Anapenda Kuangalia Machafu Kisha Anatubu, Kisha Anarudia Tena, Naye Anachukia Jambo Hili

Anapenda Kuangalia Machafu Kisha Anatubu, Kisha Anarudia Tena, Naye Anachukia Jambo Hili

www.alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Assalamu aleikum

Mimi nahitaji usaidizi wenu kawaida nkifika kazini hua nna hamu ya kuangalia machafu katika computer hua kama sina akili napokwisha kuangalia najuta na naanza kustaghfiru kwa allah subhanahu wataala, hua sipendi kuangalia lakini kama ni shaytan ananijia niangalie sifurahii kabisa lakini silijui tatizo langu liko wapi, na nnaposali namuomba allah aniepushe mbali na kuangalia lakini bado nimo katika kuangalia. Jee, munanipa ushauri gani ulio mzuri? kwa kweli inshallah nakuombeeni kheri wa billah tawfiq

 

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kupenda kutazama machafu, na baadaye kujuta.

Hukutueleza mengi kuhusu wewe mwenyewe ili tupate kukunasihi kwa hayo uliyo nayo. Kinga kubwa ya mtu kuondoka na machafu ni kuoa, kwani Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuambia:

 

“Enyi kongamano la vijana! Yeyote mwenye uwezo wa kuoa basi aoe kwani hiyo inamfanya mtu ainamishe macho chini na ni twahara kwa uchi wake. Na kwa asiyeweza basi afunge, kwani funga ni kinga” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Kwa hiyo, ni vyema uoe ikiwa una uwezo na ikiwa huna basi funga, funga ya Sunnah kwani hiyo itakulinda na machafu.

 

Pia mara nyingi hufanya makosa na madhambi kwa kutojua wala kutofahamu tunayemkosea. Tufahamu tunayemkosea ni Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Ukisha fahamu ukubwa wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) basi ufahamu huo utakufanya usiyaendee madhambi yakiwa madogo au makubwa. Ama mambo mengine ambayo unaweza kufanya ili kujiondoa na madhambi au makosa ni kama njia zifuatazo:

 

1.       Usomaji wa Qur-aan, pamoja na kuielewa maana yake na kufanya juhudi kuyatenda yaliyo ndani yake.

 

2.       Kuwa na marafiki wema ambao watakuwa ni kioo kwako na kukurekebisha unapokwenda kombo.

 

3.       Kuweka muda wa kuleta Adhkaar za asubuhi na jioni na nyenginezo, na huku unamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa ikhlaasw na Akuondoe katika madhambi.

 

4.       Kuweka muda wa kufanya mazoezi kwani kujikalia tu ndio akili huranda randa na kuvutiwa katika maovu.

 

5.       Weka muda wa kusoma vitabu vyenye kukuelekeza katika Dini na maadili na kusikiliza mawaidha ya Kidini.

 

6.       Kushiriki katika kusaidia watu wengine.

 

7.       Kuyazingatia madhara yanayopatikana kwa kutazama picha au filamu mbaya za ngono. Ukisikiliza au kusoma madhara yake hiyo itakuwa ni njia moja ya kukufanya wewe uache mbali na kuwa ni haramu na unapata madhambi.

 

Wanachuoni wamekubaliana kuwa tawbah ni lazima kwa kila dhambi mja analofanya. Kwa hiyo ni muhimu mtu kutubia na kurudi kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ili asipate adhabu anapokufa. Masharti yanayofaa kutimizwa ili asamehewe madhambi ni kama yafuatayo:

 

1.       Kuacha madhambi hayo, kuhusiana na wewe ni kuacha kutazama picha hizo chafu kwenye kompyuta.

 

2.       Kujuta kwa kufanya hilo kosa.

 

3.       Kuazimia kutorudia tena kosa ulilolifanya.

 

Ikiwa Muislamu anajua kuwa analofanya ni kosa kisha akawa hawezi kujidhibiti ila kulirudia kosa hilo hilo mara kwa mara ni kuonyesha azma yake haina nguvu. Inabidi Muislamu apigane na matamanio yake, kwani kushindwa kuyashinda ni kuwa umeyafanya hayo maaswi kuwa ndio miungu na hivyo kuingia katika ushirikina.

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate manaufaa zaidi:

 

Kurudia Makosa Kila Mara Tawbah Inafaa?

 

 

Hakika ni kuwa ukiwa na azima ya nguvu basi kuacha kosa hilo na jingine lolote itakuwa ni rahisi sana kwa Muislamu. Inatakiwa uwe kila wakati useme A‘udhu Billaahi minash Shaytwaanir Rajiym, ili upate ulinzi wa kutoka kwa Allaah Aliyetukuka.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share