07-Wasiya Kumi Katika Mwisho Wa Suwrah Al-An'aam: Kutimiza Vipimo Na Mizani Kwa Uadilifu

 

Wasiya Kumi Katika Mwisho Wa Suwrah Al-An'aam  

 

07- Kutimiza Vipimo Na Mizani Kwa Uadilifu

 

 

 

 

 Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):  

 

وَأَوْفُوا الْكَيْلَ وَالْمِيزَانَ بِالْقِسْطِ

 

Na timizeni kipimo na mizani kwa uadilifu [Al-An'aam: 152]

 

 

Ni amri ya kutekeleza haki wakati wa kutoa na kupokea, kununua na kuuza kama Anavyoonya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 وَيْلٌ لِّلْمُطَفِّفِينَ ﴿١﴾

Ole kwa wanaopunja.

 

الَّذِينَ إِذَا اكْتَالُوا عَلَى النَّاسِ يَسْتَوْفُونَ ﴿٢﴾

Ambao wanapopokea kipimo kwa watu wanataka wapimiwe kamilifu.

 

 

وَإِذَا كَالُوهُمْ أَو وَّزَنُوهُمْ يُخْسِرُونَ ﴿٣﴾

Na wanapowapimia (watu) kwa kipimo au wanawapimia kwa mizani wanapunja.

 

 

أَلَا يَظُنُّ أُولَـٰئِكَ أَنَّهُم مَّبْعُوثُونَ ﴿٤﴾

Je, hawadhanii kwamba wao watafufuliwa?

 

 

لِيَوْمٍ عَظِيمٍ ﴿٥﴾

Kwenye Siku adhimu.

 

 

يَوْمَ يَقُومُ النَّاسُ لِرَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٦﴾

Siku watakayosimama watu kwa Rabb wa walimwengu. [Al-Mutwaffifiyn: 1-6]

 

 

Kutokupima kwa uadilifu ni kumdhulumu mtu haki yake ambayo ni dhulma isiyosameheka hadi dhalimu amrudishie aliyemdhulumu hapa hapa duniani, laa sivyo Akhera itasimama mizani ya haki na hapo dhulma zote zitadhihirika na kila aliyemdhulumu mwenziwe atamlipa kwa mema yake na kutupiwa yeye dhalimu madhambi ya aliyedhulumiwa, kama ilivyothibiti katika Hadiyth:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ (صلى الله عليه و آله وسلم) قَالَ:  ((مَنْ كَانَتْ عِنْدَهُ مَظْلَمَةٌ مِنْ أَخِيهِ مِنْ عِرْضِهِ أَوْ  مِنْ شَيْءٍ  فَلْيَتَحَلَّلْهُ مِنْهُ الْيَوْمَ قَبْلَ أَنْ لاَ يَكُونُ دِينَارٌ وَلاَ دِرْهَمٌ ، إِنْ كَانَ لَهُ عَمَلٌ صَالِحٌ أُخِذَ مِنْهُ بِقَدْرِ مَظْلَمَتِهِ. وَإِنْ لَمْ يَكُنْ لَهُ أُخِذَ مِنْ سَيِّئَاتِ صَاحِبِهِ فَحُمِل عَلَيْهِ))  رواه البخاري

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu)    kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amesema: ((Aliyekuwa na kitu cha dhulma cha nduguye kutokana na kumvunjia heshima au kitu chochote, basi amuombe amhalalishie leo kabla haijafika siku ambayo hakutakuwa na dinari wala dirham. Ikiwa ana ‘amali njema, basi zitachukuliwa kwa kadiri ya alichodhulumiwa. Na ikiwa hana, basi zitachukuliwa dhambi za aliyemdhulumu abebeshwe)). [Al-Bukhaariy.]

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anahimiza kupima kwa haki katika Aayah nyinginezo kwa kauli Zake:

 

 

 وَأَوْفُوا الْكَيْلَ إِذَا كِلْتُمْ وَزِنُوا بِالْقِسْطَاسِ الْمُسْتَقِيمِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا ﴿٣٥﴾

Na timizeni kamilifu kipimo mnapopima, na pimeni kwa kipimo cha sawasawa. Hivyo ni kheri na bora zaidi matokeo yake. [Al-Israa: 35]

 

 

Na pia Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 أَلَّا تَطْغَوْا فِي الْمِيزَانِ ﴿٨﴾

Ili msivuke mipaka (kudhulumu) katika mizani.

 

 

وَأَقِيمُوا الْوَزْنَ بِالْقِسْطِ وَلَا تُخْسِرُوا الْمِيزَانَ ﴿٩﴾

Na simamisheni uzani kwa uadilifu, na wala msipunguze mizani. [Ar-Rahmaan: 8-9]

 

 

Makatazo haya yanawahusu zaidi wenye kufanya biashara. Mfanya biashara anapaswa kupima anachouza kwa haki bila ya kupunguza. Mfano ikiwa mnunuajia amelipia kitu cha kilo 2, basi muuzaji apime hivyo hivyo, isipungue ikawa kilo 1.9 au chini yake. Ama muuzaji akipenda mwenyewe kumzidishia mnunuaji, hivyo ni jambo zuri la wema lakini     kupunguza haifai kabisa.

 

 

Kipimo cha haki pia inakusudiwa kutokuuza kitu  kibaya au kughushi kwa aina yoyote ile katika uuzaji.     Yote hayo inakuwa ni dhulma katika kumuuzia mtu kitu. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Ameharamisha katika Hadiyth:

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ مَرَّ عَلَى صُبْرَةِ طَعَامٍ فَأَدْخَلَ يَدَهُ فِيهَا فَنَالَتْ أَصَابِعُهُ بَلَلاً فَقَالَ: ((مَا هَذَا يَا صَاحِبَ الطَّعَامِ؟)) قَالَ:  أَصَابَتْهُ السَّمَاءُ يَا رَسُولَ اللَّهِ. قَالَ: ((أَفَلاَ جَعَلْتَهُ فَوْقَ الطَّعَامِ كَيْ يَرَاهُ النَّاسُ، مَنْ غَشَّ فَلَيْسَ مِنِّي))  مسلم

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alipitia katika mrundo wa chakula (nafaka), akaingiza mkono wake ndani. Vidole vyake vikagusa umajimaji. Akasema: ((Ee mwenye chakula, ni nini hii?)). Akajibu: “Ee Rasuli wa Allaah! Kimepatwa na manyunyu”. Akasema: ((Si ungeliweka juu ya chakula ili watu wakione! Anayeghushi si katika mimi)). [Muslim]

 

 

Wala haipasi kuapa kwa uongo katika biashara kwa dalili Hadiyth:

 

عَنْ أَبِي ذَرٍّ (رضي الله عنه)  عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((ثلاَثَةٌ لاَ يُكَلِّمُهُمْ اللَّهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَلاَ يَنْظُرُ إِلَيْهِمْ وَلاَ يُزَكِّيهِمْ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ)) قَالَ فَقَرَأَهَا رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ثلاَثَ مِرَارٍ. قَالَ أَبُو ذَرٍّ: خَابُوا وَخَسِرُوا، مَنْ هُمْ يَا رَسُولَ اللَّهِ؟ قَالَ: ((الْمُسْبِلُ، وَالْمَنَّانُ، وَالْمُنَفِّقُ سِلْعَتَهُ بِالْحَلِفِ الْكَاذِبِ)) مسلم  

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Dharr (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: “Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Watu watatu Allaah Hatowazungumzisha Siku  ya Qiyaamah, wala Hatowatazama, wala Hatowatakasa, na watapata adhabu inayoumiza)). Akayakariri maneno hayo mara tatu. Abuu Dharr akasema: “Wamepita patupu na wamekhasirika! Ni nani hao ee Rasuli wa Allaah?”  Akasema: ((Al-Musbil - mwenye kuburuza nguo yake, mwenye kutoa na kukizungumzia [kusimbulia] alichokitoa, na mwenye kuuza bidhaa zake kwa kutumia kiapo cha uongo)). [Muslim] 

 

 

 

Watu wa mji wa Madyan ambao walitumiwa Nabiy Shu’ayb ‘('Alayhis-Salaam) walikuwa wakitenda dhulma hiyo, imetajwa katika Qur-aan:   

 

كَذَّبَ أَصْحَابُ الْأَيْكَةِ الْمُرْسَلِينَ ﴿١٧٦﴾

Watu wa Al-Aykah wamemkadhibisha Rusuli.

 

 

إِذْ قَالَ لَهُمْ شُعَيْبٌ أَلَا تَتَّقُونَ ﴿١٧٧﴾

Alipowaambia Shu’ayb: “Je hamtokuwa na taqwa?”

 

 

إِنِّي لَكُمْ رَسُولٌ أَمِينٌ ﴿١٧٨﴾

 “Hakika mimi kwenu ni Rasuli mwaminifu.

 

 

فَاتَّقُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُونِ ﴿١٧٩﴾

 “Basi mcheni Allaah na nitiini.

 

 

وَمَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ ۖ إِنْ أَجْرِيَ إِلَّا عَلَىٰ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٨٠﴾

 “Na wala sikuombeni ujira wowote juu yake.  Ujira wangu hauko isipokuwa kwa Rabb wa walimwengu.”

 

 

أَوْفُوا الْكَيْلَ وَلَا تَكُونُوا مِنَ الْمُخْسِرِينَ ﴿١٨١﴾

 “Timizeni kipimo na wala msiwe miongoni mwa wenye kupunja.

 

 

وَزِنُوا بِالْقِسْطَاسِ الْمُسْتَقِيمِ ﴿١٨٢﴾

 “Na pimeni mizani kwa uadilifu iliyosawa.

 

 

وَلَا تَبْخَسُوا النَّاسَ أَشْيَاءَهُمْ وَلَا تَعْثَوْا فِي الْأَرْضِ مُفْسِدِينَ ﴿١٨٣﴾

 “Na wala msiwapunje watu vitu vyao, na wala msieneze uovu katika ardhi hali ya kuwa ni wenye kufanya ufisadi. [As-Shu’araa: 176-183]

 

 

Kisa chao kimetajwa pia katika kauli za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 وَإِلَىٰ مَدْيَنَ أَخَاهُمْ شُعَيْبًا ۗ قَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ ۖ قَدْ جَاءَتْكُم بَيِّنَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ ۖ فَأَوْفُوا الْكَيْلَ وَالْمِيزَانَ وَلَا تَبْخَسُوا النَّاسَ أَشْيَاءَهُمْ وَلَا تُفْسِدُوا فِي الْأَرْضِ بَعْدَ إِصْلَاحِهَا ۚ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ ﴿٨٥﴾

Na kwa (watu wa) Madyan (Tuliwapelekea) kaka yao Shu’ayb.  Akasema: “Enyi kaumu yangu! Mwabuduni Allaah, hamna Mwabudiwa wa haki ghairi Yake.  Kwa yakini imekujieni hoja bayana kutoka kwa Rabb wenu. Basi timizeni kipimo na mizani wala msipunje watu vitu vyao wala msifanye ufisadi ardhini baada ya kutengenea kwake. Hivyo ni bora kwenu ikiwa mmeamini.” [Al-A’raaf: 85]

 

 

 

 

 

Share