09-Du'aa Za Ruqyah: Kinga Ya Kutolemewa Na Mitihani, Kuishilia Kwenye Naqama, Qadhwaa Mbaya na Maadui Kufurahia Misiba

 

Du’aa Za Ruqyah (Kinga): Faida Na Sharh Zake

 

Kuomba Kinga  Ya Kutolemewa Na Mitihani, Kuishilia Kwenye Naqama,

Qadhwaa Mbaya na Maadui Kufurahia Misiba

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akijilinda kwa Allaah ('Azza wa Jalla)  akisema:

 

((اللهمَّ إنِّي أعُوذُ بِكَ مِنْ جَهْدِ الْبَلَاءِ، وَدَرَكِ الشَّقَاءِ، وَسُوءِ الْقَضَاءِ، وَشَمَاتَةِ الْأَعْدَاءِ))

((Ee Allaah! Hakika mimi najilinda Kwako na kuelemewa na mitihani, kuishilia kwenye naqama, qadhwaa mbaya na kufurahia maadui misiba yangu)). [Al-Bukhaariy 6347 na Muslim 2707]

 

 

 

Faida Na Sharh:

 

 جَهْدِ الْبَلَاءِ Jahdil-Balaai maana yake ni kila zito na la tabu kubwa linalomsibu mtu,  likamlemea vibaya, naye hana uwezo wa kuliondosha au kukabiliana nalo. Ni kama kuandamwa na vyombo vya usalama kwa kupigania haki, nchi kuzama kwenye migogoro isiyomalizika, kusakamwa na magonjwa hatari na mengineyo.

 

Mitihani hii inaweza kuwa ya kimwili kama magonjwa, au ya kidhahania kama kukamiwa na watu kwa matusi, masimango, kuzushiwa na kunyanyaswa au kunyanyapaliwa.

 

 

 

درك الشقاء   Darakish-Shaqaai ni lolote lenye kumfikisha mtu pabaya na kumkosesha furaha ya maisha, sawasawa kwa upande wa maisha yake ya hapa duniani, au kwa  watu wake, au mali yake, na kadhalika. Pia kwa Aakhirah yake kama kupata adhabu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   kutokana na madhambi aliyoyachuma hapa duniani.

 

 سُوءِ الْقَضَاءِ Suw-il-Qadhwaai ni kila lile Alilokadiriwa mtu na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   ambalo linamsumbua na kumhuzunisha, au likamwingiza katika taharuki kubwa. Hili linajumuisha Dini na dunia, nafsi, ahli, mali, watoto na mwisho wa kuondoka hapa duniani.

 

 

Kuomba kinga kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  hakupingani na suala la kuridhia Alilolipitisha na kulihukumu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kwa Waja Wake. Kwa kuwa Yeye Ametutaka sisi tujilinde na qadhwaa (majaaliwa) kama hizo ingawa Yeye Ndiye Anayezipitisha. Ndio maana tunaomba katika Du’aa ya Qunuwt tunaposwali Swalaah ya Witr:

 

 

اَللَّهُمَّ اِهْدِنِي فِيمَنْ هَدَيْتَ ، وَعَافِنِي فِيمَنْ عَافَيْتَ ، وَتَوَلَّنِي فِيمَنْ تَوَلَّيْتَ ، وَبَارِكْ لِي فِيمَا أَعْطَيْتَ ، وَقِنِي شَرَّ مَا قَضَيْتَ ، فَإِنَّكَ تَقْضِي وَلَا يُقْضَى عَلَيْكَ ، إِنَّهُ لَا يَذِلُّ مَنْ وَالَيْتَ ، تَبَارَكْتَ رَبَّنَا وَتَعَالَيْتَرَوَاهُ اَلْخَمْسَةُ

(Ee Allaah! Nihidi pamoja na Uliowahidi, na Unipe ’aafiyah pamoja na Uliowapa ’aafiyah, na Nifanye kuwa ni mpenzi Wako pamoja na Uliowafanya wapenzi Wako, na Nibariki katika Ulichonipa na Nikinge na shari ya Ulilolihukumu kwani Wewe Unahukumu wala Huhukumiwi. Hakika hadhaliliki Uliyemfanya mpenzi,  Umebarikika Ee Rabb wetu na Umetukuka)  [Imetolewa na Al-Khamsah (At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah, Ahmad)]

 

 

Ni lazima tujue kuwa qadhwaa kwa upande wa mwono wa waja inagawanyika sehemu mbili; ya kheri na ya shari. Wanachotakiwa watu ni kujilinda na ile ya shari wanayoiona wao kwa akili zao za ki-bin Aadam lakini ukweli wa mambo ni kuwa qadhwaa yote ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  ambayo ni hukmu Yake na vitendo Vyake ni kheri; hakuna shari ndani yake. Kila kitu ni kwa hikma yake.  Linaloonekana ni shari kwa viumbe, basi ndani yake utakuwa pamejaa kheri kochokocho.

 

 

 

  شَمَاتَةِ الْأَعْدَاءِ Shamaatatil-a’daai ni maadui kufurahia janga linalompata hasimu yao au mtu wanayemchukia tu bila ya haki yoyote. Daima maadui hawa huomba apatwe na lolote la kumdhuru au la kumkwamisha na kadhalika. Hili likimpata mtu humchoma na kumuumiza sana kisaikolojia.

 

 

Share