032-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Mambo Yasiyotengua Wudhuu

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

032-Mambo Yasiyotengua Wudhuu

 

Alhidaaya.com

 

 

Mambo haya Maulamaa wamehitilafiana juu ya kutengua kwake wudhuu. Na kwa kuyatafiti kwa kina, itabainika kwamba hayatengui. Kati ya mambo hayo ni:

 

1- Mwanaume kumgusa mwanamke bila ya kizuizi

 

Suala hili lina kauli tatu za Maulamaa:

 

Kauli ya kwanza:

Mwanamume kumgusa mwanamke kunatengua wudhuu kwa hali yoyote. Haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy. Ibn Hazm amemuunga mkono. Ibn Mas’uud na Ibn ‘Umar wamesema hivyo hivyo. [Al-Ummu (1/15), Al-Majmu’u (2/23 na baada yake) na Al-Muhalla (1/244)].

 

Kauli ya pili:

Hakutengui kwa hali yoyote. Ni madhehebu ya Abu Haniyfah na Muhammad ibn Al-Hasan Ash-Shaybaaniy. Pia ni kauli ya Abbaas, Twaawus, Al-Hasan na ‘Atwaa. Kauli hii pia imeungwa mkono na Shaykh wa Uislamu Ibn Taymiyah, nayo ndio kauli yenye nguvu. [Al-Mabsuwtw (1/68), Al-Badaai-’i (1/30), Al-Awsatw (1/126) na Majmu’u’ Al-Fataawaa (21/410)].

 

Kauli ya tatu:

Kugusa kunatengua kama ni kwa matamanio. Haya ni madhehebu ya Maalik na Ahmad kama ilivyo mashuhuri kwake.  [Al-Mudawwanah (1/13), Haashiyat Ad-Dusuwqiy (1/119), Al-Mughniy (1/192) na Kash-Shaaf Al-Qinaa’i (1/145)].

 

Ninasema (Abu Maalik): "Kigezo cha kimsingi walichokitolea dalili waliosema kwamba wudhuu unatenguka kwa kumgusa mwanamke, ni kauli Yake Allaah Mtukufu:

 

(( أوْ لامَسْتُمُ النِّسَاءَ فَلَمْ تَجِدُوا مَاءً فَتَيَمَّمُوا))

((..au mmewagusa wanawake, na hamkupata maji, basi tayammum..)). [Al-Maaidah (5: 6)]

 

Imepokelewa kwa njia sahihi toka kwa Ibn Mas-’oud na Ibn ‘Umar wakisema: “Kugusa ni chini ya daraja ya kuingilia”. [Kauli Swahiyh: Tafsiyr At-Twabariy (1/502) kwa Sanad tofauti Swahiyh].

 

Lakini Mwanachuoni Mweledi wa umma Ibn ‘Abbaas amehitilafiana nao akisema: “Kugusa na “mubaasharah”, kunamaanisha kuingilia, lakini Allaah Hukifanyia kinaya Akitakacho kwa Akitakacho”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Twabariy (9581) na Ibn Abu Shaybah (1/166)].

 

Na hakuna shaka kwamba tafsiyr yake inapewa kipaumbele kuliko ya wengineo. Halafu, ndani ya Aayah yenyewe, kuna dalili juu yake. Neno Lake Allaah Mtukufu:

 

(( يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا قُمْتُمْ إِلَى الصَّلَاةِ فَاغْسِلُوا))

((Enyi mlioamini! Mnaposimama kwa ajili ya Swalaah, basi osheni…)).[Al-Maaidah (5: 6)]

 

Hii ni twahara ya hadathi ndogo kwa kutumia maji. Kisha Akasema:

 

(( وَإِنْ كُنْتُمْ جُنُبًا فَاطَّهَّرُوا ۚ ))

((..na mkiwa na janaba, basi ogeni..))

 

Hii ni twahara ya hadathi kubwa kwa kutumia maji. Kisha Akasema:

 

(( وَإِنْ كُنْتُمْ مَرْضَىٰ أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ أَوْ جَاءَ أَحَدٌ مِنْكُمْ مِنَ الْغَائِطِ أَوْ لَامَسْتُمُ النِّسَاءَ فَلَمْ تَجِدُوا مَاءً فَتَيَمَّمُوا))

(( Na mkiwa wagonjwa au mmo safarini, au mmoja wenu ametoka chooni, au mmewagusa wanawake na hamkupata maji, basi tayamamuni..))

 

Na Neno Lake:

  (( فَتَيَمَّمُوا))

((Basi tayamamuni)).

 

Hii ni badali ya twahara mbili. Kwa hiyo Neno Lake:

  (( أَوْ جَاءَ أَحَدٌ مِنْكُمْ مِنَ الْغَائِطِ ))

((..au mmoja wenu ametoka chooni… ))

 

…ni ubainisho wa sababu ndogo. Na Neno Lake:

  (( أَوْ لَامَسْتُمُ النِّسَاءَ ))

((Au mmewagusa wanawake..))

..ni ubainisho wa sababu kubwa. [Ash-Sharh Al-Mumti’i (1/239) na mfanowe katika Al-Awsatw (1/128)].

 

Ijulikane kwamba taawili ya Ash-Shaafi’iy mwenyewe ya maana ya Aayah Tukufu, haikuwa kwa njia ya kukata moja kwa moja, bali inavyoonekana kutokana na maelezo yake ni kuwa yeye amelielezea hilo kwa aina fulani ya tahadhari. [Ameyaelezea haya Shaykh Al-Mash-huwr (Allaah Amhifadhi) katika uhakiki wake wa “Masuala Yenye Mivutano” (2/217)].

 

Ninasema: "Na kati ya yanayotilia nguvu kwamba kumgusa mwanamke hakutengui wudhuu ni haya yafuatayo:

 

(a) Hadiyth ya ‘Aaishah aliyesema: “Nilimkosa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) usiku kitandani. Nikapapasa kumtafuta na mkono wangu ukagusa tumbo la nyayo zake mbili zikiwa zimesimamishwa na yeye yuko katika sijdah. Alikuwa akisema:

 

((اللهم إني أعوذ برضاك من سخطك))

((Ee Mola! Hakika mimi najilinda kwa radhi Zako kutokana na hasira Zako)).[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (222), Abuu Daawuud (865) na At-Tirmidhiy (3819)].

 

(b) Na imepokelewa vile vile kutoka kwa ‘Aaishah akisema: “Nilikuwa nikilala mbele ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hali ya kuwa miguu yangu iko sehemu yake ya Qibla. Anaposujudu, alikuwa akinibonyeza na mimi huikunja miguu, na anaposimama nainyoosha”. Anaongeza akisema: “Na nyumba nyakati hizo zilikuwa hazina taa”.[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (382), Muslim (272) na wengineo].

 

Na katika tamko jingine: “Hata anapotaka kuswali witri, alikuwa akinigusa kwa mguu wake”.[Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na An-Nasaaiy (1/101)].

 

(c) Waislamu wamekuwa siku zote wakiwagusa wake zao. Na hakuna yeyote aliyenukulu toka kwake (Rasuli) kuwa alikuwa akiwaamuru Waislamu kutawadha kwa kufanya hilo. Na wala haikunukuliwa toka kwa Maswahaba wakieleza kwamba alitawadha kutokana na hilo katika maisha yake. Na wala haikunukuliwa kutoka kwake kwamba alitawadha kwa sababu ya hilo, bali lililonukuliwa kutoka kwake katika As-Sunan, ni kuwa alikuwa akiwapiga busu baadhi ya wakeze na wala hatawadhi. [Maimamu wameitia doa: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (178) na An-Nasaaiy (1/104). Na waliotangulia wameitia ila. Tazama Sunan Ad-Daar Qutwniy (1/135-142)].

 

Kuwa Hadiyth hii ni Swahiyh kuna hitilafu. Lakini hata hivyo, hakuna hitilafu kuhusu kwamba haikunukuliwa kuwa yeye alitawadha kwa sababu ya kumgusa (mwanamke). [Majmu’u Al-Fataawaa (21/410, 20/222) na sehemu nyinginezo].

 

Ama kauli ya kutenguka wudhuu kwa kugusa kwa matamanio au kutotenguka kwa kugusa bila matamanio, kauli hii haina hoja. Lakini hata hivyo inaweza kusemwa: “Ikiwa atatawadha kwa sababu amemgusa mwanamke kwa matamanio lakini bila ya kumwingilia, basi itakuwa ni vizuri kwa ajili ya kuzima matamanio kama ilivyokuwa imesuniwa kutawadha kwa sababu ya hasira ili kuzituliza. Ama kulazimu kutawadha, hilo haliko. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi".

 

 

2- Kutoka damu sehemu isiyo ya kawaida sawasawa ikiwa ni kwa jeraha au kuumikwa, au ikiwa ni nyingi au kidogo

 

Hili halitengui kwa mujibu wa kauli mbili sahihi za Maulamaa. Ni madhehebu ya Ash-Shaafi'iy na Maalik. Lakini Abuu Haniyfah anasema kwamba hili linatengua. Na wafuasi wa Hanbali wanasema kuwa wudhuu hutenguka kama damu ni nyingi. [Al-Ummu (1/180), Al-Majmu’u (2/55), Al-Istidhkaar (2/269), Al-Mabsuwtw (1/74) na Al-Mughniy (1/184)].

 

Kauli ya kwanza ndio yenye nguvu zaidi kutokana na mambo yafuatayo:

 

(a) Hadiyth zinazowajibisha kutawadha kutokana na kutokwa damu si Swahiyh.

 

(b) Ni kwamba asili (ya mambo) ni uhalali. Kwa hiyo anayetawadha wudhuu sahihi, wudhuu huu hautenguki ila kwa matni au Ijma’a.

 

(c) Ni Hadiyth ya Jaabir bin ‘Abdillah katika kisa cha vita vya Dhaat Ar-Riqaa’i. Anasema: “Swahaba Muhaajir alilala, na mwenzake Mwansari alisimama kuswali. (Akiendelea kuswali) mtu mmoja alimlenga mshale. Akauchomoa akauweka mpaka ikafikia mishale mitatu. Kisha alirukuu na kusujudu na mwenzake (aliyelala) akagutuka. Na alipojua (mlenga mshale) kuwa wao wataweza kumkamata, alikimbia. Na mara Swahaba Muhaajir alipoziona damu zikimchuruzika Mwansari alisema: “ Subhaana Llaah. Kwa nini usingenigutusha mara tu alipokulenga? Akasema: “Nilikuwa nikiisoma Surah na sikupenda kuikatisha”. [Isnadi yake ni Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy kama ni Hadiyth Mu’allaq (1/280), Ahmad ameitoa kama ni Hadiyth Mawswuwl (195), Ahmad (3/343), Ibn Hibaan (1096), Al-Haakim (1/156) na Ad-Daara Qutwniy (1/223) na Sanad yake ni Dhwa’iyf kwa sababu ya ‘Uqayl bin Jaabir. Katika Swahiyh Abiy Daawuud (193), Al-Albaaniy ameiona ni Swahiyh!!].

 

Inavyojulikana ni kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alilijua hilo na wala hakumkatalia kuendelea na Swalaah baada ya kutokwa na damu. Na lau kama damu ingelikuwa inatengua wudhuu, basi Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) angelimbainishia hilo na wengineo wote waliokuwepo katika vita hivyo. Haijuzu kuchelewesha kulibainisha jambo wakati inapohitajika kufanya hivyo.  [As-Sayl Al-Jarraar (1/99)].

 

(d)  Imethibiti kuwa ‘Umar bin Al-Khattwaab alipochomwa kisu, aliswali na hali jeraha lake linafuka damu. 

 

(e) Habari zimetangaa kutoka zama hadi zama kwamba askari waliokuwa wakipigana Jihadi, walikuwa wakipata maumivu ya majeraha. Hakuna anayeweza kupinga kwamba majeraha haya hayakuwa yakitoka damu na nguo zao kutapakaa damu. Pamoja na haya, walikuwa wakiswali hivyo hivyo. Na hakuna yeyote aliyenukulu toka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba aliwaamuru watoke kwenye Swalaah au wasiswali. Na kwa ajili hiyo, Al-Hasan Al- Baswriy anasema: “Waislamu wangali wanaswali na majeraha yao”. [Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy kama ni Hadiyth Mu’allaq (1/280). Na Ibn Abi Shaybah ameifanya kuwa Hadiyth Mawswuul kwa Sanad Swahiyh kama ilivyo katika Al-Fat-h (1/281)].

 

3- Kutapika na mfano wake

 

Madhehebu ya Maulamaa katika suala hili, yako vilevile kama yalivyo katika suala la kutokwa damu. Na lililo sahihi ni kuwa kutapika hakutengui wudhuu kwa vile hoja zinazowajibisha kutawadha hazina usahihi wowote na kwamba asili ya mambo ni uhalali.

 

Ama Hadiyth ya Mi’idaan bin Twalha aliyenukuu toka kwa Abi Ddardaai kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitapika, akafungua kisha akatawadha, hakuna shaka kwamba Hadiyth hii haimaanishi kuwa ni lazima kutawadha kama mtu ametapika, kwani hicho ni kitendo tu. Na lengo la kitendo hicho ni kuonyesha kuwa ni vizuri (mustahabbu) kufanya hivyo. Na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy (87) na Abu Daawuud (2381). Tazama Al-Irwaa (111)].

 

4- Kucheka ndani ya Swalaah au nje yake

 

Maulamaa kwa sauti moja wamekubaliana kwamba kucheka nje ya Swalaah hakutengui twahara wala hakuwajibishi kutawadha, na kwamba kucheka ndani ya Swalaah huibatilisha. Lakini Maulamaa hao wamehitalifiana katika kutenguka wudhuu kwa kucheka ndani ya Swalaah. Abu Haniyfah na wenzake, Ath-Thawriy, Al-Hasan na An-Nakh’iy wanaona kwamba hilo linatengua wudhuu. Wao wameitolea hoja Hadiyth Munqati’i isiyozingatiwa, nayo ni Hadiyth ya Abu Al-‘Aaaliyah isemayo: “Mtu mmoja kipofu alikuja hali ya kuwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anaswalisha watu. Mtu yule aliporomoka katika shimo ndani ya Msikiti na baadhi ya watu wakacheka. Hapo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwamuru kila aliyecheka atawadhe na aswali upya.[Isnadi yake ni dhwa’iyf sana: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ad-Daara Qutwniy (1/162) na Ibn ‘Uday (2/716)].

 

Hadiyth iliyothibiti ni ya Jaabir, nayo ni Mawquuf isemayo: “Ni kwamba (Rasuli) aliulizwa kuhusu mtu anayecheka ndani ya Swalaah”. Naye akajibu:

 

((يعيد الصلاة ولا يعيد الوضوء))

((Atarudia tena Swalaah yake, lakini hatotawadha upya)). [Hadiyth Swahiyh Mawquwf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy ikiwa Mu’allaq (1/280), Al-Bayhaqiy kama Hadiyth Mawswuwl (1/144) na Ad-Daara Qutwniy (1/172)].

 

Hadiyth hii ndio Swahiyh. Ni madhehebu ya Ash-Shaafi'iy, Maalik, Ahmad, Is-Haaq na Abu Thawr. [Al-Majmu’u (2/61), Al-Kaafiy (1/151), Al-Mughniy (1/117) na Al-Awsatw (1/227)].

 

 

5- Kuosha maiti na kuibeba

 

Mwenye kuosha maiti au kumbeba, basi wudhuu wake hautenguki kwa mujibu wa kauli yenye nguvu. Lakini baadhi ya Maulamaa wanaona ni vizuri kuoga kwa aliyemwosha maiti, na kutawadha kwa aliyembeba. Hii ni kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah anayesema kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

((من غسل ميتا فليغتسل، ومن حمله فليتوضأ))

((Mwenye kumwosha maiti aoge, na mwenye kumbeba atawadhe)). [Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (3162), At-Tirmidhiy (993), Ibn Maajah (1463) na Ahmad (2/433). At-Tirmidhiy, Ibn Hajar na Al-Albaaniy wameifanya Hadiyth Hasan katika Al-Irwaa (1/174). Lakini linaloonekana ni kuwa inahitaji kuchunguzwa zaidi, kwani imekosolewa!!]

Lakini ikiwa Hadiyth hii ni Swahiyh.

 

 

6- Mwenye wudhuu kufanya shaka ya kutenguka wudhuu wake

 

Mwenye kutawadha wudhuu sahihi, kisha akafanya shaka kama wudhuu umemtenguka au la, basi atabakia juu ya uasili wa kile alichokiyakinisha katika utwahara mpaka atakapopata uhakika kwamba wudhuu wake umetenguka. Na ikiwa atafanya shaka nailhali yuko ndani ya Swalaah, basi hatoivunja mpaka ayakinishe kutenguka wudhuu. Hii ni kwa Hadiyth ya ‘Abdullah bin Zayd aliyesema: “Rasuli alishtakiwa kuhusu mtu anayekuwa na wasiwasi katika Swalaah”. Rasuli akasema:

((لا ينصرف حتى يسمع صوتا أو يجد ريحا))

((Haivunji mpaka asikie sauti au anuse harufu)). [Hadiyth Swahiyh: Imetangulia kuelezwa hivi karibuni].

 

Al-Baghawiy katika Sharhus Sunnah (1/353) amesema: “Maana yake: Mpaka apate uhakika wa hadathi, kwa vile kusikia sauti au kuwepo harufu ni sharti”.

 

 

Share