Hadiyth: Mtu Amwangalie Aliye Chini Yake Asimwangalie Aliyemzidi (Faida Na Sharh)

 

 

Hadiyth: Mtu Amwangalie Aliye Chini Yake Asimwangalie Aliyemzidi (Faida Na Sharh)

 

Imeandaliwa Na:   'Abdullaah Mu'aawiyah (Abu Baasim)

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

 

((انْظُرُوا إِلَى مَنْ هُوَ أَسْفَلَ مِنْكُمْ, وَلاَ تَنْظُرُوا إِلَى مَنْ هُوَ فَوْقَكُمْ فَإِنَّهُ أَجْدَرُ أَنْ لاَ تَزْدَرُوا نِعْمَةَ اللَّهِ عَلَيْكُمْ)) متفق عليه وهذا لفظ مسلم. 

 

وفي رواية البخاري: ((إِذَا نَظَرَ أَحَدُكُمْ إِلَى مَنْ فُضِّلَ عَلَيْهِ فِي الْمَالِ وَالْخَلْقِ فَلْيَنْظُرْ إِلَى مَنْ هُوَ أَسْفَلَ مِنْهُ((

 ((Mtazameni aliye chini yenu wala msimtazame aliye juu yenu, kwani [kufanya hivyo] ni haki zaidi msije  mkazidharau neema za Allaah juu yenu)).

Hii ni lafdhi ya Muslim.

 

Na katika riwaaya ya Al-Bukhaariy: ((Anapomtazama mmoja wenu aliyefadhilishwa zaidi kwa mali na umbo, basi amtazame aliye chini yake)).

 

Faida Na Sharh:

 

Sheikh Al-‘Allaamah ‘Abdur-Rahmaan bin Naaswir As-Sa’diy (Rahimahu Allaah) anasema katika kitabu chake:

“Ni uzuri ulioje wa nasaha hii yenye faida kubwa! Ni maneno ya kutosheleza na kubainisha wazi kabisa! Maneno haya yanatuhimiza tumshukuru Allaah ('Azza wa Jalla) , tuzitambue neema Zake, tuzizungumze, tuzitumie kama mwega katika kumtii Yeye Mneemeshaji, na tuzitumie njia zote zitakazotusaidia kumshukuru Allaah (‘Azza wa Jalla).

 

Kumshukuru Allaah (‘Azza wa Jalla) ndio kichwa cha ‘ibaadah, na ndio chimbuko la kheri. Hakuna neema yoyote ya ndani au ya nje aliyonayo mwana Aadam ila inatoka Kwake Allaah ('Azza wa Jalla). Na kwa ajili hiyo, Muislamu anatakikana afanye juhudi zake zote kuzilinda neema alizonazo kwa kuzitumia vyema pahala pake panapotakiwa na kuendelea kumwabudu Allaah ('Azza wa Jalla)  nyakati zote.

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  katika Hadiyth hii Tukufu, anatupa dawa ya ajabu kabisa ya kutuwezesha sisi kuzishukuru neema za Allaah ('Azza wa Jalla)   tulizonazo. Dawa hii ni Muislamu kumwangalia kila wakati yule ambaye yuko chini yake kimali, kinasaba, kiakili na kwa hali nyinginezo zote kiujumla. Akijilinganisha na watu hao, basi wakati wote atakuta kwamba Allaah ('Azza wa Jalla) kamfadhili yeye kwa mengi ambayo wengine Hakuwapa.”  Mwisho wa nukuu

 

 

-Mtu akiangalia katika jamii yake, atawakuta wengi wenye maradhi ya akili. Atamshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kwa uzima wa akili yake.

 

-Atawakuta wengine ambao hata mlo mmoja wa siku hawana uhakika wa kuupata. Atamshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kwa kile alichonacho.

 

-Atawaona wengi wamepoteza makazi yao au hawana aslani makazi, atamshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kwa nyumba aliyo nayo hata kama ni ndogo au ya kupanga.

 

-Atawaona wenye magonjwa mbalimbali ya hatari wakihangaika mahospitalini. Atamshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kwa neema ya afya na uzima.

 

-Atawaona pia wengi wamekengeuka na Dini na kumwasi Allaah, atashukuru kwa kupata tawfiyq ya kuwa katika mstari ulionyooka na kuwaombea hidaaya wengineo.

 

-Atawaona wengi waliozungukwa na ghamu, hamu na majonzi. Atamshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kwa hali ya furaha na ridhaa Aliyomtunukuu Allaah.

 

Na kwa vile shukru ndio duara la kheri na anwani yake, Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alimwambia Mu’aadh bin Jabal:

 

((Mimi nakupenda. Usiache kabisa kusema baada ya kila Swalaah:

 

اللّهُـمَّ أَعِـنِّي عَلـى ذِكْـرِكَ وَشُكْـرِك ، وَحُسْـنِ عِبـادَتِـك

Ee Allaah nisaidie juu Kukudhukuru, na kukushukuru na kukuabudu kwa uzuri utakikanao  [Abu Daawuwd, An-Nasaaiy]

 

 

Na alikuwa akisema:

 

رَبِّ اجْعَلْنِي لَكَ شَكَّارًا، لَكَ ذَكَّارًا، لَكَ رَهَّابًا، لَكَ مُطِيعًا، إِلَيْكَ مُخْبِتًا أَوَّاهًا مُنِيبًا،    

 

Rabb wangu nijaalie niwe mwenye kukushukuru, mwenye kukudhukuru, mwenye kukuogopa, mwenye kukutii, mwenye kukukhofu, mwenye kunyenyekea na kurudia kuomba tawbah.  [Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy, Ibn Maajah – Taz. Swahiyh At-Tirmidhiy (3/178) na Ahmad (1/127)

 

 

Share