049-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Kuoga

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

049-Kuoga

 

Alhidaaya.com

 

 

Kilugha maana yake ni kuchuruzika maji juu ya kitu. Ama kisharia, ni kumiminisha maji yaliyo twahara katika mwili wote kwa njia maalumu. [Kash-Shaaf Al-Qinai (1/158)].

 

Yenye Kupasisha Kuoga

 

1- Ni kutokwa na manii mtu akiwa macho au usingizini

 

Ni kwa Neno Lake (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

((وإن كنتم جنبا فاطهروا))

((Na mkiwa na janaba, basi ogeni)). [Al-Maaidah (5:6)].

 

Na  Neno Lake (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

(( يا أ يها الذين لا تقربوا الصلاة وأنتم سكارى حتى تعلموا ما تقولون ولا جنبا إلا عابري سبيل حتى تغتسلوا))

((Enyi walioamini! Msikaribie Swalaah hali mmelewa, mpaka muyajue mnayoyasema, wala hali mna janaba – isipokuwa mmo safarini – mpaka mkoge)). [An-Nisaa (4:43)].

 

Na imepokelewa toka kwa Abu Sa'iyd Al-Khudriy toka kwa Rasuli  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba amesema:

 (( إنما الماء من الماء))

((Hakika maji ni kutokana na maji)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (343) na Abuu Daawuud (214)].

 

Yaani kuoga (kwa maji), sababu yake ni kumwaga (maji), nayo ni manii.

 

Na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia 'Aliy:

((إذا فضخت الماء فاغتسل))

((Ukimwaga maji, basi oga)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (206), An Nasaaiy (193) na Ahmad (1/247). Asili yake ni kutoka Swahiyh Mbili.

 

Na katika tamko jingine:

((إذا حذفت))

((Utakapokatia))

 

Na hayawi kwa sifa hii ila yanapotoka kwa matamanio kama Alivyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

((خلق من ماء دافق))

((Ameumbwa kutokana na maji yenye kuchupa)). [At Twaariq (86:6)].

 

Na imepokelewa toka kwa Ummu Salamah (Allaah Amridhie) akisema:

"Alikuja Ummu Sulaym, naye ni mke wa Abu Twalha, kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Hakika Allaah Haonei haki hayaa. Je, inampasa mwanamke kuoga kama ameota? Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

 ((نعم، إذا رأت الماء)) 

((Naam, kama akiyaona maji)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaary (282) na Muslim (313)].

 

Kauli hii inafahamisha kuwa si lazima manii yatoke kwa matamanio na kuchupa wakati wa kuota ndipo ipase kuoga, bali itambidi kuoga anapoyaona manii katika nguo yake. Na kama hakuyaona, basi hapaswi kuoga hata kama atakumbuka kuwa aliota. Hii ni kutokana na Hadiyth ya Mama wa Waumini 'Aaishah (Allaah Amridhie) aliyesema:

"Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa kuhusu mtu anayekuta ubichi ubichi na wala hakumbuki kama aliota. Akasema: 

((يغتسل))

((Ataoga))

 

Na kuhusu mtu anayeona kwamba aliota lakini hakukuta ubichi bichi, akasema:

 ((لا غسل عليه))

((Hapaswi kuoga)).[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhy (113) na Abuu Daawuud (233)].

 

Zindushi Mbili

 

(a) Katika yote yaliyotangulia, mwanamke ni kama mwanamume, sawa kwa sawa.

 

(b) Yeyote mwenye kuchuruzikwa na manii bila ya matamanio kutokana na ugonjwa, au baridi au mfano wa hayo, basi hana lazima kuoga kwa mujibu wa kauli mbili zilizo sahihi zaidi za Maulamaa. Na haya ndiyo madhehebu ya Jamhuri kinyume na Ash-Shaafi'iy na Ibn Hazm.

 

Na Maulamaa kwa sauti moja wamesema kuwa ni lazima kuoga mtu anapotokwa na manii kwa matamanio wakati yu macho, na anapotokwa na manii akiota usingizini. [Al-Majmuu (1/139), Bidaayat Al-Mujtahid (1/58) na As-Sayl Al-Jarraar (1/104)].

 

Isipokuwa yale yaliyopokelewa toka kwa Ibraahiym An-Nakh'iy kwamba yeye alikuwa haoni kuwa inampasa mwanamke kuoga anapoota na kujimwagia. 

 

2- Kukutana tupu mbili ijapokuwa bila ya kumwaga manii

 

Kinapozama kichwa cha dhakari ya mwanamume katika utupu wa mwanamke, basi inawalazimu wote wawili kuoga ni sawa ikiwa wamemwaga manii au hawakumwaga. Hii ni kutokana na Hadiyth ya Abu Hurayrah aliyoipokea toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

(( إذا جلس بين شعبها الأربع، ثم جهدها فقد وجب الغسل)) (وإن لم ينزل))

((Anapokaa kati ya tanzu zake nne, kisha akamtoa jasho, basi ni lazima kuoga)) ((hata kama hakumwaga)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (291) na Muslim (348) na ziada ni yake yeye].

 

Na imepokelewa toka kwa Mama wa Waumini 'Aaishah (Allaah Amridhie) kwamba mtu mmoja alimuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu mtu anayemwingilia mkewe kisha akaishiliwa nguvu, je, ni lazima waoge? – nailhali Mama wa Waumini 'Aaishah yuko hapo amekaa - Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

 (( إني لأفعل ذلك أنا وهذه ثم نغتسل ))

((Hakika mimi nafanya hilo na huyu, kisha tunaoga)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (350)]

 

Amesema An-Nawawiy: "Na hili halina mvutano hivi leo. Lilikuwa na mvutano kwa baadhi ya Maswahaba na waliokuja baada yao. Kisha ikafungika Ijma’a’ juu ya tuliyoyataja."

 

Ninasema: “Ama hitilafu ya Maswahaba katika suala hili, miongoni mwake ni Hadiyth ya Zayd bin Khaalid ambapo yeye alimuuliza 'Uthmaan bin 'Affaan akimwambia: "Unasemaje endapo mtu atamwingilia mkewe na wala hakumwaga manii"? 'Uthmaan akamwambia: "Atatawadha kama anavyotawadha kwa ajili ya Swalaah na ataosha dhakari yake". Akasema 'Uthmaan: "Nimelisikia hilo toka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na nikaliulizia hilo kwa ‘Aliy bin Abi Twaalib, Az-Zubayr bin Al-'Awwaam, Twalha bin 'Ubayd Allaah na Ubay bin Ka'ab, nao wakamwamuru hilo". [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (292) na Muslim (347)].

 

Daawuud Adh-Dhwaahiriy ameelekea msimamo wa kutolazimu kuoga kama mtu hakumwaga kwa Hadiyth:

((Hakika maji ni kutokana na maji)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (348). Imeshatajwa nyuma.]

 

Na Hadiyth ya Abu Sa'iyd kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia mtu fulani:

(( إذا أعجلت ـ أو قطحت – فعليك الوضوء))

((Ukiingilia bila kumwaga, basi yakupasa kutawadha)).[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (180) na Muslim (345)].

 

Ama Maswahaba hawa, bila shaka imethibiti kutoka kwao kuwa waliachana na kauli ya kutokupasa kuoga. [Angalia athar kutoka kwao katika kitabu cha Jaami'u Ahkaamin Nisaa cha Shaykh wetu (Allaah Amhifadhi) (1/89,90)].

 

Ama kauli ya Daawuud, bila shaka imekwenda kinyume na Jamhuri ya Maswahaba wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Mafuqahaa wa Taabi-'iyna na waliokuja baada yao. Hawa wanaona kwamba Hadiyth ya ((Maji ni kutokana na maji)) na yaliyo katika maana yake, ilikuwa ni mwanzoni mwa Uislamu kisha ikanasikhiwa.

 

At-Tirmidhiy amesema (1/185):

"Na hivi ndivyo alivyopokea zaidi ya mtu mmoja katika Maswahaba wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwemo Ubay bin Ka'ab na Raafi'i bin Khudayj. [Hadiyth ya Ubayya ni Swahiyh kwa njia zake kama alivyoibainisha Shaykh wetu Abu ‘Umayr Al-Athariy- Allaah Amstareheshe katika maisha yake- katika Shifaau Al'ayyi Bitahqiyq Musnad Ash-Shaafi'iy (100)].

 

Na hili ndilo linalofanywa na Maulamaa wengi zaidi kuwa mtu anapomwingilia mkewe katika tupu, inawabidi wote wawili kuoga hata kama hajamwaga manii”.

 

Faida  [Zimetolewa toka kwenye kitabu changu cha Fiqhu As Sunnah Lin Nisaa (uk 46)].

 

1- Dhakari ya mwanamume ikigusa uchi wa mwanamke bila kuingizwa ndani, basi haiwapasi kuoga kwa makubaliano ya Maulamaa. [Al-Mughniy cha Ibn Qudaamah (1/204)].

 

Ibraahiym An-Nakh'iy aliulizwa kuhusu mtu anayemwingilia mkewe sehemu isiyokuwa tupu (farji) kisha akamwaga. Alijibu akisema:

"Atakoga yeye, lakini mkewe hakogi bali ataosha sehemu iliyochafuka". [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdu Rrazzaaq (971). Angalia athar mfano wake kutoka baadhi ya watangu wema katika  Jaami Ahkaam An-Nisaa (1/95)].

 

2- Mtu akimwingilia mkewe, akaingiza sehemu ndogo tu ya kichwa cha dhakari, kisha manii yake yakaingia katika utupu wa mkewe, na mkewe hakumwaga, basi haimpasi mke kuoga.

Amesema An-Nawawiy: "Anapoingiziwa mwanamke manii katika utupu wake wa mbele au wa nyuma kisha manii hayo yakatoka, basi hapaswi kuoga. Hili ndilo sahihi lililopitishwa na Jamhuri." [Al-Majmu’u (2/151). Tazama Al-Muhalla (2/7)].

 

3- Mtu anapomwingilia mkewe kisha mkewe akakoga, halafu baadaye yakamtoka manii ya mumewe toka kwenye utupu wake, basi hapaswi kuoga tena. Lakini je, itamlazimu kutawadha?

 

Kwa mujibu wa kauli ya Jamhuri, itamlazimu kutawadha kwa vile maji hayo yametoka kupitia moja ya njia mbili ingawa ni twahara. [Al-Majmu’u (2/151)

 

Ibn Hazm amesema:

"Wudhuu utampasa kutokana na hadathi yake yeye na wala si kutokana na hadathi ya mwingine. Na kutoka manii ya mumewe toka kwenye utupu wake hakuzingatiwi kuwa yeye ndiye anayemwaga, wala haizingatiwi kuwa ni hadathi yake yeye. Kwa hivyo, hakogi wala hatawadhi." [Al-Majmu’u (2/151).

 

Ninasema: “Ama kaida ya kutawadha kwa kila chenye kutoka katika moja ya njia mbili, kaida hii haikubaliki kama ilivyotangulia, kwani mapitio ya manii kwa mwanamke, siyo mapitio ya mkojo. Hivyo basi madhehebu ya Ibn Hazm yanakuwa na nguvu zaidi. Lakini pamoja na hivyo, pachukuliwe tahadhari kuwa manii haya yanaweza kuchanganyika na madhii ya mwanamke. Hivyo la akiba zaidi atawadhe, na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.

 

4- Mume akimwingilia mkewe mdogo ambaye bado hajaanza kuingia hedhini, au mtoto mdogo ambaye hajabaleghe akamwingilia mwanamke, basi inamlazimu mwanamke kuoga vile vile kama alivyosema Imam Ahmad:

"Hebu nielezeni! Je, 'Aaishah, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akimwingilia, alikuwa hakogi?!  [Al-Mughniy (1/206)].

 

5- Mume anapomtaka mkewe kufanya mapenzi, basi haitakikani kumkatalia hilo kwa kisingizio cha kutokuwepo maji ya kukogea.

 

Shaykh wa Uislamu katika "Al-Fataawaa" 21/454" anasema:

"Haitakikani kwa mwanamke kumkatalia mumewe tendo la ndoa. Amwachie amwingilie. Na ikiwa ataweza kuoga, basi akoge, na kama hakuweza, atatayammamu na kuswali".

 

3, 4 – Hedhi na nifasi

 

Mambo haya mawili ni sababu mbili zenye kuwajibisha kukoga. Na kwa vile kukoga kunatokana na sababu ambapo hakufanyiki ila baada ya kukatika kwake na kumalizana nayo, inabidi kukoga baada ya kukatika hedhi na nifasi.

 

Imepokelewa na Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha) kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia Faatwimah binti Abi Hubaysh:

((إذا أقبلت الحيضة فدعي الصلاة، وإذا أدبرت فاغتسلي وصلي))

((Hedhi ikija basi acha Swalaah, na ikiondoka basi oga na uswali)). [Hadiyth Swahiyh: Takhriyj yake itakuja katika mlango wa hedhi].

 

Na nifasi ni kama hedhi kwa Ijma’a. Kisha imethibiti toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiielezea nifasi kama hedhi na hedhi kama nifasi.

 

Hukmu za hedhi na nifasi zitakuja kuelezewa kwa uchambuzi InshaAllaah.

 

5- Kafiri anaposilimu

 

Maulamaa wana kauli tatu kwa upande wa hukmu ya kuoga wakati kafiri anaposilimu:

 

Kwanza:

 

Ni lazima aoge kwa hali yoyote. Haya ni madhehebu ya Maalik, Ahmad, Abu Thawr na Ibn Hazm. Pia Ibn Al-Mundhir na Al-Khattwaabiy wamelikhitari. [Mawaahib Al-Jaliyl (1/311), Al-Mughniy (1/152), Al-Majmu’u, (2/175) na Al-Muhalla (2/4)].

 

Dalili zao ni:

 

1-      Hadiyth ya Qays bin ‘Aaswim aliyesema kwamba aliposilimu, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwamuru akoge kwa maji na mkunazi. [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (355), At-Tirmidhiy (605) na An-Nasaaiy (1/109). Tazama “Al-Mishkaat” (543)]. Na asili ya amri hii ni ulazima.

 

2-      Ni yale yaliyomo katika Hadiyth ya Abu Hurayrah katika kusilimu Thumaamah bin Uthaal kutokana na kauli ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Nendeni naye hadi katika bustani ya Bani fulani, kisha mwamrisheni akoge)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (2/304) na Ibn Khuzaymah (252). Na asili yake ni kutoka Swahiyh Mbili, lakini hakuna amri ya kuoga. Angalia vilevile Al-Irwaa (128)].

 

3-      Kisa cha kusilimu Usayd bin Hudhayr. Kisa hiki kinaeleza kwamba Usayd aliwauliza Mus’ab bin ‘Umayr na As’ad bin Zuraarah: “Mnafanya vipi mkitaka kuingia katika Dini hii?” Wakajibu: “Unaoga unatwaharika, halafu unazitwaharisha nguo zako mbili, kisha unashuhudia shahada ya haki, halafu unaswali…” Hadiyth. [Isnadi yake ni Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Twabary katika kitabu cha At Taariykh (1/ 560), na Ibn Hishaam katika As Siyrah (2/285)].

 

Pili:

 

Inapendeza (imesuniwa) kafiri akoge, isipokuwa tu kama alikuwa na janaba kabla ya kusilimu, hapo italazimu akoge. Haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy na Abu Haniyfah. [Al-Majmu’u (1/174), Al-Ummu (1/38) na Ibn ‘Aaabidyn (1/167)].

 

Tatu:

 

Si lazima kukoga kwa hali yoyote. Ni madhehebu ya Abu Haniyfah. [Al-Mabsuwtw na Sharh Fat-h Al-Qadiyr (1/59)].

 

Hawa wametoa dalili zao katika haya yafuatayo:

 

1.     Neno Lake Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

(( قل للذين كفروا إن ينتهوا يغفر لهم ما قد سلف )) 

((Waambie waliokufuru, ikiwa wataacha (ukafiri), watasamehewa yaliyopita)). [Al-Anfaal (8:38)]

 

2.     Hadiyth ya ‘Amru bin Al-‘Aasw ikiwa Marfu’u:

((Uislamu unapomosha yaliyopita)).[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (121) kutoka kwa Hadiyth ya ‘Amri bin Al ‘Aasiy].

 

Katika kutolea ushahidi wa Aayah na Hadiyth, kuna mlahadha. Ni kuwa yanayokusudiwa katika Aayah na Hadiyth ni kughufiriwa madhambi. Maulamaa wamekubaliana wote kuwa anayesilimu lau kama alikuwa na deni au kisasi, basi hayo hayafutiki kwa kusilimu kwake, na hasa kwa vile kuwa kulazimika kuoga si uchukulifu au ukalifisho kwa yaliyomlazimu katika ukafiri, bali ni ulazimisho wa sharti katika masharti ya Swalaah katika Uislamu, kwani yeye ana janaba. Na Swalaah haisihi mtu akiwa na janaba. Naye havuliki na janaba hiyo kwa kuwa ameingia katika Uislamu. [Al-Majmu’u (2/174)].

 

3.     Wamesema:

“Watu wengi walisilimu wakiwa na wake na watoto lakini Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwaamrisha kuoga kwa njia ya lazima. Na lau ingelikuwa ni wajibu, basi angeliwaamrisha hilo”.

 

Na hapa kuna mlahadha:

 

Lililo dhahiri ni wajibu kuoga, kwani kuamrishwa baadhi, kuna maana kuwa wao washafikishiwa amri. Ama kudai kuwa wengineo hawakuamrishwa, hilo halifai kwa kushikilia tu, kwani ukomo wake ni wao tu kutokuwa na habari nalo, nako si kutojua kwa sababu ya kutojulikana. [Nayl Al-Awtwaar (1/281)].

 

Kwa hivyo, lenye nguvu zaidi ni kuwa inamlazimu kafiri – sawasawa akiwa kafiri wa asili au aliyeritadi – aoge kwa hali yoyote anaposilimu. Na linalotuhisisha kwamba kuoga wakati wa kuingia katika Uislamu lilikuwa ni jambo linalojulikana vizuri na Maswahaba, ni yale yaliyomo ndani ya kisa cha kusilimu mama wa Abu Hurayrah. Kisa kinaeleza kuwa mama huyo alioga na akavaa deraya yake.[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (2491) na Ahmad (7911)].

 Pia kisa kilichotangulia cha kusilimu Usayd bin Hudhayr. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

6- Swalaah ya Ijumaa

 

Kukoga siku ya ijumaa ni jambo la lazima, na mwenye kuacha, basi anapata dhambi kwa mujibu wa kauli mbili sahihi zaidi za Maulamaa. Haya yamesemwa na Abuu Hurayrah, 'Ammaar bin Yaasir, Abuu Sa'iyd Al-Khudriy na Al-Hasan. Haya yamekuja pia katika riwaya iliyopokelewa toka kwa Maalik na Ahmad. Aidha, ni madhehebu ya Ibn Hazm. [Al-Muhalla (2/12) na Al-Awsatw (4/43)].

 

Dalili za hili ni:

 

1- Hadiyth ya Abuu Sa'iyd Al-Khudriy kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) amesema:

((غسل يوم الجمعة واجب على كل محتلم)(

((Kukoga siku ya ijumaa ni wajibu kwa kila aliyebaleghe)).[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (2491) na Ahmad (7911)].

 

2- Hadiyth ya Ibn 'Umar kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) amesema:

((من جاء منكم إلى الجمعة فليغتسل))

((Anayekwenda ijumaa kati yenu, basi aoge)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (2/6) na Muslim (844)].

 

3- Hadiyth ya Abuu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) amesema:

((حق على كل مسلم أن يغتسل في كل سبعة أيام يوما، يغسل رأسه وجسده))

((Haki iliyo juu ya kila Muislamu, ni kuoga siku moja katika kila siku saba. Aoshe kichwa chake na mwili wake)).[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (2/318) na Muslim (849)].

 

4- Hadiyth ya Thawbaan kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) amesema:

((حق على كل مسلم السواك، وغسل يوم الجمعة، وأن يمس من طيب أهله إن كان))

((Haki iliyo juu ya kila Muislamu ni mswaki, kuoga siku ya ijumaa na ajipake mafuta uzuri ya ahli wake kama yapo)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (4/34). Tizama "Asw-Swahiyhah" (1796)].

 

5- Hadiyth ya Hafswa kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) amesema:

((على كل محتلم رواح الجمعة، وعلى من راح الجمعة أن يغتسل))

((Kila aliyebaleghe ni lazima aende ijumaa, na mwenye kwenda ijumaa ni lazima akoge)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (338), An-Nasaaiy (3/89) na Ahmad (3/65)].

 

6- Imepokelewa toka kwa Ibn 'Umar, amesema:

"Tuliamrishwa kukoga siku ya ijumaa, na tusitawadhe (ili kuondosha janaba) kutokana na kujamii".[Isnadi yake ni Hasan: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Bakr Al-Muruuziy katika "Ijumaa na fadhila zake”].

 

Wamesema:

“Na kuyafanya kuwa si wajibu wala si haki kwa mfano wa dalili hizi zilizotajwa hapo juu, hayo aliyoyaelezea Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) ya kwamba ni haki ya Allaahu (Subhaanahuu Wata'alaa) kwa kila Muislamu na kwamba ni wajibu kwa kila aliyeota (aliyebaleghe), basi hili ni jambo ambalo ngozi husisimka kwalo!!  [Mfano wake katika Al-Muhalla].

 

Nayo Jamhuri ya Maulamaa wakiwemo Ibn Mas'uud na Ibn 'Abbaas ambao ni katika Maswahaba, msimamo wao ni kuwa kukoga siku ya ijumaa ni jambo mustahabbu na wala si lazima. Na kati ya dalili muhimu walizozitoa ni:

 

1- Hadiyth Marfu’u ya Samurah bin Jun-dub:

((من توضأ يوم الجمعة فبها ونعمت، ومن اعتسل فالغسل أفضل))

((Mwenye kutawadha siku ya ijumaa, basi hilo ni jambo zuri, na mwenye kukoga, basi kukoga ni jambo bora)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (354), An-Nasaaiy (3/94), At-Tirmidhiy (497) na wengineo. Hadiyth hii ina njia ambazo nimezitafiti kwa kina na kuzizungumzia katika Allam-'at Fiy Aadaab Wa Ahkaam Al-Jum-'ah. Al-'Allaamah Al Al-Baaniy amesema ni Hadiyth Hasan].

 

Haya ni maneno yaliyo wazi zaidi katika dalili yao ijapokuwa Hadiyth ni Dhwa’iyf kwa kauli yenye nguvu.

 

2- Hadiyth Marfu’u ya Abuu Hurayrah:

((من توضأ فأحسن الوضوء ثم أتى الجمعة فاستمع وأنصت، غفر له ما بينه وبين الخمعة وزيادة ثلاثة أيام .....))

((Mwenye kutawadha, akatawadha ipasavyo, kisha akenda ijumaa, akasikiliza na akanyamaza, hughufiriwa yaliyo baina yake na kati ya ijumaa pamoja na nyongeza ya siku tatu…..)).[Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (857), At-Tirmidhiy (498) na wengineo].

 

Wamesema:

“Lau kama kuoga kwa ajili ya ijumaa kungelikuwa ni lazima, basi Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) asingelitaja wudhuu peke yake”.

 

Al-Haafidh ameijibu kauli hii katika "Al-Fat-h" (2/422) kwa kusema:

" Kukoga hakujakanushwa, kwani Hadiyth imekuja kwa njia nyingine katika Asw-Swahiyh kwa tamko "Mwenye kukoga". Kwa hiyo inawezekana kuwa Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi Waalihii Wasallam) ametaja wudhuu kwa yule ambaye alikwishaoga kabla ya kwenda, na akahitajia kutawadha tena".

 

Ninasema:

"Wao wana dalili nyinginezo nilizozitafiti kwa kina na kuzijadili moja baada ya nyingine katika Kitabu changu cha "اللمعة في آداب وأحكام الجمعة". Na hitimisho la suala ni kuwa wenye kusema kwamba kukoga ni wajibu, dalili zao zina nguvu zaidi, Sanad zake ni Swahiyh zaidi na kuzitumia ni salama zaidi”.

 

7- Kufa

 

Ni moja kati ya sababu zenye kuwajibisha kukoga, lakini si kwa maiti mwenyewe, bali ni kwa Muislamu aliyeko kwa maiti. Uchambuzi wake utakuja katika mlango wake wa "Kitaab Al-Janaaiz".

 

 

Share