042-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Je, Khufu Iliyotoboka Hupukuswa?

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

042-Je, Khufu Iliyotoboka Hupukuswa?

 

Alhidaaya.com

 

 

Mafuqahaa wengi wameshurutisha kwamba ili kupukusa juu ya khufu mbili kujuzu, ni lazima ziwe  ni zenye kusitiri mahala palipolazimu kuoshwa katika wudhuu. Kwa ajili hiyo, wamekataza kupukusa juu ya khufu iliyotoboka, kwani huonekana kupitia khufu hiyo, mahala pa viungo vinavyolazimu kuoshwa. Na kuosha na kupukusa havikutani pamoja, na kwa hivyo hukmu ya  kuosha inapewa uzito zaidi.

 

Haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy na Ahmad. [Al-Ummu (1/28), Masaail Ahmad cha Ibn Haani (1/18) na Al-Mughniy (1/287)].

 

Na Maalik na Abuu Haniyfah wamesema kuwa inajuzu kupukusa juu ya khufu iliyotoboka madhali inaweza kutembelewa na jina lake bado lipo. Na hivi ndivyo alivyosema Ath-Thawriy, Is-Haaq, Abu Thawr, Ibn Hazm, Ibn Al-Mundhir na Ibn Taymiyah. [Al-Mudawwanah (1/44), Al-Mabsuwtw (1/100), Al-Awsatw (1/449), Al-Muhalla (2/100) na Majmuu Al-Fataawaa (21/173)].

 

Haya ndiyo sahihi, kwani ruksa ya kupukusa juu ya khufu mbili ni ruksa jumuishi; kinaingia kila kiitwacho khufu kwa mujibu wa uhalisia ulivyo, na haiwezekani kuibagua khufu fulani ikaachwa nyingine ila kwa dalili. Na lau kama kutoboka kunazuia kupukusa, basi Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) angelibainisha hilo na hasa tukizingatia kwamba Maswahaba wengi walikuwa ni masikini katika enzi yake. Khufu za wengi wao zilikuwa hazikosi matobo.

 

Share