010-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Je, Ni Lazima (Kutumia) Maji Katika Kuondoshea Najsi? Au Inajuzu Kuondoshea Kwa Vimiminika Vinginevyo Au Mada Nyinginezo?

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

010-Je, Ni Lazima (Kutumia) Maji Katika Kuondoshea Najsi? Au Inajuzu Kuondoshea Kwa Vimiminika Vinginevyo Au Mada Nyinginezo?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Maulamaa wamehitalifiana katika suala kwa kauli mbili mashuhuri:

 

Kauli ya kwanza:

 

Ni sharti kutumia maji kuondoshea najsi. Haiswihi kwa kinginecho ila kwa dalili.

Na hili ndilo mashuhuri katika madhehebu ya Maalik na Ahmad. Na pia ni madhehebu ya Ash-Shaafi'iy katika "Al-Jadyd" (rai mpya). Ash-Shawkaany na waliomfuata, ameliunga mkono hili. [Bidaayat Al-Mujtahid (1/99), Al-Ummu (1/49) na As Sayl Al-Jarraar (1/49)].

Na hoja yao ni:

 

1- Neno Lake Ta'aala

((وَيُنَزِّلُ عَلَيْكُم مِّن السَّمَاء مَاء لِّيُطَهِّرَكُم بِهِ))

((Na Anawateremshieni maji toka mbinguni ili Awatwaharisheni kwayo)).[Al Anfaal (8:11)]

Pamoja na dalili nyinginezo zinazotaarifu kwamba maji ni twahara.

 

2- Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamuru maji yamwagwe juu ya mkojo wa bedui. [Imepasishwa na Al-Bukhaariy na Muslim].  

Wamesema kwamba amri ni ya wajibu, na kwa hivyo haitoshelezi kuondosha najsi ila kwa maji!!

 

3- Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kama ilivyo katika Hadiyth ya Abuu Tha'alabah, aliamuru kukiosha chombo cha Ahlul-Kitaab kwa maji. [Imepasishwa na Al-Bukhaariy na Muslim. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (5170) na Muslim (1930)].

 

4-Amesema Ash-Shawkaany: "Maji ndio asili katika kutwaharisha najsi kwa kusifiwa na Allaah Mpangaji sharia kuwa ni twahara yenyewe na yenye uwezo wa kutwaharisha kingine. Hivyo, haiwezekani yakaachwa kikatumika kingine ila kama litathibiti hilo toka kwa Allaah Mpangaji sharia. Na kama si hivyo, basi haiwezekani, kwani itakuwa ni kuufumbia macho ujulikano huo wa kuwa ni twahara yenye uwezo wa kutwaharisha kingine na kutumia kitu kingine kisichojulikana kuwa ni twahara chenye uwezo wa kutwaharisha kingine. Na hiyo ni kutoka nje ya vile mikondo ya kisharia inavyokwenda".

 

Kauli ya pili:

 

Inatosheleza kujitwaharisha kwa kila chenye kuweza kuondosha najsi, na si lazima maji.

Na haya ndio madhehebu ya Abuu Haniyfah, na riwaya nyingine toka kwa Maalik na Ahmad, na kauli ya zamani ya Ash-Shaafi'iy, na Ibnu Hazm. Nalo ndilo chaguo la Shaykh wa Uislamu Ibnu Taymiyah, na pia Mwanachuoni Mkubwa Ibnu 'Uthaymiyn. [Al-Badaai-’i (1/83), Fat-hul Qadiyr (1/200), Majmuu Al-Fataawaa (21/475), Al-Muhallaa (1/92-94) na Ash Sharh Al- Mumti’i (1/361-363)].

 

Ni kauli yenye nguvu kwa yafuatayo:

 

1- Kwamba maji kuwa ni twahara yenyewe na yenye uwezo wa kutwaharisha kingine, hakuzuii kingine kuwa ni chenye kutwaharisha vilevile. Kwani kaida inasema: "Kukosekana sababu maalumu, hakuhukumii kuondoka kisababisho maalumu, sawasawa ikawa dalili au isiwe dalili". Kwa vile chenye kuathiri kinaweza kuwa ni kitu kingine. Na hii ndio hali halisi kwa upande wa najsi. [Ash Sharhu Al-Mumti’i (1/362)].

 

Ninasema (Abuu Maalik): "Bali baadhi ya vimiminika kama vile siki na madawa ya kusafishia ya viwandani, huondosha najsi kama maji au zaidi kuliko maji".

 

2- Kwamba Allaah Mpangaji sharia Ameamuru kuondosha najsi kwa maji katika mambo maalumu, lakini Hakuamuru amri jumuishi kwamba kila najsi iondoshwe kwa maji.

 

3- Kwamba sharia imeruhusu kuondosha baadhi ya najsi bila kutumia maji kama kustanji kwa jiwe, au kuvisugua viatu kwa mchanga, au kutwaharika nguo inayoburuzika kwa ardhi, na mengineyo yaliyotangulia.

 

4- Kwamba kuondosha najsi hakuingii kwenye amri, bali kunaingia katika mlango wa kujiepusha na kilichokatazwa. Na ikitokea (ikaondoshwa) kwa sababu yoyote ile, basi hukmu itathibiti. Na kwa ajili hiyo, niya haishurutishwi katika kuondosha najsi. Lakini kama itaondoka kwa kitendo cha mtu aliyenuia, basi atalipwa thawabu kwa hilo. Na kama si hivyo, ikiondoshwa bila kitendo chake wala niya yake, basi athari itaondoka, na hatokuwa na thawabu wala madhambi.

 

Na hili linatiliwa nguvu na kwamba tembo inapobadilika na kuwa siki, basi inakuwa imetwaharika – kwa wale wanaosema kuwa pombe ni najsi – kwa makubaliano ya Waislamu.

 

Ninasema (Abuu Maalik): "Lenye nguvu ni kuwa najsi inapoondoka kwa kitu chochote, hukmu yake inaondoka na inakuwa ni twahara".

 

Hapa Kuna Faida Kadhaa

 

1- Mtu mwenye najsi katika nguo yake au  mwili wake, kisha akatumia mada yoyote twahara ya kusafishia – yasiyo maji – ili kuondosha najsi hiyo, basi hilo humtosheleza na wala si lazima aoshe kwa maji. 

 

2- Haijuzu kutumia vyakula au vinywaji katika kuondoshea najsi bila dharura, kwani huo ni uharibifu wa mali. [Majmuu Al-Fataawaa (21/475)].

 

3-Utwaharishaji bila maji kwa (kutumia) vimiminika vingine au mada nyinginezo, utafanyika tu katika (kiini cha) najsi yenyewe katika nguo au mwili au mahala. Ama utwaharishaji wa kihukmu (twahara ya hadathi) kama vile wudhuu, kuoga na mfano wake, haukamiliki ila kwa maji.

 

 

 

Share