Kuweka Picha Katika Album

 

SWALI:

Assalam Alaykum ndugu zangu na nawatakia kila la kheri alhidaaya wote na Mwenyezi Mungu awajaliye kila la kheri na mzidi kutusaidia....inshaalah ameen swala langu ni: najua kutundika picha katika nyumba  ni vibaya, je  ikiwa una picha katika nyumba ambazo zimo kwenye album au kama umezihifadhi katika envelop, je pia hawaingii malaika wema katika nyumba na ni vibaya?

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani kwa swali lako hili kuhusu suala la picha za fotografu na pengine michoro.

 

Suala la picha limekatazwa katika Ahaadiyth nyingi. Kadhaalika 'Ulamaa wamekemea sana na kuhadharisha watu kujishughulisha na mapicha yasiyo ya dharura ambayo shari'ah haijaruhusu.

Hadiyth hizi zifuatazo zinaonyesha ubaya wa kutundika picha na kuweka picha majumbani:

Ya kwanza:

Imetoka kwa 'Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: "Nilitayarisha chakula kisha nikamualika Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Alipokuja na akaona picha katika nyumba akageuka kuondoka. Nikamuambia: Ewe Mjumbe wa Allaah, jambo gani lililokurudisha, baba yangu na mama yangu wawe fidia yako? Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Kuna pazia katika nyumba hii ambalo lina picha, na Malaika hawaingii katika nyumba yoyote yenye picha” Ibn Maajah na Abu Ya'laa

Ya pili:

Imetoka kwa mama wa waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) ambaye alisema kwamba alinunua mito ambayo ilikuwa ina picha. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipoiona alisimama mlangoni na hakuingia. Nikatambua kuchukizwa kwake sana usoni mwake. Nikasema: "Ewe Mjumbe wa Allaah, ninatubu kwa Allaah na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Wake, nimefanya nini?" Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akauliza, “Mto gani huu?” Nikasema: Nimekununulia wewe ili uukalie na uutumie kama mto. Akasema: “Hakika watu picha hizi [katika riwaaya nyingine] ((wale wanaochora picha hizi) wataadhibiwa siku ya Qiyaamah na wataambiwa: Vipeni uhai katika vile mlivyoviumba! Nyumba ambayo inayo picha kama hizi hawaingii Malaika” ’Aaishah akasema: Hakuingia tena hadi nilivyoondosha mto". Al-Bukhaariy, Muslim na wengineo

 

Ya tatu:

Kutoka kwa Aslam mkombolewa wa 'Umar, kwamba "'Umar ibnul-Khatw-Twaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuja Ash-Shaam. Mtu mmoja katika Manaswara alitayarisha chakula na akamuambia 'Umar: 'Nitapenda uje kwangu ili unipe heshima [muwe wageni wangu wa heshima] pamoja na Swahaba zako'. (Huyo mtu alikuwa ni mkuu miongoni mwa watu wa Ash-Shaam). 'Umar akamuambia, 'Hatuingii makanisa yenu kwa sababu ya mapicha yaliyomo humo.' Al-Bayhaaqiy: Swahiyh

 

Ya nne:

Imetoka kwa Abu Mas'uud 'Uqba bin 'Aamir kwamba mtu mmoja alimtayarishia chakula kisha akamualika. Abu Mas'uud akamuuliza yule mtu: 'Je kuna picha katika nyumba?" Yule mtu alimjibu: 'Ndio'. Hivyo Abu Mas'uud alikataa kuingia hadi picha zilipovunjwa kisha akaingia. Al-Bayhaaqiy: Swahiyh

Upigaji wa picha kwa dharura na haja fulani kama picha za vitambulisho, pasi za safari, za wahalifu wanaotafutwa, n.k. hizo zinakubalika kishari'ah.

Kwa yote haya tuliyoyasema ni kuwa picha hizi za kamera hazifai kupigwa na kutundikwa wala kuwekwa kwenye ma-Album kwa sababu hakuna faida yoyote ya kufanya hayo zaidi ya kujikumbusha mambo ya kidunia na pia hazina manufaa na msaada wowote katika kujenga Iymaan na Uchaji Allaah wa mtu. vilevile kunamuingiza mtu kwenye madhara ambayo tumeyaona kwenye Hadiyth zilizopita.

Hapana shaka kuwa ni haramu kupiga picha na kuweka majumbani na maofisini kuzitundika kutani na kukusudia kuziona na kuziangalia. Na wale wanaotundika picha zao za Harusi wanazidisha maovu hayo na wengi wao huwa wanaweka picha za wake zao wakiwa wazi sehemu za mwili wao unaohitajiwa kufunikwa na kusitiriwa kisheria. Hawaoni ubaya wala wivu wanaume kuingia na kutazama picha ya mke wake akiwa wazi na huku kajipamba. Hayo yote pia husababisha fitna na kuchangia maasi mbalimbali. Na wanaoweka picha kwenye Album wakija wageni wawaonyeshe kwa fakhari waliyokuwa wameyafanya kama kusafiri nchi mbalimbali na makumbusho mbalimbali, au harusi yao ilivyofana n.k., wao pia wanaingia kwenye maasi hayo vilevile. 

Tunakushauri ndugu yetu, na wale wote wenye mapicha majumbani mwao au masanamu, au vinyago n.k. waondoshe haraka na wajilinde na adhabu za Allaah na makemeo ya Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Ama picha za vitu visivyo na roho, kama picha za kitabia kama milima, miti, bahari, mito, mbuga, pori, magari, na vyote visivyokuwa viumbe vyenye roho, basi vinakubalika kuchora, kupiga na hata kutundikwa.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share