Hadiyth: Maiti: (Faida Na Sharh)

 

Hadiyth Kuhusu Maiti:

 

(Faida Na Sharh)

 

Alhidaaya.com

 

Imeandaliwa Na:  'Abdullaah Mu'aawiyah (Abu Baasim)

 

 

 

 

Hadiyth Ya Kwanza: 

 

 Amali Zinazomtetea Muislamu Kaburini Mwake Mbele Ya Malaika Wawili

 

 

 

Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaah ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

إن الميت إذا وضع في قبره، إنه يسمع خفق نعالهم حين يولوا مدبرين، فإن كان مؤمناً كانت الصلاة عند رأسه وكان الصيام عن يمينه وكانت الزكاة عن شماله وكان فعل الخير من الصدقة والصلاة والمعروف والإحسان إلى الناس عند رجليه، فيؤتى من قبل رأسه فتقول الصلاة ما قبلي مدخل، ثم يؤتى عن يمينه فيقول الصيام ما قبلي مدخل، ثم يؤتى عن يساره فتقول الزكاة ما قبلي مدخل... الحديث.

((Maiti anapowekwa ndani ya kaburi lake, kwa hakika husikia mchakato wa viatu vyao wakati wanapoondoka na kumwacha. Akiwa ni Muumini, Swalaah itakuwa kwenye kichwa chake, Swiyaam itakuwa kuliani kwake, Zakaah itakuwa kushotoni kwake, na matendo ya kheri kati ya swadaqah, Swalaah, mema na ihsaan kwa watu, yatakuwa kwenye miguu yake miwili. Atajiwa kwa upande wa kichwa chake (na Malaika wawili), na Swalaah itasema: Hakuna maingilio upande wangu. Kisha atajiwa kwa upande wake wa kulia, na Swiyaam itasema: Hakuna maingilio upande wangu. Kisha atajiwa kwa upande wake wa kushoto, na Zakaah itasema: Hakuna maingilio upande wangu.)). [Imesimuliwa na Atw- Twabaraaniy na Ibn Hibaan. Al-Albaaniy kasema ni Hadiyth Hasan].

 

 

Faida Na Sharh:

 

Hadiyth hii inazidi kutuonyesha na kutuzindusha zaidi kuhusiana na umuhimu na wajibu mkubwa kwa Muislamu kuwajibika na amali zote alizowajibishiwa na Allaah ('Azza wa Jalla)   pamoja na amali zote za Sunnah zitakazomwongezea uzito wa amali zake za kheri Siku ya Qiyaamah. Kuwajibika na amali hizi, mbali na kuwa ni kutekeleza Amri ya Allaah ambapo mja hulipata penzi Lake, pia zinakuwa ni kinga na mtetezi kwake wakati anapokuwa amezikwa na kuachwa na vipenzi vyake, marafiki zake na kila alichokuwa akikimiliki. Hao wataweza kumsaidia kwa du’aa tu na kumtolea swadaqah. Lakini watetezi wake wa kweli, watakuwa ni mambo haya yaliyotajwa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hapa.

 

 

La kwanza ni Swalaah:  Swalaah itakayomtetea ni ile iliyoswaliwa kama inavyotakikana na iliyotekeleza vigezo vyake vyote vya shuruti zake, nguzo zake, waajibaat zake, sunan zake na kadhalika pamoja na khushuu na khudhwuu na mbali kabisa na riyaa (kujionyesha).

 

 

La pili ni Zakaah: Ambayo ni Zakaah ya fardhi na ni lazima itolewe kila mwisho wa mwaka baada ya mali kufikia kiwango. Zakaah hii bila shaka huwasaidia Waislamu masikini na kuwakidhia haja zao na huwa ni kitwaharisho cha mali ya mtoaji mwenyewe.

 

 

La tatu ni Swiyaam:  Hii ni Swawm ya faradhi ya Ramadhwaan pamoja na Swawm nyingine kama Sunnah za Jumatatu na Alkhamisi, au Ayyaamul-biydhw (Masiku Meupe)   na nyinginezo.

 

 

La nne ni matendo yote ya kheri na ihsaan:  Haya ni mengi sana yasiyo na hisabu. Hii ni hata kutabasamu kwa nduguyo Muislamu, kumtweka au kumtua mzigo, kumnasihi,  kumsalimia, kwenda kumzuru akiwa mgonjwa, kwenda kumzika, kuondosha taka njiani, na kadhalika. Na kwa ajili hiyo, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  anatuusia tusidharau lolote jema hata kama tutaliona kwa makisio yetu kuwa ni dogo.

 

Bila shaka haya yote Muislamu haoni faida yake hapa duniani. Lakini faida yake ya awali, ataanza kuiona hapo ndani ya kaburi, na kisha siku ya hisabu.

 

 

 

 

Hadiyth Ya Pili: 

 

 Maiti Hufuatwa Na Vitu Vitatu

 

 

عَنْ أَنَسِ (رضي الله عنه) قَال: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم: ((يَتْبَعُ الْمَيِّتَ ثَلاَثَةٌ: أَهْلُهُ وَمَالُهُ وَعَمَلُهُ. فَيَرْجِعُ اثْنَانِ وَيَبْقَى واحِدٌ: يَرِجِعُ أَهْلُهُ وَمَالُهُ وَيَبْقَى عَمَلُهُ)) متفق عليه

Imepokelewa toka kwa Anas (Radhwiya Allaahu Anhu) akisema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah Alayhi wa Sallam) amesema: ((Vitatu vinamfuata maiti: Watu wake, mali yake na amali zake. Vinarudi viwili na kinabakia kimoja;  watu wake na mali yake hurudi, na amali yake hubaki)). [Muttafaqun Alayhi].

 

 

Faida Na Sharh:

 

Cha kwanza kinachomfuata:  Mwanadamu anapokufa, jamaa zake wa karibu wanaompenda na vipenzi vyake, ndio wanaoshughulika zaidi kufanya taratibu zote za mazishi kuanzia ainisho la kaburi atakalozikwa, kuoshwa, kukafiniwa, kuswaliwa na mengineyo husika. Na wakati wa kwenda kuzikwa, hao hao ndio wanaokuwa mstari wa mbele katika kulibeba jeneza na kulitua, na hata wakati wa kufukia, wao wanakuwa na bidii zaidi za kupiga beleshi kulijaza kaburi haraka. Na hawa ingawa wanarudi, lakini wanaweza kumfaa maiti kwa kumwombea maghfirah na rahmah, na hata kumtolea swadaqah, au kuitumia mali aliyoacha katika njia ya kheri.

 

Ajabu kubwa ya maisha ya dunia! Ni uduni ulioje wa maisha haya! Watu hawa hawa vipenzi wa maiti huyo, lau kama watapewa mali ili mwili wa maiti wabaki nao nyumbani, wasingelikubali kabisa. Juhudi yao kubwa baada ya kufariki, ni kuuzika mwili wa maiti ili uwe mbali nao kabisa. Hawa ndio watu wanaofuatana na maiti wakati anapokwenda kuzikwa.

 

 

Cha pili kinachofuatana na maiti: Ni baadhi ya vinavyohusiana na mali yake kama watumishi wake, na wafanyikazi wake kama ni mtu mwenye uwezo au hata magari yake ya kusindikiza. Hao wote na vyote hurudi baada ya kuzikwa maiti. Au inakuwa kwa maana kuwa maiti hazikwi na mali zake, bali huziacha hapa hapa duniani. Mali hizo zinaweza kumfaa kama zitalisha watoto wake, zitawasomesha na kadhalika, kwa kuwa alizichuma kwa tabu na Allaah ('Azza wa Jalla)     Hapotezi ujira wa mtenda wema.

 

 

Cha tatu kinachomfuata maiti:  Na ambacho hakirudi bali hubakia na maiti, ni amali zake mbaya au nzuri. Amali hizi ndizo zitakazokuja kuwa kipimo cha hatima yake ya kuishilia Peponi au kuishilia motoni.

 

 

Tunamwomba Allaah Azijaalie amali zetu ziwe njema ili zituokoe na hali ngumu inayotusubiri baada ya kufa. Aamiyn.

 

 

Hadiyth hii inatukumbusha tena kuwa dunia ni mahala pa kupita tu. Vyote alivyonavyo mtu na kuvimiliki, ataviacha hapa duniani. Mwenye akili, ni yule anayetumia alivyoruzukiwa na Allaah ('Azza wa Jalla)  kwa ajili ya aakhirah yake ya kesho.

 

Mwenye uwezo ni kwa kujiwekea swadaqah endelevu kwa kusaidia miradi ya kheri, mwenye elimu kwa kuisomesha, na mwenye nguvu kwa afya yake na kadhalika. Pia kwa kuwajibika na maamrisho ya Allaah ('Azza wa Jalla)  na kujiepusha na Makatazo Yake.

 

Pia kujiweka mbali kabisa na haki za watu, kwani haki hizo zitamganda, na hazitobanduka ila kwa kuchukuliwa amali zake njema Siku ya Qiyaamah.

 

Halla halla tujitahidi tuwezavyo kutenda mema ili yabaki nasi yakituliwaza makaburini mwetu ambapo ni lazima tutakwenda wakati wowote ule kabla wakati haujapita. Mahusiano na vipenzi vyetu na mali yetu, yatakatika mara moja baada tu ya roho kutoka mwilini

 

 

 

 

Hadiyth Ya Tatu: 
 

 Ayasemayo Maiti Muislamu Na Maiti Kafiri Jeneza Linabobebwa

 

 

عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيَّ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((إِذَا وُضِعَتْ الْجِنَازَةُ وَاحْتَمَلَهَا النَّاسُ – أوِ الرِّجَالُ عَلَى أَعْنَاقِهِمْ, فَإِنْ كَانَتْ صَالِحَةً قَالَتْ: قَدِّمُونِي. وَإِنْ كَانَتْ غَيْرَ صَالِحَةٍ قَالَتْ: يَا وَيْلَهَا! أَيْنَ يَذْهَبُونَ بِهَا؟ يَسْمَعُ صَوْتَهَا كُلُّ شَيْءٍ إلاَّ الإِنْسَانَ وَلَوْ سَمِعَهُ صَعِقَ)) البخاري

Imepokelewa kutoka kwa Abu Sa’iyd Al-Khudriyy  (Radhwiya Allaahu 'anhu)  kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)     amesema:

((Linapowekwa jeneza na likabebwa na watu au wanaume shingoni mwao, basi anapokuwa [maiti] ni mwema husema: Nikadimisheni [nitangulizeni]. Lakini ikiwa si mtu mwema husema: Ole wake! Wanalipeleka wapi? Sauti yake inasikika na kila kitu isipokuwa binaadamu. Na lau angeisikia angelizimia)). [Imesimuliwa na Al-Bukhaariy]

 

Faida Na Sharh:

 

Hadiyth hii tukufu bila shaka inamtia khofu kila Muislamu wa kweli. Ni majeneza mangapi yanayoswaliwa na kubebwa kupelekwa makaburini huku watu wakiwa hawazingatii lolote kuhusiana na hali aliyonayo maiti wanayemswalia au kumbeba!?

 

Maiti huyo anabebwa juu ya mabega ya watu naye hawezi kufanya lolote. Kaviringishiwa sanda mwili wake wote bila kuachwa hata tundu ya pua! Hawezi kukimbia wala kunyanyuka! Nini anachokiona hapo?!

 

Muumini mwema wakati wa kutoka roho, humjia Malaika wa rahmah wakamtuliza kuhusiana na hatima yake anayoiendea. Humwambia: “Toka ee nafsi njema uelekee kwenye rahmah zitokazo kwa Allaah na rayhaan, na Rabb wako Hana hasira nawe.” Hapo Muumini hupata furaha kubwa kwa hayo.

 

Roho yake inaweza kutoka kwa ugumu, machungu na tabu. Lakini hayo yote ni kwa ajili ya kufutiwa madhambi na kunyanyuliwa daraja zaidi.

 

Hivyo Muislamu anapobebwa kwenye jeneza kupelekwa kaburini, husema: “Niwahisheni niwahisheni” kwa kuwa anaziona rahmah za Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) zikimsubiri mbele yaka ktk kaburi lake.

 

Ama kafiri na mtu mwovu, huyo huanza kuiona adhabu inayomsubiri mwanzo wa roho yake kutoka. Na wakati ule anapopelekwa kaburini, kafiri huyo hujizungumzia mwenyewe akisema: “Ole wake! Wanaipeleka wapi! Ilikuwa aseme: Ole wangu! Lakini kutokana na kitisho kilichopo mbele yake na yote machungu yanayomsubiri, anajisahau na kujikuta akisema: Ole wake!

 

Na tokea roho yake ilipotoka, Malaika walimjia na sanda ya moto, pamoja na mafuta ya moto yenye harufu mbaya mno. Na baada ya roho yake kutoka, Malaika hawa hupanda na roho yake mbinguni lakini haifunguliwi milango ikaingia.

 

Kafiri huyu anapiga ukelele akiwa ndani ya jeneza lakini hakuna anayemsikia mpaka anapofika kaburini mwake: Wapi wanaipeleka! Sauti yake husikiwa na kila kitu, lakini haisikiwi na wanadamu na majini. Na lau kama mwanadamu angeisikia, basi angelikufa kutokana na ubaya wake.
                                                 

 

Share