10-Du'aa Za Ruqyah: Kinga Dhidi Ya Kuporomokewa, Kuanguka Toka Mwinuko Mrefu, Kughariki, Kuteketea Moto, Kuzugwazugwa Na Shaytwaan Wakati Wa Kifo, Kufa Mtu Akiikimbia Njia Ya Allaah, Kifo Kitokanacho Na Kuumwa Na Kiumbe Chenye Sumu

 

Du’aa Za Ruqyah (Kinga): Faida Na Sharh Zake

 

10-Kuomba Kinga Dhidi Ya Kuporomokewa, Kuanguka Toka Mwinuko Mrefu, Kughariki, Kuteketea Moto, Kuzugwazugwa Na Shaytwaan Wakati Wa Kifo, Kufa Mtu Akiikimbia Njia Ya Allaah Na Kifo Kitokanacho Na Kuumwa Na Kiumbe Chenye Sumu

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alikuwa ajilinda kwa Allaah akisema:

 

 

 اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنَ الْهَدْمِ، وَأَعُوذُ بِكَ مِنَ التَّرَدِّي، وَأَعُوذُ بِكَ مِنَ الْغَرَقِ، وَالْحَرَقِ، وَالْهَرَمِ، وَأَعُوذُ بِكَ أَنْ يَتَخَبَّطَنِيَ الشَّيْطَانُ عِنْدَ الْمَوْتِ، وَأَعُوذُ بِكَ أَنْ أَمُوتَ فِي سَبِيلِكَ مُدْبِرًا، وَأَعُوذُ بِكَ أَنْ أَمُوتَ لَدِيغًا

((Ee Allaah! Hakika mimi najilinda Kwako kuporomokewa na jengo, na najilinda Kwako na kuanguka toka sehemu ndefu, na najilinda Kwako kufa maji, kuungua moto na uzee. Na najilinda Kwako shaytwaani kunizugazuga wakati wa kufa, na najilinda Kwako kufa wakati nikiikimbia Njia Yako, na najilinda Kwako kufa kwa kuumwa na kiumbe chenye sumu)). [Imekharijiwa na Abuu Daawuwd 1552, An-Nasaaiy 5546, Ahmad 14/303 na Atw-Twabaraaniy katika  Al- Kabiyr 19/170. Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika Swahiyh An Nasaaiy 3/1123]

 

 

Faida na Sharh:

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)   amejilinda na kuporomokewa na jengo au jengo kuanguka mtu akiwa ndani, kuanguka toka sehemu ya mwinuko mrefu kama juu ya ghorofa refu, kughariki kama meli kuzama au kuvamiwa na mafuriko, kuteketea kwa moto na uzee.

 

Mambo haya pamoja na kwamba ndani yake ni kufariki katika daraja ya Shuhadaa kwa mujibu wa baadhi ya Hadiyth,  - yaani ikiwa yatakuwa sababu ya kifo kwa Muislamu anakufa akiwa shahidi - lakini hata hivyo, Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amejilinda nayo. Amejilinda nayo kwa kuwa ni magumu na mazito mno kwa mtu kuweza kuwa na uimara wa kutosha kuyakabili ambapo wakati huo shaytwaan anaitumia nafasi hiyo kuiteteresha iymaan ya Muislamu.

 

 

Aidha, matukio haya mara nyingi hutokea ghafla bila mtu kuyatarajia. Yanamkuta akiwa pengine hajaacha wasia au hakujiandaa ingawa mtu anatakiwa ajiandae na safari ya mauti wakati wote.

 

 

Kadhalika, matukio haya hutisha sana na hususan kwa wale wenye kuwashuhudia wahanga wakiteseka, wakipaparika, wakihaha na kuangamia bila wakati mwingine kuwa na uwezo wa kuwaokoa. Inakuwa ni hali ya kutisha na kuogofya mno.

 

Kufariki Shahidi katika matukio haya ni Shahidi ndogo kinyume na Shahidi halisia ya kufia vitani Muislamu akiipigania Dini ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).  Kufariki huku kama Shahidi  kila Muislamu anatamani na anaendea mbio ikiwa itabidi kama walivyokuwa Maswahaba pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)   katika vita mbalimbali.

 

 

Lakini ajali hizi alizojilinda nazo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  hapa, ni lazima Muislamu ajihadhari nazo na kutumia njia zote kuziepusha.

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  anatutaka kabla ya kulala, tuzime taa zote na tuhakikishe kuwa vyombo vyote vimefunikwa vyema. Kwa wenye mitungi ya gesi, wahakikishe mtungi au mitungi imefungwa vyema. Pia mabomba ya maji yamefungwa vyema, milango ya nyumba imekomelewa vizuri na kadhalika. Hii yote ni kwa ajili ya kuepusha ajali na kuchukua hadhari.

 

 

Vilevile, Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amejilinda  na kufa huku mtu akiikimbia Jihadi au kutetea Dini au haki au kumwokoa nduguye Mwislamu au bin Aadam yeyote vyovyote iwavyo Dini yake na mfano wake. Hili bila shaka ni jambo baya mno, na ni moja kati ya madhambi makubwa yenye kumwangamiza mtu.

 

 

Kadhalika, amejilinda kufa kwa kuumwa na viumbe wenye sumu kama nyoka, nge na kadhalika. Mauti haya yanakuwa ni ya kushtukiza, na pia mtu anaweza kuteseka kwa maumivu makali baada ya kuumwa, akateseka yeye pamoja na jamaa zake wanaomuuguza.

 

Bila shaka umuhimu wa kuomba du’aa hii uko wazi kabisa kutokana na tunayoyaona na kuyasikia kuhusiana na matukio kama haya. Ni matukio ya kutisha na kuogofya mno ambayo inabidi kuyachukulia hadhari zote na kuomba Msaada wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) nyakati zote.

 

 

 

 

Share