009-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Namna Ya Kuzitwaharisha Aina Za Najsi Zilizobainishwa na Hadiyth

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

009-Namna Ya Kuzitwaharisha Aina Za Najsi Zilizobainishwa na Hadiyth

 

Alhidaaya.com

 

 

  

1- Kuitwaharisha nguo yenye damu ya hedhi

 

Inakuwa ni kwa kuikwangua na kuigandua, kisha kuisugua kwa ncha za vidole ili iachiane na itoke, kisha utaiosha kwa maji. Ni kutokana na Hadiyth ya Asmaa binti Abu Bakr, amesema: "Mwanamke mmoja alikuja kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Mmoja wetu nguo yake ikiingiwa na damu ya hedhi, afanyaje"? Akasema Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

تحته, ثم تقرصه بالماء ثم تنضحه, ثم تصلي فيه

((Ataipikicha, kisha ataikwangua kwa ncha za vidole na maji, kisha atainyunyizia maji, na halafu ataswalia)).

[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy na Muslim (291)].

 

Na kwa Hadiyth ya 'Aaishah, amesema: " Mmoja wetu alikuwa akipatwa na hedhi, huikwangua damu  kwenye nguo yake wakati anapotwaharika, kisha huiosha, na hunyunyizia maji sehemu iliyobaki, halafu huswali nayo". [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (308), na Ibn Maajah (630)].

 

Na kama mwanamke atapenda kutumia kijiti au kinginecho  ili kuondosha damu, au kuosha nguo kwa maji na sabuni na mfano wake katika madawa ya kusafishia, basi itakuwa ni bora zaidi.

 

Hii ni kwa Hadiyth ya Ummu Qays binti Muhswan, amesema: "Nilimuuliza Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu damu ya hedhi iliyoingia kwenye nguo, naye akasema:

 

((حكيه بضلع، واغسليه بماء وسدر))

 

((Ikwangue kwa ujiti, na uioshe kwa maji na mkunazi)). [Hadiyth Hasan. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (363), An-Nasaaiy (1/195) na Ibn Maajah (628)].

 

 

 

2-      Kuitwaharisha nguo yenye mkojo wa mtoto mchanga

Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

((يغسل من بول الجارية, ويرش من بول الغلام))

 

((Huoshwa ikiingia mkojo wa mtoto wa kike, na hurashiwa maji ikiingia mkojo wa mtoto wa kiume)). [Hadiyth Swahiyh “Lighayrih”. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (376), An Nasaaiy (1/158), na Ibn Maajah  (526). Kuna Hadiyth kama hii iliyopokelewa na Swahaba mwingine].  

 

 

 

3-       Kuitwaharisha nguo yenye madhii

 

Na  kwa vile madhii yanakithiri sana kutoka na  kuwa uzito kwa wengi, Allaah Mwekaji wa sharia, Ametuhafifishia namna ya kuyatwaharisha. Inatosha kuinyunyizia nguo maji sehemu iliyoingia madhii kutokana na Hadiyth ya Sahl bin Hunayf kwamba yeye alikuwa akipata tabu na uzito kutokana na madhii. Akamuuliza Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Ni vipi kwa yale yanayoingia katika nguo yangu? Akasema:

 

((يكفيك أن تأخذ كفا من ماء فتنضح به ثوبك حيث ترى أنه قد أصاب منه))

 

((Inakutosha kuchukua teko la maji, ukanyunyizia kwalo nguo yako pale unapoona yameingia)). [Hadiyth Hasan. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (210), At-Tirmidhiy, na Ibn Maajah (506)]. 

 

 

4-     Kuitwaharisha ncha ya nguo ya mwanamke (inayoburuzika)

 

Inaponajsika sehemu ya nguo ya mwanamke inayoburuzika, basi hutwaharika kwa kugusana na ardhi iliyo twahara. Mwanamke mmoja alimuuliza mke wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Ummu Salamah akimwambia: "Mimi ni mwanamke ninayerefusha ncha za nguo yangu na ninatembea sehemu chafu". Ummu Salamah akamwambia: Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

((يطهره ما بعده))

 

((Huitwaharisha (ardhi) iliyo baada yake)). ]        Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (383), At-Tirmidhiy (143) na Ibn Maajah (531).]

 

 

 

5-    Kuitwaharisha soli ya viatu

 

Imepokelewa na Abuu Sa’iyd Allaah Amridhie kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((اذا جاء أحدكم المسجد فليقلب نعليه ولينظرفيهما، فان رأى خبثا فليمسحه بالأرض، ثم ليصل بهما))

 

((Anapokuja mmoja wenu Msikitini, basi avipindue viatu vyake na aangalie vina nini. Ikiwa ataona najsi, basi aipanguse kwa ardhi, kisha aswali navyo)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (646)].

 

 

6-      Kukitwaharisha chombo mbwa akikitia ulimi

Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

((طهور اناء أحدكم اذا ولغ فيه الكلب أن يغسله سبع مرات أولاهن بالتراب))                     

 

 ((Kukitwaharisha chombo cha mmoja wenu mbwa akitia ulimi wake ndani, ni akioshe mara saba, ya kwanza yake kwa udongo)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (279) na Abuu Daawuud (71)].  

 

 

7-      Kuitwaharisha ngozi ya nyamafu

Ni kwa kusafishwa na kukaushwa kwa madawa. Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

((اذا دبغ الاهاب فقد طهر))  

((Ngozi ya nyamafu ikisafishwa na kukaushwa kwa madawa, basi imetwaharika)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim na wengineo].

 

 

8-     Kuitwaharisha ardhi iliyoingia mkojo na mfano wake

 

Ni kwa kumiminia maji juu yake kama alivyomrisha ((Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumwagia maji juu ya mkojo wa bedui Msikitini. [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (219) na Muslim (283)].

 

Bila shaka aliamuru hilo kwa ajili ya kuharakia usafi. Na kama si hivyo, lau kama angeliacha mpaka ukakauka na athari ya najsi ikaondoka, basi (ardhi) ingekuwa imetwaharika.

 

 

 

9-      Kukitwaharisha kisima au samli inapoingia ndani yake najsi

 

Ni kwa kuichota na kuiondosha najsi pamoja na sehemu za pambizoni mwake, na iliyosalia inabakia twahara. Ni kwa Hadiyth ya Ibnu ‘Abbaas kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa kuhusu panya aliyeangukia katika samli akasema:

 ((ألقوها، وما حولها فاطرحوه، وكلوا سمنكم))

((Mtupeni, na sehemu za pambizoni mwake ziondosheni, na samli yenu itumieni)).  [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (Wanyawa wa kuchinjwa mlango wa 34)].

 

 

 

Share