024-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Inajuzu Kwa Mwanaume Kuogea Kwa Mabaki Ya Maji (Aliyojitwaharishia Mwanamke)

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

024- Inajuzu Kwa Mwanaume Kuogea Kwa Mabaki Ya Maji (Aliyojitwaharishia Mwanamke)

 

Alhidaaya.com

 

 

'Ulamaa wana mielekeo miwili katika hukmu ya mtu kujitwaharisha kwa maji yaliyobakia baada ya mwanamke kutawadhia au kuogea.

 

Mwelekeo Wa Kwanza:

 

Haijuzu kwa mwanaume kujitwaharisha kwa mabaki ya mwanamke. Na haya ni madhehebu ya Ibn ‘Umar, ‘Abdullaah bin Sarjas, Mama wa Waumini Juwayriyah bint Al-Haarith, Al-Hasan, Ahmad bin Hanbal, Is-haaq, Ash-Sha’abiy na Daawuud Adh-Dhaahiriy. [Al-Awswat (1/292) na Al-Mughny (1/282)].

 

Hoja yao ni:

 

1- Yaliyopokewa toka kwa Al-Hakam bin ‘Amr kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza mtu kutawadhia mabaki ya maji aliyojitwaharishia mwanamke. [Maulamaa wameitia ila. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (82), At-Tirmidhiy (64), An-Nasaaiy (1/179), Ibn Maajah (373) na Ahmad (5/66). Al-Bukhaariy, Ad-Daarqutwniy na An-Nawawy wameitia dosari pia. Ama Ibn Hajar na Al-Albaaniy, wao wamesema ni Swahiyh katika “Al-Irwaai (1/43)].

 

2- Imepokelewa toka kwa Humayd Al-Humayriy akisema: “Nilikutana na mtu aliyesuhubiana na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa miaka minne kama alivyosuhubiana Abu Hurayrah. Alisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza mwanamke kuogea mabaki ya mwanaume, au mwanaume kuogea mabaki ya mwanamke. (wachote wote kwa pamoja)”.[Isnadi yake ni Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (81), An-Nasaaiy (1/130) na Al-Bayhaqiy (1/190)].

 

3- Ni yale yaliyopokelewa toka kwa ‘Aliy bin Abiy Twaalib aliyesema: “Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na ahli wake, walikuwa wakiogea chombo kimoja, na haogei mmoja wao kwa mabaki ya mwenzake”.[Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Maajah (1/133)].

 

Mwelekeo Wa Pili:

 

Inajuzu mtu kujitwaharisha kwa mabaki ya mwanamke. Yamesemwa haya na “Umar, Abu Hurayrah, ‘Abdullah ibn ‘Abbaas, Ibn ‘Umar, Sa’ad bin Abiy Waqqaas, mjumuiko wa watangu wema, Abu ‘Ubayd na Ibn Al-Mundhir. Haya pia ndio madhehebu ya Hanafi, Maalik, Ash-Shaafi’iy na riwaya ya Ahmad. [Muswannaf ya ‘Abdur-Razzaak (1/110), Ibn Abi Shaybah (1/38), Al-Awswat (1/297), At-Twahuwr cha Abu ‘Ubayd (236), Al-Mabsutw (1/61), Al-Ummu (1/8) na Al-Mughny (1/283)].

 

Wametoa hoja kwa haya yafuatayo:

 

1- Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiogea kwa mabaki ya Maymuunah. [Hadiyth Swahiyh. Imeshafanyiwa “ikhraaj” hapo nyuma].

 

2- Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas akisema: “Ahli mmoja wa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliogea kwenye beseni. Na Rasuli alipokuja alimwambia: Ee Rasuli wa Allaah! Mimi nilikuwa na janaba. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: 

(( إن الماء لا ينجس))

 ((Hakika maji hayapati janaba)).  [Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (68), At-Tirmidhiy (65), An-Nasaaiy (1/173) na Ibn Maajah (370). Baadhi ya Maulamaa wameitia ila kwa riwaya ya Simaak toka kwa ‘Ikrimah. Riwaya hii imekorogeka. Lakini Al-Haafidh katika kitabu cha Al-Fat-h amewajibu kwamba Shu-’ubah amepokea toka kwake, na yeye hapokei toka kwa Mashaykh zake isipokuwa Hadiyth Swahiyh.. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi].

 

3- Imepokelewa toka kwa Mama wa Waumini ‘Aaishah aliyesema: “Nilikuwa mimi na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) tukioga katika chombo kimoja nailhali wote tuna janaba)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (299) na Muslim (321)].

Na katika riwaya nyingine: ((…wote tunachota humo)).

 

 

Lenye Nguvu:

 

Lenye kuridhisha na kuondosha shaka katika dalili za mwelekeo wa kwanza ni  Hadiyth ya mtu aliyesuhubiana na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa miaka minne (ingawa Al-Bayhaqiy ameitia ila) pamoja na dalili zote za mwelekeo wa pili. Na dalili hizo zinaweza kuoanishwa kwa moja ya mawili: [Fat-hul Baary (1/300- Al Ma-’arifah), Subulus Salaam (1/28), na Naylul Awtwaar (1/26)].

1- Hadiyth zinazokataza zichukuliwe juu ya maji yanayochuruzika toka kwenye viungo, na Hadiyth za kujuzisha zichukuliwe juu ya maji yenye kubaki ndani ya chombo. Hivi ndivyo Al-Khatwaabiy alivyooanisha.

 

2- Katazo lichukuliwe juu ya ukaraha pamoja na kujuzu yote mawili.

 

Ninasema: “Na huenda hili la pili ndilo bora zaidi. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi".

 

 

Share