021-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Kufuga Ndevu

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

021-Kufuga Ndevu

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Hukmu ya kufuga ndevu

 

Kufuga ndevu ni lazima kwa wanaume, na hii ni kwa Hadiyth zifuatazo:

 

1- Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameamuru kuzifuga. Agizo hili ni la wajibu, kwani hakuna kiashirio chochote chenye kulipindisha na kulifanya liwe ni la Sunnah. Kati ya maagizo hayo ni neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

((خالفوا المشركين: وفروا اللحى وأحفوا الشوارب))

((Khalifianeni na washirikina. Fugeni ndevu na punguzeni masharubu)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (5892) na Muslim (259)].

 

Na neno lake:

((جزوا الشوارب، وأرخوا اللحى، خالفوا المجوس))

((Kateni masharubu, ziachilieni ndevu, khalifianeni na wamajusi)).[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (260)].

 

1- Anayezinyoa, anajifananisha na makafiri kama ilivyotangulia katika Hadiyth hizo mbili.

2- Anayezinyoa, anabadili Umbile la Allaah na anamtii shaytwaan aliyesema:

 

(( وَلَآمُرَنَّهُمْ فَلَيُغَيِّرُنَّ خَلْقَ اللَّهِ ))

((Na kwa hakika, nitawaamrisha, na wao bila kusita, watalibadilisha Umbile la Allaah)). [An-Nisaa (4:119].

 

3- Anayezinyoa, anajifananisha na wanawake. Na Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewalaani wanaume wanaojifananisha na wanawake. [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (5885) na At-Tirmidhy (2935)].

 

Na kwa ajili hiyo, Sheikh wa Uislamu anasema: “Ni haramu mtu kunyoa ndevu zake”. [Al-Ikhtiyaarat Al-Fiqhiyyah cha ‘Alaaud Diyn Al Baaly (uk 10). Angalia pia Al-Furu’u cha Ibn Muflih (1/291)].

 

Ibn Hazm na wengineo, ameinukuu Ijma’a ya Maulamaa kwamba ni haramu kunyoa ndevu. [Maratibul Ijma’a na Raddul Mukhtaar (2/116)].

 

Je, Inajuzu Kunyoa Ndevu Zilizozidi Mkamato Wa Mkono?

 

Baadhi ya Maulamaa wanaona kwamba inajuzu kuzikata ndevu zilizozidi mkamato wa mkono kwa kigezo cha Hadiyth ya Ibn ‘Umar ya kwamba alipokuwa anahiji au kufanya ‘Umrah, alikuwa akikamata ndevu zake, na zile zinazozidi, huzikata.[Hadiyth Swahiyh.  Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (5892) na Muslim (259)].

 

Wanasema: “Yeye ndiye mpokezi wa Hadiyth inayoamuru kufuga ndevu, na kwa hivyo, anayajua zaidi madhumuni yake”.

 

Hujja ya Maulamaa hawa haina mashiko katika athari hii kutokana na haya yafuatayo: [Ameyaelezea haya Sheikh Al-Habiyb Wahiyd ‘Abdus Salaam Baaly – Allaah Ainyanyue hadhi yake – katika kitabu cha Al-Ikliyl].

 

1- Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu Anhu) alikuwa akilifanya hilo wakati anapojifungua na ihram ya Hijjah au ya ‘Umrah. Lakini wao wanalijuzisha hilo katika hali zote.

 

2- Kitendo hiki cha Ibn ‘Umar, kinatokana na yeye kuliawilisha Neno Lake Allaah Mtukufu:

((مُحَلِّقِينَ رُءُوسَكُمْ وَمُقَصِّرِينَ))

((Mkinyoa vichwa vyenu na mkipunguza)).[Al-Fat-h (48:27].

 

..kuwa ni katika amali ya Hijjah. Kunyoa ni kwa kichwa, na kupunguza ni kwa ndevu. [Angalia Sharhul Kirmaany Al-Bukhaary (21/111)].

 

3- Swahaba akisema au akifanya kinyume na aliyoyasimulia, basi kinachoangaliwa ni kile alichokisimulia, si ufahamu wake wala kitendo chake. Kinachoangaliwa ni kile alichokisema Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) moja kwa moja.

 

Kutokana na vigezo hivi, la sahihi ni kuwa kufuga ndevu ni wajibu na kuzikata haijuzu kwa msingi wa kuyafuata maagizo jumuishi yaliyokuja kwenye Hadiyth nyingi Swahiyh kama wanavyoona Jamhuri ya Maulamaa. Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.

 

 

 

 

Share