031-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Yanayotengua Wudhuu

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

031-Yanayotengua Wudhuu

 

Alhidaaya.com

 

 

 

1-    Ni kutoka mkojo, au kinyesi, au upepo katika moja ya njia mbili (utupu wa mbele au wa nyuma)

 

Ama mkojo na kinyesi, ni kwa Neno Lake Subhaana:

 أَوْ جَاءَ أَحَدٌ مِّنكُم مِّنَ الْغَائِطِ 

((Au mmoja wenu ametoka chooni)). [Al Maaidah (5:6)] 

 

“Al-Ghaait” ni kinaya cha kukidhi haja ndogo au haja kubwa. Wanachuoni wote wamekubaliana kuwa wudhuu unatenguka kwa kutoka kinyesi au mkojo toka moja ya njia mbili (mbele au nyuma). [Al-Ijma’a (uk 17), na Al-Awsatw (1/147) cha Ibn Al-Mundhir].

Ama ikiwa vitatoka sehemu isiyo ya mbele au nyuma kama kutoka kwenye jeraha la kwenye kibofu au tumbo, hapa wanachuoni wamevutana. Wanachuoni wenye kukizingatia kile tu kinachotoka (kiini chenyewe) kama Abu Haniyfah, Ath-Thawriy, Ahmad na Ibn Hazm, hao wamesema: “Wudhuu unatenguka kwa kila najsi inayobubujika toka mwilini iliyotokea sehemu yoyote”. Ama wale wenye kuyazingatia matokeo mawili (nyuma na mbele) kama Ash-Shaafi’iy, hao wamesema: “Unatenguka kinapotoka kitu chochote toka sehemu hizo mbili hata kama si najsi kama kijiwe na mfanowe”. [Al-Muhalla (1/232), Bidaayat Al-Mujtahid (1/40) na Al-Awsatw (1/137)].

 

 

Ama upepo, ikiwa utatoka kwa nyuma, kwa sauti au bila sauti, basi unatengua wudhuu. Hii ni kwa Ijma’a ya Maulamaa na kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

   لا يقبل الله صلاة أحدكم إذا أحدث حتى يتوضأ

((Allaah Haikubali Swalaah ya mmoja wenu akipata hadathi mpaka atawadhe)).

 

Mtu mmoja toka Hadhramawt akauliza: “Ni nini hadathi ee Abu Hurayrah? Akajibu: “Ni ushuzi wa kimya kimya au wa sauti ”. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (135) na Muslim (135), lakini kwake bila kauli ya Abu Hurayrah].

 

Na ikiwa upepo utatokea utupu wa mbele, Jamhuri ya Maulamaa wamesema  unatengua. [Bidaayat Al-Mujtahid (1/40) na Al-Ummu (1/17)].

 

Lakini Abu Haniyfah aliyeungwa mkono na Ibn Hazm amesema upepo huo hautengui wudhuu kwa vile ushuzi wa kimya na ushuzi wa sauti ni majina mawili ambayo hayaitwi upepo ila tu kama utatokea kwa nyuma. [Al-Muhalla (1/232) na Al-Mabsuwtw (1/83)].

 

Ninasema: “Ikiwa mtu atauhisi upepo unaojulikana (kwa harufu yake), basi utatengua wudhuu sawasawa ukiwa umetoka kwa mbele au kwa nyuma. Na ikiwa hauna harufu, basi ni ule tu unaotoka nyuma”.

 

 

Tanbihi

 

Mwanamke anaweza kuhisi kitu kinachofanana na upepo kikitoka kwenye utupu wake wa mbele. Hiki si kingine bali ni mjazo na mtaharuki wa ndani kwa ndani na wala si ushuzi unaotoka. Huo hautengui wudhuu wake, kwani ni kama kuteuka na mfano wake. Lakini ikiwa mwanamke huyo ni yule ambaye njia yake ya haja ndogo na kubwa zimeingiliana, basi atatawadha kiakiba tu kwa kuwepo uwezekano wa kuwa pengine upepo huo umetokea nyuma. Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.

 

 

2-    Kutoka manii, wadii na madhii:

 

Kutoka manii kunatengua wudhuu kwa ijmai ya Wanazuoni na kunawajibisha kuoga kama itakavyokuja. [Al-Ifswaah (1/87) na Al-Ijma’a (uk 31)].

 

Na kila lile lenye kupasisha kuoga, basi linabatilisha wudhuu kwa Ijma’a ya Wanazuoni.

 

Na madhii nayo inatengua kwa Hadiyth ya ‘Aliy bin Abiy Twaalib Allaah Amridhie aliyesema: “Nilikuwa ni mtu ninayetokwa sana madhii. Nikamwamuru mtu mmoja amuulize Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kutokana na hishma ya binti yake. Akamwuliza, naye akasema:

  توضأ واغسل ذكرك

((Tawadha na uoshe utupu wako)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (269) na Muslim 303)].

 

Madii pia ni hivyo hivyo. Ni wajibu mtu aoshe utupu wake na atawadhe.

 

Ibn ‘Abbaas anasema: “Manii, wadii na madhii; ama manii, ni yale ambayo inapasa kuoga kwa kutoka. Ama wadii na madhii, akasema: Osha utupu wako, au nyuchi zako, na utawadhe wudhuu wako wa Swalaah”.[Isnadi yake ni Swahiyh: Al-Bayhaqy (1/115)].

 

Faida

 

Aliyepata bahati mbaya ya kusumbuliwa na kichocho cha mkojo au cha madhii, au akawa mara kwa mara anatokwa na kimoja ya viwili hivyo vilivyotangulia kutokana na kasoro ya kimwili mpaka ikawa ni uzito kwake, basi huyo ataosha nguo yake na mwili wake, na atatawadha kwa kila Swalaah kama mwanamke mwenye damu ya istihaadhwah (maelezo yatakuja). Kisha hakitakuwa na neno     kitakachomtoka akiwa ndani ya Swalaah au kati ya wudhuu wake na Swalaah yake.

 

 

3- Usingizi mzito wa kutojifahamu: 

 

Athar zilizokuja kuhusu kutawadha baada ya mtu kulala zimetofautiana, na maana zake kama zinavyoonekana zimegongana. Kuna Hadiyth ambazo maana zake kama zinavyoonekana, huonyesha kuwa kimsingi hakuna kutawadha kwa sababu ya kulala (usingizi), wakati ambapo kuna nyingine maana yake ya nje inalazimisha kuwa kulala ni hadathi (kunatengua). Kwa hivyo basi, Maulamaa katika suala hili, wameelekea mielekeo miwili: Madhehebu ya kukusanya na Madhehebu ya kutilia nguvu.

 

Maulamaa wa madhehebu ya kutilia nguvu, hawa ima wameliondosha kabisa suala la kutawadha baada ya kulala wakisema kuwa (kulala) si hadathi, au ima wameliwajibisha hilo moja kwa moja wakisema kuwa kulala ni hadathi. Ama Maulamaa wa madhehebu ya kukusanya, hawa wamesema kuwa kulala si hadathi bali ni kwa kuzoeleka kuwa hupelekea katika hadathi. Maimamu hawa wamehitalifiana kuhusu namna ya ulalaji unaowajibisha kutawadha.

 

Na kutokana na mielekeo hii mitatu ya Maulamaa hawa, pamechipuka kauli nane. [Ziangalie katika vitabu vya Al-Muhalla (1/222-231), Al-Istidhkaar (1/191), Al-Awsatw (1/142), Fat-h Al-Baariy (1/376), Sharhu Muslim cha An-Nawawiy (370) na Nayl Al-Awtwaar (1/241)].

 

Nazo ni:

 

Kwanza: Kulala hakutengui wudhuu kabisa

 

Haya yameelezewa yakinukuliwa toka kwa kundi la Maswahaba akiwemo Ibn ‘Umar na Abu Musa Al-Ash‘ariy. Nayo ni kauli ya Sa‘iyd bin Jubayr, Mak-huul, ‘Ubaydah As-Salmaaniy, Al-Awzaa‘iy na wengineo. Hoja yao ni:

 

(a) Hadiyth ya Anas bin Maalik (Allaah Amridhie) aliyesema: “Swalaah ilikimiwa nailhali Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anazungumza chemba na mtu fulani. Basi aliendelea kuzungumza naye mpaka Maswahaba zake wakalala. Halafu alikuja, akawaswalisha”.[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (6192) na Muslim (376), na tamshi ni lake].

 

 

(b) Imenukuliwa toka kwa Qataadah akisema: “Nilimsikia Anas akisema: “Maswahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) walikuwa wakilala, kisha wanaswali wala hawatawadhi”. Akasema: Nikasema: Je, umesikia toka kwa Anas? Akasema: Ndiyo, naapa kwa Allaah”.[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (376) na At-Tirmidhy (78)].

 

 

Na tamko jingine lasema: Wakingojea Swalaah, wakasinzia mpaka vichwa vyao vikajigonga (vikainamia chini), kisha husimama wakaswali”.

 

 

(c) Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas aliyesema: “Nililala kwa mama yangu mdogo Maymuunah. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasimama, nami nikasimama upande wake wa kushoto. Akauvuta mkono wangu akanisimamisha upande wake wa kulia. Nikawa kila ninaposinzia, hunivuta ndwele ya sikio. Aliswali rakaa 11”.[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (117) na Muslim (763), na tamshi ni lake].    

  

 

(d) Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas wakati alipolala kwa Maymuunah. Anasema: “…kisha Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alilala mpaka nikasikia mkoromo wake, kisha alitoka akaenda kuswali”.[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (117), Muslim (184), na Ahmad (1/341)].

 

Na katika tamko jingine: Kisha alisimama, akaswali na wala hakutawadha”.

 

 

Pili: Kulala kwa hali yoyote kunatengua wudhuu

 

Hakuna tofauti kati ya kulala kidogo au kulala sana. Haya ni madhehebu ya Abu Hurayrah, Abu Raafi’i, ‘Urwa bin Zubayr, ‘Atwaa, Al-Hasan Al-Baswriy, Ibn Al-Musayyib, Az-Zuhriy, Al-Mazniy, Ibn Al-Mundhir na Ibn Hazm. Ni chaguo la Al-Albaaniy. Ni kwa hoja zifuatazo:

 

 

(a) Ni kwa Hadiyth ya Swafwaan bin ‘Assaal. Amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akituamuru tunapokuwa safarini, tupukuse (tupanguse kwa maji) juu ya khofu zetu na wala hatuzivui kwa muda wa siku tatu hata kama tutakwenda haja kubwa au ndogo au kulala, ila kwa janaba”. [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na An-Nasaaiy (1/32), At-Tirmidhiy (3535) na Ibn Maajah (478). Angalia pia kitabu cha Al-Irwaai (104)].

 

Wamesema: “Hapa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amechukulia kiujumla usingizi wote wala hakuhusisha usingizi hafifu au mzito, wala hali hii kwa ile, na akaufanya sawa na haja kubwa na ndogo”.

 

(b) Ni kwa yaliyohadithiwa toka kwa ‘Aliy bin Abi Twaalib (Allaah Amridhie) aliyepokea toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 ((العينان وكاء السه، فمن نام فليتوضأ))

((Macho mawili ni kizibo cha tundu la haja kubwa. Basi mwenye kulala, atawadhe)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (203), Ibn Maajah (477) na wengineo. Ni dhwa’iyf kwa kauli yenye nguvu. Al-Albaaniy amesema ni Hadiyth Hasan].

 

"السه" ni tundu la nyuma la haja kubwa, na  "الوكاء"ni uzi unaofungiwa mdomo wa kiriba. Kwa hiyo kuwa macho kwa jicho, kumefanywa ni kama kizibo cha kiriba. Na jicho linapolala, kifuniko hicho huchopoka na hadathi huwa.

 

(c) Ni kwa Hadiyth ya ‘Aaishah kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((إذا نعس أحدكم وهو يصلي فليرقد حتى يذهب عنه النوم، فإن أحدكم إذا صلى وهو ناعس لا يدري لعله يستغفر فيسب نفسه))

((Anaposinzia mmoja wenu wakati anaswali, basi alale mpaka usingizi umwishe, kwani mmoja wenu anaposwali hali ya kuwa anasinzia, hajui pengine yeye anaona kuwa anaomba maghfirah huku kumbe anajitukana mwenyewe)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (212) na Muslim (222)].

 

Katika “Swahiyh yake”, Al-Bukhaariy ameitolea dalili Hadiyth hii juu ya ulazima wa kutawadha baada ya kulala. Lakini ninaloliona mimi ni kuwa kuna kijinukta cha kukizungumzia katika utoaji dalili kwa kutumia Hadiyth hii. Ikiwa ataifanya sababu ya kuikatiza Swalaah kutokana na usingizi ni kuchelea kujiombea mwenyewe vibaya, au kusoma asichokijua, au kutouhudhurisha moyo wake kukawa hakuna khushui, basi haya hayana uhusiano na kutawadha baada ya kulala. Bali huenda wenye kusema kuwa wudhuu hautenguki kwa usingizi wameitumia dalili hii kuthibitishia hoja yao. Basi atazame.

 

(d) Wamesema: "Maulamaa wote wamekubaliana kwamba ni lazima kutawadha kwa mtu aliyeondokewa na akili kwa wendawazimu au kupotewa na fahamu kwa hali yoyote iwayo. Pia aliyelala".

 

 

Tatu: Usingizi mzito unatengua kwa hali yoyote, na mwepesi hautengui

 

Hii ni kauli ya Maalik, riwaya ya Ahmad, Az-Zuhriy Rabi‘ah na Al-Awzaa‘iy!! Wameichukulia Hadiyth ya Anas ya kulala Maswahaba kuwa ni usingizi hafifu. Na pia wametolea dalili kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah:

من استحق النوم فقد وجب عليه الوضوء

((Mwenye kustahiki kulala, basi lazima atawadhe)). [Hadiyth Swahiyh Mawquwf. Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Abi Shaybah (1/158) na ‘Abdur-Raaziq (481) ikiwa Mawquwf kwa Sanad Swahiyh. Na imepokelewa ikiwa Marfu’u. Na si Swahiyh, kama alivyosema Ad-Daara Qutwniy katika Al’Ilal (8/954). Angalia Adh-Dhwa’iyfah (954)].

 

 

Lililo sahihi ni kuwa Hadiyth hii ni Mawquwf. Na Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas:

((وجب الوضوء على كل نائم إلا من خفق رأسه خفقة أو خفقتين))

 ((Ni lazima kutawadha kwa kila aliyelala, isipokuwa kwa yule aliyegonga kichwa mara moja au mara mbili)). [Hadiyth Dhwa’iyf Mawquwf Marfu’u. Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdur Raaziq (479), na Al- Bayhaqiy (1/119). Angalia  ‘Ilal Ad Daaru Qutwniy].

 

 

Nne: Kulala hakutengui ila kama atalala kwa ubavu au kwa kuegemea

 

Mwenye kulala kwa umbo lolote kati ya maumbo ya Swalaah kama kwa staili ya mwenye kurukuu, au mwenye kusujudu, au mwenye kusimama, au mwenye kukaa, basi wudhuu wake hautenguki, sawasawa akiwa katika Swalaah au nje ya Swalaah. Hii ni kauli ya Hammaad, Ath-Thawriy, Abu Haniyfah na wenzake, Daawuud na Ash-Shaafi’iy. Na hoja yao ni:

 

(a) Ni yale yaliyohadithiwa toka kwa ‘Amri bin Shu’ayb toka kwa baba yake aliyepokea toka kwa babu yake ya kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

  ليس على من نام جالسا وضوء حتى يضع جنبه

((Hakuna kutawadha kwa aliyelala kwa kukaa mpaka aweke ubavu wake)).

[Hadiyth Munkar: Imefanyiwa “ikhraaj” na ibn ‘Uday katika Al-Kaamil (6/2459), Ad-Daara Qutwniy (1/160) na At-Twabaraaniy katika Al-Awsatw..

 

Ni Hadiyth Dhwa’iyf, haifai.

 

(b) Ni Hadiyth ya Anas toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliyesema:

 

((إذا نام العبد في سجوده باهى الله تعالى به الملائكة يقول: أنظروا إلى عبدي روحه عندي وجسده في طاعتي))

((Anapolala mja katika sijda yake, Allaah Hujifaharisha kwake kwa Malaika Akiwaambia: “Mwangalieni Mja Wangu; roho yake iko Kwangu na mwili wake uko katika kunitii Mimi)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Angalia  kitabu cha As-Silsilat Adh-Dhwa’iyfah (953).

 

Na wamevipimia vipambo vingine vya mwenye kuswali kwa sijda.

 

 

Ninasema: “Hadiyth hii Sanad yake ni Dhwa’iyf. Al-Bayhaqiy amesema: “Kisha hakuna linaloashiria kuwa hatoki kwenye Swalaah yake. Na makusudio ya yaliyoelezwa - kama yatakuwa ni sawa - ni kumsifia mja anayedumu katika Swalaah mpaka usingizi ukamlemea”.

 

 

Tano: Hakutengui ila kwa aliyelala kwa umbo la kurukuu au kusujudu

 

An-Nawawiy ameinasibisha kauli hii kwa Ahmad. Na huenda mwono wake ni kuwa mwinamo wa kurukuu na kusujudu ulivyozoeleka, hupelekea kutenguka wudhuu.

 

 

Sita: Hakutengui ila kwa aliyelala kwa umbo la kusujudu 

 

Kauli hii imepokelewa vilevile toka kwa Ahmad. 

 

 

Saba: Usingizi ndani ya Swalaah hautengui kabisa, lakini nje ya Swalaah hutengua

 

Kauli hii imepokelewa na Abu Haniyfah kwa mujibu wa Hadiyth iliyotangulia katika kauli ya nne.

 

 

Nane: Wudhuu hautenguki kama atalala kwa kuambatisha barabara makalio yake chini, sawasawa ikiwa ni ndani ya Swalaah au nje yake, usingizi ukiwa mzito au mwepesi.

 

 

Haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy, kwa vile kwa mujibu wa anavyoona yeye ni kuwa usingizi wenyewe si hadathi, bali ilivyozoeleka ni kuwa hupelekea kwenye hadathi. Anasema Ash-Shaafi’iy: “Kwa vile mwenye kulala, hujiambatisha barabara na ardhi na hakiwezi kutoka chochote isipokuwa hukishtukia”. Ash-Shawkaaniy ameichagua kauli hii.

 

 

Ninasema: “Wenye kuisema kauli hii, wameichukulia Hadiyth ya Anas ya kulala Maswahaba juu ya kuwa walikuwa wamekaa. Al-Haafidh katika kitabu chake cha “Al-Fat-h” (1/251) amelijibu hilo kwa kusema: “Lakini katika musnadi ya Al-Bazzaar kwa Sanad Swahiyh katika Hadiyth hii (panaelezwa): “Wakaweka ubavu wao, wengine wakilala, kisha hunyanyuka wakaswali”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bazzaaz. Na kama hiyo hiyo, imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud katika kitabu cha Masaail Ahmad (uk.318). Na Isnadi yake ni Swahiyh kwa sharti ya Mashaykh Wawili. Tazama pia katika Tamaam Al-Minnah (uk.100)].

 

 

Lenye Nguvu

 

Usingizi mzito wa kutojifahamu kiasi ambacho mtu hawezi kusikia sauti, au kuhisi kudondoka kitu toka mkononi mwake, au kutokwa na udenda na mfano wa hayo, bila shaka usingizi huo unatengua wudhuu, kwani ilivyozoeleka hupelekea hadathi. Ni sawasawa ikiwa mtu amesimama, au amekaa, au amelala ubavu, au amerukuu au amesujudu, hakuna tofauti kati ya milalo hiyo.

 

Na ikiwa wenye kauli ya kwanza wanamaanisha usingizi wa aina hii, basi sisi tuko nao. Na kama si hivyo, basi usingizi mwepesi wa kusinzia ambao mtu huhisi yanayopita, hautengui wudhuu kwa hali yoyote iwavyo. Ni kwa Hadiyth ya kulala kwa Maswahaba mpaka vichwa vyao vikajigonga (vikainama). Pia kwa Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas aliposwali na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Na kwa haya, zinakusanyika dalili zote zilizokuja katika mlango huu.

 

Ni Zake Allaah Himdi na Ihsaan.

 

Faida

 

Ilivyokuwa usingizi umezoeleka kuwa hupelekea kwenye hadathi yenye kuwajibisha kutawadha, basi kutenguka kwake kutategemezewa kwa mwenye wudhuu kwa mujibu wa mwenyewe alivyolala na kwa jinsi dhana yake itakavyopondokea. Na ikiwa atafanya shaka kama alivyolala kunatengua au la, basi lililo na nguvu ni kuwa asihukumie kutenguka wudhuu wake, kwa vile twahara ni yenye kuthibiti kwa yakini na haiondoki kwa shaka. Na hili ndilo alilolichagua Shaykh wa Uislamu katika kitabu cha Al-Fataawaa (21/230).

 

 

4- Kuondokewa na akili kwa kulewa au kupoteza fahamu au wendawazimu:

 

Hili linatengua wudhuu kwa makubaliano ya Maulamaa wote. [Al-Awsatw cha Ibn Al-Mundhir (1/155)].

Na kupatwa na mfadhaiko au mshtuko kuna uzito zaidi kuliko kulala.

 

 

5- Kugusa utupu bila kizuizi sawasawa ikiwa ni kwa matamanio au bila ya matamanio

Maulamaa wana kauli nne kuhusu kugusa utupu baada ya kutawadha. Kauli mbili  kwa kutilia nguvu na kauli mbili kwa kukusanya.

 

 

Kauli ya kwanza:

 

Kugusa utupu hakutengui kabisa wudhuu.

 

Ni madhehebu ya Abuu Haniyfah na riwaya moja toka kwa Maalik. Pia kauli hii imepokelewa toka kwa kikundi cha Maswahaba. [Al-Badaai-’i (1/30), Sharhu Fat-hil Qadiyr (1/37), Al-Mudawwanah (1/8-9) na Al-Istidhkaar (1/308 na baada yake)].

Hoja zao ni haya yafuatayo:

 

(a) Ni Hadiyth ya Twaliq bin ‘Aliy kwamba mtu mmoja alimwuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu mtu anayegusa utupu wake baada ya kutawadha. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

هل هو إلا بضعة منك

((Hakika hiyo ni sehemu tu ya mwili wako)). [Isnadi yake ni Tepetepe: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (182), At-Tirmidhiy (85) na An-Nasaaiy (1/101). Maulamaa wamekhitalifiana juu ya kuwa ni Swahiyh au la. Kauli yenye nguvu ni kuwa Hadiyth hii ni Dhwa’iyf kwa ajili ya Qays bin Twaliq. Lakini Al-Albaaniy ameipasisha kuwa ni Swahiyh. Kwa hiyo kila mmoja na mwono wake. Na sisi hatuubani wasaa. Na Allaah Ndiye Mwelewa zaidi].

 

Na katika kauli nyingine, mwenye kuuliza alisema: “Wakati nikiwa katika Swalaah, niliingia kukuna paja langu na mkono wangu ukagusa dhakari yangu”. Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

إنما هو منك

((Hiyo ni sehemu ya mwili wako)). [Isnadi yake ni Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Dawuud (183), Ahmad (4/23), Al-Bayhaqiy (1/135) na wengineo].

(b) Wamesema: Wote wanakubaliana kwamba dhakari ikiligusa paja, basi hakuwajibishi kutawadha, na hakuna tofauti kati ya mkono na paja. Hakuna mahitilafiano yoyote kati ya Maulamaa katika suala hili. Na wameizungumzia Hadiyth ifuatayo ya Bisarrah inayogusia amri ya kutawadha kwa kuugusa uume. [Al-Awsatw (1/203). Na tizama pia Sharhu Ma’aaniy Al-Aathaar (1/71-79)].

 

Kauli ya pili:

 

Kugusa utupu kunatengua wudhuu kwa hali yoyote.

 

Ni madhehebu ya Maalik – kama anavyojulikana - , Ash-Shaafi’iy, Ahmad na Ibn Hazm. Kauli hii imepokelewa toka kwa Maswahaba wengi. [Al-Istidhkaar (1/308), Al-Mudawwanah (1/8-9), Al-Ummu (1/19), Al-Majmu’u (1/24), Al-Mughniy (1/178), Al-Insaaf (1/202), Al-Muhalla (1/235)].

Hoja yao ni:

 

(a) Hadiyth ya Bisarrah binti Swafwaan kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

من مس ذكره فليتوضأ

(( Mwenye kugusa dhakari yake, basi atawadhe)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (181), An-Nasaaiy (1/100) na Ibn Hibaan (1112)].

 

(b) Hadiyth ya Ummu Habiybah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

من مس فرجه فليتوضأ

((Mwenye kuugusa utupu wake, basi atawadhe)). [Ni Swahiyh kwa Hadiyth nyingine kama hii iliyopokelewa na Swahaba mwingine. Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Maajah (481), Abu Ya-’alaa (7144) na Al-Bayhaqiy (1/130). Angalia Al-Irwaa (117)].

 

Mfano wa Hadiyth hizi mbili umepokelewa katika Hadiyth ya Abuu Hurayra iliyohadithiwa na Binti Unays, ‘Aaishah, Jaabir, Zayd bin Khaalid na ‘Abdullahi bin ‘Amri.

Wamesema: Hadiyth ya Bisarrah inatiliwa nguvu kuliko Hadiyth ya Twaliq. Hii ni kwa sababu zifuatazo:

 

(a) Kwamba Hadiyth ya Twaliq ina kasoro. Imekosolewa na Abu Zar-’a, na Abu Hatim. Na An-Nawawiy katika Majmu’u (2/42), amezungumza sana akieleza kuwa wahafidhi wamekubaliana kuifanya Hadiyth hii dhwa’iyf!!

 

(b) Ingelikuwa ni Swahiyh, basi Hadiyth ya Abuu Hurayrah yenye maana sawa na Hadiyth ya Bisarrah, ingelitangulizwa, kwa vile Twaliq alikuja Madiynah wakati wanaujenga Msikiti nailhali Abu Hurayrah alisilimu mwaka wa Khaybar baada ya hilo kwa miaka sita. Na kwa ajili hiyo, Hadiyth yake itaondosha hukmu ya Hadiyth ya Twaliq. [Na kati ya waliosema kuwa hukmu yake imeondoshwa (naskh) ni: At-Twabaraaniy katika  Al-Kabiyr (8/402), Ibn Hibaan (3/405), Ibn Hazm katika Al-Muhalla (1/239), Al-Haazimiy katika Al-I’itibaar (77), Ibn Al-‘Arabiy katika Al-‘Aaridhwa (1/117) na Al-Bayhaqiy katika Al-Khilaafiyyaat (2/289)].

 

(c) Kwamba Hadiyth ya Twaliq inaubakisha uasili, lakini Hadiyth ya Bisarrah ni yenye kunukuu. Nayo hutangulizwa kwa vile hukmu za kisharia ni zenye kunukuu yale waliyokuwa wakiyafanya.

 

(d) Kwamba wapokezi wa kutenguka wudhuu kwa kugusa ni wengi na Hadiyth zake ni mashuhuri zaidi.

 

(e) Ni kauli ya Maswahaba wengi.

 

(f) Kwamba Hadiyth ya Twaliq imechukuliwa kuwa yeye alijikuna paja akaigusa dhakari yake juu ya nguo kama inavyoonyesha riwaya kuwa yeye alikuwa katika Swalaah.

 

 

Kauli ya tatu:

 

Wudhuu unatenguka ikiwa mtu kagusa dhakari yake kwa matamanio, na kama si kwa matamanio, basi hautenguki.

 

Hii ni riwaya toka kwa Maalik, na ni kauli iliyochaguliwa na Al-‘Allaamah Al-Albaaniy. [Angalia vitabu rejea vilivyotangulia vya madhehebu ya Maalik na kitabu cha Tamaam Al-Minna (uk 103). Hapo ameinasibisha kauli hii kwamba ni chaguo la Ibn Taymiyah. Amesema: “Ninavyokumbuka”. Ninasema: “Bali ni madhehebu ya nne ya Ibn Taymiyyah kama utakavyokuja kuona. Ametukuka Allaah Asiyesahau”].

 

Wenye kusema hivi, wameichukulia Hadiyth ya Bisarrah juu ya kama itakuwa ni kwa matamanio, na Hadiyth ya Twaliq juu ya kama si kwa matamanio. Wamesema kuwa kiashirio cha hilo ni neno lake:

 

((Hiyo ni sehemu ya mwili wako)).

 

Kwa hiyo kama ataugusa utupu wake bila ya matamanio, basi anakuwa ni kama aliyegusa kiungo chake kingine chochote.

 

 

Kauli ya nne:

 

Kutawadha kwa sababu ya kugusa dhakari kumesuniwa kwa hali yoyote na wala si wajibu.

Ni madhehebu ya Ahmad katika moja ya riwaya zake mbili  na  Shaykh wa Uislamu Ibn Taymiyah. Ni kauli ambayo Al-‘Allaamah Ibn ‘Uthaymiyn - Allaah Amrehemu – anaonekana kuwa ameipondokea zaidi, isipokuwa amelijaalia hilo kuwa ni Sunnah endapo kama ataigusa dhakari bila matamanio, na akatilia nguvu kuwa ni wajibu kama ni kwa matamanio kwa njia ya tahadhari. [Majmu’u Al-Fataawaa (21/241) na Ash-Sharhu Al-Mumti’i (1/233)]. Kwa hivyo wameichukulia Hadiyth ya Bisarrah kuwa ni Sunnah na Hadiyth ya Twaliq kuwa maswali yaliyoulizwa yalikuwa ni kwa upande wa wajibu.  

 

Kauli mbili za mwisho zinazosimamia juu ya mkondo wa kukusanya zinatolewa dalili kwa haya yafuatayo:

 

(a) Ni kwamba dai la kuwepo “naskh” kwa vile Twaliq alitangulia kusilimu kabla ya Bisarrah, ni lazima liangaliwe. Kwa kuwa dai hilo si dalili ya kuwepo “naskh” kwa upande wa wahakiki waliobobea katika fani ya taaluma ya “Uswuul”, kwa sababu aliyetangulia kusilimu anaweza kuwa alihadithia akiwa amenukulu toka kwa mwingine.

 

(b) Katika maelezo ya Twaliq, kuna sababu ambayo haiwezi kuondoka, nayo ni kuwa dhakari ni sehemu ya mwili wake. Na kama hukmu itafungamanika na sababu isiyoweza kuondoka, basi hukmu haiondoki. Kwa hiyo “naskh” haiwezekani kuwepo.

 

(c) Kisha ni kuwa suala halipelekwi katika “naskh” ila baada ya kushindikana kukusanya na hasahasa tukizingatia kuwa haifai kufanya “naskh” kama ilivyotangulia.

 

Ninasema: "Kauli ya mwisho ndiyo yenye nguvu kwa mujibu wa hali. Lakini endapo kama Hadiyth ya Twaliq bin ‘Aliy itakuwa ni Swahiyh - na hili liko mbali bali kauli ya kuifanya Dhwa’iyf ndiyo yenye mwelekeo zaidi - , basi kauli itakayokuwa na uzito ni ile isemayo kuwa kugusa uume kunatengua wudhuu kwa hali yoyote, ni sawasawa ikiwa ni kwa matamanio au bila ya matamanio, kwa vile matamanio hayana mpaka na wala hakuna dalili ya kipimo chake. Na Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.

 

Faida Kuhusu Yaliyotangulia

 

(a) Mwanamke akigusa utupu wake atatawadha:

Ni kwa Hadiyth ya ‘Amri bin Shu’ayb toka kwa baba yake aliyenukuu toka kwa babu yake, amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

((من مس ذكره فليتوضأ، وأيما امرأة مست فرجها فلتتوضأ))

((Mwenye kuigusa dhakari yake atawadhe, na mwanamke yeyote aliyeugusa utupu wake, basi atawadhe)). [Swahiyh kwa nyingine: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (2/223) na Al-Bayhaqiy (1/132)].

 

Hadiyth hii inatiliwa nguvu na kauli ya ‘Aaishah Allaah Amridhie isemayo:

 

“Mwanamke akiugusa utupu wake, atawadhe”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ash-Shaafi’iy katika “Musnadi yake” (90) na Al-Bayhaqiy (1/133). Al-Haakim amesema ni Swahiyh (1/138)].

 

Na asili ni kwamba wanawake ni washiriki wa wanaume katika hukmu. Na haya ndiyo madhehebu ya Ash-Shaafi’iy na Ahmad kinyume na Abu Haniyfah na Maalik!!

 

(b) Kugusa utupu wa mwingine:

 

Ikiwa mwanamume ataugusa utupu wa mkewe, au mkewe akaigusa dhakari yake, basi hakuna dalili ya kutenguka wudhuu wa yeyote kati yao isipokuwa tu kama madhii au manii yatatoka. Hapo wudhuu utatenguka kwa kutokwa na maji hayo na si kwa kuguswa. Lakini Maalik na Ash-Shaafi’iy wamesema kuwa ni lazima kutawadha kwa kujengea juu ya madhehebu yao kuwa wudhuu unatenguka kwa kumgusa mwanamke. Baadaye tutakuja kuona kwamba kauli yenye nguvu ni kinyume cha hivyo. [Mawaahib Al-Jaliyl (1/296) na Al-Ummu (1/20)].

 

Aidha, wudhuu hautenguki ikiwa mwanamke au mwanamume ataugusa utupu wa mtoto. Maalik amekubaliana na hili. Nayo pia ni kauli ya Az-Zuhriy na Al-Awzaa’iy. [Al-Kaafiy cha Ibn ‘Abdu Al-Barri (1/149) na Al-Awsatw (1/210)].

 

 

(c) Yote ni sawasawa kuugusa utupu kwa makosa au kwa kukusudia [Al-Muhalla (1/241) na Al-Awsatw (1/205-207)].

 

Ni madhehebu ya Al-Awzaa’iy, Ash-Shaafi’iy, Is-Haaq na Ahmad.

 

Na kundi la Maulamaa linaona kuwa lenye kutengua wudhuu ni kukusudia kuugusa. Kati yao ni Mak-huul, Jaabir bin Zayd na Sa’iyd bin Jubayr. Pia ni madhehebu ya Ibn Hazm aliyetolea dalili kwa Neno Lake Subhaanah:

 

 ((وَلَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ فِيمَا أَخْطَأْتُمْ بِهِ وَلَٰكِنْ مَا تَعَمَّدَتْ قُلُوبُكُمْ ۚ وَكَانَ اللَّهُ غَفُورًا رَحِيمًا))

((Wala si lawama juu yenu kwa mlivyokosea, lakini zipo lawama katika yale ziliyofanya nyoyo zenu kwa makusudi)). [Al Ahzaab (33:6)]

 

Yenye nguvu zaidi ni kauli ya kwanza. Ibn Al-Mundhir amesema: “Inampasa  aliyekufanya kuugusa utupu kwa maana ya hadathi yenye kuwajibisha kutawadha, akufanye kukusudia kwake au kutokusudia kuwa ni sawa kama ilivyo kwa hadathi nyinginezo”.

 

Ninasema: “Kukosea na kusahau kwa yanayohusiana na masharti na nguzo, kunasamehewa lakini hakuondoshi hukmu. Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi".

 

 

(d) Kugusa juu ya nguo hakutengui:

 

Kwa vile hili haliitwi kugusa kama inavyoonekana. Hili linatiliwa nguvu na Hadiyth ya Abu Hurayrah ambayo ni marfu’u:

 

إذا أفضى أحدكم بيده إلى ذكره ليس بينهما شيئ فليتوضأ

((Akipeleka mmoja wenu mkono wake katika dhakari yake bila kuwepo kizuizi kati yao, basi atawadhe)). [Hadiyth Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ad-Daara Qutwniy (1/147) na Al-Bayhaqiy (1/133). Na tizama pia katika Asw-Swahiyhah (1235)].

 

 

(e) Kugusa tundu ya nyuma hakutengui [Al-Muhallaa (1/238) na Al-Awsatw (1/212)].

 

Ni kwa vile tundu ya nyuma haiitwi utupu. Na si sahihi kuwekwa mizani moja na dhakari kwa kutokuwepo sababu jumuishi kati ya kugusa tundu ya nyuma na dhakari. Na kama mtu atasema kuwa sehemu zote mbili ni mapitio ya najsi, basi atajibiwa kuwa hiyo siyo sababu ya kutenguka wudhuu kutokana na kugusa. Halafu ikiwa kugusa najsi hakutengui wudhuu, basi vipi utenguke kwa kugusa mapitio yake?!! Hii ni kauli ya Maalik, Ath-Thawriy na Abuu Haniyfah na wenzake kinyume na Ash-Shaafi’iy.

 

 

6- Kati ya yanayotengua wudhuu ni kula nyama ya ngamia:

 

Aliyekula nyama ya ngamia sawasawa ikiwa mbichi, iliyopikwa au ya kuchoma, ni lazima atawadhe. Hii ni kwa Hadiyth ya Jaabir bin Samrah anayesema kwamba mtu mmoja alimuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Je, tutawadhe kwa kula nyama ya kondoo au mbuzi?” Akamjibu:

 ((إن شئت توضأ، وإن شئت فلا تتوضأ))

((Ukitaka tawadha, ukitaka usitawadhe)).

Akamuuliza: “Je, tutawadhe kwa kula nyama ya ngamia?” Akasema:

 ((نعم، توضأ من لحوم الابل))

((Ndiyo, tawadha ukila nyama ya ngamia)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (360) na Ibn Maajah (495)].

 

Na imepokelewa toka kwa Al-Barraa bin ‘Aazib kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 توضأوا من لحوم الابل، ولا توضأوا من لحوم الغنم

((Tawadheni kwa kula nyama ya ngamia, na msitawadhe kwa kula nyama ya kondoo na mbuzi)).[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (184), At-Tirmidhiy (81) na Ibn Maajah (494)].                                                                                  

 

Na haya ni madhehebu ya Ahmad, Is-haaq, Abu Khaythamah, Ibn Al-Mundhir na Ibn Hazm. Pia ni moja kati ya kauli mbili za Ash-Shaafi’iy na ni chaguo la Shaykh wa Uislamu. Aidha, ni kauli iliyopokelewa toka kwa Ibn ‘Umar na Jaabir bin Samrah.

 

Lakini Jamhuri ya Maulamaa kama Abu Haniyfah, Maalik, Ash-Shaafi’iy, Ath-Thawriy na kundi la watangu wema, hawa wanaona kwamba si lazima kutawadha kwa kula nyama ya ngamia bali ni Sunnah. [Al-Mabsuwtw (1/80), Mawaahib Al-Jaliyl (1/320), Al-Majmuu (1/57), Al-Mughniy (1/138), Al-Muhalla (1/241) na Al-Awsatw (1/138)].

 

 

Na hii ni kutokana na Hadiyth ya Jaabir aliyesema: “Amri mbili za mwisho toka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni kutotawadha kwa kula kilichoivishwa kwa moto”.[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (192), Attirmidhiy (8) na An-Nasaaiy (1/108)].

 

Wakiizungumzia kauli hii wamesema: “Neno lake “kile kilichoivishwa kwa moto” linakusanya nyama ya ngamia vilevile, nayo imethibiti kunasikhiwa”.

Hili linajibiwa kwa mambo mawili: [Al-Muhallaa (1/244) na Al-Mumti’i (1/249)].

 

 

La kwanza:

 

Ni kwamba Hadiyth ya Jaabir ni jumuishi, na yale yaliyopokelewa katika kutenguka wudhuu kwa kula nyama ya ngamia ni hali maalumu. Na jambo jumuishi hutangulizwa kabla ya jambo maalumu, na hapo hutoka lile ambalo umaalumu wake umeainishwa na dalili.  Na hapa naskhi haizungumziwi kwa vile inawezekana kukusanya.

 

La pili:

 

Amri iliyokuja kuamuru kutawadha kwa kula nyama ya ngamia, ni hukmu inayohusiana na iliyoivishwa kwa moto au mbichi. Kwa hiyo kuivishwa kwa moto hakuwajibishi kutawadha, na kwa hivyo hukmu yake inakuwa nje ya habari zilizokuja kuhusu kutawadha kwa kula kilichopikwa na kwa kunaskh wudhuu.

 

Baadhi yao wanasema kwamba makusudio ya wudhuu katika Hadiyth ni kuosha mkono!! [Majmu’u Al-Fataawaa (21/260 na baada yake)].

 

Hili ni batili kwani hakuna wudhuu mwingine uliokuja kupitia maneno ya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) zaidi ya wudhuu wa Swalaah. Kisha, katika Hadiyth ya Jaabir bin Samrah iliyopokelewa na Muslim, amri ya kutawadha kwa sababu ya kula nyama ya ngamia, imefungamanishwa na kuswali katika sehemu ya malalio yao kwa kutofautisha kati ya hilo na kuswali katika mapumzikio ya mbuzi. Hivi ndivyo unavyojulikana wudhuu wa Swalaah bila mjadala.

 

Lenye Nguvu:

 

Ni kuwa ni lazima kutawadha kwa kula nyama ya ngamia kwa hali yoyote ile. Na kwa ajili hiyo, An-Nawawiy katika kitabu cha “Sharh Al-Muslim” (1/328) anasema: Madhehebu  haya yana nguvu zaidi ingawa Jamhuri ya Maulamaa wako kinyume nayo.

 

Tanbihi:

 

Ya kwanza:

 

 Katika “Sharh Al-Muslim” (1/328), An-Nawawiy ameinasibisha kauli ya kutolazimu kutawadha kwa kula nyama ya ngamia kwa Makhalifa Wanne Waongofu!! Madai haya hayana dalili yoyote wala haijulikani Sanad yoyote kwao inayohusiana na hilo. Ibn Taymiyah Allaah Amrehemu ametanabahisha kuhusu madai haya akisema: “Ama yule aliyenukulu toka kwa Makhalifa Waongofu au Jamhuri ya Maswahaba kwamba wao walikuwa hawatawadhi kwa kula nyama ya ngamia, basi amewatendea kosa. Hilo anakuwa ameliwazia na kulidhania tu kutokana na yale yaliyonukuliwa kuhusu wao ya kuwa walikuwa hawatawadhi kwa kula kilichoivishwa kwa moto…”. [Al-Qawaaid An-Nuwraaniya (uk.9) ikinukulu toka kwa Tamaam Al-Minnah (uk.105)].

 

 

Ya pili:

Kisa Mashuhuri Cha Uzushi  [Tizama Adh-Dhwa’iyfah ya Al-Albaaniy (1132) na Qaswasun Laa Tathbut cha Mash-huur Hasan (uk.59)].

 

Kimetangaa baina ya watu wa kawaida kisa wanachokihadithia mara kwa mara. Kisa hiki wamekisikia toka kwa wanafunzi wanaoeleza kwamba ni lazima kutawadha kwa kula nyama ya ngamia. Kisa hiki kinaeleza kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa katika kundi la Maswahaba wake, akasikia harufu ya ushuzi kwa mmoja wao. Swahaba huyo akaona haya kunyanyuka kati ya watu, naye alikuwa amekula nyama ya ngamia. Hapo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

 ((من أكل لحم جزور فليتوضأ))

((Aliyekula nyama ya ngamia basi akatawadhe)).

Hapo wote waliokuwa wamekula ngamia wakanyanyuka wakaenda kutawadha!!

Kisa hiki ni Dhwa’iyf kwa upande wa Sanad na Munkari kwa upande wa Matni.

 

 

 

 

Share