavyomzuia na kumlazimisha Muislamu asiingie kwenye shirki, kwani ukweli umeshambainikia juu yake. Ni sawa na mtu mwenye akili timamu aliyeoga, akajipaka manukato mazuri na kuvaa nguo za halali akataka kujichafua. Mtu huyo tutamtambua ni mtovu wa adabu tu. Hivyo, Muislamu sahihi hatakiwi kugeuka kuwa Murtadi na ni kosa la jinai ndani ya Uislaam.

 

 

Jamii ya Waislamu duniani imekuwa ikihadaiwa sana na utamu huu wa dunia hadi kufikia Waislamu kubadili dini na wengine kuoa/kuolewa na wasokuwa Waislamu mpaka kupelekea nao pia kubadili dini. Mambo haya hata Zanzibar yanatendeka, kwani Waislamu wanadanganywa kwa kupewa mali au cheo na kadhalika kisha kuingia katika ukafiri. Baadhi ya murtadi wenye asili ya kizazi cha Zanzibar wamefikia hadi kubakia na majina yao asili yanayoonesha kuwa ni Waislamu ilhali wanaingia Kanisani na kunena kuwa Mungu (Allaah) ni watatu. Murtadi huyu kama si jasusi kwa Waislamu wa Zanzibar ni nani?

 

 

Kuzungumza ukweli ni kuwa Katiba ya Zanzibar ni chimbuko la Tamko la Pamoja Kuhusiana na Haki Kuu za Binaadamu (Universal Declaration of Human Rights) kwani misingi yake ya haki ya kuabudu inafanana sana na Kifungu cha 18 cha Tamko la Pamoja Kuhusiana na Haki Kuu za Binaadamu[14].

 

 

Dini Tukufu ya Kiislamu hairuhusu Muislamu kuukana Uislaamu na hivyo vikwazo vimewekwa kwa anayejaribu au atakayebadili dini na tunarudia kusema ni kosa la jinai. Tofauti na Tamko la Pamoja Kuhusiana na Haki Kuu za Binaadamu (Universal Declaration of Human Rights) Kifungu cha 18 kinachoruhusu mtu kubadili dini. Itambulike kuwa Kifungu hicho hakina nafasi kwa Waislamu na hatakiwi kuwa huru kupita mipaka kwa kuzicheza shere Sheria za Kiislamu.

 

 

Mmoja anaweza kusema Kifungu hicho cha 18 cha Tamko la Pamoja Kuhusiana na Haki Kuu za Binaadamu kinaleta maelewano baina ya wananchi na hivyo Uislaam ni budi ufuate uhuru wa kubadili dini. Tunamjibu kuwa Uislaam umekamilika na zipo sheria zinazoeleza namna ya kukaa na Mushrikuun kwa kuandikiana Mkataba baina ya Taifa la Kiislamu na Mushrik aliye chini ya himaya ya Dola la Kiislamu (Dhimmi). Mtu huyo ana haki kamili za kuabudu, kutangaza dini yake, kuishi kwa amani na mali yake, pamoja na kumhakikishia kuwa damu yake inalindwa kama ilivyo ya Muislamu. Hayo ni maelewano na uhuru tosha lakini sio uhuru wa kuchupa mipaka kwa murtadi kuutukana Uislaam (kwa kisingizio cha uhuru wa kuabudu) na kuachiwa huru kama vile hakufanya kosa. Hilo haliwezi kukubalika wala kuvumiliwa ndani ya Uislaam.

 

 

XI   Marejeo:

 

 

 

 • Apostacy And Its Punishment In Islam, Rahman S.
 • The Punishment of The Apostate According To Islamic Law, Islamic Publishers Ltd, Lahore – Pakistan, 1963.
 • Black’s Law Dictionary, Bryan A Garner, West Paul, United States Of America, 7th Edition, (1999).
 • Criminal Law Of Islam, Vol. 1, 2, 3, And 4. Abdul-qadir.
 • Criminal Law Cases And Materials, Smith & Hogan, 7th Edition, Butterworths, London, Edinburgh, Dublin (1999).
 • Islam And The Modern Materialistic Thought, 1985.
 • Katiba Ya Zanzibar, 1984.
 • Punishment in Islamic Law, Mohammed S., 1st Edition, (2001).
 • Shariah The Islamic Law, Abdur – Rahman I 1984, Reprint In1997.
 • Haki Za Wasio Waislamu Katika Dola Ya Kiislamu, Profesa Swalih Husayn Al-aayid, Mfasiri: Abu Filistin Ghazzaawi.
 • Tafsiri Ya Qur-aan Na Sheikh Abdullah Saleh Al-farsy (allaah Amrehemu).
 • Usulul Al Ma’ashirati Al-zawjiyah (misingi Ya Maisha Ya Ndoa), Sh. Muhammad Ahmad Kan’ani, Chapa Ya Kwanza, (1996), Beirut-lebanon.
 • Zanzibar Penal Act No. 6 Of 2004

 

 

 Websites:

 

 

[1] Rudia makala ya Hapana Kulazimishana Katika Dini.

 

[2] Kifungu 28 cha Makosa ya Jinai Zanzibar Namba 6 ya mwaka 2004.

 

[3] The Punishment of the Apostate according to Islamic Law, published by Islamic 

   Publishers Ltd., Lahore, 1963.

 

[6] Ibid.

 

[7] Bryan A Garner, Black’s Law Dictionary, West Paul, United States of America, 7th edition, (1999)

 

[8] The Universal Declaration of Human Rights signed on 10/12/1948, published by the United Nations Department of Public Information, Article 18 page 11, Reprint – DPI/876/Rev.2 – 98- 08598- April 1998.

 

[9] Sheria ya Mufti 2001 (Zanzibar’s 2001 Mufti Act)

 

 

[10] Angalia gazeti la GUARDIAN Machi 6, 2003 lenye habari inayosomeka “Zanzibar Muslims must get Mufti’s permit before meetings”.

 

[11] Apostacy In Islam  pg 2 of 6.

 

[12] The United Kingdom Criminal Law Act 1977, Section 1.

 

[13] Aayah hii ameieleza mwanachuoni wa Marekani Edwin Calgary katika kitabu chake The Near East: Society And Culture, pp. 163-16 kama ifuatavyo: “Hakuna aya tukufu katika Quran ambayo imejaa ukweli na busara, na inayojulikana na Waislamu wote. Kila mmoja anatakiwa kuijua pia; ni ile inayosema ‘Hakuna kulazimishwa mtu kuingia katika dini’.

 

[14] Universal Declaration of Human Rights, Article 18 reads: “Everyone has the right to freedom of thought, conscience and religion; this right includes freedom to change his religion or belief, and freedom, either alone or in community with others and in public or private, to manifest his religion or belief in teaching, practise, worship and observance.” [Emphasis underlined].

 

 

 

Share