048-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Nne: Kupaka Juu Ya “Al Jabiyrah”

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

048-Nne: Kupaka Juu Ya “Al Jabiyrah”

 

Alhidaaya.com

 

 

"Al Jabiyrah" ni majiti mawili ambayo huungiwa kwayo mifupa iliyovunjika ili ishikamane. Na katika maisha yetu ya leo, plasta ya jasi (piopi) hutumiwa badala yake.

 

Na mtu ambaye katika kiungo chake kimoja cha wudhuu kutakuwa na "jabiyrah" (piopi) kama mikono miwili au miguu miwili, basi inajuzu kwake kupukusa kwa mujibu wa rai ya Jamhuri ya Maulamaa wakiwemo Maimamu wanne na wengineo. [Sharh Fat-h Al-Qadiyr (1/140), Al-Mudawwanah (1/23), Al-Mughniy (1/203) na Al-Majmu'u (2/327)].

 

Wao wametolea dalili yafuatayo:

 

1- Hadiyth ya Jaabir kwa yule aliyepatwa na mpasuko usoni, na kauli ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Hakika inamtosheleza tu kufunga jeraha lake kwa kitambaa, kisha akapukusa juu yake)). Na hii ni Hadiyth Dhwa’iyf. [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (236) na wengineo. Angalia Al-Irwaa (105)].

 

2- Ni kauli ya Ibn 'Umar: "Mwenye jeraha lililofungwa, atatawadha na atapukusa juu ya bendeji, na ataosha pembezoni mwa bendeji".[Isnadi yake ni Swahiyh: Imekharijiwa na Ibn Abi Shaybah (1/126) na Al-Bayhaqiy (1/228)].

 

Na hajulikani Swahaba yeyote aliyekwenda kinyume na Ibn 'Umar.

 

3- Ni kuchukulia kipimo cha kupukusa juu ya khufu mbili, kwani kupukusa juu ya khufu mbili kunajuzu bila ya dharura, basi vipi kwa upande wa "jabiyrah" (piopi) ambayo ni dharura? Hivyo inachukua uzito zaidi.

 

Na Ibn Hazm ameshikilia msimamo wa kuwa mwenye kufungwa "jabiyrah", basi halazimiki kupukusa juu yake na kwamba hukmu ya mahali hapo inaondoka. [Al-Muhallaa (2/74)].

 

Ninasema: "Hii ni kwa vile Ibn Hazm amezichukulia Hadiyth za kupukusa juu ya bendeji, plasta n.k kuwa ni Dhwa’iyf na wala haoni Qiyaas kuwa ni hujjah!! Na Hadiyth hizi hazifai kama alivyosema. Ama Qiyaas, bila shaka itakuwa ni hujjah endapo kama nguzo na sharti zake zitakuwepo. Lakini inaweza kusemwa kuwa Qiyaas hapa hakifai kutokana na kutofautiana tanzu na asili. Ni Qiyaas waajib (kupukusa juu ya piopii kwa Jamhuri ya Maulamaa) juu ya mubaah (kupukusa juu ya khufu mbili). Na hapa basi, madhehebu ya Ibn Hazm yanang'aa. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.

 

Faida

 

1- Kupukusa juu ya "jabiyrah" (piopi) kunatosheleza, sawasawa katika wudhuu au katika kuoga, kwa vile "jabiyrah" (piopi) ni jambo lisilo na budi, na kwa hivyo hakuna tofauti ndani yake kati ya hadathi ndogo na hadathi kubwa. Ni kinyume na kupukusa juu ya khufu mbili, kwani hili limeruhusiwa (kwa atakaye).

 

2- Si lazima kufungwa "jabiyrah" wakati mtu ana twahara wala hakuna muda maalumu wa kupukusa juu yake.

 

Hii ni kwa vile, hilo linakwenda kinyume na makusudio ya sharia katika kuruhusu kupukusa kati ya kuondosha uzito na tabu. Aidha, kufungwa (piopi) ni hali ya kulazimika ambayo huja ghafla bila kutegemewa kinyume na khufu mbili. Mbali ya hivyo, hakuna matni au Ijma’a.

Hivyo basi, hakuna muda maalumu wa kupukusa juu ya "al-Jabiyrah". Lakini wakati wowote atakapoliondosha au kiungo kikapona, basi haitojuzu kupukusa.

 

3- Bendeji na plasta za kitiba (hospitali) zilizofungwa katika kiungo cha wudhuu, zina hukmu ya "al-Jabiyrah" (piopi) kama lilivyohakikiwa hilo na Shaykh wa Uislamu. [Majmuu Al-Fataawaa (21/185)].

 

 

Share