06-Wasiya Kumi Katika Mwisho Wa Suwrah Al-An'aam: Kutokuikaribia Mali ya Yatima Ila Kwa Kukusudia Ihsaan

 

Wasiya Kumi Katika Mwisho Wa Suwrah Al-An'aam  

 

06-Kutokuikaribia (Kutumia) Mali ya Yatima Ila Kwa Kukusudia Ihsaan

 

 

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

 

 وَلَا تَقْرَبُوا مَالَ الْيَتِيمِ إِلَّا بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ حَتَّىٰ يَبْلُغَ أَشُدَّهُ

 

“Na wala msiikaribie mali ya yatima isipokuwa kwa njia ya ihsaan mpaka afikie umri wa kupevuka. [Al-An’aam: 152]

  

 

Mwenye kula mali ya yatima bila ya haki ni kama kula moto tumboni mwake na juu ya hivyo atapata adhabu ya moto. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

إِنَّ الَّذِينَ يَأْكُلُونَ أَمْوَالَ الْيَتَامَىٰ ظُلْمًا إِنَّمَا يَأْكُلُونَ فِي بُطُونِهِمْ نَارًا ۖ وَسَيَصْلَوْنَ سَعِيرًا ﴿١٠﴾

Hakika wale wanaokula mali ya mayatima kwa dhulma hapana shaka kwamba wanakula katika matumbo yao moto, na watauingia moto uliowashwa vikali mno. [an-Nisaa: 10]

 

 

Hali kadhalika haifai kuikaribia mali ya yatima kwa ubadhirifu, na kuwabadlishia vizuri vyao kwa vilivyo vibaya. Anaonya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa): 

 

وَآتُوا الْيَتَامَىٰ أَمْوَالَهُمْ ۖ وَلَا تَتَبَدَّلُوا الْخَبِيثَ بِالطَّيِّبِ ۖ وَلَا تَأْكُلُوا أَمْوَالَهُمْ إِلَىٰ أَمْوَالِكُمْ ۚ إِنَّهُ كَانَ حُوبًا كَبِيرًا ﴿٢﴾ 

Na wapeni mayatima mali zao, na wala msibadilishe kibaya (chenu) kwa kizuri (chao). Na wala msile mali zao pamoja na mali zenu. Hakika hilo limekuwa ni dhambi kubwa. [An-Nisaa: 2]

 

Anayelea Yatima amekuwa na jukumu kubwa mbele ya Allaah, kwa hivyo inampasa mlezi huyo atahadhari mno na ajiepushe kuwadhulumu kwa hali yoyote ile.

 

Zilipoteremshwa Aayah hizo kuhusu mayatima pamoja na Aayah ya 10 Suwratun-Nisaa tuliyoinukuu juu hapo, Maswahaba waliokuwa wakilea mayatima, walikhofu hata kuchanganyika kula nao. Khofu yao iliwafanya hadi kwamba waogope kula chakula chao kilichokuwa kikibakia, wakawa wanakiweka na kurudia tena kuwapa au kukiwacha kiharibikeHali hii ilikuwa ngumu kwao ndipo walipomkabili Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuuliza. Maelezo ni kama ilivyothibiti katika Hadiyth:

 

عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ، قَالَ لَمَّا نَزَلَتْ هَذِهِ الآيَةُ ((‏وَلاَ تَقْرَبُوا مَالَ الْيَتِيمِ إِلاَّ بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ))‏ وَ‏((‏إِنَّ الَّذِينَ يَأْكُلُونَ أَمْوَالَ الْيَتَامَى ظُلْمًا‏))‏ قَالَ: اجْتَنَبَ النَّاسُ مَالَ الْيَتِيمِ وَطَعَامَهُ فَشَقَّ ذَلِكَ عَلَى الْمُسْلِمِينَ فَشَكَوْا ذَلِكَ إِلَى النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم فَأَنْزَلَ اللَّهُ: ((‏وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْيَتَامَى قُلْ إِصْلاَحٌ لَهُمْ خَيْرٌ‏)) ‏ إِلَى قَوْلِهِ ‏((‏لأَعْنَتَكُمْ‏)).

 

Imepokelewa kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kwamba pale Aayah hizi zilipoteremshwa: 

 

 ‏وَلاَ تَقْرَبُوا مَالَ الْيَتِيمِ إِلاَّ بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ

 

 “Na wala msiikaribie mali ya yatima isipokuwa kwa njia ya ihsaan…”

 

إِنَّ الَّذِينَ يَأْكُلُونَ أَمْوَالَ الْيَتَامَى ظُلْمًا‏)

 

 “Hakika wale wanaokula mali ya mayatima kwa dhulma…”   akasema: Watu walijiepusha na mali ya yatima pamoja na chakula chake, ikawa ni mashaka kwa Waislamu wakashitaki kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)     hapo ikataremka:

 

 ‏وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْيَتَامَى قُلْ إِصْلاَحٌ لَهُمْ خَيْرٌ

“Na wanakuuliza kuhusu mayatima. Sema: “Kuwatengeneza ni kheri…” mpaka kauli Yake:

 

لأَعْنَتَكُمْ‏

“Angelikutieni katika shida.” [Sunan An-Nasaaiy katika Kitaab Al-Wiswaayaa, Baab maa lil-waswiyyi min maal al-yatiym idhaa qaama ‘alayhi].

 

 

 Aayah kamili ni kama ifuatavyo:

 

 وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْيَتَامَىٰ ۖ قُلْ إِصْلَاحٌ لَّهُمْ خَيْرٌ ۖ وَإِن تُخَالِطُوهُمْ فَإِخْوَانُكُمْ ۚ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ الْمُفْسِدَ مِنَ الْمُصْلِحِ ۚ وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ لَأَعْنَتَكُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ ﴿٢٢٠﴾

Na wanakuuliza kuhusu mayatima. Sema: “Kuwatengeneza ni kheri.  Na Allaah Anamjua fisadi na mtengenezaji. Na lau Angetaka Allaah Angelikutieni katika shida.” Hakika Allaah ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote. [Al-Baqarah: 2:220]

 

 

 

 

 

Share