055-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Kuoga Mwanamke Hedhi Na Nifasi

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

055-Kuoga Mwanamke Hedhi Na Nifasi

 

Alhidaaya.com

 

 

[Ni kutoka kitabu changu cha Fiqh As-Sunnah Lin An-Nisaai (uk. 49) na Jaami’u  Ahkaamin Nisaai cha Shaykh wetu (1/116 na ya baada yake) pamoja na nyongeza kidogo].

 

Namna ya kuoga hedhi na nifasi ni sawa na kuoga janaba. Lakini pamoja na hivyo, wakati wa kuoga hedhi na nifasi huongezewa yafuatayo:

 

1- Kutumia sabuni na mfano wake kama mada za kusafishia pamoja na maji.

 

Hii ni kutokana na Hadiyth ya ‘Aaishah aliyeeleza kwamba Asmaa alimwuuliza Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) kuhusu kuoga hedhi. Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) akamwambia:

((Atachukua mmoja wenu maji na mkunazi ajitwaharishe. Ajitwaharishe vizuri, kisha ajimiminie maji kichwani na ajisugue msuguo wa nguvu mpaka maji yafike katika mashina ya kichwa chake. Kisha atajimwagia maji na atachukua kitambaa ajisafishe nacho)).

Asmaa akasema: “Ni vipi atajisafisha nacho”?!

‘Aaishah akasema: “Subhaana Allaah! Unajisafisha nacho hivi”.

‘Aaishah akasema kana kwamba hataki lisikike: “Utafuatisha kwacho athari ya damu)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (314) na Muslim (332) na tamko ni lake].

 

2- Kufumua nywele ili maji yafike hadi katika mashina ya nywele.

 

Ni kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) katika Hadiyth iliyotangulia:

“Kisha ajimwagie kichwani, na akisugue msuguo wa nguvu mpaka yafike kwenye ngozi ya kichwa”.

 

Na Hadiyth hii ni dalili ya kuwa haitoshi tu kujimwagia maji kama ilivyo katika josho la janaba, na hasahasa pakizingatiwa kuwa katika Hadiyth hiyo hiyo, bibi huyo alimuuliza kuhusu kuoga janaba naye akasema:

“Kisha ajimwagie kichwani, na akisugue mpaka yafike kwenye ngozi ya kichwa”.

 

Na hapa Rasuli hakutaja kusugua kwa nguvu ili kutofautisha kati ya josho la janaba na josho la hedhi.

 

Maulamaa wametofautiana kuhusiana na hukmu ya kufumua nywele wakati wa kuoga hedhi. Ash Shaafi’y, Maalik, na Abuu Haniyfah wanaona kwamba hilo ni jambo mustahabu na wala si lazima. [Al-Mughniy (1/227), Al-Muhallaa (2/38), Nayl Al-Awtwaar (1/311) na Tahdhiyb As-Sunan (1/293) pamoja na Al-‘Awn]. Dalili zao ni:

 

1- Hadiyth haielezei wazi juu ya ulazima wa kufumua nywele.

 

2- Hadiyth ya ‘Aaishah aliyoielezea kuhusiana na Hijjah ya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) anaposema: “Ikanifikia Siku ya Arafah nami niko hedhini. Nikamlalamikia Rasuli  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam), naye akaniambia: “Acha ‘Umrah yako, fumua nywele zako na hirimia Hajji..” [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (317) na Muslim (1211)].... ni kuwa, josho hili linahusiana na ihraam, na wala si josho la hedhi. Kwa hivyo, Hadiyth hii haifai kuwa ni dalili.

 

3- Hadiyth ya ‘Aaishah isemayo kwamba Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) alimwambia wakati yuko hedhini: “Fumua nywele zako na uoge”.[Isnadi yake ni Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Maajah (641). Angalia pia Al-Irwaa (1/167).]…ni kuwa jibu la Hadiyth hii ni kama jibu la Hadiyth iliyopita, zote ni Hadiyth moja. Na tamshi la “uoge” wamelichukulia kwa maana ya josho la ihraam.

 

4- ‘Abdullah bin ‘Amri alipowaamuru wanawake kufumua nywele zao wakati wa kuoga, Bi ‘Aaishah alikipinga kitendo hicho.

 

Ama Maimamu wanaosema ni wajibu kufumua nywele wakati wa kuoga hedhi, hao ni pamoja na Al Imaam Ahmad, Al Hasan, na Twaawuus. Dalili zao ni Hadiyth hizo hizo zilizopita. Hayo yamehakikiwa na Al-’Allaamah Ibn Al-Qayyim (Rahimahul Laah) [Tahdhiyb As-Sunan (1/293 na kurasa zinazofuatia) pamoja na ‘Awn Al-Ma’abuwd]….. ambaye amezijibu pingamizi za Jamhuri kwa haya yafuatayo:

 

1- Wanaposema kuhusiana na Hadiyth ya ‘Aaishah wakati akihiji kwamba ilikuwa ni katika ihram, basi ni sahihi. Lakini josho la hedhi ndilo josho lililokaziwa zaidi kuliko majosho mengineyo yote, kwani Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam), ameamuru katika josho hilo mambo ambayo hakuyaamuru katika josho jinginelo kama vile kujitwaharisha kwa ukina na umakinifu zaidi. Na kwa ajili hiyo, alimwamuru azifumue nywele ikiwa ni kumzindusha juu ya ulazima wa kufanya hivyo, kwani kufanya hivyo, kunaondosha hadathi kwa njia fanisi zaidi.

 

2- Ama Hadiyth yake alipokuwa na hedhi isemayo: “Fumua nywele zako na uoge”… ni kuwa Hadiyth hii kusemwa katika wakati usio wa Hijjah kunawezekana sana na hususan tunapojua kwamba wapokezi wake wa Sanad ni katika waliohifadhi Hadiyth nyingi.

 

3- Ama ‘Aaishah kukipinga kitendo cha ‘Abdullah bin ‘Amri, bila shaka ilikuwa ni pale bwana huyo alipowaamuru akina mama kufumua nywele zao wakati wa kuoga janaba. Bibi ‘Aaishah alisema: “Anastaajabisha sana Ibn ‘Amri huyu!! Ati anawaamrisha wanawake wafumue nywele zao wakati wa kuoga!! Kwa nini basi asiwaambie wakanyoa nywele zao kabisa!! Mimi nilikuwa naoga pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) katika chombo kimoja..”[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (331), An Nasaaiy (1/203), na Ibn Maajah (604)].

 

Bila shaka ni kuwa Bi ‘Aaishah alikuwa akioga pamoja na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihii wa sallam) janaba ambapo walikuwa wakiogea chombo kimoja, lakini si katika josho la hedhi!! Na juu ya msingi huu, ni wajibu kwa mwanamke afumue nywele zake hasahasa wakati wa kuoga hedhi na nifasi, na hili ndilo la akiba zaidi. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

 

3- Kufuatilisha athari ya damu kwa kitambaa kilichotiwa miski au mafuta uzuri mengine yoyote.

 

 Itakuwa ni vizuri atumie kitambaa au pamba iliyochovewa kidogo miski, kisha aiingize kwenye utupu wake baada ya kuoga. Pia atazisafisha vizuri sehemu zote zilizoingiwa na damu katika mwili wake, na hii yote ni kwa ajili ya kujitakasa na harufu mbaya. Haya yote yamethibiti katika Hadiyth ya ‘Aaishah iliyotangulia.

 

Mwanamke anaruhusiwa kufanya hivi hata kama yuko katika kipindi cha eda ya kufiwa na mumewe, au mtu wake mwingine kutokana na Hadiyth ya Umuu ‘Atwiyyah inayohusiana na mambo anayokatazwa mwenye eda isemayo: “Wala hatujitii manukato, wala hatuvai nguo za rangi rangi isipokuwa nguo za kawaida zisizovutia. Alitupa ruhusa wakati wa kujitwaharisha pale mmoja wetu anapooga hedhi tujitie kidogo mafuta uzuri”.

 

Haya yatakuja katika mlango wake katika kitabu hiki InshaAllaah Ta’alaa.

 

 

 

Share